Imaam 'Abdul-'Aziyz Bin 'Abdillaah Bin Baaz (رحمه الله)

 

Imaam 'Abdul-'Aziyz Bin 'Abdillaah Bin Baaz (Rahimahu-Allaah)

 

(12 Dhul-Hijjah 1330 H – 27 Al-Muharram 1420 H)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

“Moja kati ya pigo kubwa sana linalowafika waja wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa), ni kufiliwa na Mwanachuoni wao (‘Aalim).  Ummah wa Kiislamu umempoteza Mwanachuoni maarufu sana, Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Ibn Baaz.  Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amrehemu na Amlaze mahala pema, Aamiyn.”

[Shaykh Muhammad As-Subayl-Imaam-Msikiti Mkuu- Makkah].

 

 

Historia Fupi 

 

Shaykh Ibn Baaz alizaliwa katika mji wa Riyadh, tarehe 12-Dhul-Hijjah-1330 H katika nchi ya Saudi Arabia. 

 

Shaykh Ibn Baaz alizaliwa akiwa na macho yake mazuri, na aliwahi kusoma elimu yake ya mwanzo akiwa hana matatizo yoyote.  Katika mwaka wa 1346 H akiwa na umri wa miaka kumi na sita, alipatwa na maradhi ambayo yalikuwa ndiyo sababu ya kukosa kuona kwake.  Kufikia mwaka wa 1350 H akiwa na umri wa miaka ishirini tu, alipatwa na upofu, na akawa haoni kabisa.

 

 

Katika Kutafuta Elimu

 

Shaykh Ibn Baaz alianza kutafuta elimu ilhali yungali ni mdogo sana.  Kabla ya kubaleghe kwake, alikuwa tayari ni mwenye kuihifadhi Qur-aan yote.  Alizidi kuzama katika elimu ya shari’ah na lugha, na vile vile alivihifadhi kwa moyo vitabu vingi vya Hadiyth.

 

 

Waalimu Wake

 

Shaykh Ibn Baaz aliwahi kusomeshwa na Ma’ulamaa mashuhuri sana.  Kati ya hao wakiwa ni:

 

·     Shaykh Muhammad Ibn ‘Abdil-Latwiyf Ibn ‘Abdir-Rahmaan Ibn Hasan Ibn Ash-Shaykh Muhammad Ibn ‘Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah).

 

·     Shaykh Sa’ad Ibn Hammaad Ibn ‘Ariyq (Qaadhi mkuu wa Riyadh).

 

·    Shaykh Swaalih Ibn ‘Abdul-‘Aziyz Ibn ‘Abdir-Rahmaan Ibn Hassan Ibn Muhammad Ibn ‘Abdul Wahhab (Qaadhi mkuu wa Riyadh).

 

·     Shaykh Hammaad Ibn Faaris (Naibu mkuu wa nyumba ya Hazina Riyadh).

 

·     Shaykh Sa’ad Ibn Waqqaas Al-Bukhaariy.

 

·    Shaykh Muhammad Ibn Ibraahiym Ibn ‘Abdil-Latwiyf Aaluush Shaykh (Aliyekuwa Mufti wa Saudi Arabia). Shaykh Ibn Baaz alisoma kutoka kwake matawi yote yaliyohusiana na shariy’ah ya Kiislamu kwa kipindi cha miaka kumi.

 

 

Kazi Alizozifanya – Na Nyadhifa Alizozishikilia

 

·     Qaadhwiy wa wilaya ya Al-Kharaj kwa miaka 14.  

 

·     Alisomesha katika Al-Mahad Al-‘Ilmiy (Riyadh kwa mwaka mmoja).

 

·    Amesomesha Fiqh, Uswuul Al-Fiqh na Tawhiyd katika chuo cha shariy’ah kwa miaka saba.

 

·  Alipewa cheo cha unaibu mkuu wa Chuo Kikuu Cha Kiislamu huko Madiynah katika mwaka wa 1381 H, mpaka kufikia mwaka wa 1390 H.

 

·   Alishikilia wadhifa wa Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Madiynah kutoka 1390 AH mpaka 1395 H.

 

·   Katika mwaka wa 1414 H, alichaguliwa kama Mufti Mkuu wa Saudi Arabia.  Alikuwa ni Rais wa kamati ya Ma’ulamaa wakubwa, pamoja na kuwa Rais wa utendaji wa mas-alah ya utafiti wa kisayansi, na Hukmu za kishariy’ah.

 

·    Alikuwa ni Rais wa Baraza Kuu la Misikiti-Duniani.

 

·  Mpaka kufa kwake, Shaykh Ibn Baaz alishikilia nyadhifa nyingi zaidi zilizohusiana na shariy'ah katika serikali ya Saudi Arabia.

 

 

Vitabu Vyake

 

Katika kujishughulisha kwake, Shaykh ametumia muda mrefu sana katika kuandika vitabu vya Dini vilivyogusia mada mbali mbali.  Vitabu ambavyo vitatumika kwa manufaa ya Ummah wa Kiislamu kwa jumla.

 

Shaykh Ibn Baaz alishinda tuzo kubwa la mchango wa Wanachuoni wa Kiislamu duniani, nayo ni tunzo ya Malik Fayswal ambayo aliipata katika mwaka wa 1402 H, kwa kazi zake nzuri kwa ajili ya Ummah wa Kiislamu. 

 

Shaykh amewahi vile vile kujenga vituo vya Kiislamu pamoja na Misikiti na vituo vya elimu katika sehemu mbali mbali kutokana na kazi zake.

 

Shaykh amepata wafuasi wengi, na ametoa Wanachuoni wazuri kutoka sehemu nyingi za dunia ambao kwa hakika wamefaidika kutokana na elimu na busara zake. 

 

Kwa kweli, Shaykh alikuwa ni mchaji Allaah aliyejitolea kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa), Mwanachuoni mzuri wa Kiislamu, na hapana shaka yoyote, kifo chake ni khasara kubwa kwa Ummah wa Kiislamu.  Tunamuomba Rabb (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amrehemu Imaam huyu mkuu wa nyakati hizi zetu za leo (Aamiyn). 

 

 

Maisha Yake Ya Kila Siku

 

Shaykh Ibn Baaz alikuwa akianza siku yake kwa kuswali Tahajjud nyumbani kwake pamoja na ahli yake.  Baada ya kuisikia adhaan ya Al-Fajiri, alikuwa anakwenda kwenye ukumbi wake wa mikutano, na kuswali Sunnah ya Qabliyah ya Swalaatul-Fajr, kisha akilalia ubavu wake wa kulia na kuanza kuzisoma du’aa Masnuun (Du’aa zilizothibiti kutoka kwa Nabiy).  Kisha huelekea Msikitini kwa Swalaah ya Al-Fajr, na anapomaliza huendelea na du’aa zake na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kabla ya kuanza kuwasomesha wanafunzi wake. Kisha hula chakula cha Asubuhi pamoja na marafiki zake, wanafunzi, na wageni wake huko nyumbani kwake.  Halafu huelekea katika maktaba yake ambako wasaidizi wake, pamoja na makatibu, huwa wanamsubiri kwa maagizo yake juu ya mas-alah mbali mbali.

 

Shaykh alikuwa mara nyingi akiiswali Swalah ya Adhuhuri katika Msikiti wa Riyadh, au mara nyengine katika maktaba yake ambayo alishajengewa Msikiti wa Jami’ah hapo hapo.  Akishamaliza Swalaah ya Adhuhuri, alikuwa anarudi katika maktaba yake, na kufanya kazi mbali mbali. Alikuwa na tabia ya kuondoka mwisho kabisa baada ya wafanyakazi wote kuelekea majumbani kwao. 

 

Ilikuwa ni tabia yake kuwaalika marafiki zake, na watu kwa jumla kwa chakula cha mchana huko nyumbani kwake.  Baada ya kuswali Swalaah ya Alasiri, Shaykh alikuwa ana tabia ya kujipumzisha kidogo.  Alikuwa akiswali Swalah ya Maghrib Msikitini, na kisha mamia ya watu humsubiri katika ukumbi, ambako alikuwa akitoa mihadhara, pamoja na kuyajibu masuala mbali mbali.  Halafu baina ya Adhaana na Iqaamah ya Swalaah ya ‘Ishaa, alikuwa akitoa khutbah fupi.

 

Katika kujihimiza sana na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Shaykh alikuwa akifunga katika siku za Jumatatu na Alkhamiys, na akipendelea kusafiri katika siku hizi, na vile vile katika siku ya Jumamosi.  Akipendelea sana kusikiliza radio, na akisomewa magezeti ya kila siku ili apate kujua yale yanayoendelea ulimwenguni.  Katika tatizo lolote, alikuwa akitafuta ufumbuzi kutokana na Qur-aan na Sunnah, na alikuwa hajinasibishi na dhehebu lolote lile. 

 

Katika siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhwaan, Shaykh alikuwa akikaa Makkah, na katika siku za Hajj, alipendelea kuwa karibu na watu kwa kuwafunza, kuwapa mawaidha na kuwaongoza katika njia ya hakki.  Baada ya Hajj, alikuwa anakwenda Twaaif kwa mapumziko ya siku kidogo.  Popote alipokuwepo, kazi yake ya Da’awah iliendelea kama kawaida.

 

Hakika Shaykh Ibn Baaz pamoja na kukosa kuona (upofu) lakini hakunyimwa elimu. Alikuwa Mwanachuoni, ‘Aalim Aliyejaa bahari ya elimu, Faqiyh, Qaadhwiy, Mufti, Mchaji Allaah, Kipenzi, Mkarimu. Ametuachia hazina kubwa ya elimu isiyo mithali.

 

Shaykh Ibn Baaz alifariki mwaka mmoja na Mwanachuoni mkubwa wa Ummah huu; Shaykh Al-Albaaniy, kisha baada ya chini ya miaka miwili akafuatiwa na kifo cha Mwanachuoni mwengine mkubwa kabisa, Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn. Ilikuwa pigo kubwa kwa Ummah wa Kiislamu kupoteza Wanachuoni watatu wakubwa kwa wakati wa karibu karibu.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amruzuku yeye na Wanachuoni wenzake Jannat Al-Firdaws. Aamiyn

 

Share