Nani Aliyemuua Al-Hasan (رضي الله عنه)?

Nani Aliyemuua Al-Hasan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ)

 

Imetafsiriwa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’ay (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Suali:

 

Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na mwanawe Yaziyd wanatuhumiwa ndani ya baadhi ya vitabu vya Shia kuwa wao ndio waliofanya njama ya kumuua Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa kumtilia sumu ndani ya chakula chake. Wakaendelea kusema kuwa walimkinaisha mmoja katika wake zake Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akubali kuifanya kazi hiyo, na kwamba eti mwanamke huyo aliahidiwa kuolewa na Yaziyd mwana wa Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Je, ukweli uko wapi?

 

Majibu:

 

Tuhuma yoyote ile lazima iambatane na ushahidi usiopingika. Kumtuhumu mtu bila kuwa na ushahidi ulio thabiti isipokuwa kufuata uvumi tu, ni katika makosa makubwa na bila shaka tuhuma namna hizo haziwezi kukubalika.

 

Hata kama mtu ataleta ushahidi, basi ushahidi huo hautoweza kukubalika ikiwa umekosekana na jambo moja muhimu sana; nalo ni kuthibiti kwa ushahidi huo. Kwa sababu mtu akishindwa kuuthibitisha ushahidi wake, basi ushahidi huo unakuwa si chochote isipokuwa ni tuhuma tu isiyo na uzito wowote ule.

Hii ni kanuni inayotumiwa katika mahakama zote ulimwenguni. Tuchukue mfano wa tuhuma alizoziandika Salmaan Rushdi katika kitabu chake kiitwacho ‘Satanic verses’ alipowatuhumu Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rushdi huyu hakuzibuni tuhuma hizo kichwani mwake, bali alizikuta ndani ya vitabu vya historia. Isipokuwa jambo aliloshindwa kulifanya Rushdi ni kuleta ushahidi thabiti wa kuthibitisha tuhuma zake hizo, na yeye bila shaka hakujali juu ya ukweli wa tuhuma zake hizo. Kwa nini? Kwa sababu yeye alikuwa na lengo lake na sababu zake zilizomfanya auandike uongo wake huo.

 

Kwa hivyo mtu anapomtuhumu Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) au anapomtuhumu mtu yeyote yule kuwa amemtilia sumu Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na asijali juu ya uthabiti na ukweli wa ushahidi wake, isipokuwa anafanya hivyo kwa ajili ya kumchukia kwake tu Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), basi mtu huyu anakuwa hana tofauti yoyote na Salman Rushdi na walio mfano wake. Wala hakhitilafiani nao katika kueneza kwao tuhuma za uongo juu ya Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wala haijali kauli ya Allaah Alipotuamrisha kuwa tunapotoa ushahidi tuwe waadilifu, na kuchukiana kwetu na watu kusitupeleke kutowafanyia insaafu (uadilifu) wale tunaowachukia.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّـهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا َعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾ 

Enyi walioamini!  Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Maaidah: 8]

 

 

Hadiyth Sahihi Juu Ya Maudhui Haya Inasemaje?

 

Hadiyth iliyo sahihi kuhusu tukio hili ni ile inayosema kuwa; pale Al-Hassan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa amelala kitandani huku akikata roho kutokana na sumu. Ndugu yake Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuuliza:

 “Ndugu yangu niambie nani aliyekutilia sumu?”

Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akajibu: “Kwa nini? Ili upate kumuua?”

Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Ndiyo”.

Ndipo Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipomuambia: “Sitokuambia lolote, kwa (sababu) ikiwa (yule aliyeniua) ndiye ninayemdhania, basi malipo ya Allaah ni makali zaidi. Na ikiwa si yeye, basi Wa-Allaahi sikubali auliwe mtu asiye na makosa kwa ajili yangu[1]

 

 

Hadiyth hii iliyo sahihi, ni dalilli kuwa hata Al-Hasan mwenyewe (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hana uhakika na hamjui nani aliyemtilia sumu. Na juu ya yote hakutaka kumpa hata ndugu yake jina la yule anayemdhania.

 

 

Jambo la ajabu, Wa-Allaahi, ni kuona kuwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe amechukua tahadhari katika jambo hili akihofia asije akawatuhumu wasio na makosa. Wakati watu siku hizi, bila kujali wala kuogopa, wanamtuhumu Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ndiye aliyemtilia sumu Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Jambo kubwa lililokuwa likimshughulisha Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni umoja wa Ummah. Kwa ajili hiyo alikubali kufanya sulhu na Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika mwaka wa 41 H. Na tukio hili muhimu lilibashiriwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth maarufu aliposema: “Hakika mwanangu huyu (Al-Hasan) ni bwana. Na karibu utakuja wakati ambao kupitia kwake Allaah Atasuluhisha makundi mawili makubwa ya Waislam.”

 

 

Kwa ajili hiyo Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hajakubali kumtaja yule aliyemdhania, kwa ajili ya kuchunga na kujitahidi usije ukatokea mfarakano katika Ummah wa Kiislamu (kwa ajili ya dhanna tu). Hata kama ikibidi akose haki katika haki zake.

 

 

Ingelikuwa anayemtilia shaka ni Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ndiye aliyemtilia sumu basi angelimuambia tu ndugu yake Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Naogopa kukuambia kwa sababu itaweza kusababisha vita baina ya Waislamu ukitaka kunilipia kisasi changu.”

 

Lakini kinyume na hayo Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hajagusia hata kidogo juu ya kuleta mfarakano katika Ummah. Isipokuwa alielezea hofu yake tu asije akauliwa mtu asiye na makosa kwa ajili yake. Kutokana na haya, tunapata uhakika kuwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakumtilia shaka Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hata kidogo.

 

 

Isitoshe, Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliishi miaka kumi baada ya kufariki kwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Wakati wote huo Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) shujaa asiyeogopa chochote, alikuwepo, na walikuwepo pia ndugu yake kwa baba Muhammad al-Hanafiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na bin ‘ami zake ‘Abdullaah bin ‘Abbaas na ‘Abdullaah bin Ja’afar na wengi katika watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini hatukupata kusikia hata mmoja kati yao kuwa aliwahi kumtuhumu Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ndiye aliyemtilia sumu Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Bali kinyume na hayo, watu hao wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa na uhusiano mzuri sana na Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na hasa Ibn ‘Abbaas na ‘Abdullaah bin Ja’afar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) hawakupata hata siku moja kusema neno lolote juu ya Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amehusika na kuuliwa kwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Hawakupata kutamka hayo mbele za watu wa kawaida na wala hata kwa walio karibu nao. Haya yote yakiwa ni dalili nyingine kuwa tuhuma hizo juu ya Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni za uongo zisizo na msingi na za upuuzi mtupu.

 

 

Hebu tuyachunguze maelezo yaliyopatikana katika vitabu vya historia kuhusu tukio hilo. Maelezo ya pekee ya kumtuhumu Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ndiye aliyepanga kumtilia sumu Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) yameelezwa na mwana historia aitwae Muhammad bin ‘Umar al-Waaqidi na maelezo hayo yanasema hivi:

 

‘(Al-Waaqidi) amesema: ‘Nilisikia baadhi ya watu wakisema kuwa Mu’awiyah alimpanga kwa siri mmoja katika watumishi wake amtilie sumu.’[2]

 

Juu ya kuwa mlolongo wa wapokezi wa maelezo haya (narrators) ni watu wanaojulikana kwa uaminifu wao, lakini mtu huyu Al-Waaqidi, anajulikana katika elimu ya Hadiyth kuwa si mtu wa kuaminika. Kama tutaandika maelezo yote juu ya kutoaminika kwake, basi itabidi tujaze kurasa nyingi sana. Lakini inatosha tu kuiandika kauli ya Imaam Shaafi’iy (Rahimahu Allaahu) aliyeishi wakati wake na aliyekuwa akimjua vizuri mtu huyu (Al-Waaqidi) aliposema juu yake:

 

 

‘Katika mji wa Madiynah kulikuwa na watu saba waliokuwa wakitunga Hadiyth kisha wakijitungia wapokezi wake, na mmoja wao alikuwa Al-Waaqidi.[3]

 

 

Udhaifu wa pili wa maelezo haya yanatoa mwanga zaidi, nao ni kuwa Al-Waaqidi huyu hakutaja majina ya waliompa habari hizo. Alisema tu kuwa ‘Nilisikia baadhi ya watu wakisema…”

 

 

Juu ya kuwa kabla ya kutoa habari hizi alitangulia kutoa maelezo mengi yaliyoambatana na majina ya watu aliopokea kutoka kwao habari mbali mbali, lakini alipoifikia habari hii alisema tu: “Nilisikia baadhi ya watu wakisema...”

 

 

Kutokana na habari kama hizi zisizothibitika, watu leo wako tayari kuwatuhumu Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni wauaji? Bila shaka tuhuma za aina hii zisizokuwa na msingi wowote wa kielimu hazileti faida yoyote isipokuwa kuridhisha matamanio ya nafsi.

 

 

Tuhuma Kwa Mke Wa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu)

 

 Yapo maelezo mengine yanaomtuhumu mke wa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na jina lake ni Ja’dah bint al-Ash’ath, kuwa ndiye aliyemtilia sumu mumewe. Habari hizi zinasema kuwa Yaziyd mwana wa Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyemhadaa Bibi Ja’dah akakubali kumtilia mumewe sumu hiyo na alimuahidi kumuowa ikiwa atafanikiwa.

 

Habari hizi zimeelezwa na Muhammad Ibn Salaam al-Jumahi, na zimepokelewa na al-Mizziy katika kitabu cha ‘Tahdhiybul-Kamaal’ kama ifuatavyo:

 

“Kutoka kwa Muhammad bin Salaam al-Jumahi amesema kuwa amesikia kutoka kwa Ibn Ju’dubah kuwa Ja’dah binti wa Ash’ath bin Qays, aliyekuwa mke wa Al-Hasan bin ‘Aliy, alipelekewa habari na Yaziyd kwa njia ya siri akiambiwa: ‘Mtilie sumu Al-Hasan kisha mimi nitakuwa mumeo.’ Akafanya hivyo na baada ya Al-Hasan kufariki akatuma habari kwa Yaziyd kuwa na yeye atimize ahadi yake akamjibu kwa kumwambia: “Hatujakubali uwe mke wa Al-Hasan, tutakubali uwe mke wetu sisi?”[4]

 

Hivi ndivyo habari hizo zilivyoandikwa ndani ya vitabu vya historia.

 

Kwa mtu asiyekuwa na elimu yoyote ya mapokezi ya habari wala Hadiyth, anaweza kuzikubali habari hizi kuwa ni ushahidi unaokubalika. Kwa mwenye kuzisoma habari hizi huku moyo ukiwa umekwishajazwa chuki dhidi ya Yaziyd, ataziona habari hizi kuwa ni ushahidi usiopingika.

 

Lakini kwa mwenye kuitafuta elimu ya kweli na ushahidi wa kweli usio na upendeleo, bila shaka hatokubali kutawaliwa na hisia zake. Bali kwanza ataupima ushahidi huo, ataufanyia tahakiki, atafungua vitabu, kisha atatoa uamuzi wake. Kwa mwenye kuutafuta ukweli, hisia zake zinajengwa kwa ushahidi na wala hawezi kukubali ushahidi wake ujengwe kwa hisia.

 

Tukirudia maudhui yetu na kuyachambua vizuri maelezo haya, tutaona kuwa Ibn Ju’dubah huyu, ambaye Muhammad bin Salaam amezipata habari hizi kutoka kwake, jina lake hasa ni Yaziyd bin Iyaad bin Ju’dubah aliyeishi mji wa Madiynah wakati wa Imaam Maalik (Rahimahu Allaahu).

 

Mmoja katika wanafunzi wa Imaam Maalik aitwae ‘Abdur-Rahmaan bin al-Qaasim, aliwahi kumuuliza Imaam Maalik akitaka kujua rai yake juu ya mtu mmoja aitwae Ibn Sam’aan. Imaam Maalik akamjibu: ‘Huyu ni muongo’. Ibn al-Qaasim akauliza tena: “Na Ibn Ju’dubah je?”. Imaam Maalik akajibu: ‘Muongo mkubwa zaidi, bali muongo mkubwa sana’.[5]

 

Isitoshe, inajulikana kuwa Ibn Ju’dubah huyu alifariki dunia wakati wa Al-Mahdi aliyekuwa Khaliyfah wakati wa utawala wa al-Abbasiyah (Abbasid) aliyehukumu hadi mwaka wa 165 H na kwamba aliishi miaka 70. Tuseme ikiwa Ibni Ju’dubah huyu alizaliwa katika mwaka 95 H. Basi atakuwa alizaliwa baada ya kupita nusu karne tokea alipofariki dunia Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Kwa ajili hiyo habari za mpango wa Yaziyd na Ja’dah mke wa Hassan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) zilimfikia kupitia kwa watu asiotaka kuwataja, au zitakuwa ni dhana zake mwenyewe zilizompitikia akilini mwake.

 

Mmoja katika ’ulamaa wa Hadiyth aitwae Ahmad bin Swaalih al-Masri anasema: ‘Alikuwa mtungaji wa habari.[6] Kutokana na zama alizoishi, tunapata ushahidi kamili kuwa mpango huo wa kutiliwa sumu ni Hadiyth aliyoitunga yeye mwenyewe Ibn Ju’dubah huyu.

 

 Hitimisho

 

Kwa kumaliza tunasema kuwa: Yafuatayo ni ushahidi kamili kuwa Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na mwanawe Yaziyd hawahusiki hata kwa mbali na kifo cha Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

 

1-    Kukataa kwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutaja jina la mtu anayemtilia shaka.

 

 

2-   Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe alitamka maneno yafuatayo ‘Sitokwambia lolote, ikiwa ndiye ninayemdhania…’ Hii ikimaanisha kuwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe alikuwa akimdhania tu mtu mmoja na wala hakuwa na uhakika naye.

 

 

3-  Habari za kumhusisha Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) zimeletwa na mtu anyejulikana na ’Ulamaa wote wa wakati wake kuwa ni mtu anayependa kutunga hadiyth za uongo.

 

4-   Habari za kumhusisha Yaziyd na Ja’dah zimeletwa na Ibn Ju’dubah aliyezaliwa miaka 50 baada ya kifo cha Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Wala hakutaja majina ya watu waliompa habari hizo. Isitoshe habari hizo alizielezea wakati wa utawala wa Al-Abbasiyyah, wakati chuki nyingi zilikuwepo dhidi ya watu wa Bani Umayyah, na bila shaka kwa vile Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anatokana na kabila la Bani Umayyah, kwa hivyo wakati ule ulikuwa mzuri kwa kumsingizia uongo wowote na ukakubalika.

 

 

5- Habari za Bibi Ja’dah kumtilia sumu Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) zingekuwa za kweli basi sidhani kama angetokea mtu yeyote aliyekuwa tayari kumuoa Bibi huyo, wachilia mbali mtu huyo awe wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini ukifuatilia habari za Ja’dah, utaona kuwa baada ya kufariki kwa mumewe na kumaliza eda yake, Bibi huyu aliolewa na ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni bin ‘ami yake ‘Aliy bin Abi Twaalib baba yake Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na Allaah Akawaruzuku mtoto wa kiume waliyempa jina la Muhammad na mtoto wa kike waliyempa jina la Quraybah.[7]

 

 

6- Baada ya kifo cha Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa na uhusiano mzuri na Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) huko Damascus.

Kutokana na yaliyotangulia, unathibitika ukweli wa maneno ya Ibn Kathiyr (Allaah Amrehemu) kama alivyoeleza katika kitabu chake cha Al-Bidaayah wan-Nihaayah aliposema:

 

‘Waletaji wa habari hizi, wote wamethibiti kielimu kuwa ni watu wasioaminika, na kwa ajili hiyo habari zao hizo haziwezi kuthibitika. Ninashangazwa, inakuwaje watu bila kufanya tahakiki wanaweza kuzithibitisha tuhuma za hatari kama hizi na kuzisadiki habari kama hizi zilizopokelewa kutoka kwa watu waongo.’[8]

 

 

 

[1] Ibn Kathiyr, al-Bidaayah wan-Nihayah vol. 7, uk 41 (Daarul-Hadyith, Cairo 1414/1994); adh-Dhahabiy, Siyar A‘lam an-Nubalaa, uk. 273 Beirut 1410/1990); al-Mizzi, Tahdhiyb al-Kamaal, mj. 6, uk. 251 (Mu’assasat ar-Rrisaalah, Beirut 1413/1992); Ibn Hajar, al-Isabah, mj. 2 uk. 13 (Daarul-Kutub al-‘Ilmiyyah, Beirut); Ibn ‘Abdul-Barr, al-Isti‘aab, mj. 1, uk. 390 (Daarul-Jiil, Beirut 1412/1992).

 

[2] Al-Bidaayah wan-Nihaayah, vol. 7, uk. 41; Tahdhiybul-Kamaal, vol. 6, uk. 251.

 

[3] Tahdhiybul-Kamaal, mj. 26, uk. 194.

 

[4] Kama ilivyotangulia, mj. 6, uk. 253.

 

[5] Tahdhiybul-Kamaal, mj. 32, uk. 223.

 

[6] Kama ilivyotangulia, mj. 32, uk. 224.

 

[7]  Ibn Sa‘d, at-Twabaqaatul-Kubra, mj. 5, uk. 241 (Daarul-Kutub al-‘Ilmiyyah, Beirut 1410/1990).

 

[8] Al-Bidaayah wan-Nihaayah.

 

 

 

Share