082-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Damu Ya Istihaadhwah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

082-Damu Ya Istihaadhwah

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni damu inayomtoka mwanamke katika nyakati zisizo za hedhi au nifasi, na wala haina uhusiano nazo. Ni damu isiyo ya kikawaida au kimaumbile, bali inatokana na mshipa uliokatika wenye kutoa damu nyekundu isiyokatika ila baada ya kupona.  [Huitwa kuvuja damu]

 

Hukmu Yake

 

Mwanamke anapotokwa na damu hii, anabakia kuwa twahara, na damu haimzuii kuswali au kufunga kwa mujibu wa Ijma’a ya Maulamaa. Ikiwa damu hii itatoka katika wakati usio wa hedhi au nifasi bila kuwa na uhusiano navyo, basi hakuna tatizo.

 

Ikiwa damu hii haikatiki, nini mwanamke atafanya?

 

Tunasema:

Mwanamke huyu haepukani na moja kati ya hali nne:

 

1- Ima atakuwa anaingia hedhini kawaida na anakijua kipimo cha hedhi yake. Huyu ataangalia kipimo hicho, kisha ataoga na ataswali. Na damu itakayoendelea baada ya hapo, itakuwa ni damu ya istihaadhwah na wala si ya hedhi.

 

Imepokelewa na Mama wa Waumini 'Aaishah akisema: "Ummu Habiybah alimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu damu. Mama wa Waumini 'Aaishah akamwambia: Nimeona beseni lake limejaa damu. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

(( امكثي قدر ما كانت تحبسك حيضتك ثم اغتسلي وصلي))

((Kaa kitambo cha hedhi inavyokuzuia, kisha oga na uswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (uk. 264), Abuu Daawuud (279), na An-Nasaaiy (1/119)].

 

2- Ima atakuwa haijui hedhi yake, lakini anaweza kupambanua kati ya damu ya hedhi na damu ya istihaadhwah. Hapo ataisubiri damu yake ya hedhi, ataacha kuswali, kisha ataoga na kuswali baada ya kumalizika hedhi yake.

 

Imepokelewa na Mama wa Waumini 'Aaishah akisema:

"Alikuja Faatwimah binti Abu Hubaysh kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke nipataye damu ya istihaadhwah na wala sitwahariki, je, niache kuswali? Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi waalihi wa sallam) akamwambia:

(( لا، إنما ذلك عرق، وليس بحيض، فإذا أقبلت حيضتك فدعي الصلاة، وإذا أدبرت فاغسلي عنك الدم ثم صلي)).

((Hapana, huo ni mshipa, na wala si hedhi, na ikija hedhi yako basi acha Swalaah, na ikimalizika, jitwaharishe kisha swali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al Bukhaariy (228) Muslim (uk. 262) na wengineo].

 

3- Ima atakuwa ndio mwanzo wa kupata hedhi na hawezi kupambanua kati ya damu ya hedhi na damu nyingineyo. Huyu ataiangalia hali ya wanawake wengi inavyokuwa. Na kama hali ya wanawake wengi anaoishi nao ni kudumu hedhi yao kwa muda wa siku sita au saba kila mwezi kwa mfano, basi atasubiri pale inapoanza hedhi yake, kisha atahesabu siku sita au saba na kuzifanya ndio siku za hedhi yake, kisha baada ya hapo ataoga. Na damu itakayoendelea baada ya hapo, ataizingatia kuwa ni damu ya istihaadhwah.

 

Imepokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Himnah binti Jahsh:

((إنما هذه ركضة من ركضات الشيطان، فتحيضي ستة أو سبعة في علم الله ثم اغتسلي، حتى إذا رأيت أنك قد طهرت واستنقيت فصلي أربعا وعشرين ليلة أو ثلاثا وعشرين وأيامهن، وصومي، فإن ذلك يجزيك، وكذلك فافعلي في كل شهر، كما تحيض النساء وكما يطهرن لميقات حيضهن وطهرن)).

((Hakika hii ni adha katika adha na masumbufu ya shaytwaan. Basi kaa na hedhi yako, siku sita au saba kwa mujibu wa Hukmu ya Allaah, kisha oga. Mpaka utakapoona umetwaharika na umetakasika kabisa, basi swali siku ishirini na tatu au ishirini na nne, na ufunge, hilo litakutosheleza. Fanya hivyo hivyo kila mwezi kama wanavyopata wanawake hedhi na kutwaharika katika nyakati zao)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (287), Ash-Shaafi'iy katika Al-Ummu (1/51), Ibn Maajah (622) na At-Tirmidhiy katika mlango wa 95 wa twahara, na Sanad yake ni Layyin. Katika Al-Irwaa (205), Al-Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan]

 

4- Ima awe mwanamke amesahau ada yake kwa kiasi chake na wakati wake wa kuja, na hawezi kupambanua kati ya damu ya hedhi na istihaadhwah. [Maulamaa wanamwita mwanamke huyu "mbabaikaji"]

 

Maulamaa wamezungumza kauli kadhaa kuhusiana na mwanamke huyu. Kauli iliyo dhahiri zaidi ni kuwa mwanamke huyu anakuwa ni kama yule mwanamke anayeanza kupata hedhi ambaye hukmu yake ishaelezwa katika hali ya tatu iliyotangulia. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Share