083-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Hukmu Zinazohusiana Na Mwanamke Mwenye Istihaadhwah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

083-Hukmu Zinazohusiana Na Mwanamke Mwenye Istihaadhwah

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Hukmu yake ni kama mwanamke aliye twahara, hakatazwi lolote katika yale aliyokatazwa mwenye hedhi.

 

2- Anaruhusiwa kuswali, kufunga, kusoma Qur-aan, kugusa Msahafu, kusujudu sajdah ya kisomo, na sajdah ya kumshukuru Allaah, na mengineyo anayoruhusiwa aliye twahara. Na hii ni kwa Ijma’a’ ya Maulamaa.

  

3- Halazimiki kutawadha kila Swalaah madhali hakutengukwa na wudhuu, kwani kauli yenye nguvu inaashiria kuwa habari zote zinazogusia hilo ni dhwa’iyf. [Zirejelee katika kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/230) na yanayofuatia]

 

Lakini lililobora pamoja na hivyo, ni kutawadha au kuoga kwa kila Swalaah kutokana na Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah kwamba Mama wa Waumini Ummu Habiybah alipatwa na damu ya istihaadhwah kwa muda wa miaka saba. Akamuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha akoge akimwambia:

(( هذا عرق))

((Huu ni mshipa)), na akawa anaoga kwa kila Swalaah. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (327), Muslim (262) na wengineo].

 

4-Mumewe anaweza kumwingilia madhali si wakati wa hedhi hata kama damu inamtoka. Hii ndiyo kauli ya Maulamaa wengi. [Al Majmu’u (2/372), na Al-Mughny (1/339)]

 

5-Inajuzu kukaa ‘itikaaf Msikitini. Imepokelewa na ‘Aaishah akisema:

“Mmoja katika wakeze wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikaa naye ‘itikaaf. Alikuwa akitokwa na damu na unjano na beseni liko chini yake huku akiswali”. [Al-Bukhaary]

 

An-Nawawy katika Sharhu Muslim (1/631) ameinukulu Ijma’a ikisema kwamba mwenye istihaadhwah katika ‘itikaaf, ni kama mwanamke yeyote mwingine mwenye twahara.

 

 

Share