12-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Masharti Ya Uharamu (Umahram) Kwa Sababu Ya Kunyonya: Idadi Ya Manyonyesho Ya Kuleta Uharamu (Umahram): Kauli Ya Tatu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

12-Masharti Ya Uharamu (Umahram) Kwa Sababu Ya Kunyonya: Idadi Ya Manyonyesho Ya Kuleta Uharamu (Umahram):  Kauli Ya Tatu:

 

Manyonyesho matano na zaidi ndiyo yanayoharamisha.  Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm.  Ni kauli pia ya ‘Atwaa na Twaawuws.  Imepokewa vile vile toka kwa ‘Aaishah, Ibn Mas-‘uwd na Ibn Az-Zubayr.  Dalili ni:

 

1-  Hadiyth ya ‘Aaishah:

 

" كانَ فِيمَا أُنْزِلَ مِنَ الْقُرْآنِ: عَشْرُ رَضَعَاتٍ مَعْلُومَاتٍ يُحَرِّمْنَ. ثُمَّ نُسِخْنَ بِخَمْسٍ مَعْلُومَاتٍ"

 

“Ilikuwa katika yaliyoteremshwa katika Qur-aan ni:  “Manyonyesho kumi yaliyothibitika yanaharamisha”.  Kisha yakafutwa kwa matano yaliyothibitika.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafariki nayo yakabaki yakisomwa kwenye Qur-aan”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1452) na Abu Daawuwd (2062)]

 

An-Nawawiy kasema:  “Maana yake ni kwamba kufutwa manyonyesho matano kulikuja mwisho mwisho kabla ya kufariki Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi.  Na kwa vile habari ya kufutwa ilikuwa haijawafikia watu wengi, waliendelea kusoma "خَمْسُ رَضَعَاتٍ"  kama ni sehemu ya Qur-aan, lakini ilipowafikia baada ya hapo habari ya kufutwa, waliachana na kisomo hicho na wakakubaliana kwa pamoja kwamba hilo halisomwi”. 

 

Ninasema:  “Hii ni Qur-aan iliyofutwa kisomo lakini hukmu yake ikabakia kama Aayah ya kupigwa mawe mzinifu”. 

 

2-  Hadiyth ya ‘Aaishah kuhusiana na kisa cha Sahlah bint Suhayl, kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: 

 .

"أَرْضِعِي سَالِمًا خَمْسَ رَضَعَاتٍ فَيَحْرُمُ بِلَبَنِهَا"

 

“Mnyonyeshe Saalim manyonyesho matano, atakuwa mahram kwa kunyonya”.

[Abdulrazzaaq ameikhariji kwa tamko hili (13886), Maalik (1284) na Ahmad (6/201).  Asaaniyd zake hazikuungana, na asili yake iko kwa Muslim (1453)]

 

Kwa kifupi kuhusiana na Hadiyth hii ni kwamba Abu Hudhayfah bin ‘Utbah na mkewe Sahlah bint Suhayl, walimlea Saalim huyu akiwa mtoto wa kupanga kama ilivyokuwa enzi ya ujahilia na akawa kama mtoto wao wa kuzaa. Saalim akakua na kubaleghe, na hapo ikashuka Aayah ya tano ya Suwrat Al-Ahzaab iliyobatilisha uhalali wa kuwafanya watoto wa kupanga kama watoto wa kuzaa.  Hapo bi Sahlah akakimbilia kwa Rasuli kutaka kujua mambo yatakuwaje kwa kuwa Saalim ameshakuwa kama ni mtoto wao wa kuzaa, anaishi nao pamoja, anakula nao, anaingia vyumbani vyao bila ukakasi wowote na kadhalika.  Sasa mambo yatakuwaje?  Ndipo Rasuli akamwambia amnyonyeshe manyonyesho matano na ukubwa wake huo, na hapo atakuwa mahram yake.  Hii ilikuwa ni kesi maalum inayomhusu Saalim tu pasi na mwingine yeyote.

 

3-  ‘Aaishah amesema:

 

 "لاَ يُحَرِّمُ دُونَ خَمْسِ رَضَعَاتٍ مَعْلُومَاتٍ "

 

“Manyonyesho chini ya matano yaliyothibitika, hayamfanyi mtoto mwenye kunyonya kuwa mahram”.  [Isnaad yake ni swahiyh]

 

Share