08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: Haki Zinazompasa Mke Kumtendea Mumewe: 7-Amtumikie Mumewe Pamoja Na Wanawe

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

 

Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume

 

Alhidaaya.com

 

 

07:  Haki Zinazompasa Mke Kumtendea Mumewe: 7-Amtumikie Mumewe Pamoja Na Wanawe:

 

"فَقَدْ كَانَتْ فَاطِمَةَ بِنْتِ رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ تَخْدُمُ زَوْجَهَا حَتَّى اشْتَكَتْ إِلَى رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَا تَلْقَى مِنَ الرَّحَى فِي يَدِهَا"

 

“Faatwimah binti Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anamtumikia mumewe mpaka akamshitakia Rasuli wa Allaah sugu ya mkono wake kutokana na jiwe la kusagia nafaka”.  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (361) na Muslim (2182)]

 

Naye Asmaa bint Abiy Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:

 

"كُنْتُ أَخْدُمُ الزُّبَيْرَ بن العَوَّامَ خِدْمَةَ الْبَيْتِ كُلّهِ، وَكَانَ لَهُ فَرَسٌ، وَكُنْتُ أَسُوسُهُ، وكُنْتُ أَحْتَشُّ لَهُ وَأَقُومُ عَلَيْهِ"

 

“Nilikuwa namtumikia Az Zubayr bin Al-‘Awwaam (mumewe) huduma zote za nyumbani.  Alikuwa na farasi ambaye nilikuwa namfunza kutii maelekezo, nilikuwa namkatia majani ya malisho na kumsimamia kwa mambo yote”. 

 

Alikuwa pia anamlisha farasi majani, anachota maji, anashona ndoo ya ngozi, anakanda unga, anabeba kichwani kokwa za tende toka shamba la Az-Zubayr hadi nyumbani umbali wa kilometa nne”.  [Al-Bukhaariy (5224) na Muslim (2182)]

 

Sheikh wa Uislamu amesema katika Al-Fataawaa (34/90-91):

 

“’Ulamaa wamevutana katika:  Je, ni lazima mke amtumikie mumewe katika kuipanga nyumba, kumtayarishia chakula, kumletea majani ya malisho mnyama wake kama anaye na mfano wa hayo?

 

Kati yao kuna waliosema kwamba si wajibu kwake kumtumikia, lakini kauli hii ni dhaifu.  Ni dhaifu mithili ya waliosema kwamba si wajibu kwake kumpa mumewe unyumba, kwa kuwa hili halileti maana ya kutangamana naye kwa wema.  Mume ndiye mwenza wake katika safari yao ya maisha, na kama hakumsaidia kwenye maslaha yao ya pamoja, nyumba yao itakuwa katika hali gani?

 

‘Ulamaa wengine wamesema kwamba ni wajibu mke kumhudumia mumewe, kwani mume ndiye bwana wake kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah, na mateka wa mume kwa mujibu wa Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mateka ni lazima atumikie, na huu ndio wema.

 

Kuna wengine pia wamesema ni lazima amtumikie huduma nyepesi nyepesi, na wengine wanasema amtumikie kwa mujibu wa ada na desturi, na hii ndio sawa.  Ni wajibu kwake amtumikie huduma zinazofanana na mazingira yao na kwa mujibu wa hali.  Huduma za mke wa vijijini kwa mumewe ni tofauti na za mjini, na hata mjini kwenyewe kunatofautiana kwa mujibu wa hali ya kila mmoja”.

 

Ninasema:  “Kauli hii ndiyo iliyoungwa mkono na Abu Thawr, Abu Bakr bin Abi Shaybah, Abu Is-Haaq Al-Juwzajaaniy katika ‘Ulamaa wa Kihanbali.

 

Lakini Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba si wajibu mke kumhudumia mume, bali ni lazima mume amwekee mhudumu wa kumtumikia haja zake!!  Kwa sababu, kwa mujibu wa ‘aqdi ya ndoa, kipengele kinachohusika ni kustarehe naye tu kimwili, hivyo mke halazimiwi na mengineyo”.

 

Kiufupi, tunasema kwamba mke kumhudumia mume ni jambo la kimaumbile.  Ni mwanamke gani ambaye yuko tayari kukaa tu ndani ya nyumba yake bila kujishughulisha kwa lolote, halafu asubiri mume aje amfanyie kazi za ndani pamoja na majukumu yake mengine ya kumtafutia riziki.  Hakuna mwanamke wa aina hii kabisa.  Isitoshe, Faatwimah binti Rasuli alikuwa akifanya kazi ngumu ya nyumbani kwake hadi kumlalamikia baba yake, na baba yake hakumwambia mumewe ‘Aliy kwamba mkewe asifanye tena kazi hizo na kwamba yeye ndiye afanye.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hampaki yeyote mafuta kwa lolote linalohusiana na hukmu au sharia.  Kadhalika, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwona Asmaa amebeba majani ya farasi kichwani akiwa pamoja na mumewe Az Zubayr, hakumwambia Az Zubayr kwa mfano:  “Huyu asifanye tena kazi hizi, hii ni dhulma”, bali alinyamaza, na kunyamaza kwake ni kulikubalia na kuliridhia jambo kuwa liko sawa.   Vile vile, aliwaachilia Maswahaba wengineo kuwatumikisha wake zao huku akijua kuwa baadhi ya wake wako radhi kwa hilo na wengine hawako radhi, na kuwa jambo hili halina shaka yoyote.

 

Kadhalika, hayo yote yako ndani ya wigo wa kusaidiana katika wema na taqwa.  Lakini pamoja na hivyo, haina maana ya kuwa mume asimsaidie mkewe kwenye baadhi ya majukumu ya nyumbani na mengineyo kama alivyokuwa akifanya Rasuli, kwani hilo linaongeza pia penzi na huruma kati ya mke na mume.

 

Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alipoulizwa nini anafanya Rasuli anapokuwa nyumbani, alijibu:

 

"كَانَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي مِهْنَةِ أَهْلِهِ، فَإِذَا حَضَرتِ الصَّلَاةُ خَرَجَ إِلَى الصَّلَاة"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anawasaidia wake zake na kuwahudumia, na wakati wa swalaah unapofika, hutoka akaenda kuswali”.  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (676)]

 

Mume anatakiwa achunge hali ya mkewe, asimchoshe au kumbebesha asiyoyaweza.

 

 

Share