012-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Yananayomnufaisha Maiti Baada Ya Kufa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

012-Yananayomnufaisha Maiti Baada Ya Kufa

 

Alhidaaya.com

 

1- Kuombewa du’aa na Waislamu

 

Allaah Mtukufu Anasema:

((وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ))

((Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu)). [Al-Hashr (59:10)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: (( Du’aa ya mtu Muislamu kwa nduguye kwa siri, inajibiwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2733) na wengineo].

 

2- Kulipiwa deni lake na mtu yeyote

 

Ni kwa Hadiyth iliyoelezewa nyuma ya Abu Qataadah kumlipia deni mtu aliyekufa. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa mwanzoni mwa mlango huu].

 

3- Walii wake kumlipia Swawm

 

Ni kwa Hadiyth ya 'Aaishah (Radhwiya Allaahu Anhaa) ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Aliyekufa na anadaiwa Swawm, basi walii wake atamfungia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147)].

 

Na hii inajumuisha deni la Ramadhwaan na deni la Swawm ya nadhiri. Hii ndiyo kauli sahihi zaidi ya Maulamaa kama itakavyokuja kuelezwa kwenye mlango wa Swawm Apendapo Mola.

 

4- Kumlipia nadhiri ikiwa ni Swawm au jingine lolote

 

Sa'ad bin 'Ubaadah alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Mama yangu amefariki na nadhiri yake hajaitekeleza". Rasuli akamwambia: ((Mlipie wewe)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2761) na Muslim (1638)].

 

5- Matendo mema anayoyafanya mtoto mwema

 

Allaah Anasema:

((وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ))

((Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi)). [An-Najm (:39)]

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika chema zaidi akilacho mtu, ni kile alichokichuma mwenyewe, na hakika mtoto wake ni chumo lake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3511), At-Tirmidhiy (1369) An-Nasaaiy (7/241) na Ibn Maajah (2137)].

 

6- Anayoyaacha maiti kati ya mabaki mema na swadaqah endelevu

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwanadamu anapokufa, amali zake hukatika isipokuwa matatu:  Swadaqah endelevu, au elimu yenye manufaa, au mtoto mwema anayemwombea)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1631), Abu Daawuud (2863), At-Tirmidhiy (1390), na  An-Nasaaiy (6/251)]

 

· Nini Hukmu Ya Kumtunuku Maiti Thawabu Za Kisomo Cha Qur-aan?

 

Allaah Amesema:

((وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ))

((Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi)). [An-Najm (:39)]

 

Asili ni kuwa maiti hanufaiki na chochote kutokana na matendo ya walio hai isipokuwa kwa lile ambalo limehusishwa na dalili kutoka kwenye ujumuishi wa yaliyotajwa nyuma. Ama yasiyo hayo, hayo hubakia kwenye ujumuishi kama inavyoelezwa kwenye uswuul.

 

Na kwa sababu hii, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuuhimiza Umma kutoa thawabu za kisomo kwa wafu, na wala hakuwaelekeza kufanya hivyo, bali hili halikunukuliwa toka kwa Swahaba yeyote –kwa mujibu wa tujuavyo- lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelekeza kumwombea maiti maghfirah akisema: ((Mtakieni maghfirah ndugu yenu, na mwombeeni uthibiti, kwani yeye hivi sasa anaulizwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3221) na wengineo].

 

Kwa Hadiyth hii, tunapata kujua kwamba kisomo hakimnufaishi maiti. Lakini huu ni msimamo wa Ash-Shaafi'iy kinyume na Jamhuri.

 

 

 

Share