19-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: (ii) Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Amjengee Dhana Njema
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume
18: Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: 15-Amjengee Dhana Njema:
Allaah Ta’aalaa Amesema:
"لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا"
“Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao khayr?” [An-Nuwr: 12]
Na Amesema tena Allaah:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ"
“Enyi walioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi”. [Al-Hujuraat: 12]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا أَطَالَ أَحَدُكُمُ الْغَيْبَةَ فَلاَ يَطْرُقْ أَهْلَهُ لَيْلاً"
“Mmoja wenu akiwa mbali kwa muda mrefu, basi asimjie mkewe usiku”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (5244)]
Lakini, pamoja na dhana njema, mume anatakiwa awe chonjo, lakini pia azuie visababisho vya uharibifu na makosa ya kisharia.
Wanaume toka ukoo wa Haashim walipoingia nyumbani kwa Asmaa bint ‘Umays (Radhwiya Allaah ‘anhaa) ambaye ni mke wa Abu Bakr, na Abu Bakr alipoingia akachukizwa na hilo, alikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumweleza hilo, lakini alimwambia: “Sijaona lolote ila kheri”. Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"إِنَّ اللَّهَ قَدْ بَرَّأَهَا مِنْ ذَلِكَ"
“Hakika Allaah Amemtakasa kutokana na hayo (uchafu)”. Kisha akasimama juu ya mimbari akasema:
"لاَ يَدْخُلَنَّ رَجُلٌ بَعْدَ يَوْمِي هَذَا عَلَى مُغِيبَةٍ إِلاَّ وَمَعَهُ رَجُلٌ أَوِ اثْنَانِ"
“Baada ya leo hii, asiingie mtu yeyote kwenye nyumba ya mwingine naye hayuko, ila akiwa pamoja naye mtu mmoja au wawili”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (2173)]
Ushahidi hapa ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkanushia Asmaa uovu na akamwekea dhana njema, lakini pamoja na hivyo, aliwawekea wanaume marufuku ya kuingia nyumba za wengine wakati wao hawako ila wakiwa wamesuhubiana na mtu mwingine ili kutomruhusu shaytwaan kuvuruga mambo.
