Nasaha Kwa Kila Shia
Nasaha Kwa Kila Shia
Imetarjumiwa na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa'ay (Rahimahu Allaah)
Hii Ni Zawadi Kwa Kila Shia Mwenye Hisia Huru – Mwenye Kufikiri – Mpenda Haki Na Kheri - Anayetaka Kujuwa Na Kufahamu – Kwa Wote Hawa Nawapa Zawadi Hii Fupi Na Simuombi Zaidi Ya Kuwa Ayasome Makala Haya Nikiwa Na Imani Kuwa Nitakuwa Nimempa Nasaha Njema - Wassalaam –
Utangulizi
Bismillah Wal HamduliLLah wasw-Swalaatu wa Ssalaamu ‘Alaa Rasuli Allaahi Nabiyyina Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Swahabihi wa sallam.
Wabaad – Kusema kweli mimi sikuwa nikijuwa chochote kuhusu Madhehebu ya ki-Shia zaidi ya kuwa wao ni watu wanaowapenda Ahli l Bayt, na kwamba wao ni Waislamu wanaovuka mipaka katika kuwapenda watu wa nyumba ya Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Ahli-l-Bayt’, wanawanusuru, na kwamba hitilafu baina yao na Masunni ‘Ahli Sunnah’ ni ndogo sana, nayo ni katika mambo yanayohusu sharia na kwamba wao huzifasiri vibaya tu baadhi ya aya na baadhi ya Hadiyth za Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Kwa ajili hiyo, nilikuwa nikighadhibika sana pale ninapowaona baadhi ya Masunni wakiwataja Mashia kuwa ni Mafasiq, au pale ninapowasikia wakiwatoa katika itikadi za Kiislam. Fikra zangu hizi hazikudumu muda mrefu. Mmoja katika ndugu zangu aliponishauri nisome kitabu cha jamaa hawa (Mashia) ili niweze kutoka hukmu yangu kwa ukamilifu na usahihi juu ya Itikadi ya ki-Shia. Akanishauri nikisome kitabu kiitwacho Al Kaafi, na hiki ni kitabu kitukufu sana kwao chenye kuyathibitisha madhehebu yao.
Nikakisoma na kupata ndani yake ukweli wa kitaalamu ulionifanya niwape udhuru wote waliokuwa wakinikosowa kwa kuwaunga mkono kwangu wenye kufuata Madhehebu ya ki-Shia. Kwani nilikuwa nikitegemea kuwa huenda nikaweza kuziondoa baadhi ya chuki zilizopo baina ya Ahlus-Sunah na kundi hili linalojinasibisha na Uislam kwa haki au kwa batil.
Na leo nakuleteeni uhakika nilioupata kutoka katika kitabu chao muhimu sana wanachokitegemea katika kuyathibitisha Madhehebu yao nikimuomba kila mwenye kufuata Madhehebu ya Ki-Shia asome na atafakari juu ya ukweli huu kwa ikhlas na uadililifu, kisha atoe uamuzi wake juu ya Madhehebu yake na juu ya kujinasibisha kwake nayo. Ajiamulie mwenyewe. Iwapo atatowa hukumu kuwa Madhehebu yake haya ni sawa na kwamba kujinasibisha kwake na Madhehebu haya ni haki na kwamba ni bora, basi na aendelee nayo, ama iwapo atatambua ubatilifu wa Madhehebu yake basi itampasa kila Mwenye kufuata Madhehebu haya ya Ki-Shia ainasihi nafsi yake na kumuomba Mola wake amsaidie katika kuyaacha, na yamtosheleze yale yanayowatosheleza mamilioni ya Waislam ulimwenguni kote, nayo ni Kitabu cha Allaah (Qur-aan) na Mafundisho sahihi ya Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Kisha mimi najikinga kwa Allaah kutokana na kila Muislam utakayembainikia ukweli, kisha akauacha na kuifuata batili kwa jeuri tu, au kwa kuiga au kwa ajili ya ukabila au utaifa kwa kutaka manufaa ya kidunia, huku akiighushi nafsi yake na kuipeleka katika njia ya unafiki na kujihadaa, akiwa ni mtihani kwa wanawe na ndugu zake na vizazi vitakavokuja baadaye, wote hao atakuwa amewaondoa katika njia ya haki kwa ajili ya kufuata batili yake na kuwabaidisha mbali na Mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwatia katika Uzushi na kutoka katika Uislam sahihi na kuwaingiza katika Madhehebu maovu.
Ee Mwenye kufuata Madhehebu ya Ki-Shia, upokee ukweli huu wa kitaalamu juu ya asili ya Madhehebu yako yaliyowekwa na mikono miovu kabla yako na nafsi zilizojaa shari ili uwe mbali kabisa na Uislam wa kweli na Haki.
Pokea ee Mfuasi wa Madhehebu ya Shia mafungu saba ya ukweli yaliyohifadhiwa ndani ya kitabu cha Al-Kaafi, kitabu kinachotegemewa katika kuyathibitisha Madhehebu yako na ambacho ni chimbuko la Ushia wako. Kitazame vizuri, tafakari vizuri na umuombe Mola wako Mtukufu akuonyeshe ukweli na akusaidie katika kuufuata na akuwezeshe kuubeba, kwani hapana Mola isipokuwa Yeye na hakuna Muweza isipokuwa Yeye.
Uhakika Wa Mwanzo
Ahlul-Bayti Hawaihitajii Qur-Aan Kwa Sababu Wana Vitabu Vya Allaah Vilivyotangulia Kuteremshwa, Navyo Ni Tarati Na Injili.
Ukweli huu unathibitishwa na yale yaliyoandikwa katika kitabu cha Al Kaafi Juzuu ya kwanza Kitabul Hojjah ukurasa wa 207, nayo ni haya yafuatayo;
((Mlango wa Maimam Alayhimu Salaam wanavyo vitabu vyote vilivyoteremshwa kutoka kwa Allaah na kwamba wao wanavijua vyote, juu ya kuhitilafiana kwa lugha zake)).
Ushahidi aloutegemea mwenye kitabu cha Al Kaafi ni hadithi mbili zilizosimuliwa na Abi Abdullahi kwamba yeye alikuwa akivisoma vitabu vya Taurati na Injili na Zaburi kwa lugha ya kisiri.
Na maana ya maneno haya yaliyomo ndani ya kitabu chao hicho ni maarufu, nayo ni kuwa Maimam wao na wafuasi wao hawana lazima ya kushikamana na Qur-aan Al-Kariym kutokana na wanayoyajua katika vitabu vilivyotangulia. Hii ni hatua kubwa inayowatenga Mashia mbali na Uislam na Waislam, kwa sababu bila shaka yoyote ile, yeyote anayeamini kuwa hana lazima ya kuifuata Qur-aan kwa njia yoyote ile anakuwa keshatoka katika dini ya Kiislam na keshateleza mbali na ndugu zake Waislam. Kwani Qur-aan ndiyo inayowaunganisha umma huu wa Kiislam katika itikadi zake na hukmu zake na adabu zake na kuwafanya wawe Umma mmoja.
Si katika kuiacha Qur-aan, pale mtu anapoiacha kuisoma na badala yake akavifuatilia na kuvidurusu vitabu vilivyotangulia vilviyobadilishwa na kupotoshwa?
Kutojilazimisha kushikamana na Qur-aan si Kufru hiyo na kuukimbia Uislam? Vipi inajuzu kuvisoma vitabu vile vilivyobadilishwa na kupotoshwa wakati Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona ''Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akiwa na karatasi zilizoandikwa maandishi ya Taurati, alimnyang’anya na kumwambia;
“Kwani sikukuleteeni (kitabu) cheupe kisafi?”
Ikiwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuridhika pale alipomuona''Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akizitazama karatasi tu za Taurati – Inaingia akilini kweli kuwa yeyote katika Ahlul-Bayti waliotahirika kuwa amevijumuisha vitabu vyote hivyo vya kale na kuvidurusu kwa lugha zake tofauti na kuiacha Qur-aan? Na kwa nini kwa ajili gani?
Allahumma wote huo ni uwongo mtupu waliowazulia watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kuupiga vita Uislam na Waislam.
Na mwisho, kila Shia inampasa kutambua kuwa kutokuwa na haja ya Qur-aan Al-Kariym, kitabu cha Allaah alichokihifadhi ndani ya vifua vya Waislam, kitabu kilichopo mikononi mwao (Waislam) ambacho halijapungua ndani yake hata neno moja wala kuzidishwa na wala haiwezekani hivyo abadan (kuzidishwa wala kupunguzwa), kwa sababu Allaah amekwishatoa ahadi ya kukihifadhi kitabu hiki pale aliposema:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al- Hijr: 9]
Na kwamba Qur-aan ipo vile vile kama ilivyoteremshwa na Jibril mwaminifu kwa Bwana wa Rusuli yote, ipo vile vile kama alivyoisoma Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakaisoma maelfu ya Swahaba wake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na wakaisoma waliokuja baada yao miongoni mwa mamilioni ya Waislam kwa wingi mpaka wakati wetu huu.
Mtu yeyote anapoitakidi kuwa hana lazima ya kuifuata yote au hata baadhi yake kwa njia yoyote ile anakuwa kesha rtaddi (keshatoka katika dini ya Kiislam). Mtu wa aina hiyo habaki kuwa na sehemu yoyote ya Usilamu au ya Waislamu
Uhakika Wa Pili
Kuitakidi Kuwa Hapana Sahaba Yeyote Aliyewahi Kuikusanya Au Kuihifadhi Qur-Aan Tukufu Isipokuwa Ali Na Maimam Wa Ahlul-Bayt (Radhwiya Allaahu 'Anhu) Peke Yao.
Itikadi hii imethibitishwa katika kitabu cha Al Kaafi Juzuu ya kwanza kitabu cha Al-Hojjah ukurasa wa 26, kikiwahakiki-Shia wenye kufuata Madhehebu ya ki-Shia kwa kutegemea ushahidi wanaosema kuwa ni kauli ya Jabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa amesema;
“Nimemsikia Aba Jaafar alayhi ssalaam akisema;
“Yeyote atakayejidai kuwa eti ameihifadhi Qur-aan yote, basi huyo ni mwongo, kwani hapana aliyeikusanya na kuihifadhi kama ilivyoteremshwa isipokuwa Ali bin Abi Talib na Maimam waliokuja baada yake".
Lazima utambue ewe unayefuata madhehebu ya Shia, namuomba Allaah aniongoze mimi na akuongoze wewe katika haki na katika njia yake iliyonyooka kuwa; Itikadi kama hii, nayo ni kuwa hapana mtu aliyewahi kuikusanya Qur-aan na kuihifadhi sipokuwa watu wa Ahlul-Bayti na wafuasi wao tu, ni ufisadi na shari kubwa sana, tunamuomba Allaah atuepushe nayo. Shari hii inamaanisha yafuatayo;
1- Kumkadhibisha kila aliyesema kuwa ameihifadhi Qur-aan, kama vile 'Uthmaan na Ubay bin Kaab na Zeid bin Thabit na Abdillahi bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) na wengineo katika Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambao idadi yao ni kwa mamia. Huko ni kuwakadhibisha wote hao na kuuondoa uadilifu wao. Maneno kama haya hayawezi kabisa kutamkwa na watu wa Ahlul-Bayt waliotahirika, bali yanasemwa na maadui wa Uislam na wanaopinga Uislam kwa ajili ya uhasama na kuufarikisha umma.
2- Itikadi hii inaleta maana kuwa Waislam wote wamepotoka isipokuwa Mashia wa Ahlul-Bayt tu peke yao, kwa sababu yeyote atakayeifanyia kazi Qur-aan nusu nusu bila ya ukamilifu atakuwa ametenda kitendo cha ukafiri na upotevu kwa sababu hatokuwa amemuabudu Rabb wake kwa ukamilifu, kwani huenda hiyo sehemu ya Qur-aan isiyowafikia Waislam, ikawa imebeba baadhi ya itikadi, ibada, mwenendo, na hukmu.
Itikadi hii pia inaikadhibisha kauli ya Allaah pale aliposema;
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijr:9]
Na kuikadhibisha kauli ya Allaah ni kufru, na kufru kubwa iliyoje?
3. Je! Inajuzu kwa Ahlul-Bayt kujihusisha peke yao na kitabu cha Allaah bila ya kuwahusisha Waislam wengine isipokuwa wale wanaowataka tu miongini mwa Mashia wao? Je! Huku si katika kutowashirikisha Waislam wenzao katika kufaidika na Rehma ya Allaah na kuiteka nyara?
Ee Mola wetu sisi tunaelewa kuwa watu wa nyumba ya Rasuli wako hawamo katika hatia hii ya uwongo huu na umlani kila anayesema uongo juu yao.
Itikadi hii inaleta maana kuwa Wenye kufuata Itikadi ya Ki-Shia peke yao ndio wenye kufuata haki, na wanaoisimamia, kwa sababu wao ndio wenye kitabu cha Allaah kilichokamilika bila kupungua kitu ndani yake. Kwa hivyo wao wanamuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa sheria iliyokamilika, ama wengine wasiokuwa wao, hao ni wapotevu kwa ajili ya kukosa sehemu kubwa ya kitabu cha Allaah na kuukosa uongofu wake.
Ee mwenye kufuata Madhehebu haya ya Ki-Shia, uongo kama huu hata mwendawazimu hawezi kuukubali, sembuse wewe unayejinasibisha na Uislam na Waislam. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufa ila baada ya Allaah kukamilisha kukiteremsha kitabu chake na baada ya kukibainisha na kuwahifadhisha Waislam vifuani pao na kukiandika na kukieneza baina yao, kila mtu, na Ahlul-Bayt na Waislamu wenzao, wote sawa sawa hakuna hitilafu baina yao. Na anayedai kinyume cha hivyo basi huyo amesema uongo.
Unaonaje huyu aliyeandika maneno haya, akitakiwa kutuonyesha hiyo Qur-aan waliohusishwa nayo Ahlul-Bayt atakuwa na msimamo gani? Subhaanaka Allahumma – huu ni uongo mkubwa kabisa.
Uhakika Wa Tatu
Kuhusishwa Ahlul-Bayt Na Wafuasi Wao Tu Kwa Baadhi Ya Miujiza Ya Rusuli Kama Vile Jiwe Na Fimbo.
Uhakika huu umeandikwa ndani ya kitabu hiki cha Al-Kaafi pale mwandishi wa kitabu hiki aliposema;
Kutoka kwa Abi Baswiyr, kutoka kwa Jaafar alayhis-salaam amesema:
“Usiku mmoja wa kiza alitoka Amirul-Muuminina huku akisema;
"Hamhamah – hamhamah, na usiku wa kiza, amekutokeeni Imam akiwa na nguo ya Adam na mkononi mwake ana pete ya Suleiman na fimbo ya Musa!”
Na imeandikwa ndani ya kitabu hicho pia katika Juzuu ya kwanza Kitabu cha Al Hojjah, ukurasa wa 227 kuwa; “Kutoka kwa Abi Hamza, kutoka kwa Abi Abdillahi – alayhis-salaam kuwa nimemsikia akisema;
“Mbao za Musa zipo kwetu na fimbo ya Muwsaa ipo kwetu na sisi ndio warithi wa Rusuli!"
Baada ya haya ewe mwenye kufuata Madhehebu ya ki-Shia, ujuwe kuwa itikadi hii kwa hakika inakufanya uingie katika mambo ya ufisadi mkubwa kabisa na uovu, na wewe ukiwa ni mwenye akili timamu huna budi kujitenga nayo na kuyakanusha. Nayo ni;
1- Kumkadhibisha Ali (Radhwiya Allaahu 'anhu) – kwani Ali (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipoulizwa;
“Je Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekuhusisheni Ahlul-Bayt kwa lolote (peke yenu)?”
Akasema;
“La – isipokuwa kilichomo ndani ya ala ya upanga wangu huu”.
Akatoa karatasi iliyoandikwa ndani yake mambo manne yaliyotajwa na ‘Ulamaa wa Hadiyth kama vile Bukhari na Muslim.
2 Mwenye itikadi hii anakuwa amemkadhibisha na kumdharaulisha Ali (Radhiya Allaahu 'anhu) na ni dalili iliyowazi ya ujinga wa fahamu yake na upungufu wa akili zake na kutoiheshimu nafsi yake. Kwani iwapo mtu huyu ataulizwa;
'Iwapi hiyo pete na iwapi hiyo fimbo na ziwapi mbao (za Nabiy Muwsaa)', angeshindwa kujibu na asingeweza kuleta chochote kati ya vitu hivyo, na kwa ajili hii unabainika uongo wa kisa hiki mwanzo wake mpaka mwisho wake.
Na lilio wazi kuliko hilo, ukimuuliza anayeamini hivyo;
'Kwa nini basi Aali Bayti wasiitumie miujiza hiyo ya fimbo na pete katika kuwaangamiza maadui wao na kuwamaliza kwani wao wamepata tabu sana kutokana na shari nyingi walizotendewa.
Lengo la uongo huu ni kujaribu kuthibitisha kuongoka kwa Mashia na kupotoka kwa wasiokuwa wao katika Waislam, ili kuyafanya Madhehebu ya Ki-Shia kubaki peke yake nje ya mwili wa Waislam na ili wahakikishe viongozi wao na wale waliojificha nyuma yao, wenye nia ovu na tamaa wapate kile wanachokitaka bila kujali kuwa wanaubomoa Uislam na kuuvunja umoja wa Waislam.
Na iwapo itikadi hii inaleta ufisadi na shari kama hii, basi ni itikadi ovu ilioje na ubaya ulioje wa mweye kuwa na itikadi hii au mwenye kuridhika nayo.
Uhakika Wa Nne
Itikadi Kuwa Ahlul-Bayt Na Wafuasi Wao Wana Elimu Ya Rusuli Na Ya Allaah Wasiokuwa Nayo Waislam Wengine.
Uhakika huu umeelezwa katika kitabu cha Al-Kaafi Juzuu ya kwanza kitabu cha Al Hojjah Ukurasa wa 138, pale aliposema;
“Kutoka kwa Abi Basiyr amesema; ‘Niliingia kwa Abu Abdillaah, alayhis-salaaam nikamwambia; Nimejitolea mhanga kwa ajili yako, wafuasi wako wanasema kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemfundisha Ali Alayhis-salaam milango elfu ya elimu inayofungua milango elfu mingine’, Akasema;
"Ee Aba Muhammad, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemfundisha Ali alayhis-salaam, milango elfu ya elimu, na kila mlango unafungua milango elfu mingine’. Akasema, nikamuuliza;
"Hii kwa ile?"
Akasema;
"Ee Aba Muhammad! Sisi pia tunayo Al-Jaamiah na kipi kinachokujulisha ukaijuwa hii Al Jaamiah?" Akaendela kusema; “(Huu) ni ukurasa, urefu wake dhiraa sabini kwa dhiraa ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimsomea kwa mdomo wake na huku (Ali) akiandika kwa mkono wake wa kulia yote yaliyohalalishwa na yaliyoharamishwa na kila kinachohitajiwa na wanadamu hata uchokozi na kujichuna".
Nikamwambia;
“Nakwambia; 'hii ndiyo elimu ya kweli”.
Akasema;
“Hakika hii ni elimu na si ile. Kisha akanyamaza muda kidogo, kisha akasema;
“Tunayo pia Al-Jafar (maandishi ya siri) na kipi kitakachokujulisha ukaijuwa hiyo Al-Jafar? Hiki ni Chombo kilichotoka kwa Adam, ndani yake mna elimu ya Rusulu na ya waliousiwa na elimu ya ‘Ulamaa waliotangulia wa Bani Israil”.
Nikamwambia;
“Hii ndiyo elimu ya kweli”
Akasema; Hii ni elimu ya kweli na si ile, kisha akanyamaza muda, kisha akasema;
“Na kwetu pia tunao Mswahafu wa Faatwimah Alayhas-salaam, wanaujuwaje wao msahafu wa Faatwimah?”
Nikamuuliza;
“Ni kitu gani hiki kinachoitwa mswahafu wa Faatwimah?”
Akasema;
“Mswahafu, ndani yake mna mfano wa Qur-aan yenu hii mara tatu! Wallahi hamna ndani yake yaliyomo ndani ya Qur-aan yenu hii hata herufi moja”.
Nikamwambia;
“Na elimu ni ya Allaah”
Akanambia;
“Sisi kwetu tunayo elimu ya yaliyotangulia na yanayotokea na yatakayotokea mpaka siku ya Kiama !!”
Ameyatamka haya kama yalivyoandikwa.
Itikadi batili hii inaleta natija ifuatayo;
1- Kutokuwa na haja ya kitabu cha Allaah, na hii ni kufru.
2- Kuwahusisha Ahlul-Bayt kuwa wana elimu na ujuzi wasiokuwa nao Waislam wenzao. Na hii inaleta maana ya kumtuhumu Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ameifanya hiyana elimu aliyopewa. Na bila shaka kumtuhumu Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amefanya hiyana, ni kufru.
3- Kumkadhibisha Ali (Radhwiya Allaahu 'anhu). Kwani katika Hadiyth Swahiyh Ali (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikwishasema;
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hajatuhushisha sisi Ahlul-Bayt na chochote”.
Na kumsingizia uwongo Ali (Radhwiya Allaahu 'anhu) ni haramu kama ilivyokuwa haramu kumsingizia uwongo mtu yeyote yule.
4- Kumsingizia uwongo Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hili ni katika makosa makubwa kabisa, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;
“Kunisingizia uongo mimi ni tofauti na kumsingizia uwongo mmoja kati yenu. Atakayenisingizia uongo kusudi, ataingia Motoni”.
5- Kumsingizia uongo Faatwimah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kuwa eti ana Mswahafu wake mkubwa kuliko Qur-aan mara tatu, na kwamba hamna ndani yake katika maandishi ya Qur-aan hata herufi moja.
Mwenye itikadi hii hawezi kuwa Muislam, au kuhesabiwa kuwa ni mmoja wao, wakati yeye anaishi katika elimu na uongofu wasiokuwa nao Waislam wenzake.
6- Na mwisho, Je! Uzushi huu na batili hii na uongo huu wa kipuuzi unasihi kunasibishwa na Uislam, dini ya Allaah ambaye haikubali dini nyingine isipokuwa hii?
وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٨٥﴾
Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Aali ‘Imraan: 85]
Kwa ajili hiyo ewe Mwenye kufuata Madhehebu ya ki-Shia, ili tuokoke na tatizo hili kubwa, sema pamoja nami;
“Rabb wangu mimi nakukanushia yale waliyokusingizia waongo hawa, Wewe pamoja na Rasuli wako na Ahlul-Bayt yake waliotahirika, kwa ajili ya kuwapotosha waja wako na kuifisidi dini yako na kuuvuruga umma wako Umma wa Rasuli wako (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Uhakika Wa Tano
Itikadi Kuwa Musa Kadhim Amjitolea Mhanga Kwa Ajili Ya Kuwaokoa Mashia.
Mwandishi wa kitabu cha Al Kaafi ameandika katika kitabu hicho katika Juzuu ya kwanza kitabu cha Al Hojjah, Ukurasa wa 260 kuwa;
Hakika Abal-Hassan Kadhim (huyu ni Imam wa saba katika maimam wa madhehebu ya Ithnaasheri) amesema;
“Allaah Azza wa Jalla alighadhibika na Mashia akanitaka nichague ama mimi ama wao, na mimi nikakubali kuwakinga kwa nafsi yangu”.
Sasa ewe ndugu yangu unayefuata Madhehebu ya Ki-Shia, hebu nambie; Kisa hiki wanachokutaka wewe ukiamini kinataka kutufundisha kitu gani?
Maana ya kisa hiki ni kuwa;
Musa Kadhim, Allaah amrehemu, amejitolea mhanga kufa yeye kwa ajili ya kuwaokoa wafuasi wake ili Allaah awaghufurie na kuwaingiza Peponi bila kuhesabiwa. Jaribu kutafakari ewe unayefuata Madhehebu ya Ki-Shia – Namuomba Allaah aniongoze mimi na wewe katika yale anayoyapenda na kuridhika nayo katika itikadi na maneno na matendo mema. Hebu tafakari juu ya uwongo huu, kwani huu bila shaka ni uwongo ulio mbali kabisa na haki na ukweli.
Ukiutafakari uongo huu utajikuta unalazimika kuitakidi mambo makubwa mengi usiyopenda wewe mwenyewe kunasibishwa nayo wala kujinasibisha nayo, nayo ni haya yafuatayo;
1- Kumsingizia uongo Allaah (‘Azza wa Jalla) kuwa eti amemfunulia Wahyi Musa bin Kadhim kwamba eti ameghadhibika na Mashia na kwamba Musa bin Kadhim amejitolea nafsi yake mhanga kwa ajili ya kuwaokoa Mashia. Huu Wallahi ni uongo aliosingiziwa Allaah anayesema katika Qur-aan;
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا …﴿٢١﴾
Na nani mdhalimu zaidi kuliko yule anayemtungia Allaah uongo…. [Al-An'aam: 21]
2- Kumsingizia uongo Musa Al Kadhim Allaah amrehemu, ambaye Wallahi si Rasuli (si Rasul wala Nabiy) na hii kauli aliyosingiziwa kuwa eti amesema kuwa;
“Allaah Azza wa Jalla alighadhibika na Mashia akanitaka nichague ama mimi ama wao, na mimi nikakubali kuwakinga kwa nafsi yangu”.
Kauli hii ya kuridhika kujitolea mhanga kwa ajili ya Mashia ni dalili ya kusingiziwa Unabii huyu Musa bin Khadhim (Rahimahu Allaah)!! Wakati katika itikadi ya Kiislam, mtu kuitakidi kuwa yupo rasuli baada ya Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kufru, kwa sababu huku ni kuikadhibisha kauli ya Allaah pale aliposema;
مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ ...﴿٤٠﴾
Hakuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Rasuli wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. [Al-Ahzaab: 40]
3- Itikadi ya Madhehebu ya ki-Shia kukubaliana na itikadi ya Manasara juu ya kusulubiwa na kutolewa mhanga, kwani Manasara wanaitakidi kuwa Issa (AS) amejitolea mhanga nafsi yake kwa ajili ya kuwaokoa wanadamu kutokana na ghadhabu ya Allaah juu yao. Na Mashia wanaitakidi hivyo hivyo kuwa Musa Al Kadhim alishauriwa na Mola wake iwapo anahiari Mashia waangamizwe au afe yeye, akakubali afe yeye ili awaokowe Mashia wake na kuwakinga na ghadhabu ya Allaah. Kwa hivyo Mashia na Manasara itikadi yao ni moja na Manasara ni makafiri kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Allaah. Je! Mwenye kufuata madhehebu ya Ki-Shia yuko radhi naye awe kafiri?
Mwisho nakuomba uiokowe nafsi yako ewe mwenye kufuata Madhehebu ya ki-Shia na uikanushe batili hii, na mbele yako ipo njia ya Allaah iliyonyoka, njia ya Waislam.
Uhakika Wa Sita
Kuitakidi Kuwa Maimam Wa Mashia, Daraja Lao Ni Sawa Na Daraja La Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Katika Kukingwa Wasifanye Madhambi Wala Makosa Na Pia Katika Kufunuliwa Wahyi Na Katika Kutiiwa (Ta-A) Na Mengine. Isipokuwa Katika Kuowa, Wao Hawaruhusiwi Kuowa Kama Alivyoruhusiwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam).
Itikadi hii inayowapandisha Maima wa Ki-Shia kuifikia daraja ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), imeandikwa na kuthibitishwa na mwandishi wa kitabu cha Al Kafi kwa kuegemea ushahidi wake kutoka katika riwaya mbili.
Ya Kwanza; Hadiyth iliyosimuliwa katika ((kitabu cha Al Hojjah - ukurasa wa 229)); pale aliposema;
"Al Mufadhal alikuwa kwa Abu Abdillaah akamuuliza;
"Nimejitolea mhanga kwa ajili yako, ni kweli kuwa Allaah anaweza kuwafaridhishia watu kumtii mtu kisha akamzuilia mtu huyo kheri itokayo mbinguni?
Abu Abdillahi (katika maimaam wa Mashia) akamjibu;
"La- Allaah ni Mkarimu na Mwenye Huruma na Mpole zaidi kwa waja Wake, hawezi kuwafaridhishia waja wake kumtii mtu, kisha amzuwilie mtu huyo kheri itokayo mbinguni asubuhi na jioni".
Maneno ya riwaya hizi yanatujulisha kuwa (kutokana na itikadi za Ki-Shia) watu wamefaridhishiwa kuwatii maimam asubuhi na jioni, kwa amri itokayo mbinguni na kwamba kuwatii huko kuwe kwa ukamilifu usio na mipaka mfano wa taa-a tulivyoamrIshwa kumtii Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kwamba Maimam hao wa Ki-Shia wanafunuliwa wahyi na kwamba wanapata habari kutoka mbinguni asubuhi na jioni, na kwa ajili hiyo wao na Rusuli (Anbiyaa na Mursaliyn) ni sawa sawa hapana tofauti yoyote baina yao.
Kuitakidi kuwa yupo anayefunuliwa Wahyi baada ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kurtadi kutoka katika dini ya Kiislam na ni kufru, na jambo hili maulamaa wote wamekubaliana bila hitilafu yoyote baina yao.
Subhaana-Allaah vipi mwenye kufuata madhehebu ya Ki-Shia anakubali kutungiwa uwongo na kulazimika kuukubali huku akiishi mbali kabisa na Uislam wa kweli akiitakidi itikadi za kikafir wakati nia yake ilikuwa ni kuitakidi itikadi za Kiislam kwa ajili ya kufuzu ili awe mmoja wao.
Allaah ukate mkono wa muovu wa mwanzo aliyewaweka mbali Nawe na kuwatenga mbali na njia yako .
Ya Pili; Hadiyth iliyosimuliwa katika ((Juzuu ya kwanza ya kitabu cha Al Hojjah - ukurasa wa 229)).
Amesema;
'Kutoka kwa Muhammad bin Salem, amesema; "Nimemsikia Aba Abdillaah alayhis-salaam akisema;
"Maimamu daraja lao ni sawa na daraja la Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), isipokuwa wao si Manabii na hawaruhusiwi kuowa kama alivyoruhusiwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kwa mengine yasiyokuwa hayo, daraja lao ni sawa na la Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)".
Riwaya hizi, ingawaje kwa dhahiri yake zinaonesha kama kila moja inaikanusha nyengine, lakini undani wake ni sawa na riwaya zilizotangulia zinazothibitisha kukingwa kwa maimamu hao wasifanye madhambi na pia kuwajibika kuwatii na kwamba wanafunuliwa wahyi, kwa sababu daraja ya Imam kwao wao ni daraja lililo sawa na daraja la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), isipokuwa katika kuowa tu, na kwamba wao wamekingwa na Allaah wasifanye kitendo chochote cha dhambi, pamoja na kuwajibika kuwatii na kwamba wamehusishwa na kila alohusishwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukamilifu.
Kusudi la kweli la uongo huu ewe mwenye kufuata Madhehebu ya Ki-Shia ni kutaka kuufarikisha umma wa Ki-Shia na Uislam, ili kupiga vita kwa hoja kuwa eti umma wa ki-Shia hawana haja na kile walicho nacho Waislam katika Wahyi wa Kitabu kitukufu na Uongofu wa Mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu wao wanao Mswahafu wa Faatwimah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambao ni bora kuliko Qur-aan tukufu na maandishi ya siri yaliyokusanya ndani yake elimu zote pamoja elimu ya Rusuli iliyotangulia na kwamba Maimam waliokingwa wanafunuliwa kama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifunuliwa isipokuwa katika masaala ya kuowa zaidi ya wake wanne na mengine yaliyo na mfano huo yanayowatoa Mashia nje ya Uislam kama unywele unavyotolewa ndani ya unga uliokandwa
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) aikate roho ya shari iliyoukata mwili huu mpenzi kutoka katika mwili wa Umma wa Kiislam kwa jina la Uislam na kuwabaidisha viumbe wengi kwa kutumia njia ya Aali Bayti, kwa mwito wa kuwanusuru Ahli l Bayti.
Uhakika Wa Saba
Kuitakidi Kuwa Swahaba Wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa Sallam) Wote (Radhwiya Allaahu 'Anhum) Wamertaddi Na Kukufuru Baada Ya Kufa Kwake Isipokuwa Ahlul-Bayt Na Wengine Wachache Kama Vile Salman Na Ammar Na Bilal (Radhwiya Allaahu 'Anhu)
Hii ni itikadi inayokubaliwa na karibu wanavyuoni wote wakubwa wa Madhehebu ya Ki-Shia, na kwa ajili hiyo vitabu vyao vyote vinazungumza juu ya maudhui hayo. Kutokutangaza kwao rasmi katika vyombo vya habari ni kwa ajili ya itikadi yao nyingine iitwayo 'Taqiya' (kutokusema ukweli), itikadi hii ni wajibu katika Madhehebu yao.
Ama ushahidi wa ukweli huu na ili kuupata uhakika wake, tunakuleteeni dalili zifuatazo;
1- Katika kitabu cha Rawdhwatul Kaafi cha Al Kilaniy mwenye kitabu hiki cha Al Kaafi, ukurasa wa 202 anasema;
"Kutoka kwa Hanan kutoka kwa Abi Jaafar amesema;
"Hao (wasiokufuru peke yao) ni Mikidadi, Suleiman na Aba Dhar."
Katika Tafsiri ya Al Saafi - na hii ni Tafsiri maarufu sana na inayoheshimiwa sana katika Madhehebu ya Ki-Shia na inayotambulika zaidi, zimo ndani yake riwaya nyingi sana zinayoitilia nguvu itikadi hii ya kuwa Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walirtadi (walitoka katika dini ya Kiislam) mara baada ya kufariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa Ahlul-Bayt na watu wachache wengine kama vile Suleiman na Ammar na Bilaal Radhwiya Allaahu Ta’aalaa anhum.
Ama kuhusu Masahaba wawili wakubwa, nao ni Abu Bakr na ''Umar Radhwiya Allaahu ‘anhumaa, ndani ya vitabu vyao mna maelezo mengi sana yasiyohesabika katika kuwakufurisha.
Miongni mwa maelezo hayo ni kauli zilizoandikwa katika kitabu cha Al Kiliniy - ukurasa wa ishirini, pale aliposema;
"Nilimuuliza Aba Jaafar juu ya Maswahaba wawili wakubwa hawa, akanambia;
'Wamefariki dunia bila ya kutubu wala kukumbuka yale waliyomtendea Amiri wa Waislam (Ali bin Abi Talib (Radhwiya Allaahu 'anhu), iwapate laana ya Allaah na ya Malaika wake na ya watu wote kwa ujumla !!!."
Na ameandika pia katika ukurasa wa 107 kuwa;
"Unaniuliza juu ya Abu Bakr na ''Umar? Naapa kwa umri wangu kuwa wamefanya unafiki na kuyakataa maneno ya Allaah na kumfanyia mzaha Rasuli Wake na hawa ndio makafiri wawili, iwapate laana ya Allaah na ya Malaika na ya watu wote kwa ujumla!!!"
Baada ya yote haya, ewe mwenye kufuata madhehebu ya ki-Shia, kweli inaingia akilini kuwahukumu kuwa makafiri na kuwa wamertaddi Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambao ni wanafunzi wake na wao ndio walioinusuru dini yake na waloibeba sharia yake, hawa ambao Allaah ametaja kuridhika Kwake nao katika kitabu chake na kuwabashiria Pepo kwa ulimi wa Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Allaah amewachagua hawa kuwa walinzi wa dini Yake na kuitukuza dini Yake na kuwafanya waendelee kutajwa ndani ya Qur-aan mpaka Siku ya Kiama. Hebu kwa ajili ya Rabb wako sema ewe mwenye kufuata Madhehebu ya Ki-Shia; Katika kuwakufurisha na kuwalani na kuwatoa katika Uislam Swahaba hawa wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) si pana lengo lililokusudiwa?
Bila shaka yoyote ewe mwenye kufuata Madhehebu ya ki-Shia, lengo lake ni kuupiga vita Uislam ambao ni adui mkubwa wa Mayahudi na Wamajusi na adui wa kila Shirki na kila mwenye kumuabudu mwengine asiyekuwa Allaah.
Kusudi la kuwakufurisha Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuirudisha dola ya ki Majusi iliyokuwa ikiongozwa na Kisra baada ya Uislam kuzibomoa nguzo zake na kuziangusha arshi zake na kufuta kuwepo kwake na hayo yataendelea milele In Shaa Allaah Ta’aalaa.
Hebu tizama mwenyewe dalili zisizohitaji kushereheshwa.
Aliyemuuwa Khalifa wa pili wa Kiislam ni nani mwingine kama si kijana wa Ki Majusi?
Aliyeibeba bendera ya fitna dhidi ya 'Uthmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kusababisha kuuliwa na hapo ndipo mbegu ya mwanzo ya shari na fitna ilipopandishwa katika ardhi ya Waislam ni nani mwingine isipokuwa Myahudi Abdillahi bin Saba-a?
Kutokana na mimba ovu hii akazaliwa Shetani wa ki-Shia akiwa amebeba bendera ya Uzushi iitwayo (Wilaya ya Imam), na kuwa mfano wa panga mbili zilizoelekezewa juu ya kichwa cha Uislam na Waislam katika kuwaita watu katika utawala wa Imamu na kuwakufurisha Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kuwalani na kumkufurisha kila aliyeridhika nao au kuwataka watu waridhike nao katika Waislam.
Kutokana na Uzushi wa Uimam zikapangwa hila nyingi dhidi ya Makhalifa wa Kiislam na vita vingi vikali kuchochewa na damu kumwagika na misingi kubomoka na Uislam ukaishi katika mfarakano, maadui walio ndani yake ni sawa na maadui walio nje yake na wapinzani wake wanaojinasibisha nao wakiwa sawa na maadui zake walioukanusha.
Kutokana na yote haya, ewe mwenye kufuata Madhehebu ya Ki-Shia, ndio itikadi za Ki-Shia zikawekwa ili iwe dini nyingine mbali na dini ya Kiislam. Dini yenye asili zake, chimbuko lake, vitabu vyake na mafundisho yake, elimu na maarifa yake.
Katika risala hii niliutanguliza ushahidi juu ya ukweli wa maneno haya, kwa hivyo rudia tena kuusoma na utafakari vizuri iwapo bado unashaka yoyote ile.
Ingelikuwa kusudi lao si baya, wasingeligeuza itikadi ya Wilaya kuwa ni jambo la kuwafarikisha Waislam na kupandisha mbegu ya shari, fitina na uadui baina yao.
Miongoni mwa Ahlus-Sunnah wal Jamaa-a ambao wao ndio wanaostahiki kuitwa Waislam wa kweli hakuna hata mmoja kati yao anayewachukia Ahlul-Bayt. Kwa nini basi kundi la Mashia peke yao ndio wanaojipa haki ya kuwa wao ni wapenzi wa Ahlul-Bayt na kuigeuza haki hiyo kuwa ni lengo lao kubwa na kwa ajili hiyo kuwafanyia uadui Waislam, bali wanawakufurisha na kuwalani kama tulivyoona katika ushahidi nilioutanguliza.
Na kuhusu Uimam pia; Si itakuwa upuuzi na ujinga iwapo Waislam hawatoachwa kujichagulia wenyewe mtu mahiri, mwenye sifa za uongozi, wanayemuona kuwa anastahiki kuwaongoza na kuwahukumu kwa sheria ya Allaah na uongofu wa Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na uwezo wake na uhodari wake?
Madhehebu ya Ki-Shia yanasema;
"La - lazima awe aliyeusiwa kwa kutajwa na awe amekingwa kutokana na madhambi na awe anafunuliwa Wahyi".
Lini Waislam watampata kiongozi wa aina hii? Kwa ajili hii ndiyo Mashia wanajitenga na kuwalani Waislam na kuwafanyia uadui?
Unaonaje ukaikomboa nafsi yako na usiwe mateka wa itikadi batili na kujitowa nje ya madhehebu haya yasiyokuwa na nuru na yenye kuangamiza!!!?
Ee mwenye kufuata Madhehebu ya Ki-Shia; Kumbuka kuwa utakuja kuulizwa juu ya nafsi yako na juu ya aila yako. Kwa hivyo anza kuiokowa kutokana na adhabu ya Allaah, na juwa ya kwamba hayo hayawi ila kwa kufuata Imani iliyo sahihi, na kwa matendo mema yasiyopatikana isipokuwa katika kitabu cha Allaah na katika mafundisho ya Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na kumbuka pia kuwa wewe ukiwa ni mfungwa katika jela ya Madhehebu mapotofu ya kiSshia huwezi kuipata Imani iliyo sahihi wala kutenda matendo mema ila iwapo utajiunga na Ahlus-Sunnah wal Jamaa-a, hapo utakipata kitabu cha Allaah kilichotakasika na kisichochanganyika na taawil zisizokuwa sahihi zilizoingizwa kusudi na viongozi wa ki-Shia kwa ajili ya kuwapotosha watu na kwa ajili ya ufisadi.
Utayakuta pia Mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyo sahihi yasiyochanganywa na uongo na upendeleo. Kwa ajili hiyo unaweza kuipata Imani iliyo sahihi na Itikadi ya Kiislam iliyosalimika na matendo mema yaliyowekewa sheria ya Allaah kwa ajili ya waja wake ili wajitakase kwayo nafsi zao, na yenye kuwapa ahadi ya ushindi.
Kwa hivyo ihame itikadi hiyo, ee mwenye kufuata Itikadi ya Ki-Shia na uelekee kwa Rabb wako na Mafundisho ya Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani utapata pahala pengi pa kukimbilia.
Mwisho kabisa, nataka uelewe kuwa mimi sikukutangulizia Nasaha hii kwa ajili ya tamaa ya kile ulicho nacho au kilichopo kwa bin-Aadam yeyote yule mwengine, au kwa kukuogopa wewe au mwengine yeyote yule katika wana-Aadam, sivyo Wa-Allaahi, bali nimekutangulizia haya kwa ajili ya undugu katika Uislam na kwa ajili ya kuwajibika kupeana nasaha kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah na kwa ajili ya Kitabu chake na Mafundisho ya Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa ajili ya Waislam wote.
Haya ndiyo yaliyonifanya nikuletee Nasaha hii nikitarajia kutoka kwa Allaah nasaha hii ikufungue kifua chako na akuongoze katika yale yatakayokufurahisha katika dunia yako na Aakhirah yako.
Wasalaamun alal- Mursaliyna wal-Hamdu li-LLaahi Rabil-aalamiyn