056-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kukausha Viungo Baada Ya Kuoga

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

056-Kukausha Viungo Baada Ya Kuoga

 

Alhidaaya.com

 

 

Katika kuelezea huko nyuma namna Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alivyokuwa akioga, Hadiyth ya Maymuunah inasema: “Nikampa nguo, (na katika riwaya nyingine: taulo), naye hakuichukua huku akiikung’uta mikono yake miwili”. Hadiyth hii imetolewa hoja kwamba ni karaha kujifuta mwili baada ya kuoga. Madai haya hayana mashiko kwa haya yafuatayo:

 

1-Lililofanyika ni tukio la hali inayoweza kubeba tafsiri tofauti. Inawezekana kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakuichukua taulo kwa sababu ya jambo jingine lisilohusiana na ukaraha wa kujifuta, bali kwa jambo linalohusiana na taulo yenyewe, au inawezekana alikuwa na haraka na kadhalika.

 

2-Hadiyth hii ni dalili kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) ilikuwa ni kawaida yake kujifuta. Na kama haikuwa kawaida yake, basi asingeletewa taulo.

 

3-Kukung’uta maji kwa mkono wake ni dalili kwamba hakuna ukaraha wa kujifuta maji, kwani yote mawili ni tendo la kuondosha maji mwilini.

 

Kikhulasa tunasema: “Hakuna ubaya kujifuta maji baada ya kuoga. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

 

Share