02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Hukmu Ya Kuchinja Udhwhiyah

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

02-Udhwhiyah: Hukmu Ya Kuchinja Udhwhiyah:

 

 ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya udhwhiya kwa kauli mbili:

[Al-Mabsuwtw (12/8)].

 

Ya kwanza:  Ni waajib kwa mwenye uwezo

 

Ni kauli ya Rabiy-‘ah, Al-Awzaa’iy, Abuu Haniyfah, Al-Layth na baadhi ya Wamaalik.  Dalili walizotoa ni:

 

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

 

Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja.  [Al-Kawthar : 02].

 

Wamejibiwa:  Kwamba ‘Ulamaa wana kauli tano katika kuiawilisha Aayah hii, na kauli yenye nguvu zaidi ni ile isemayo kuwa muradi ni:  Swali kwa ajili ya Allaah, na chinja kwa ajili ya Allaah.

 

 

2-  Hadiyth ya Jundub bin Sufyaan (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:   

 

 "مَنْ ذَبَحَ قَبْلَ أَنْ يُصَلِّيَ فَلْيَذْبَحْ أُخْرَى مَكَانَهَا، وَمَنْ لَمْ يَذْبَحْ فَلْيَذْبَحْ"

 

“Atakayechinja kabla hajaswali, basi achinje mnyama mwingine badala yake, na ambaye hakuchinja, basi na achinje”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5562) na Muslim (1960)].

 

Wamejibiwa:  Kwamba makusudio ni kubainisha sharti la kukubalika udhwhiyah kisharia.  Hii ni kama kwa mfano kumwambia aliyeswali Swalaah ya Dhuhaa kabla ya jua kuchomoza:  Jua likichomoza, swali tena Swalaah yako.

 

 

3-  Hadiyth ya Al-Baraa kwamba Abu Burdah alisema:

 

"يَا رَسُوْلَ اللهِ ، ذَبَحْتُ قَبْلَ أَنْ أُصَلِّيَ ، وَعِنْدِيْ جَذَعَةٌ خَيْرٌ مِنْ مُسِنَّةٍ ، فَقَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : اجْعَلْهَا مَكَانَهَا ، وَلَنْ تُجْزِئَ عَنْ أَحَدٍ بَعْدَكَ"

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Nimechinja kabla sijaswali.  Nami nina jadh-‘a ambaye kwangu ni mbora zaidi kuliko musinnah.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Mfidie huyo huyo mahala pa uliyemchinja, na hatofaa kwa yeyote baada yako”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5560)].

 

 

4-  Hadiyth ya Al-Baraa bin ‘Aazib kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أَرْبَعَةٌ لا يُجْزِيْنَ فِي الأَضَاحِي : العَوْرَاءُ البَيِّنُ عَوْرَهَا و........."

 

“Wanne hawatoshelezi katika wanyama wa kudhwahi:  Mwenye chongo la wazi linaloonekana……..”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2802), At-Tirmidhiy (1497), An-Nasaaiy (7/215), Ibn Maajah (3144) na wengineo].

 

Wamesema (kutilia nguvu hoja yao):  Neno lake “hawatoshelezi”, ni dalili juu ya uwajibu wa kudhwahi!  Kwa kuwa neno “haitoshelezi” halisemwi kwa linalohusiana na sunnah. Wakasema pia kuwa kutokuwa mnyama na kasoro yoyote kunazingatiwa kwa wanyama walio wajibu kuchinjwa, ama wale wa sunnah, hao inajuzu kujikurubisha kwa Allaah kwa aliye chongo au mwenye kasoro nyingineyo yoyote mwilini.

 

Wamejibiwa:  Kwamba wanyama wa kudhwahi ni dhabihu ya kafara ya Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo yeye anajikurubisha kwayo kwa Allaah ‘Azza wa Jalla kwa mujibu wa alivyoletewa sharia kuhusiana na hilo.  Nayo pia ni hukmu ambayo imewekewa wakati maalum, hivyo haifai mtu apetuke kwayo Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuwa ni mustahili ajikurubishe nayo kwa jambo ambalo limekatazwa kwa ulimi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  [At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barri (20/167].

 

 

5-  Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ كَانَ لَهُ سَعَةً وَلَمْ يُضَحِّ فَلَا يَقْرُبَنَّ مَسْجِدَنَا وَمُصَلَّانَا"

 

“Atakayekuwa na uwezo na asidhwahi, basi asiukaribie kabisa Msikiti wetu na sehemu yetu ya kuswalia”.  [Hadiyth Dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Ibn Maajah (3123), Ahmad (2/321), Al-Haakim (2/389), Ad-Daaraqutwniy (4/285), na Al-Bayhaqiy (9/260)]. 

 

Ya pili:  Kudhwahi ni sunnah na si waajib

 

Haya ni madhehebu ya Jumhuwr; Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr, Al-Mazniy, Ibn Al-Mundhir, Daawuwd, Ibn Hazm na wengineo.  Wametoa dalili hizi zifuatazo:

 

 

1-  Hadiyth ya Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا دَخَلَتِ الْعَشْرُ وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ فَلاَ يَمَسَّ مِنْ شَعَرِهِ وَبَشَرِهِ شَيْئًا ‏"

 

“Linapoingia kumi (la mwanzo la mwezi wa Dhul-Hijja) na mmoja wenu akaazimia kudhwahi, basi asikate chochote katika nywele zake na kucha zake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1977), An-Nasaaiy (7/212), Ibn Maajah (3149), na Ahmad (6/289).  Wamekhitalifiana katika kuwa kwake Marfuw’u au Mawquwf.  Linaloonekana kuwa na nguvu zaidi ni Marfuw’u].

 

Wamesema:  Neno lake “akaazimia kudhwahi” ni dalili kuwa kudhwahi si waajib.

 

 

2-  Imekuja kwa njia sahihi kutoka kwa Maswahaba kwamba kudhwahi si waajib, na wala haikupokelewa kutoka kwa yeyote kati yao kwamba ni waajib.  Al-Mawruwdiy amesema:  “Imepokelewa toka kwa Maswahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum) linalofungika kwalo Ijma’a ya kupomoka uwajibu”.  [Al-Haawiy (19/85) na Al-Muhallaa (7/358)].

 

Kati ya hayo ni:

 

(a)  Abu Sariyhah amesema:

 

"رَأَيْتُ أَبَا بَكْرِ وَعُمَرَ ، وَمَا يُضَحِّيَانِ"

 

 “Nimewaona Abu Bakr na ‘Umar hawadhwahi”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (8139) na Al-Bayhaqiy (9/269)]. 

 

(b)  Abu Mas-‘uwd Al-Answaariy (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:

 

"إِنِّي لأَدَعُ الأَضْحَى ، وَإِنِّيْ لَمُوْسِرٌ ، مَخَافَةَ أَنْ يَرَى جِيْرَانِي أَنَّهُ حُتِمَ عَلَيَّ"

 

“Mimi huacha kudhwahi, nami nina uwezo, kwa sababu ninachelea majirani zangu kudhani kwamba ni lazima kwangu”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (8149) na Al-Bayhaqiy (9/265)].

 

Ninasema:  “Linaloonekana ni kwamba dalili za wenye kuwajibisha hazina nguvu wala vigezo vya kuwajibisha.  Na kwa muktadha huu, kauli inayozingatiwa ni ya Maswahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum) na Jumhuwr ya ‘Ulamaa”. 

                                                                     

 

 

 

Share