004-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Kumwosha Maiti

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

004-Kumwosha Maiti 

 

Alhidaaya.com

 

 

· Hukmu yake

 

[Al-Majmu’u (5/128), Al-Ummu (1/243), Al-Muhalla (5/113) na Al Fat-h (3/125)]

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba kumwosha maiti ni Fardhi Kifaayah, bali An-Nawawiy kanukulu Ijma’a juu ya hilo!!

 

Al-Haafidh kasema: “ Na hili ni la kushangaza sana, kwani makhitilafiano katika mas-ala haya ni mashuhuri mno kwa Maalik”.

 

Dalili za Jamhuri ni hizi:

 

1- Ni pale Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Ummu Salamah pamoja na wanawake walioshirikiana naye katika kumwosha binti yake: ((Mwosheni mara tatu au mara tano)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake iko njiani].

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na mtu aliyehirimia ambaye ngamia wake alimwangusha akavunjika shingo na kufa: ((Mwosheni kwa maji na mkunazi)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake iko njiani].

 

Muktadha wa agizo katika Hadiyth hizi mbili ni wajibu, na hakuna kigeuzi cha kuifanya kuwa Sunnah, na anayesema kwamba ni Sunnah basi hasikilizwi.

 

3- Ndivyo Waislamu wanavyofanya toka enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka hivi leo

 

Ninasema: “ Maiti wote wa Kiislamu wa kiume na kike wako sawa katika hili la kuoshwa; mkubwa au mdogo, muungwana au mtumwa, isipokuwa kwa aliyeuawa kishahidi kwenye vita vya kupambana na makafiri kama itakavyokuja kuelezwa mbeleni”.

 

· Je, Mtoto Wa Mimba Iliyoharibika Ataoshwa?

 

Mwanamke akiharibikiwa na mimba ya zaidi ya miezi minne, basi kitoto kitaoshwa na kuswaliwa. Na kama ni chini ya miezi minne, basi hakioshwi wala kuswaliwa, bali hutatiwa kwenye kitambaa na kuzikwa. Hii ni kwa vile  huwa kishapuliziwa roho baada ya miezi minne, na kabla ya hapo hakiwi ni kiumbe bali huwa kama kitu kisicho na roho na damu, hivyo hakiswaliwi. [Al-Majmu’u (5/256) na Al-Mughniy (2/522)].

 

· Shahidi Wa Vita Haoshwi

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwakusanya watu wawili katika nguo moja katika maiti wa vita vya Uhud kisha huuliza: (( Ni yupi kati yao aliyehifadhi zaidi Qur-aan?)) Anapoonyeshwa, humtanguliza kwenye mwanandani na husema: ((Mimi ni Shahidi kwa hawa Siku ya Qiyaamah)), kisha huamuru wazikwe na damu zao, hawakuoshwa wala hawakuswaliwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1343), Abu Daawuud (3135) na Ahmad (3/128)].

 

Sababu ya kutooshwa shahidi inaelezwa katika Hadiyth ya Jaabir toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu maiti wa Uhud aliposema: (( Msiwaoshe, kwani kila jeraha –au kila damu- litatoa harufu ya miski Siku ya Qiyaamah)). Hawakuswaliwa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/399). Ina Hadiyth mweza kwa Al-Bayhaqiy (4/11)]. Shahidi asiyeoshwa ni yule aliyekufa akiwa kwenye vita ya kupambana na makafiri sawasawa kwa kuuliwa na kafiri, au kwa kupigwa kimakosa na silaha ya Muislamu, au kwa kudhuriwa na silaha yake mwenyewe, au kwa kuanguka toka juu ya farasi wake, au kwa kukanyagwa na mnyama wake au wanyama wa Waislamu wenzake. Pia kwa kukutwa amekufa baada ya vita kumalizika hata kama sababu ya kifo chake haikujulikana, ni sawa akikutwa na athari za damu au hakukutwa, au akifa papo hapo au akabakia muda hivi kisha akafariki kabla ya kumalizika vita. [Al-Majmu’u (5/261)].

 

· Shahidi Akiuawa Naye Ana Janaba

 

Haoshwi pia kwa mujibu wa kauli Swahiyh ya Maulamaa. [Al-Majmu’u (5/26) na Al-Mughniy (2/530)].

 

Na hii ni kwa mambo mawili:

 

1- Kwa ujumuishi wa dalili zilizotangulia wa kutooshwa shahidi.

 

2- Kuacha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwosha Handhwalah bin Abiy ‘Aamir wakati alipouawa na kusema: ((Hakika mwenzenu anaoshwa na Malaika)). Wakamuuliza mkewe akasema:  “Yeye alitoka aliposikia mbiu ya vita akiwa na janaba”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (3/204) na Al-Bayhaqiy (4/15). Angalia As-Swahiyhul Musnad Min Fadhwaaili As Swahaabati cha Sheikh wetu (Allaah Amhifadhi)].

 

Hadiyth hii imetolewa hoja kwamba inajuzu kumwosha kutokana na kitendo cha Malaika. Lakini haifichikani hapa kwamba hoja ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyeacha kumwosha na si kwa kuwa Malaika walimwosha. Kwa kuwa makusudio yake ni wanadamu kutaabudia kwa hilo, na kama kumwosha kungelikuwa ni wajibu, basi kusingetenguliwa kwa kuoshwa na Malaika.

 

· Je, Shahidi Aso Wa Vita Huoshwa?

 

Shahidi aso wa vita kama aliyekufa kwa ugonjwa wa tumbo, tauni, kughariki na kuporomokewa na nyumba, huoshwa na huswaliwa kama maiti wengineo. Hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa. [Al-Mughniy (2/536). Ikichelewa mwili wake kunyambuka kwa maji, hatooshwa kwa maji bali atatayamamishwa ikiwezekana. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi].

 

· Si Lazima Kumwosha Kafiri

 

Ni sawa akiwa dhimmiy (kafiri aishiye chini ya himaya ya Waislamu) au mwingineyo, kwa kuwa si mtu wa ‘ibaadah wala mtu wa kujitwaharisha.

 

Lakini inajuzu kwa Muislamu kuwaosha akaribu zake mapagani, au mkewe dhimmiyyat, na kusindikiza jeneza zao na kuwazika, lakini hawaswalii. Na akaribu zake makafiri wana haki zaidi kwake kuliko akaribu zake Waislamu. [Al-Majmu’u (5/144) na Al-Ummu (1/235)].

 

Ama yaliyosimuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru ‘Aliy amwoshe baba yake, Sanad zote za Hadiyth hiyo hazina nguvu na hazina mashiko. [Angalia Al-Ghuslu wal Kafan cha Sheikh wetu Mustwafa bin Al-‘Adawiy – Allaah Ainyanyue hadhi yake uk 120].

 

· Nani Anastahiki Zaidi Kumwosha Maiti?

 

Imesuniwa maiti aoshwe na mtu wa karibu zaidi katika jamaa zake ikiwa ana sifa na ujuzi wa kuosha. “Kwa kuwa waliomwosha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘Aliy na jamaa zake”. [Hadiyth Swahiyh: Ibn Maajah ameikhariji maana yake (1467), Al-Haakim (1/362) na Al-Bayhaqiy (3/388)].

 

Imepokelewa toka kwa Saalim bin ‘Ubayd Al-Ashja’iy ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki, walimwambia Abu Bakr: “Ee swahibu wa Rasuli wa Allaah! Nani atamwosha?” Akasema: “Ni wanaume wa watu wa nyumba yake; wa karibu zaidi kisha wa karibu zaidi”. Wakauliza: “ Wapi tutamzika?” Akasema: “Mzikeni katika kiwanja ambacho Allaah Amemfisha, Hakumfisha isipokuwa katika kiwanja ambacho yeye anakipenda zaidi”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/395). Katika Sanad yake yuko Suwadah bin Salamah bin Bunayt. Sheikh wetu kasema: “Sikuipitia sera ya maisha yake”].

 

Shughuli ya kumwosha inaweza kufanywa na wasio akaribu wake (na hasa wakiwa ni wajuzi wa kazi hiyo). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaamuru akaribu wa binti yake Zaynab kumwosha, bali waliomwosha ni Ummu ‘Atwiyya na wengineo kama itakavyokuja kuelezwa.

 

· Inajuzu Mume Kumwosha Mke Wake

 

[Al-Muhalla (5/174), Al-Majmu’u (5/132) na Al-Ummu (1/242)].

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliposema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alirejea kwangu siku hiyo toka Baqiy’i kwenye mazishi, nami nahisi maumivu ya kichwa na kulalama kwa maumivu. Akasema: (( Lau hilo likituka ukafa kabla yangu nikakuosha na kukuvika sanda, kisha nikakuswalia na kukuzika)). Nikasema: Lakini mimi au kana kwamba mimi kwako naapa kwa Allaah, laiti ungenifanyia hayo, ukarejea nyumbani kwangu, na ukalala humo na baadhi ya wakezo. Akasema: Rasuli wa Allaah akatabasamu, kisha yakamuanza maumivu yaliyokuwa sababu ya kifo chake”. [Swahiyhun Lighayrihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6/228), Ibn Maajah (1465) Ad-daaramiy (1/37) na wengineo].

 

Na pia Allaah Mtukufu Amemwita mwanamke wa mtu kwa jina la mke baada ya kufariki Aliposema:

((وَإِن كَانَ رَجُلٌ يُورَثُ كَلَالَةً أَوِ امْرَأَةٌ وَلَهُ أَخٌ أَوْ أُخْتٌ فَلِكُلِّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا السُّدُسُ ۚ))

(( Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye kaka au dada, basi kila mmoja kati yao atastahiki sudusi )). [An-Nisaa (4:12)]

Na kwa kuwa hakukuweko kizuizi cha kumwogesha wakati wa uhai wake, basi uhalali wa hilo unaendelea hata baada ya kufariki bila tofauti ya uhai na umauti isipokuwa kwa Aayah au Hadiyth, na hivyo havipo.

 

An-Nawawiy na Abu Haniyfah wanasema kwamba mwanamume hamwoshi mkewe, kwa kuwa angelitaka, angelimwoa dada yake wakati alipokufa!! Yaliyoelezwa ni hoja inayowarudi.

 

· Inajuzu Mke Kumwosha Mumewe [Vyanzo vya kifiqhi vilivyotangulia].

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “ Laiti ningelijua jambo hili mwanzoni. Hawakumwosha Rasuli wa Allaah isipokuwa wakeze”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3141) na Al-Bayhaqiy (3/398)].

 

Al-Bayhaqiy kasema (3/398): “ Nikahuzunishwa na hilo, na halihuzunikiwi ila lenye kujuzu”.

 

Imepokelewa kwa jumla ya Sanad ya kwamba wakeze Abu Bakri walimwosha kutokana na wasia alioutoa”. [Muswannaf ‘Abdul Razzaaq (6117-6119-6123-6124) na Ibn Abiy Shaybah. Angalia Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/466)].

 

·Je, Mtu Anaweza Kumwosha Binti Yake?

 

[Al-Majmu’u (5/151), Jaami’u Ahkaamin Nisaa cha Sheikh wetu (1/475) na nukuu kutoka kwake katika kitabu changu cha Fiqhu As-Sunnat Lin-Nisaa (ukurasa 186)].

 

Tumeshasema kwamba Ummu ‘Atwiyyah ndiye aliyemwosha binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na (Hadiyth itakuja kulizungumzia hilo). Lakini kama hakuna wanawake wa kumwosha maiti, au wakawepo lakini ujuzi wao ni mfinyu, basi hakuna kizuizi chochote kilichoripotiwa cha kumzuia mtu kumwosha binti yake. Mtu kwa binti yake ni kama mwanamume mwenzake kwa upande wa utupu na ufaragha. Haya yameelezewa na baadhi ya watangu wema. Imepokelewa toka kwa Abu Haashim kwamba Abu Qulaabah, alimwosha binti yake. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/251)].

 

Hili pia wamelisema Al-Awzaa’iy, Maalik na Ash-Shaafi’iy.

 

· Wanawake Wanaweza Kumwosha Mtoto Wa Kiume

 

[Al-Mughniy (2/455) na Al-Majmu’u (5/149)].

 

Ibn Al-Mundhir kasema: “Maulamaa wote wamekubaliana kwamba mwanamke anaweza kumwosha mtoto mdogo wa kiume”.

 

Imethibiti toka kwa Hasan kwamba yeye alikuwa haoni tatizo mwanamke kumwosha ghulamu kama asha acha kunyonya akiwa amesitiriwa na kitu. Pia limethibiti hilo toka kwa Ibn Syriyna. [Isnadi zote mbili ni Swahiyh: Zimefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/251)].

 

Ninasema: “Mahala pa kujuzu huku ni pale kama mtoto hajafikia umri wa kutamaniwa kimwili na mwanamke. Kama kafikia, basi wanawake hawamwoshi. Hivi ndivyo An Nawawiy alivyoliwekea kidhibiti”.

 

· Mwanamume Akifa Na Hakuna Wa Kumwosha Isipokuwa Wanawake Peke Yao, Au Mwanamke Na Hakuna Wa Kumwosha Ila Wanaume

 

Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na hili:

 

Ya kwanza: Ataoshwa akiwa na nguo.

 

Ya pili: Atatayamamishwa na haoshwi, kwa kuwa anakuwa katika hukmu ya mtu asiyepata maji.

 

Imepokelewa kwa njia Mursal toka kwa Makhuwl toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba kasema: ((Mwanamume akifa na hakuna isipokuwa wanawake tu, au mwanamke na hakuna isipokuwa wanaume tu, watatayamamishwa na kuzikwa, nao wako katika hukmu ya mtu asiyepata maji)). [Hadiyth Mursal: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/413) na Al-Bayhaqiy (3/398)].

 

Hadiyth hii inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Sinaan bin Gharafah –alikuwa na usuhuba- toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na mwanamke anayekufa akiwa na wanaume ambao si maharimu isemayo: ((Hutayamamishwa na haoshwi, na pia mwanaume)).[Al-Bayhaqiy kaitaja (3/398)].

 

· Sifa Za Mwoshaji

 

[Al-Ghuslu wal Kafan cha Sheikh wetu (ukurasa 62-65) kwa mabadilisho kidogo].

 

Mwenye kumwosha maiti ni lazima awe na sifa mbili:

 

1- Awe mwema mwenye maadili mema

 

Kwa kuwa mwenye sifa hii, anaijua vyema Mipaka ya Allaah na sharia ya dini yake. Na kwa sifa hii, ataisitiri aibu yoyote ya maiti. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kumsitiri Muislamu, Allaah Atamsitiri Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2442) na Muslim (2580)].

 

Pia hatamtusi na mfano wa haya. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiwatusi wafu, kwani hakika wao washayafikia waliyoyatanguliza)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1393)].

 

Kadhalika, atahifadhi siri yake na hatomsengenya. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na kusengenya: ((Ni kumtaja nduguyo kwa analolichukia)). Na akasema: ((Ikiwa unalolisema analo, basi umemsengenya, na kama hanalo, basi umemzushia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2589)].

 

Imepokelewa toka kwa Raafi’i (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kumwosha maiti akamsitiri aliyonayo, Hughufiriwa mara arobaini. Na mwenye kumkafini maiti, Allaah Atamvisha sun-dus na hariri nzito ya Peponi. Na mwenye kuchimba kaburi la maiti akamsitiri humo, hutiririshiwa malipo kama malipo ya nyumba aliyomweka aishi mpaka Siku ya Qiyaamah)).[Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/354-362) na Al-Bayhaqiy (3/395)].

 

2- Awe mjuzi wa kuosha

 

Mwenye kuijua kazi ya kuosha, huitekeleza ipasavyo Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Humtendea vyema maiti na humwosha itakikanavyo. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpeleka Ummu ‘Atwiyyah ili amwoshe binti yake. An-Nawawiy ameeleza – kwa kumtaja bayana Ibn ‘Abdul Barr – kwamba Ummu ‘Atwiyya alikuwa mwosha maiti za wanawake.

 

Na hili linatiliwa nguvu ya kwamba: “ ‘Aliy alipotaka kumwosha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliingiza mkono ili atoe uchafu anaotolewa maiti na hakuupata, akasema: Baba yangu ni fidia kwako. Wewe ni mtwaharifu. Ni mtwaharifu ukiwa hai, ni mtwaharifu ukiwa maiti”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1467), Al-Haakim (1/362) na Al-Bayhaqiy (3/388)].

 

Na hapa kuna dalili kwamba ‘Aliy alikuwa ni mjuzi wa kuosha na anajua hali anayokuwa nayo maiti. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Faida:

 

Mwenye janaba au hedhi anaweza kumwosha maiti kwa kuwa hakuna dalili ya kuzuia hilo.[Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/187)].

 

 

 

Share