Maandazi Ya Ufuta Ya Kuoka (Baked Sesame Maandazi)

Maandazi Ya Ufuta Ya Kuoka (Baked Sesame Maandazi)

 

 

Vipimo

 

Unga - 3 Magi

Sukari - 1 Kikombe

Mayai - 2

Hamira - 2 Vijiko vya chakula

Hiliki - 1 Kijiko cha chai

Nazi - 1 Ya kopo

Samli - 2 Vijiko vya chakula (jaza)

Ufuta- 3 Vijiko vya chakula  
 

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika 

 

  1. Unatia hamira kwenye kibakuli na maji kama robo kikombe hivi ikisha unaichanganya mpaka ichanganyike na unaiweka pembeni.  
  2. Unautia unga kwenye bakuli au sinia ikisha  unatia na sukari na hiliki, unapasha moto samli na unaitia ikisha unauchanganya unga na samli mpaka uchanganyike uzuri.  
  3. Unapiga mayai kwenye bakuli unayatia, unauchanganya tena halafu unatia na ile hamira ulokwisha ivuruga, huku unaendelea kuuchanganya.  
  4. Hapo sasa ndio unachukuwa ile nazi ya kopo unaitia kidogo kidogo huku unaukanda mpaka ulainike. Unga wa maandazi haya unakuwa mlaini zaidi kuliko maandazi ya mafuta.  Kama nazi haitatosha unaweza kuongeza maziwa au hata maji kidogo mpaka ulainike vizuri unga.   
  5. Ukishamaliza kuukanda utie kwenye bakuli na uwache kwa dakika 10, halafu uchanganye tena bila kuutia kitu chochote.  
  6. Halafu chukuwa treya ipakae mafuta au samli, kisha chukuwa unga usokote kama unavouona hapo juu, au kama unataka kuufanya staili nyingine pia unaweza, unausokota mpaka unamaliza unga wote.
  7. Ukimaliza nyunyiza ufuta juu ya maandazi ulokwisha yasokota, halafu tia treya ya maandazi ndani ya jiko (oven) lakini usiwashe moto, subiri mpaka maandazi yaumuke vizuri.  
  8. Maandazi yakisha kuumuka vizuri sana, washa moto (bake) kwenye jiko na uweke namba 350 kwa muda wa dakika 15, na baada ya hapo punguza moto weka 300 mpaka ukishakuyaona yamewiva.  
  9. Yakiwiva yatoe kwenye jiko na uyapake mafuta juu kidogo ili yalainike   na uyawache yapoe, na yakishapoa yatakuwa tayari kuliwa.

 

 

 

Share