005-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Sifa Ya Kumwosha Maiti

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

005-Sifa Ya Kumwosha Maiti

 

Alhidaaya.com

 

 

Mhimili katika mlango huu ni Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyyah (Radhwiya Allaahu Anhaa). Yeye alishiriki kumwosha binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akalihadithia hilo na akalifanya kwa utimilivu. Maswahaba na Maulamaa wa Taabi’iyna huko Basrah, walikuwa wakipata maelekezo toka kwake juu ya namna ya kuosha maiti, na maimamu wakajifunza kutoka kwao.

 

Imepokelewa  toka kwa Ummu ‘Atwiyyah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwetu nasi tunamwosha binti yake (Zaynab). Akatuambia: (( Mwosheni mara tatu au mara tano au zaidi ya hivyo kwa maji na mkunazi, na mwisho mtieni kafuri. Na mkimaliza, basi niiteni)). Tulipomaliza, tulimwita, akaturushia izari yake akisema: ((Mtatieni nayo mwilini)).

 

Katika tamko jingine: ((Mwosheni kiwitri)). Na jingine: ((Tatu, au tano au saba)).  Pia: ((Anzeni kulia kwake na viungo vyake vya wudhuu)). Aidha, Ummu ‘Atwiyyah kasema: “Na tukamchana nywele makuruni matatu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1254), Muslim (939), Abu Daawuud (3142), An-Nasaaiy (4/32) na Ibn Maajah (1458). Katika mlango huu, kuna Hadiyth ndefu Marfu’u katika konteksi ya sifa ya kuosha maiti toka kwa Ummu Sulaym ambayo iko kwa Al-Bayhaqiy (4/4), lakini ni Dhwa’iyf. Bali Abu Haatim kasema kwenye Al-‘Ilal (1/361): “Kana kwamba ni batili inayofanana kuwa maneno ya Ibn Syriyna. Pamoja na hivyo, washereheshaji wengi wameitegemea].

 

Vitendo vya kumwosha maiti vinaweza kuelezwa kiufupi kwa mujibu wa yaliyokuja katika Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyyah na mengineyo yaliyoelezewa na Maulamaa katika haya yafuatayo:[Al-Ghuslu wal Kafan cha Sheikh wetu (uk. 67 – 105) kwa mabadilisho kidogo na kwa muhtasari].

 

1- Maiti avuliwe nguo zake na utupu wake usitiriwe

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (kuhusiana na kisa cha kufariki Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) akisema: “ Walipotaka kumwosha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walisema: Wal-Laahi hatujui. Je, tumvue nguo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tunavyowavua maiti wetu, au tumwoshe na nguo zake?”. [Hadiyth Hasan: “Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3141), Ahmad (6/267), Al-Haakim (3/59) na Al-Bayhaqiy (3/387)].

 

Hadiyth inakamilisha ikifahamisha kwamba walikuwa wakiwavua nguo maiti. Lakini pamoja na hivyo, uchi wa maiti ni lazima usitiriwe kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwanaume asiutizame uchi wa mwanaume, wala mwanamke asiutizame uchi wa mwanamke)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (338)]

 

Na kwa haya, Ibn Syriyna, Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad wanasema kwamba maiti husitiriwa uchi (kati ya kitovu na magoti). [Al-Mughniy (2/453)].

 

2- Mwanamke afumuliwe mistari ya nywele kama amesuka

 

Ni kwa aliyoyasema Ummu ‘Atwiyyah (katika riwaya ya Al-Bukhaariy 1260 na wengineo): “ Tulifunga makuruni matatu katika kichwa cha binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tulizifumua nywele, tukaziosha, kisha tukaweka makuruni matatu”.

 

3- Kazi yote ya uoshaji ifanywe kwa upole na utuvu

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika upole hauwepo katika kitu chochote ila hukipamba, na hauondoshwi kwenye kitu chochote isipokuwa hukiharibu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2594)].

 

Na kwa kuwa pia hishma ya maiti, ni sawa na hishma ya aliye hai. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kuvunja mfupa wa maiti, ni kama kuvunja mfupa wa aliye hai)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3207), Ibn Maajah (1616) na Ahmad (6/58)].

 

4- Maji yachanganywe na mkunazi au sabuni na mfano wake (katika majosho ya mwanzo)

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwosheni kwa maji na mkunazi)).

 

Na kama kutahitajika maji kupashwa moto ili uchafu uondoke vizuri na mfano wake, basi litafanywa lenye tija zaidi.

 

5- Uanze kuoshwa upande wake wa kulia na kwenye viungo vyake vya wudhuu baada ya niya na kupiga Bismil-Laah

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Anzeni kwa upande wake wa kulia, na kwenye viungo vyake vya wudhuu)).

 

Na hii ni pamoja na kumsukutusha, lakini kama itahofiwa maji kuingia ndani ya mwili na kusababisha mwili kuharibika au kutoka kwenye sanda yake, basi itakuwa bora kupangusa meno yake na pua yake kwa kitambaa cha maji mpaka visafike.

 

6- Kichwa kioshwe vizuri kwa maji na mkunazi (sabuni) mpaka kwenye maoteo ya nywele, na kisha nywele zichanwe kwa upole

 

[Al-Ummu (1/249) na Al-Mughniy (2/458)]

 

Kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika josho la janaba akiteka mateko matatu na kukipachanisha kichwa chake hadi kufikia kwenye maoteo ya nywele kama ilivyotangulia kwenye mlango wa twahara.

 

7- Uoshwe upande wa kulia wa mwili wake

 

Ni kwa kummiminia maji toka ubapa wa kulia wa shingo yake mpaka kwenye unyayo wake wa kulia. Ataosha pia mkato wa kifua, ubavu wake, paja lake, na muundi wake wote wa kulia. Mtu mwingine atautaharakisha mguu ili maji yapenye vizuri kati ya mapaja yake, kisha atachukua maji aoshe upande wa kulia wa mgongo wake. [Al-Ummu (1/249)]

 

8- Upande wake wa kushoto utafanywa kama ulivyofanywa upande wa kulia

 

9- Ageuzwe kwa ubavu kisha aoshwe kichogo, mgongo na makalio mawili na yanayofuatia hayo ambayo haikuwezekanika kuoshwa kwa mbele.

 

10- Achanwe nywele, na nywele za mwanamke zisukwe mikia mitatu.

 

Mkia mmoja uwepo upande wa kulia wa kichwa, mwingine upande wa kushoto, na wa tatu utosini, na kwa mwanamke nywele zilazwe kwa nyuma. Usukaji mikia utakuwa katika josho la mwisho.

 

Katika Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyya iliyoko kwa Al-Bukhaariy (263): “Tukamsuka makuruni matatu tukailazia kwa nyuma”.

 

11- Josho likaririwe mara nyingi

 

Ili asafike na anadhifike vizuri kutokana na neno lake Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): (( Au zaidi kama mtaona)). Na imesuniwa iwe kwa hisabu ya witr kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwosheni kwa witr)).

 

12- Kafuri (au miski na mfanowe) iongezwe katika osho la mwisho

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Na iwekeni mwisho kafuri)), isipokuwa kama maiti ni muhrim, hapo hatawekewa manukato kama itakavyokuja kubainishwa mbeleni.  

 

13- Baadhi ya Maulamaa wanaona kuwa:[Al-Ummu (1/249) na Al-Majmu’u (5/168)].

 

Baada ya kumwosha, mikono na miguu irejeshwe na kuambatishwa na ubavu wa kulia na kushoto, nyayo zinyooshwe sawa, na kifundo kimoja kiambatishwe na kingine, mapaja yashikanishwe, kisha akaushwe kwa nguo. Wanaona pia akamuliwe kwa ulaini tumboni wakati wa kuoshwa ili kitoke kilichoko humo, na akalishwe mwisho wa kila josho.

 

14- Mwoshaji asiuguse utupu wa maiti kwa mkono mtupu ila kwa dharura

 

Aviringishe kitambaa kwenye mkono wake amfute nacho ili asipate kuugusa uchi wake, kwa kuwa kuangalia utupu wake ni haramu, na kuugusa ni haramu zaidi. [Al-Ummu (1/249) na Al-Mughniy (2/457)].

 

· Je, Kucha Za Maiti Hukatwa Na Nywele Za Kinena Hunyolewa?

 

[Al-Ghuslu wal Kafan (uk 97), Al-Ummu (1/248) na Al-Majmu’u (5/178)].

 

Maulamaa wana kauli mbili kuhusu hili:

 

Ya kwanza:

 

Linafanywa lile lililokuwa ni fitwrah katika maisha yake. Na kwa kuwa hilo ni usafi, basi ni haki yake ili kuondosha uchafu. Ash-Shaafi’iy kalisema hili katika madhehebu mapya.

 

Hili linaweza kutolewa dalili kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusu kisa cha kuuawa Khubayb (Radhwiya Allaahu Anhu). Anasema: “ Khubayb akashikiliwa kwao mateka mpaka walipokata shauri la kumuua. Akaazima wembe wa kujinyolea kinena kutoka kwa binti mmoja wa Al-Haarith, naye akampa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3989), Ahmad (2/294), Abu Daawuud (2660) na wengineo].

 

Ni kana kwamba alijinyoa kinena kwa ajili ya kujiandaa na kifo, kwa kuwa yuko mikononi mwa washirikina ambao hawatamfanyia hilo baada ya kufa.

 

Imepokelewa toka kwa Abu Qulaabah: “Kwamba Sa’ad alimwosha maiti, akaitisha wembe akamnyoa”. [Wapokezi wake wanaaminika: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/247). Wapokezi wake ni watu madhubuti, na hakuna kinachochelewa isipokuwa Irsaal ya Abu Qulaabah].

 

Hadiyth kama hii imepokelewa toka kwa Bakr bin ‘Abdallah Al-Mazniy.

 

Ya pili:

 

Ni makruhu, kwa kuwa ni kukata sehemu ya mwili wake, ni kama kutahiri. Kayasema haya Al-Mazniy katika wafuasi wa Ash-Shaafi’iy. Na imepokelewa toka kwa Ibn Syriyn: “Kwamba ilikuwa inampendeza mgonjwa anapozidiwa sana, anyolewe sharubu zake, kucha zake na kinena chake. Na kama atafariki, asinyolewe chochote”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/246)].

 

Ninasema: “Linaloonekana imara ni kuwa ikiwa itaonekana kwa maiti nywele iliyokaa vibaya ambayo imesuniwa kuinyoa, basi hakuna ubaya kuinyoa. Cha kuangaliwa katika hili, ni lenye kumfaa maiti. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

· Faida: Zitafanywa Nini Nywele Alizonyolewa Maiti, Au Kucha Alizokatwa, Au Kilichotoka Katika Hivyo?

 

Maulamaa wengi wamesema kuwa vitawekwa pamoja na maiti na kuzikwa naye. Kuna jumla ya athar zinazozungumzia hili toka kwa Masalaf zilizopo kwa Ibn Abiy Shaybah (3/247). Unaweza kuzipitia.

 

· Mwanamke Akifariki Na Tumboni Kuna Kitoto Hai

 

Mwanamke akifariki na ujauzito, kama kuna matumaini ya kuwa kitoto ni hai, basi tumbo litafanyiwa upasuaji ili kitolewe. Na kama hakuna matumaini ya uhai, basi kitaachwa humo humo. Ni kauli ya Hanafiy, Ash-Shaafi’iy, Hanbali na baadhi ya wafuasi wa Maalik. [Al-Fataawaa Al-Hin-diyyah (1/157), Ghaayatul Muntahaa (1/254) na Bulghat As-Saalik (1/232)].

 

· Mwanamke Akifa Na Hedhi Au Janaba, Ataoshwa Josho Moja Tu

 

Kwa kuwa akifa, anakuwa hayuko tena ndani ya hukmu za makalifisho, na hana tena ‘ibaadah ya wajibu. Bali kumwosha maiti ni ‘ibaadah ya twa’a, na ili atoke hapa duniani akiwa msafi kabisa na maridadi. Na haya yote hupatikana kwa josho moja tu, na josho hili hutosheleza mawajibiko mawili aliyonayo maiti kama hedhi na janaba. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (2/463) kwa mabadilisho kidogo].

 

· Aliyeosha Maiti, Je Ataoga?

 

Imesimuliwa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliyeosha maiti aoge, na aliyembeba atawadhe)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3161), Ahmad (2/433), Al-Bayhaqiy (1/303) na wengineo. Sanad zake zote zina kasoro. Angalia Al-Ghuslu wal Kafan (uk. 110 na zinazofuatia). Lakini pamoja na hayo, Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Kila mmoja na mtazamo wake].

 

Hadiyth hii ni Mudhtwarib. Maulamaa wa Hadiyth; Ibn Al-Madiyniy, Ahmad bin Hanbali, Muhammad bin Yahya, Ash-Shaafi’iy, Ibn Al-Mundhir, Al-Bayhaqiy na wengineo, wamesema ni Dhwa’iyf.

 

Na imesimuliwa toka kwa ‘Aaishah: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akioga kwa mambo manne: Janaba, Siku ya Ijumaa, kuumikwa na kuosha maiti”. [Hii pia Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3160), naye kasema Dhwa’iyf.  Al-Bukhaariy kasema hivyo hivyo kama ilivyo kwa Al-Bayhaqiy (1/302)].

 

Na katika Hadiyth ya Naajiyah bin Ka’ab (kuhusu kisa cha kufa Abu Twaalib), na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia ‘Aliy: ((Nenda ukamzike baba yako, na usifanye kitu mpaka unijie)). Akasema: “ Nikaenda, nikamzika, kisha nikamjia. Akaniamuru, nikaoga na akaniombea”. [Kuna ulaini katika Sanad yake. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3214), An-Nasaaiy (4/79) na Ahmad. Sanad yake ni Layyin. Je yaweza kuwa Hasan kwa mjumuiko wa Sanad nyinginezo? Hili ni la kutafitiwa. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].

 

Kuna mvutano kuhusu kuizingatia Hadiyth Hasan kwa msingi kwamba haikuelezwa kuwa ‘Aliy alimwosha.

 

Na kwa haya yaliyotangulia, inabainika kwamba hakuna Hadiyth yoyote toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayothibitisha wajibu wa kuoga baada ya kumwosha maiti, bali iko Hadiyth ya kinyume chake iliyopokelewa na Ibn ‘Abbaas anayesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Si lazima kwenu kuoga kwa kumwosha maiti wenu mtakapomwosha, kwa kuwa maiti wenu si najisi. Inawatosheni kuosha mikono yenu)). [Imetiwa kasoro kwa wakf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/386) na Al-Bayhaqiy (1/306) ambaye kasema kuwa ni Dhwa’iyf. La sawa ni kuakifiwa kwa Ibn ‘Abbaas].

 

Hadiyth hii pia imetiwa kasoro, na sahihi ni kuakifiwa kwa Ibn ‘Abbaas.

 

Alaa kulli haal, Jamhuri ya Maulamaa katika Maswahaba na waliowafuatia, hawaoni wajibu wa kuoga kwa kumwosha maiti, bali wanaliona hilo kama ni jambo la Sunnah. [Al-Ummu (1/235), Al-Majmu’u (5/185) na Ma’alim As Sunan (3/512)].

 

Hili limethibiti toka kwa Ibn ‘Abbaas, Ibn Mas-’oud, Sa’ad bin Abiy Waqqaas, Ibn ‘Umar na ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anhum) kwa Sanad Swahiyh. [Angalia Al-Ghuslu wal Kafan (uk. 120-125)].

 

Baadhi ya wanachuoni kama Abu Daawuud wamesema kwamba hii ni mansukh baada ya kuileta Hadiyth ya Abu Hurayrah.

 

· Maji Yakikosekana, Au Yakawa Vigumu Kutumika, Je Maiti Atatayamamishwa

 

Kama itashindikana kumwosha maiti kwa kukosekana maji, au ikahofiwa kwamba akioshwa atanyumbuka kutokana na kuungua moto na mfano wake, basi atatayamamishwa. Tayamumi hii ni wajibu kwa kuwa ni utwaharisho usiohusiana na kuondosha najisi. Hivyo ni lazima kuuguria kama maji hakuna kama inavyokuwa katika josho la janaba. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ardhi imefanywa kwangu Masjid na kitwaharishio tukikosa maji)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa kwenye mlango wa tayammum].

 

· Maiti Akizikwa Bila Kuoshwa

 

Jamhuri wamesema ni lazima afukuliwe ili aoshwe kama bado hajaharibika.

 

Abu Haniyfah kasema kwamba si lazima afukuliwe baada ya kufukiwa!! [Al-Majmu’u (5/300) na Al-Muhalla].

 

Ninasema:Hadiyth ya Jaabir inataarifu kwamba inajuzu kumtoa maiti kaburini kwa sababu ya kisharia. Anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliliendea kaburi la ‘Abdullah bin Ubayya baada ya kuingizwa shimoni. Akaamuru atolewe, akamweka kwenye magoti yake mawili, akampulizia cheche za mate kwa ulimi wake, na akamvisha nguo yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1350) na Muslim (2773)].

 

 

 

Share