02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa:Hukumu Zinazohusiana Na Mtoto Anayezaliwa: Je, Kichanga Huadhiniwa Kwenye Sikio Lake La Kulia Na Kuqimiwa Kwenye Sikio Lake La Kushoto?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
مِنْ أَحْكَامِ المَوْلُودِ
Hukumu Zinazohusiana Na Mtoto Anayezaliwa
02: Je, Kichanga Huadhiniwa Kwenye Sikio Lake La Kulia Na Kuqimiwa Kwenye Sikio Lake La Kushoto?
Suala hili limetajwa kwenye baadhi ya Hadiyth, lakini sanadi zake ni dhwa’iyf. Kati yake ni Hadiyth ya Abu Raafi’u aliyesema:
"رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أذَّنَ فِي أُذُنِ الحَسَنِ ابنِ عليٍّ حِينَ وَلَدَتْهُ فَاطِمَةُ"
“Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimwadhinia Al-Hasan bin ‘Aliy kwenye sikio lake wakati alipozaliwa na Faatwimah”. [Abu Daawuwd (5105), At-Tirmidhiy (1514) na Al-Haakim (3/179) kwa Sanad Dhwa’iyf). Al-Albaaniy alisema kwamba Hadiyth hii ina hadhi ya “Hasan Lighayrihi” katika Al-Irwaa (1173), lakini alijirudi baadaye na kusema ni Hadiyth Dhwa’iyf]
Kwa muktadha huu, Hadiyth hii ya Abu Raafi’u ni Dhwa’iyf, haifai kutumika mpaka ipatikane nyingine ya kuitilia nguvu. Ibn Al-Qayyim aliitaja Hadiyth hii pamoja na Hadiyth nyingine mbili katika Kitabu cha Tuhfatul Mawluwd (ukurasa wa 101), lakini Hadiyth hizo mbili pia ni Dhwa’iyf.
Imesuniwa Kukilambisha Kichanga Kitu Tamu:
Ni vizuri kuitafuna au kuisaga tende na kumsugulia kwayo kichanga ndani ya kinywa. Toka kwa Abu Muwsaa amesema:
"وُلِدَ لِي غُلاَمٌ، فَأَتَيْتُ بِهِ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، فَسَمَّاهُ إِبْرَاهِيمَ، فَحَنَّكَهُ بِتَمْرَةٍ، وَدَعَا لَهُ بِالْبَرَكَةِ، وَدَفَعَهُ إِلَيَّ "
“Niliruzukiwa mtoto wa kiume, nikaenda naye kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), (akamchukua) na akampa jina la Ibraahiym kisha akamlambisha tende. Lakini pia alimwombea barakah, halafu akanirudishia”. [Mtoto alikuwa wa kwanza wa Abu Muwsaa].
