Imaam ‘Abdur-Rahmaan Bin Naaswir As-Sa’diy (رحمه الله)

 

 

Imaam ‘Abdur-Rahmaan Bin Naaswir As-Sa’diy

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

 

Jina lake ni Abuu ‘Abdillaah ‘Abdir-Rahman bin Naaswir bin ‘Abdillaah bin Naaswir ‘Aliy Sa’diy wa kabila la Tamiymiy.

 

 

 

Alizaliwa katika jiji la ‘Unayzah, Qasiym mnamo tarehe 12 Muharram, 1307H. Mama yake alifariki dunia wakati yeye alipokuwa na umri wa miaka minne na baba yake alifariki dunia wakati yeye alipofikisha miaka saba. Hivyo, alikua yatima, lakini licha ya haya alikuwa na makuzi mema.

 

 

Alikuwa na akili sana na alikuwa na raghba kubwa ya kujifunza. Baada ya baba yake kufariki alikuwa tayari ameshajua kuisoma vizuri Qur-aan na kuihifadhi akiwa na umri wa miaka kumi na mmoja. Baada ya hapo alitumia muda mwingi akisoma kwa ‘Ulamaa wa mjini  mwake na ambao waliokuja kuzuru mji huo. Alijibidiisha masomoni mwake mpaka akafanya vyema katika aina mbalimbali za sayansi za ‘Ilmu ya Kiislamu.  Alipofikisha umri wa miaka ishirini na mitatu alikuwa tayari akifundisha. Alijitolea kwa hali zote kwa kujifunza na kufundisha. Mnamo mwaka 1351H akapewa mamlaka ya usimamizi wa ‘Ilmu ya Dini katika mji wake mshauri na mwelekezi kwa wanafunzi wote.

 

 

Walimu Wake:

 

 

Alisoma chini ya ‘Ulamaa waliokuwa wakiongoza katika wakati wake, miongoni mwao alikuwa Shaykh Ibraahiym bin Hamd bin Jaasir.  

 

 

Pia alisoma chini ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Kariym Ash-Shibl ambaye amesoma somo la Fiqh kwake pamoja na lugha na masomo mengineyo. 

 

Pia amesoma Tawhiyd, Tafsiyr na Uswuwl Al-Fiqh na lugha kwa Shaykh Swaalih bin ‘Uthmaan ambaye alikuwa  Hakimu wa ‘Unayzah. Alisoma kwake zaidi ya wengineo na kushikamana naye hadi alipofariki mwalimu wake huyo.

 

 

Walimu wake wengineo ni Shaykh ‘Abdullaah ibn ‘Aariydhw Shaykh Sa’iyd Al Twuwayjiriy, Shaykh ‘Aliy ibn As-Sinaan, Shaykh ‘Aal  Naaswir, Shaykh Abuu Waadi’yy ambaye alisoma kwake Hadiyth na Vitabu sita vikubwa na akasoma masomo mengineyo kwake.

 

 

Pia walimu wake wengineo ni Shaykh Muhammad mtoto wa Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Aal Muhammad Al-Maaniy ambaye alikuwa Mudiri wa Elimu katika Mamlaka ya Saudi wakati huo. Pia alisoma kwa  Muhammad Al-Mukhtaar Ash-Shanqiytwiy.

 

 

Sifa Na Khulqa Zake:

 

 

Imaam As-S’dy (Rahimahu-Allaah) alikuwa na sifa nzuri zilizomuainisha na watu wengineo. Alijulikana kwa taqwa yake ya hali ya juu,  maadili mema na unyenyekevu kwa wadogo, wakubwa, matajiri na masikini. Kila mara alikuwa akitumia muda wake kukutana na wale waliotaka wakutane naye na alikuwa mkarimu kwa masikini, mayatima na wageni, akiwasaidia kwa kadiri ya uwezo wake.

 

 

Alikuwa na hikma katika kupatanisha migogoro ya watu na hivo kuhukumu kwake  kuliacha pande zote mbili kuridhika.

 

 

Alikuwa na huruma kwa wanyonge na masikini  na akiwasaidia kila alipokuwa na uwezo na akiwashajiisha wenye mapenzi na uwezo kusaidia katika khayraat.

 

 

Alikuwa mwalimu mahiri aliweza kufafanua jambo kwa ufanisi.  Alipanga ratiba muwafaka za wanafunzi na akiandaa midahalo ya kuchangamsha bongo zao.  Akishajiisha pia  wanafunzi wake   kwa kuwapa  zawadi pindi wanapoweza  kuhifadhi Vitabu na hakuwacha mwanafunzi yeyote aliyejitahidi kuhifadhi ila alipewa zawadi. 

 

Kusoma Kwake Na Umahiri Wake:

 

Imaam As-Sa’dy alibobea katika Fiqh na Uswuwl Al-Fiqh, hatimaye akawa katika madhehebu ya Hanbal kama walivyokuwa walimu wake wote. 

 

 

Kazi yake ya kwanza katika Fiqhi iliandikwa kwa mtindo wa kimashairi juu ya madhehebu ya Hanbal ambayo ndiyo pia ilikuwa rai yake. Alisoma kazi ya Ibn Taymiyyah na Ibn Al-Qayyim kwa undani na akanufaika kutokana nao.

 

 

Alipoendelea na masomo yake hakujifunga sana na madhehebu ya Hanbal bali alifuata njia aliyoamini kuwa ilihakikishiwa ushahidi uliokuwa na nguvu zaidi. Hata hivo, kamwe hakuweza kuwalaumu au kuwadharau wale waliofuata madhehebu fulani.

 

 

Kadhalika alikuwa bingwa katika Tafsiyr, akiwa amesoma kazi nyingi za Tafsiyr na akiwa ameisoma chini ya walimu wake na kwa kweli alihariri Tafsiyr yeye mwenyewe. Wote waliomsikia akikielezea Kitabu cha Allaah ('Azza wa Jalla)  walitamani aendelee kutokana na uzungumzaji wake wa namna ya kuvutia  na faida nyingi alizozipata kutoka katika Aayah zake.

 

Alihariri kazi nyingi na miongoni mwake zilikuwa:

   

 

1-Taysyir Al-Karyim Ar-Rahman, Fiy Tafsiyr Kalaam Al-Mannaan.

 

 

2-Irshaad Li-Albaswaair  Wal-Albaab Li-Maarifatil  Al-Fiqh Biaqrab Atw-Twurq Wa Aysar Al-Asbaab 

 

 

3-Ad-Durrah Al-Mukhtaswarah fiy Mahaasin Ad-Diyn Al-Islaam

 

 

4-Al-Qawaaid Al-Hisaan Al-Muta’allaqah Bitafsiyr Al-Qur-aan

 

 

5-Al-Qawl As-Sadiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd

 

 

6-Taysiyr Al-Latwiyf Al-Mannaan Fiy Khulaasat Tafsiyr Al-Qur-aan.

 

 

7-Tafsiyr Asmaa Allaah Al-Husnaa

 

 

 

8-Bahjatul-Quluwb  Al-Abraar Wa Qurrat ‘Uyuwn Al-Akhyaar Fiy Sharh Jawaami’ Al-Akhbaar

 

 

9-Majmuw’ Al-Khutwab  Fiy Al-Mawaadhwiy’ An-Naafi’ah

 

 

10-Manhaj As-Saalikiyn Wa Tawdhwiyh Al-Fiqh Fid-Diyn

 

   

Kufariki Kwake:

 

Imaam As-Sa’dy alifariki mji wa ‘Unayzah  mnamo mwaka 1376H akiwa na umri wa miaka 69. Allaah Amrehemu na Amlipe  kheri na mema kwa juhudi zake za kunufaisha Ummah na Amuingize katika Jannah Yake ya Al-Firdaws. Aamiyn.

 

Share