013-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Kuyazuru Makaburi Na Yanayohusika

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

013-Kuyazuru Makaburi Na Yanayohusika

 

Alhidaaya.com

 

 

Kuyazuru makaburi kunaruhusika kwa ajili ya kuwaidhika nayo na kuikumbuka aakhirah. Na hii ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): (( Nilikuwa nimewakatazeni kuyazuru makaburi, basi yazuruni [yatawakumbusheni aakhirah])). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake yaja].

 

· Je, Wanawake Wanaruhusiwa Kuyazuru Makaburi?

 

Maulamaa wana kauli tatu kuhusu hili: Ya kwanza ni haramu, ya pili ni makruhu, na ya tatu ni mubaha bila karaha. Ni riwaya toka kwa Ahmad, na kauli ya Maalik na baadhi ya Mahanafi. [Tahdhiyb As-Sunan cha Ibn Al-Qayyim (9/58 –‘awn al ma’abuwd) kwa mabadilisho kidogo].

 

Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi kwa sharti ziara iwe kwa ajili ya kukumbuka mauti na aakhirah pamoja na kujiepusha maharamisho. Na hii ni kwa dalili zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya Anas –iliyotangulia- isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpitia mwanamke mmoja anayelia mbele ya kaburi akamwambia: ((Mche Allaah na fanya subira)).  [Hadiyth Swahiyh: Al-Bukhaariy (1283) na Muslim (926)]

 

Na hapa Rasuli hakumkataza kuzuru makaburi.

 

2- Bibi ‘Aaishah alilizuru kaburi la kaka yake. Imepokelewa toka kwa Ibn Abiy Mulaykah: “Kwamba ‘Aaishah alikuja siku moja akitokea makaburini. Nikamuuliza: Ee Mama wa Waumini! Umetokea wapi? Akasema: Natoka kwenye kaburi la kaka yangu ‘Abdul Rahmaan bin Abi Bakri. Nikamwambia: Si Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekataza kuyazuru makaburi? Akasema: Ndio, alikuwa amekataza, kisha akaamuru kuyazuru”. [Hadiyth Swahiyh: Al-Haakim (1/376), Al-Bayhaqiy (4/78), na asili yake ni kwa Ibn Maajah (1569) kwa ufupi, nayo ni Swahiyh].

 

3- Bibi ‘Aaishah alimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Nitasema vipi ee Rasuli wa Allaah? [yaani akienda makaburini]. Akasema: ((Sema: As Salaam ‘alaa ahlid diyaar minal Mu-uminiyna wal Muslimiyna, wayarhamul Laahu al mustaqdimiyna minnaa wal musta-akhiriyna, wainnaa in shaa Allaah bikum lalaahiquwna)). [Hadiyth Swahiyh: Muslim (974), Ahmad (6/221), ‘Abdul Razzaaq (6712) na Al-Bayhaqiy (4/79)].

 

4- Ujumuishi wa neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Nilikuwa nimewakatazeni kuyazuru makaburi, basi yazuruni)). [Hadiyth Swahiyh: Muslim (977), Abu Daawuud (3235) kwa ufupi, An-Nasaaiy (4/89) na At-Tirmidhiy (1054)].

 

· Zindushi

 

[Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/581) kwa mabadilisho kidogo. Pia kwenye kitabu changu cha Fiqhu Sunnat An Nisaaa (uk 204) nikiwa nimenukuu toka kitabu hicho].

 

1- Kukipatikana uhakika kwamba wanawake wakienda makaburini watalia kwa sauti, wataomboleza, watawalalamikia maiti, na watafanya bid-’a na maharamisho, hapo itakuwa ni haramu kwao kuzuru makaburi.

 

2- Kukipatikana uhakika kwamba wao wanayaendea makaburi ya wanaioitwa watu wema au mawalii ili kuwaomba wawaondoshee matatizo, wawakidhie haja zao na wawaondoshee ghamu, basi hii ni shirki, na hapo bila shaka watazuiliwa wasende.

 

3- Ikiwa wanawake wataiweka siku mahsusi kwa ajili ya kuyazuru makaburi kama inavyotokea siku za ijumaa, ‘Iyd na kadhalika, basi hii ni bid-’a.

 

4-Haijuzu wanawake kutoka kwenda makaburini na kwingineko wakiwa wamevalia mavazi yasiyo sitara, wamejipamba na kujitia manukato.

 

· Miongoni Mwa Adhkaar Zilizothibiti Wakati Wa Kuyazuru Makaburi

 

1- ((As Salaam ‘Alaykum daara qawmin Mu-uminiyna, wainnaa waiyyaakum wamaa tuw-’aduwna ghadan muajjaluwna, wainnaa in Shaa Allaahu bikum laahiquwna. Allaahumma Ghfir liahli (atataja makaburi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (974), An Nasaaiy (1/287) na wengineo].

 

2- ((As Salaam ‘Alaykum Ahlad diyaar minal Mu-uminiyna wal Muslimiyna, wainnaa in Shaa Allaahu [bikum] lalaahiquwna. As-alul Laaha lanaa walakumul ‘aafiyah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (975), An Nasaaiy (2040) na Ibn Maajah (1547)].

 

3- ((As Salaam ‘Alaa Ahlid diyaar minal Muuminiyna wal Muslimiyna, wa Yarhamul Laahu al mustaqdimiyna minnaa wal mustaakhiriyna, wainnaa in shaa Allaahu bikum lalaahiquwna)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (974) na Ahmad (6/221)].

 

 

Share