Nataka Kutubia...Lakini!!

 

Nataka Kutubia ….Lakini!!

 

Imetayarishwa na: Ummu Faraj

 

Alhidaaya.com

 

AlhamduliLlaahi Rabbil ‘alamiyn was-swalatu was-salaamu ‘alaa ashrafil anbiyai wal mursaliyn nabiyinaa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa as-swhaabihi waman tabi’ahum bi-ihsaani ilaa yawmid-diyn

Amma baad:

 

Hatari Ya Kudharau Madhambi: 

Jueni ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewaamrisha waja Wake wafanye Tawbah Kwake Yeye na imekua kufanya tawbah ni wajibu kama Alivyosema Allah: 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَعْتَذِرُوا الْيَوْمَ ۖ إِنَّمَا تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٧﴾

Enyi waliokufuru! Msitoe nyudhuru Leo! Hakika mtalipwa yake mliyokuwa mkiyafanya. [At-Tahriym: 7]

 

Na Allaah Akatupa wakati wa kutubia madhambi yetu kabla Malaika wa madhambi hajaandika. Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):      

                                                                               

إ ن صا حب الشمال ليرفع القلم ست ساعات عن العبد المسلم المخطئ , فإن ند م وستغفرالله منها ألقاها, وإلا كتبت واحدة (رواه الطبرانى و البيهقى, وحسنه البانى)

“Hakika ya malaika wa kushoto hunyanyua kalamu kwa masaa sita kwa mja muislamu aliyekosea, basi akijuta (kwa kosa lake alilolifanya) na akamtaka msamaha Allaah, huacha kuandika (kosa lile), na ikiwa hakutaka msamaha litaandikwa kosa moja) [Imepokewa na Attabrany na Bayhaqiy, na Shaykh Al-Albaaniy kasema ni 'hasan']

 

Na muda mwengine Alioutoa Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kuandika na kabla ya kufikwa na Mauti. Yaani kuna nafasi iwapo mtu atakuwa kwa muda ule alipofanya makosa hakutaka msamaha wala hakutubia basi anayo nafasi ya kuleta Tawbah kabla hajahudhuriwa na mauti. 

 

Na msiba mkubwa leo hii kwa watu wengi hawana hishima na Allaah, wanamuasi Allaah katika kila aina ya madhambi usiku na mchana, isitoshe miongoni mwa makundi mengi wanayadharau madhambi, wanaona katika nafsi zao baadhi ya madhambi ni madogo, wanasema mathalan: - Kwani kuna ubaya gani nikiangalia mwanamke, au kupeana mikono baina ya mwanamme na mwanamke ajnabiya (Ajnabii ni mwanamke unayeweza kumuoa) mtu anaona ni kitu kidogo tu. Na hawaoni ubaya wowote wa dhambi wanayoifanya, wanaangilia mambo yaliyo haramishwa katika Televisheni, magazeti n.k. mpaka badhi yao wanazoea yale madhambi na kuona ni kitu cha kawaida tu, na pindi wanapojua kama wayafanyayo ni madhambi basi huuliza kwa dharau; hivi kuangalia mapicha ya utupu ni dhambi kubwa au ndogo? Kwa mtazamo huo hebu tuangalie wema waliotangulia katika watu kusema madhambi haya ni madogo, wanasemaje:

 

Katika Sahihi [Al-Bukhaariy Rahimahu Allaahu] 

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Llaahu 'anhu) amesema: - Hakika nyinyi mnafanya matendo ambayo mnayaona katika macho yenu ni kama unywele, (yaani mepesi) Sisi wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tulikuwa tunayaona ni katika yenye kuangamiza.

Na kutoka kwa Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) Amesema:- “Hakika Mu’umin anayaona madhambi yake ni kama vile amekaa chini ya jabali anaogopa lisimuangukie juu yake, na Hakika mtu muovu anayaona madhambi ni kama nzi tu ametua juu ya pua yake akamfukuza kwa mkono wake.

 

Je, ndugu yangu unayedharau madhambi, hujaona au hujasoma Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema:-

“Ole wenu na kudharau madhambi, kwa hakika mwenye kudharau madhambi mfano wake ni kama watu wameteremka katika bonde na kila mmoja wao akaleta kikuni kidogo mpaka vikaweza kupika chakula kwa kuni zile, na kwa hakika kuziona dhambi ni nyepesi ndio kutampelekea mtu kuangamia” na katika upokezi mwingine amesema:- Ole wenu na kuziona dhambi nyepesi kwa hakika hizo zitajikusanya kwa mtu mpaka zimuangamize)”. [Imepokewa na Ahmad, na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyhul Jaami’i]

 

Na wametaja watu wa Elimu kwamba dhambi ndogo imekutana na uchache wa hayaa (yaani kutokuwa na aibu) na kutokujali na kuacha kumuogopa Allaah pamoja na kuyadharau, hivyo inayafanya kuwa ni katika madhambi makubwa bali inayarutubisha. Na kwa ajili hiyo ndio ikawa hakuna dogo pamoja na makusudi wala kubwa pamoja na msamaha.

 

Kwa maana hakuna dhambi ndogo pamoja na kuifanyia kusudi kila siku unairudia rudia mwishowe huwa kubwa. Na dhambi kubwa pamoja na kutaka msamaha husamehewa kwa kutoifanyia dharau na kutokuirudia. Na wanasema katika hali hiyo basi usiangalie udogo wa maaswi bali muangalie yule unaye muaswi.

 

Na kwa hakika maneno haya yatamfaa In shaa Allah aliye mkweli, ambae anahisi ubaya wa madhambi na hadharau wala haendelei katika mambo ya batili. Na kwa hakika hawa ni wale walioamini kauli ya Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliposema:

 

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٤٩﴾وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ﴿٥٠﴾

(Ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Wajulishe waja Wangu, kwamba: Hakika Mimi ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. Na kwamba Adhabu Yangu, ndiyo adhabu iumizayo.[Al-Hijr: 49-50]

 

Kama walivyoamini kauli yake

 

Shuruti Za Tawbah Na Mambo Yanayokamilisha:

Neno 'Tawbah' ni neno kubwa ndani yake kuna uzito mkubwa si kama wanavyodhania wengi. Kwamba Tawbah ni kutamka tu katika ulimi kisha ukawa unaendelea na madhambi yako na uzingatie kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyosema:

وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ 

Na kwamba: Mwombeni Rabb wenu maghfirah kisha tubuni Kwake..[ Huwd: 3]

 

Na kwa hakika jambo hilo ni jambo kubwa kwa hiyo hakuna budi kuweko na shuruti, na bila shaka wametaja ‘Ulamaa shuruti za Tawbah ambazo wamechukua katika aya na Hadiyth. Na hizi ndizo shuruti za Tawbah:

 

1) - Kuiacha dhambi hapo hapo.

2) - Kujuta juu ya yalokupita (uliyoyafanya).

3) - Kuazimia kutorudia tena (dhambi)

4) - Kurudisha haki za watu uliowadhulumu, na kutafuta njia ya kujiweka mbali na hayo.

 

Kwa hakika hakuna budi kutimiza shuruti za Tawbah ili uweze kufutiwa madhambi yako ambayo ni kuiacha dhambi hapo hapo pale tu unapoambiwa kuwa hili haifai, na kujuta iwapo umelifanya, pia kuazimia kutokuirudia tena hiyo dhambi, na ikiwa ulichukuwa haki za watu, ulimsengenya, ulimzulia au ulimvunjia heshima yake basi huna budi kuzirejesha hizo haki kwa njia yoyote ile ambayo haitaleta madhara.

 

Na vile vile wametaja baadhi ya wanachuoni kwa kufafanua zaidi shuruti nyingine za Tawbah yenye kukubaliwa, Ni hizi pamoja na mifano:-

 

Kwanza:

Ni kuiwacha dhambi kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wala si kwa ajili ya kitu chochote, au kwamba huwezi tena kuifanya au kwa kuogopa maneno ya watu:

 

Basi haitokuwa Tawbah ikiwa umeiwacha dhambi kwa sababu ya kuogopa kupoteza cheo chako au kusikia maneno ya watu au hata kupoteza kazi yako. Kwa hivyo unaogopa kufanya dhambi ile ili usije ukafukuzwa kazi na mfano wake.

 

Wala haiwi Tawbah kwa kuacha dhambi kwa sababu ya kuogopea Afya yako au nguvu zako, kama kuacha zinaa na mambo machafu kwa kuogopa maradhi yenye kuangamiza, mfano kama (UKIMWI) na maradhi mengineyo au kuogopa kudhoofika mwili.

 

Wala haiwi Tawbah kwa kuacha kuiba kwa sababu hukuweza kuingia katika nyumba au hukuweza kufungua khazina, au kwa kuogopa Polisi.

 

Wala haiwi Tawbah kwa kuacha kutoa Rushwa ukaogopa kwa sababu unaempa ni mtu wa kitengo cha kuzuia Rushwa.

 

Wala haiwi Tawbah kwa kuacha kunywa ulevi (POMBE) au madawa ya kulevya kwa sababu ya kuogopa kufilisika.

 

Vile vile haiwi Tawbah kwa mtu ambae hawezi tena kuyafanya hayo maasi, kama kuacha kusema uongo kwa kupata maradhi ya kupooza ikawa mdomo hauwezi tena kutamka, au mzinifu anapokuwa hawezi tena kufanya zinaa kwa sababu ya ugonjwa au amekuwa mzee sana hata hakuna tena amtakae, au mwizi hawezi kuiba kwa sababu ya kupatwa mambo ambayo yanamfanya hawezi tena kuiba. Bali hawana budi watu hawa kujuta kwa waliyoyafanya na kuacha kutamani na kusema moyoni 'mimi ningekuwa mzima ningefanya kadha wa kadha'. Inavyotakiwa ni kujuta na kuondosha kabisa fikra za kutamani maasi. Kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(الندم توبة) " رواه أحمد وإبن ماجه" 

“Kujuta ni Tawbah” [Imepokewa na Ahmad Na Ibn Maajah]

 

Na Allaah Anamuweka Mtu mwenye kutamani maasi katika daraja ya kama yule aliyefanya. Jueni kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amesema: 

 

[إنما الدنيا لأربعة نفر , عبد رزقه الله مالاوعلما فهو يتقى فيه ربه, ويصل فيه رحمه , ويعلم لله فيه حقا , فهذا بأفضل المنا زل . وعبد رزقه الله علما , ولم يرزقه مالا , فهو صاد ق النية , يقول: لو أن لى  مالا لعملت بعمل فلان ,  فهو بنيته , فأجرهما سواء . وعبد رزقه الله مالا ولم يرزقه علما يخبط فى ماله بغيرعلم ولا يتقى فيه ربه , ولا يصل رحمه , ولا يعلم لله فيه حقا , فهذا بأ خبث المنا زل . وعبد لم يرزقه الله مالا ولاعلما فهو يقول:  لو أن لى مالا لعملت فيه بعمل فلان , فهو بنيته , فوزرهما سواء  (روا ه أحمد و الترميذى وصححه ‘  صحيح الترغيب والترهيب 1/9.)

“Kwa hakika Dunia ni makundi manne, Mja ameruzukiwa na Allaah mali na Elimu nae anamcha Rabb wake, na anaunga udugu, na anajua haki za Allaah, basi huyu ni bora materemkio yake. Na Mja ameruzukiwa na Allaah Elimu, na hakuruzukiwa mali, basi nia yake ikawa nzuri, anasema lau mimi ningelipewa mali basi ningefanya kama alivyofanya Fulani, basi kwa nia yake atalipwa sawa kama aliyefanya. Na Mja ameruzukiwa na Allaah mali lakini hakupewa Elimu anayachezea mali yake bila ya Elimu wala hamchi Rabb wake, wala haungi udugu, wala hajui haki za Allaah, basi huyu materemkio yake ni mabaya. Na Mja hakuruzukiwa na Allaah mali wala Elimu naye anasema: lau mimi ningekuwa na mali ningelifanya kama anavyofanya Fulani, basi kwa nia yake atabeba malipo kama aliyefanya” [Imepokewa na Ahmad na At-Tirmidhy].

 

Pili:

Aitakidi ndani ya nafsi yake kuwa kuna ubaya wa ile dhambi na kuna madhara. Na hii itakuwa Tawbah sahihi wala haitompelekea kutamani yale madhambi na kuyaona tamu na kuyafurahia pindi atakapokumbuka madhambi yaliyopita, au kuyatamani tena ayarudie kuyafanya. Na ametaja huyu mwanachuoni Ibn Qayyim (Rahimahu Allaahu) katika kitabu Adda-a wa Dawaa na tunapata faida za kujua miongoni mwa madhara mengi ya madhambi miongoni mwa hayo ni:

 

Kunyimwa Elimu, Kutokuwa na utulivu wa moyo, mambo kuwa magumu, kudhoofika mwili, kunyimwa utiifu, baraka kuondoka, uchache wa Tawfiyq ya kufanya kheri, dhiki katika kifua, kuzaliana madhambi, Na kuyazoea Madhambi, kuwa darja ya chini mbele ya Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Na watu kukudharau, Na kulaaniwa na wanyama, kuvalishwa nguo ya udhalilifu, kulaaniwa, Na Dua kutopokelewa, hayaa (aibu) kuondoka, neema kuondoka, kuteremka maangamizo, kupata mwisho mbaya na kupata adhabu za Akhera n.k. Na inampasa mtu kuyajua madhara ya madhambi ili aweze kujiepushe nayo yote, kwani kuna baadhi ya watu wanatoka katika maasi haya na kuingia katika maasi mengine kwa sababu ya kuitakidi hivi:

 

a)     Anaitakidi kwamba madhambi haya ni afadhali kuliko haya.

 

b)     Kwa sababu nafsi imeelemea sana katika hayo na matamanio yake yana nguvu.

 

c)     Kwa sababu ameyaona madhambi aina hii ni mepesi sana kuliko madhambi mengine na akayatafautisha kwa kuona bora kufanya dhambi hii kuliko dhambi hii.

 

d)     Sababu nyingine ni kubaki na marafiki waovu ambao wanaendelea kufanya maasi hivyo si rahisi naye kuyaacha.

 

e)     Sababu nyingine ni mtu kupata umaarufu na jaha kutokana na madhambi yake baina yake na watu wake, hivyo anapata nguvu juu ya dhambi yake ile na kuendelea nayo ili asipoteze hadhi yake, Kama wanavyofanya baadhi ya viongozi mambo ya shari na ufisadi, na hivi ndivyo alivyokuwa mshairi Abuu Nuwasi alipokuwa akitoa mashairi yenye kuhamasisha maasi akapewa nasiha na mshairi mwenzie Abuu ‘Itaahiyah ambae mashairi yake yalikuwa yakihamasisha kheri, Abuu Nuwaas akamjibu kwa shairi hili:-

 

Je, Huoni ewe ‘Itaahiy          Kuacha yale ninayoyapenda

Huoni yataniharibia              cheo changu kwa watu?

 

Kwa maana hiyo miongoni mwa watu wapo kama Abu Nuwaas wanamuasi Allah kwa ajili wasipoteze hadhi yao, cheo chao n.k. hali hao wanaowataka wawape sifa na cheo si lolote si chochote mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na hawataweza kuwanusuru na Adhabu ya Allaah. Hao yatawafika majuto kwa kutokutubia kwao na kudharau kila dhambi waifanyayo na kuiona ni nyepesi si lolote si chochote.

 

Tatu:

Mja afanye haraka kuleta Tawbah, asicheleweshe kwani kuna baadhi ya watu unapowambia hii ni dhambi tubia kwa Rabb wako anakwambia yeye bado kijana mpaka awe mzee, kama kwamba amejulishwa muda wa kuondoka hapa Duniani. Na kwa kufanya hivyo kuna hatari ya kufa bila ya kuleta Tawbah.  

 

Nne:

Mwenye kutubia awe anaogopa juu ya Tawbah yake ni katika upungufu, wala asichukulie moja kwa moja kuwa Tawbah yake imekubaliwa, kwa kuitakidi hivyo kutaifanya nafsi yake itulie na ajiaminishe kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na hili halitakiwi kwani mara moja linaweza kukurudisha kwenye maasi. Inavyotakiwa kila unapokumbuka ujute.

 

Tano:

Kutoa haki za Allaah zilizokupita ikiwa itawezekana, kama kutoa zakah ambazo ulizuia kutoa wakati uliopita nazo zilikua ni haki za mafaqiri

 

Sita:

Kuondoka sehemu za maasi, ikiwa kukaa hapo kutasababisha kurudi katika maasi kwa mara nyingine. 

 

Saba:

Kuwahama marafiki wenye kukusaidia maasi au mji ulofanya maaswi, na huu ni muelekeo na faida tunaipata katika kisa cha mtu aliyeua watu mia ambacho nitakielezea hapo baadae.

 

Na Allaah Amesema: 

الْأَخِلَّاءُ يَوْمَئِذٍ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ إِلَّا الْمُتَّقِينَ﴿٦٧﴾

Marafiki wapenzi Siku hiyo watakuwa maadui wao kwa wao isipokuwa wenye taqwa. [Az-Zukhruf: 67])       

   

Na makundi maovu watalaaniana wenyewe kwa wenyewe siku ya qiyama, na vile vile ni juu yako Ewe mwenye kutubia kujitenga na hayo makundi maovu na kujihadhari nayo ikiwa hutoweza kuwalingania, wala sheitwani asikudanganye akakupambia ukachanganyika nao ukarudi kwa mlango wa kuwalingania na hali wewe unajijuwa kuwa nafsi yako ni dhaifu hutoweza kuwa thabiti bali watakushinda nguvu, ni bora kujiepusha.

 

Na hali kama hizi huwapata watu wengi kurudi katika makundi waliyokuwa nayo mwanzo na kurudi tena katika kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Nane:

Kuondosha au kuvivunja au kuvichoma moto vitu vyote ambavyo vitakuletea vishawishi na kukurudisha tena katika maasi, Mfano kama ulikuwa ukipiga muziki basi uvunje ala za miziki zote, na kama ulikuwa ukisikiliza basi utupe kanda zote na cds, kama ni mlevi uvunje glasi zote na chupa na kila kitakachokufanya ukumbuke wakati unapoona, pia picha, filamu zilizo haramu kuangalia, na kusoma vitabu au magazeti yenye kuhamasisha mambo maovu, basi ondosha ili isikufanye kukumbuka na kuhisi raha na kutamani, hayo yote ukiyaleta karibu yatakufanya urudi tena kwenye maasi baada ya uongofu.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuthibitishe juu ya twaa na Tawbah iliyo ya kweli. AAMIYN!

 

Tisa:

Ni juu ya mwenye kutubia kutafuta marafiki wema ambao watamsaidia juu ya nafsi yake katika kheri badala ya marafiki waovu ili iwe badili na kuweza kuwa karibu na mambo ya kheri, na afanye pupa katika kuzikimbilia kheri kama kuhudhuria vikao vya Elimu ya dini, kumkumbuka kwa wingi Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na muda wako mwingi uwe katika mambo ya kheri mpaka sheytwaani asipate nafasi ya kukukumbusha maovu yaliyopita. Kwani kuwa faragha muda mwingi bila ya kujishughulisha na kheri yoyote kunampa nafasi sheytwaani kukumbusha yaliyopita.

 

Kumi:

Ajitahidi mwenye kutubia kuutumia mwili wake ambao aliulea katika maovu, augeuze na kujibebesha Twa’a ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na awe na pupa kufanya ya halali mpaka mwili ukae vizuri na kuwa na hadhi.

 

Kumi Na Moja:

Afanye Tawbah kabla ya mkoromo (wa kufikiwa na mauti), au kabla ya jua kuchomoza magharibi.

 

Koromo (gharghar) ni sauti inayotoka kwenye koo wakati wa kutolewa roho inapovutwa, na makusudio ni kabla qiyama kidogo kutoka roho (kufa) na qiyamah kikubwa ni hicho cha wote siku ya mwisho. Kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amesema:

 

[من تاب إلى الله قبل أن  يغرغر قبل الله منه] "رواه أحمد وترميذى" وقوله [من تاب قبل أن تطلع الشمس من مغربها تاب الله عليه]  "رواه مسلم"

“Mwenye kutubia kwa Allaah kabla ya gharghar (mkoromo wa mauti) Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) humkubalia Tawbah yake.”  [Imepokewa na Ahmad na Tirmidhy]

 

Na kauli nyingine:

“Mwenye kutubia kabla ya kuchomoza jua upande wa magharibi Allaah anaikubali Tawbah yake.”- [mepokewa na Muslim].

 

Tawbah Iliyokubaliwa:

Na tutataja mifano ya Tawbah kubwa kabisa za watu wa mwanzo wa ummah huu, nao ni Swahaba za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Kutoka kwa Buraydah (Radhwiya Allaahu 'anhu): kwamba ‘Aaiz bin Maalik Al –Aslamiy alikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu na nimezini, na mimi ninataka unitakase (Nabiy) akamrudisha. Ilipofika kesho yake akenda tena, akasema: Ee Rasuli wa Allaah hakika mimi nimezini akamrudisha mara ya pili. Basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatuma mjumbe kwa watu wake, akasema: "Je, mnajua akili yake iko sawa haina chochote?" wakasema: hatuna tujuacho isipokuwa akili yake ni timamu, ni katika wema tunavyomuona, basi akaja tena kwa mara ya tatu. (Nabiy) akatuma tena mjumbe, akawauliza nipeni khabari kwamba huyu hana neno wala akili yake haina upungufu. Basi alipokuja kwa mara ya nne likachibwa shimo, kisha (Nabiy) akaamrisha apigwe mawe”.

 

Na Amesema: akaja mwanamke wa ghaamidiyah, akasema: “Ee Rasuli wa Allaah hakika mimi nimezini basi nitakase, nae akamrudisha, ilipofika kesho yake, akasema: Ee Rasuli wa Allaah kwa nini unanirudisha? Huenda ukanirudisha kama ulivyomrudisha Maa’iz, basi naapa kwa Allaah mimi nina mimba, akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ama haiwezekani nenda mpaka uzae". Amesema: pindi alipomzaa kitoto kichanga. Akasema: huyu mtoto nimeshazaa. Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) "nenda na ukamnyonyeshe mpaka aweze kula". Alipoweza kutafuna (kula) alikwenda na mtoto wake na mkononi kamshikisha kipande cha mkate, basi akasema huyu Ee Rasuli wa Allaah sasa anaweza kutafuna na kula chakula, basi (Nabiy) akampa mtoto yule mmoja katika waislamu (Ili amlee) kisha akaamrisha achimbiwe shimo akafukiwa mpaka kwenye kifua, na akawaamrisha watu (Swahaba) wampige mawe. Basi Khaalid bin Al-Waliyd akampiga jiwe juu ya kichwa damu ikaruka ikamuingia Khaalid usoni akamtukana, akasikia Rasuli wa Allaah matusi aliyotukanwa mwanamke yule, Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Subiri ewe Khaalid! Naapa kwa yule ambae nafsi yangu iko mikononi mwake bila shaka ametubia huyu mwanamke Tawbah lau angetubia mwenye kukusanya kodi (ambaye anachukuwa kinyume na sheria) basi angelisamehewa". Kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha kumswalia, na akazikwa)". [Imepokewa na Muslim]

 

Katika upokezi mwingine amesema 'Umar Ee Rasuli wa Allah tumempiga mawe kisha tunamswalia! Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Kwa hakika ametubia Tawbah lau itagawanywa kwa watu sabini wa Madina (wenye madhambi) basi ingaliwatosha (kusamehewa)", je, hujaona jambo lolote ambalo ni bora kuliko kujitolea nafsi kwa ajili ya Allaah Mtukufu)  [Imepokewa na Abdul Razzaaq]

 

Tawbah Inafuta Yaliyotangulia:

Na wamesema wenye kusema: nataka kutubia lakini kitu gani kitanidhamini kupata msamaha wa Allah ikiwa nitatubia, na mimi ninaogopa kuthibiti katika njia hiyo, lakini ninahisi kama sitosamehewa, na lau kama nitajua Allaah atanisamehe basi ningetubia?! .

 

Basi haya anayoyahisi mtu yamewaingia watu wengi katika nafsi, na waliokuwa kabla katika Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na lau utazingatia Hadiyth mbili hizi na ukawa na yaqini itaondoka shaka katika nafsi yako [In Shaa Allaah]

 

Hadiythi ya kwanza:

Imepokewa na Imam Muslim (Rahimahu Allaahu) kisa cha kusilimu swahaba 'Amru Ibn Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

Pindi aliponijaalia Allaah Uislam katika moyo wangu nilikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikasema (kumwambia Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nyoosha mkono wako wa kulia nikupe bai’ya, akanyoosha mkono wa kulia nikampa mkono nikamshika. Akasema: una nini ewe 'Amru? Amesema: Nikasema nataka kutoa sharti. Akasema (sharti gani?) nikasema: Kwamba nisamehewe (madhambi yangu yaliyopita). Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Hivi hujui ee 'Amru kuwa Uislamu unafuta madhambi yaliyokuwa kabla yake na kwamba Hijra (kuhama) inafuta yaliyopita, na Hajj inafuta yaliyopita?).

 

Hadiyth ya pili:

Imepokewa na Imam Muslim kutoka kwa Ibn Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu): Hakika ya watu katika watu wa shirki wameua kupita mpaka, na wakazini kupita mpaka kisha wakenda kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakasema: Hakika ambayo tunasema na kuomba kwa wema, lau mtatupa khabari na tukajua kwamba haya ni kafara (tukasamehewa madhambi). Basi ikateremka Aya ya Allaah Mtukufu:

 

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾

Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu. [Al-Furqaan: 68]

 

Na ikashushwa: 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).; [Az-Zumar: 53)

 

Je, Allaah Atanisamehe?

Na asema mwenye kusema nataka kutubia lakini dhambi zangu ni nyingi sana sikuacha aina ya dhambi na katika maovu isipokuwa nimeyafanya, wala dhambi unayoifikiria na usiyoifikiria asipokuwa nimeifanya kiasi cha kwamba ninafikiria kuwa je, Allaah atanisamehe madhambi niliyoyafanya kwa muda mrefu? 

 

Na ninakwambia Ee ndugu yangu Mtukufu, matatizo haya si yako peke yako bali ni matatizo ya wengi wanaotaka kutubia, kumbuka mfano wa kijana ambaye aliyeuliza mara moja kwamba yeye alianza kufanya madhambi mapema akiwa na umri mdogo miaka kumi na saba tu kitabu chake kimejaa maovu ya kila namna; makubwa na madogo kwa aina tofauti kwa watu wa kila aina; wakubwa kwa wadogo mpaka dhambi ya kubaka mtoto mdogo wa kike, na akaiba mara nyingi hazina idadi kisha anasema, ''nimetubia kwa Rabb wangu Mtukufu'', ikawa anajitahidi kufanya kheri anaamka baadhi ya usiku anaswali na anafunga Jumatatu na Alkhamiys, na anasoma Qur-aan baada ya Swalah ya Alfajir, Je nitakubaliwa Tawbah yangu?

 

Ama kwa hakika watu wa Kitabu na Sunnah katika kutafuta hukmu na uhalali na ponyo ya matatizo haya, pindi walipokichukuwa Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) (Qur-aan) walikuta kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): Isemayo:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. Na rudini kila mara kutubu kwa Rabb wenu na jisalimisheni Kwake. [Az-Zumar: 53-54]

 

Na hili ndio jawabu la matatizo ambayo tumeyataja nalo liko wazi kabisa halihitaji kushereheshwa (kubainishwa). Ama hisia ya kwamba madhambi ni mengi mno kuliko msamaha wa Allaah huko ni mtu kutokuwa na yakini kwamba rehma za Rabb wake ni pana mno,

 

Kwanza:

Upungufu wa imaani kuwa Allaah ni Muweza wa kusamehe madhambi yote.

Pili:

Kudhoofika kwa tendo muhimu katika matendo ya moyo nayo ni matarajio. (الرجاء)

Tatu:

Kutokuweza kuifanya hiyo Tawbah wakati inafuta madhambi.

Nne:

Ni wajibu kuyatubia hayo madhambi na kuwa nayo yote hayo tuliyoyataja.

Ama ya Kwanza: inamtosha ubainisho wa kauli ya Allaah Mtukufu Aliposema:  

 

 وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ

“Na rahmah Yangu imeenea kila kitu” [Al-A’raaf: 156]

 

Ya pili:  Inamtosha hadiyth Qudsiy Sahihi:

 

وقال تعا لى  من علم أنى ذو قد رة على مغفرة الذنوب غفرت له ولا أبا لى , ما لم يشرك بى شيئا (رواه الطبرانى)  

“Amesema Allaah Mtukufu atakayejua kwamba Mimi nina uwezo wa kusamehe madhambi basi nitamsamehe wala sitojali, maadam hakunishirikisha na chochote” (vile vile mja atakapokutana na Rabb wake huko Akhera) [Imepokewa na At-Twabaraany]

 

Hakika tujue Allaah ni Mwenye kusamehe maadamu hutomshirikisha. Kwani dhambi ya shirki Allah Haisamehe wailla mtu atubie hapahapa ulimwenguni kabla ya mauti.

 

Ama ya Tatu:

 

Inamtosha mtu kuwa ni ponyo katika Hadiyth Qudsiy Aliposema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

عن أنس رضي الله عنه   قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وآله وسلم  يَقُولُ:  ((قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ مَا دَعَوْتَنِي وَرَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ عَلَى مَا كَانَ مِنْكَ وَلاَ أُبَالِي. يَا ابْنَ آدَمَ لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنَانَ السَّمَاءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ . يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الأَرْضِ خَطَايَا ثُمَّ لَقِيتَنِي لاَ تُشْرِكُ بِي شَيْئًا لاَتَيْتُكَ بِقُرَابِهَا مَغْفِرَةً))  رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ. 

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ‘ambaye alisema: Nilimsikia Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam akisema: Allaah amesema: Ee Mwana wa Aadam utakaponiomba na kuweka matumaini kwangu, basi nitakusamehe makosa uliyoyafanya na sitojali. Ee Mwana wa Aadam kama dhambi zako zingefika mawingu ya mbingu na wewe ukaomba msamaha kwangu, ningekusamehe wala sitojali.  Ee Mwana Wa Aadam kama ungelinijia na dhambi kubwa kama dunia na ukanikabili bila ya kunishirikisha nitakupa maghfira (msamaha).  [Imepokelewa na At-Tirmidhi na kasema ni hadiyth Hasan Sahihi]

 

Ama Ya Nne: inamtosha mtu kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 "Mwenye kutubia madhambi ni kama hana dhambi" [Imepokelewa na Ibn Maajah]

Na yeyote anayeona madhambi yake ni mengi na akakata tamaa kwamba Allaah labda Hatomsamehe madhambi yake basi na aangalie Hadiyth hii.

 

Hadythi iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim:

Kutoka kwa Abu Sa'iyd Sa'ad bin Maalik bin Sinaan Al-khudriy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amesema:-

 

Kulikuweko mtu kabla yenu ameua watu tisini na tisa (99) basi akauliza kwa watu katika ardhi ile ili aonyeshwe mtu akamuulize, akaelekezwa kwa Raahib (Kiongozi ambae hana elimu) akenda na akamuuliza na kumwambia hakika ya mimi nimeua watu tisini na tisa je, ninayo Tawbah? Akamwambia huna Tawbah wewe, basi akamuua yule mtu akatimiza watu mia (100), kisha akawauliza wenye kujua wamuelekeze akaonyeshwa mtu mwenye elimu akamwambia hakika mimi nimeua watu mia (100) je, ninayo Tawbah? Akamwambia ndio unayo Tawbah, na ni nani atakayezuia baina yako na baina ya Tawbah?! Nenda mpaka katika ardhi kadha wa kadha kwa hakika huko utawakuta watu wanamuabudu Allaah Mtukufu basi nenda ukamuabudu Allaah pamoja nao wala usirudi katika ardhi hii kwa hakika ardhi hii ni ovu (mbaya). Akenda mpaka alipofika nusu ya njia yakamjia mauti akafa basi wakajikusanya Malaika wa rahma na Malaika wa adhabu. Wakasema Malaika wa rahma huyu ni wetu amekuja na hali moyo wake ameuelekeza kufanya Tawbah kwa Rabb wake. Wakasema Malaika wa adhabu huyu ni wetu hajawahi kufanya amali yoyote ya kheri katu. Basi akaja Malaika mwingine kwa sura za kibinaadamu akajaalia kuwa hakimu baina yao akasema: Pimeni baina ya ardhi mbili basi ikiwa anakotoka ni mbali na anakokwenda ni karibu basi huyo ni wa peponi, na kama anakotoka ni karibu na anakokwenda ni mbali basi huyo ni wa motoni. Basi wakapima wakakuta ile ardhi anayokwenda ni karibu akachukuliwa na Malaika wa rahma na akawa ni katika watu wa Jannah.

 

Katika riwaya nyingine wanasema alikuwa karibu kabisa na kijiji kile cha watu wema kwa shibri basi akawa katika watu wale wema. Na katika riwaya nyingine ambayo ni sahihi wanasema Allaah akaifanya ile ardhi iliyokuwa mbali na akaifanya kuwa karibu walipopima wale Malaika wakakuta ardhi anayokwenda ni karibu kwa shibri akawa ni mwenye kusamehewa.

 

Naam, na nani ambae atazuia baina yako wewe na baina ya Tawbah!! Je! hujaona ewe mwenye kutaka kutubia jinsi gani madhambi ya mtu huyu aliyotajwa katika hadiyth yalivyokuwa makubwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemsamehe basi kwa nini wewe unakata tamaa? hail Allaah katika Qur'aan amesema:

 

 وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾

Na wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri. [Yuwsuf: 87].

 

Hivi hujui ndugu yangu Muislam kwamba Allaah hupokea Tawbah za waja wake pindi wanaporejea kwake? Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ 

Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayepokea tawbah ya waja Wake,. [At-Tawbah: 104]

 

Hapa moja kwa moja Allah Anampokelea mja Tawbah yake bila ya kupitia Wasila (njia) yoyote, umuombe Allah peke Yake wala usimshirikishe na chochote katika Ibada zake zote na Allah Atakusamehe. Kasema Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu. Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Qiyaamah, na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika. Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Furqan: 68-70]

 

Wakataja wanawazuoni kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anayabadilisha maovu kwa wema nayo ni aina mbili:

Kwanza: 

Kubadilishiwa sifa mbaya kuja sifa nzuri hapa hapa duniani mfano; kutoka katika shirki kuja katika Iymaan, kutoka katika uzinifu hadi kusamehewa, uongo kuwa mkweli, khiana kuwa muaminifu na mfano wake.

Pili:

Kubadilishiwa maovu yako ambayo umeyafanya kuwa ni mema siku ya Qiyamah. Ambayo tukizingatia kauli ya Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) "Atakubadilishieni Allaah mabaya yenu kuwa ni mema".

 

Ndugu zangu katika Iymaan:

Tunaona kuwa hii ni katika fadhila kubwa kabisa itokayo kwa Rabb wetu Mtukufu ambayo ametupa waja wake. Basi tusisubiri muda ukatupita bali tulete Tawbah na Istighfari kwa wingi turejee kwa Allah ili tupate msamaha na mazuri hapa Duniani na kesho Akhera yasije yakatupata majuto siku ya Qiyamah na tukakosa wa kutunusuru.

 

Hebu tumuangalie Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye yeye amesamehewa madhambi yake yaliyopita na yatakayokuja baadae, Je, mimi na wewe ndugu yangu?

 

Kutoka kwa Al-Agharr bin Yaasir Al-Muzani (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Enyi Watu! Tubuni kwa Allaah na mtake msamaha kwake kwa hakika yangu mimi ninatubu kwa Allaah kila siku mara mia" [Imesimuliwa na Muslim].

 

Enyi ndugu zangu wapenzi katika Iymaan hatuna budi na sisi kufanya Tawbah kwa wingi kwani milango ya Tawbah iko wazi mpaka jua litakapochomoza upande wa magharibi.

 

Na Ananadi Allaah Mtukufu Anasema: "Enyi waja wangu hakika nyinyi mnafanya makosa usiku na mchana Mimi nasamehe dhambi zote basi nitakeni msamaha Mimi ili nikusameheni" [Imesimiliwa na At- Tabraniy].

 

Na Allaah Ananyoosha mkono wake usiku kupokea Tawbah kwa aliyekosea mchana, na Ananyoosha Mkono Wake mchana kupokea Tawbah kwa aliyekosea usiku.

Vile vile kwa hakika Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawapenda wenye kutubia na kujitakasa.

 

Mwisho Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuhifadhi na kila mabaya na Atujaalie tuwe ni wepesi wa kuyaendea Maghfira.

 

Ee Rabb wetu Mtukufu tunakuomba kwa Utukufu wako na Ufalme wako Wewe Ndiye wa kukusudiwa Hukuzaa wala Hukuzaliwa wala hakuna Uliyefanana naye hata mmoja.

 

Ee Rabb wetu Mtukufu Tupe mema hapa duniani na Akhera na Utuokoe na adhabu ya moto. Aamiyn.

 

Wa Allaahu A'alam

 

Share