13-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: (ii) Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Asimpige Akamjeruhi Usoni Au Kumwambia Ni Mbaya
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume
12: Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: 9-Asimpige Akamjeruhi Usoni Au Kumwambia Ni Mbaya:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"وَلَا تَضْرِبِ اَلْوَجْهَ، وَلَا تُقَبِّحْ"
“Wala usipige uso, na wala usimkashifu (kumwambia) ni mbaya”. [Hadiyth Hasan. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2142), Ibn Maajah (1850), Ahmad (4/447) na An-Nasaaiy katika (Al-‘Ishrah) (269)]
Na anasema tena Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
"لَا يَجْلِدْ أَحَدُكُمُ امْرَأَتَهُ جَلْدَ الْعَبْدِ ثُمَّ يُجَامِعْهَا فِي آخِرِ الْيَوْمِ"
“Asimpige mmoja wenu mkewe kama anavyompiga mtumwa wake, kisha tena aje amuingilie usiku (linawezekana kweli hilo!!)”. [Al-Bukhaariy (4942) na Muslim (2855)]
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kamwe kumpiga yeyote katika wake zake wala mtu yeyote ila vitani. ‘Aaishah amesema:
"ما رَأَيْتُ رسولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَضْرِبُ خادمًا لَه قَطّ ولا امرأةً، ولا ضربَ بيدِهِ شيئًا قَطّ إلَّا أَنْ يُجَاهِدَ في سَبيلِ اللهِ"
“Sikuwahi kumwona kamwe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimpiga mtumishi wake wala mwanamke, na hakupiga kwa mkono wake kamwe kitu chochote isipokuwa anapokuwa kwenye Jihaad ya Allaah”. [Muslim (2328), At-Tirmidhiy katika Ash-Shamaail (331), An-Nasaaiy katika Al-‘Ishrah (281) na Ibn Maajah (1984)]
Faida:
Kumpiga mke ni jambo lililoruhusiwa kisharia ikiwa atakuwa mkorofi na akaacha kumsikiliza mumewe. Na hili linakuwa kwa mtiririko wa hatua zilizoelezewa na Allaah Ta’aalaa katika Kauli Yake:
وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا "
“Na wale ambao mnakhofu uasi wao wa ndoa, basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni (kipigo kisichodhuru). Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima Ni Mwenye Uluwa, Mkubwa wa Dhati, Vitendo na Sifa”. [An-Nisaa: 34]
Katika aayah hii, kupiga huko kuna vidhibiti vitatu:
1- Kuje baada ya kufeli kumwonya na kumhama kitanda.
2- Liwe pigo dogo la kuadabisha na si kubwa la kuvunja mfupa au saikolojia yake.
3- Mume aache kumpiga kama atatii amri.
