03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa:Hukumu Zinazohusiana Na Mtoto Anayezaliwa: Imesuniwa Kumfanyia ‘Aqiyqah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
مِنْ أَحْكَامِ المَوْلُودِ
Hukumu Zinazohusiana Na Mtoto Anayezaliwa:
03: Imesuniwa Kumfanyia ‘Aqiyqah:
Asili ya neno “Aqiyqah”, ni nywele zinazokuwepo kwenye kichwa cha mtoto baada ya kuzaliwa. Na mbuzi au kondoo anayechinjwa kwa ajili yake anaitwa ‘aqiyqah. Kadhalika, chinjo lenyewe la mbuzi au kondoo linaitwa ‘aqiyqah.
‘Aqiyqah hii imesuniwa kufanywa siku ya saba ya kuzaliwa mtoto. Baba yake atamchinjia kondoo au mbuzi wawili kama ni wa kiume, na mbuzi mmoja au kondoo mmoja kama ni wa kike.
Toka kwa Salmaan bin ‘Aamir Ad-Dhwabiy amesema: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَعَ الْغُلاَمِ عَقِيقَتُهُ، فَأَهْرِيقُوا عَنْهُ دَمًا، وَأَمِيطُوا عَنْهُ الأَذَى"
”Sambamba na kila mtoto (anayezaliwa), pana mnyama wake wa ‘aqiyqah. Basi mwageni damu kwa niaba yake, na mwondosheeni adha”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma].
.
Naye ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa), amesema:
عَنِ اَلْغُلَامِ شَاتَانِ مُكَافِئَتَانِ، وَعَنْ اَلْجَارِيَةِ شَاةٌ "
“Mtoto wa kiume achinjiwe kondoo wawili wenye umri sawa, na wa kike kondoo mmoja”. [At-Tirmidhiy (1513) na Ahmad (6/31). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Al-Irwaa (1166)]
Kadhalika, Samurah amesema: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"الغُلاَمُ رَهِينَةٌ بِعَقِيقَتِهِ ، تُذْبَحُ عَنْهُ يَوْمَ سَابِعِهِ ، وَيُحْلَقُ ، وَيُسَمَّى"
“Mtoto ni rehani kwa mnyama wake wa aqiyqah, huchinjiwa siku yake ya saba, hunyolewa, na hupewa jina”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2838), An Nasaaiy (7/166), At-Tirmidhiy (1522), Ibn Maajah (3165) na wengineo].
Imesuniwa Kuila, Kulisha Na Kuigawa Nyama Aa ‘Aqiyqah.
Mnyama wa ‘aqiyqah ni lazima awe na vigezo sawa na mnyama wa ‘udh-hiyah kama kuwa mbuzi au kondoo asiye na kasoro yoyote na mfano wa hayo.
