Maulidi: Historia Yake, Hukmu Na Kauli Za 'Ulamaa

 

Maulidi – Historia Yake, Hukmu Na Kauli Za 'Ulamaa

 

Abuu 'Abdillaah

na

 Abuu Al-Khatwaab

 

 Alhidaaya.com

 

 

BismiLlaahi Rahmaani Rahiym

 

1.0 Utangulizi

 

Huu ni mwito kwa kila Muislamu anayetaka kufikia kwenye haki na awe ni mwenye kumuabudu Allaah kwa uoni na elimu ya wazi kabisa.

 

Ndugu Waislamu! Kwa yakini kila mmoja wetu ana mapenzi makuu katika vifua vyetu kwa Mtume wetu mtukufu na kipenzi na ruwaza njema na Imamu wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pamoja na familia yake na Swahaba zake na wenye kuzifanyia kazi Sunnah zake na kufuata uongofu wake mpaka Siku ya Qiyaamah. Mahaba haya ni msingi mkuu wa Dini yetu na yeyote asiyempenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakuwa kafiri na tunajiweka mbali sana na Allaah kwa kumchukia na kumbughudhi, na hiyo ni sifa ya wanafiki. Allaah Anatuelezea kuhusu wao: 

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا ﴿١٤٥﴾

Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika moto; na wala hutompata kwa ajili yao mwenye kunusuru. [An-Nisaa: 145].

 

Tunawekea makala haya mafupi kwa unyenyekevu baina ya mikono na macho yenu ili muyasome kwa uoni, ikhlasi na kuwa na nia ya kutaka kuifikia haki na kila mtu ayasome kwa ajili ya kupata mazingatio na bila ya kufuata Wanachuoni wa nchi zao au wengineo kimbumbumbu au madhehebu yao au ada na mazoea yao. Ikiwa yaliyo ndani ni haki tuyakubali kwa moyo mkunjufu na hivyo kwayo tuende katika kumtii Allaah na Nabiy Wake, ambao wametuamrisha kufuata haki na ikiwa kuna batili ndani yake au makosa, tunakushuhudisha kwa Allaah usiwe ni mwenye kufuata hayo kwani sisi hatufai kufuata isipokuwa yale ya haki ambayo yana dalili katika shari‘ah yetu tukufu.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuwafikishe sote katika kufuata njia nyoofu ambayo ametuchagulia Nabiy wetu na Allaah Ndiye Mwenye kutia tawfiki na Kwake ndio mategemeo yetu.

 

 

2.0 Historia

 

Yeyote mwenye kutazama maisha ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na historia ya Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum), Taabi‘iyna na waliowafuata kwa wema mpaka kufikia zaidi ya mwaka wa 350 Hijri hatumuoni hata mwanachuoni mmoja wala mahakimu (viongozi) na wala watu wa kawaida waliokuwa wakifanya mawlid au wakaamrisha au wakahimiza au wakazungumza juu yake. Amesema al-Haafidhw as-Sakhawiy: “Shughuli za kufanya Mawlid matukufu hayakupokelewa na watangu wema (Salafus Swaalih) wa karne tatu bora za mwanzo. Kwa hakika jambo hili lilizuliwa baada yake.” [Imenukuliwa kutoka kwa Subulul Hudaa war Rashaad cha As-Salihiy, Mj. 1, uk. 439].

 

Suala la sisi kujiuliza ni kuwa; Je, haya Mawlid yalianza lini? Jawabu ya suala hili kwa mwanachuoni wa Ki-Sunnah, Al-Imaam al-Maqriyziy:

 

“Katika kipindi cha uongozi wa Faatwimiyyuun (hawa walikuwa ni Rawaafidh (Mashia) katika kipote cha Ismailiyyah [Makoja] katika nchi ya Misri) walikuwa wanachukuwa hii ni misimu ya sherehe ambapo walikuwa wakiwakunjulia hali za raia zao na kuwakithirishia neema. Na walikuwa hawa watawala wa Faatwimiyyuun katika mwaka mzima wana misimu ya sherehe na Idi zao nazo ni kama zifuatazo: Msimu wa kichwa cha mwaka, Msimu wa mwanzo wa mwaka, Sherehe za ‘Aashuraa, na Mawlid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Mawlid ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na Mawlid ya Hasan na Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhuma), na Mawlid ya Faatwimah az-Zahraa (Radhwiya Allaahu ‘anha), na Mawlid ya kiongozi wao aliye hai kwa wakati ule, usiku wa kwanza wa Rajab, na usiku wa kati ya Rajab, na Mawlid ya usiku wa Ramadhwaan na mwisho wa Ramadhaan na Msimu wa 'Iydul Fitwr na Msimu wa 'Iydul Adh-ha na Idi ya Ghaadir, Msimu wa ufunguzi wa Ghuba na Siku ya Nairuuz na Siku ya Ghatas na Siku ya Mazazi, na Siku ya Vipandio, Kis-wa (nguo) ya Msimu wa Kusi na Kaskazi, Alhamisi ya Adasi na Siku ya Ubatizo.” [Al-KhutwatMj. 1, uk. 490 na baada yake]. na amesema tena katika kitabu chengine: “Na katika mwezi wa Rabi’ul Awwal walijilazimisha watu kuwasha kandili usiku katika njia zote na vichochoro vyake huko Misri.”

 

Na amesema tena al-Maqriiziy katika maudhui nyengine: “Shughuli za Mawlid ya Nabiy mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa zikifanyika rasmi kama desturi yake katika mwezi wa Rabi’ul Awwal.” Kila mmoja anatakiwa azingatie jinsi gani Mawlid yalivyoanzishwa pamoja na uzushi mkubwa mfano: Uzushi wa kukataa na kuchupa mipaka juu ya familia ya Mtume kwa kusimamisha mawlid ya ‘Aliy, Faatwimah, Hasan na Husayn.

 

Uzushi wa kusherehekea Idi ya Nayruuz, na Idi ya Ghatas na kuzaliwa kwa Masihi nazo ni Idi za Wakristo. Amesema Ibn Turkumani kuhusu hizi Idi za Wakristo: “Na miongoni mwa uzushi inayoleta hizaya ni wanaofanya Waislamu katika siku ya Nayruuz ya Kikristo na misimu yao mengine na siku kuu ('Iyd) kwa kupeana chakula kwa wingi. Na sadaka ya chakula isiyokubalika itarudi kwa mwenye kutoa kwa haraka au baadae. Na kwa uchache wa tawfiki na kufaulu ni yale wanayofanya Waislamu waovu kwa inayotambuliwa kama siku ya mazazi (yaani kuzaliwa kwa 'Iysaaa).” [Al-Lam‘i Fil Hawaadith wal Bid’ah, Mj. 1, uk. 293 – 316]. Na imenukuliwa kutoka kwa Wanachuoni wa Hanafiyyah kwamba yeyote ambaye atafanya mambo yaliyotangulia atakuwa kafiri mfano wao (hao Wakristo). Na wakataja idadi za Idi kadhaa za Wakristo ambao Waislamu walio wajinga wanashiriki, na jinsi zilivyo uharamu wake katika Kitabu na Sunnah na yale misingi ya kishariy'ah yaliyo kamili.

 

Watu wa kwanza kuzua kile kinachoitwa Mawlid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Bani ‘Ubayd ambao walikuwa wakijulikana kama Faatwimiyyuun. Haya yametajwa na Wanachuoni wengi mfano Mufti wa Misri wa zamani, Shaykh Muhammad Bakhiit al-Mutii‘y katika kitabu chake Ahsanul Kalaam Fi maa Yata‘alaq Bis Sunnah wal Bid‘ah Minal Ahkaam; Shaykh ‘Aliy Mahfuudh katika kitabu chake Al-Ibda‘ Fiy Madh-har al-Ibtidaa‘; Shaykh Isma‘iyl al-Answaariy katika kitabu chake Al-Qawlul Fasl Fiy Hukmil Ihtifaal Bi Mawlid Khayrir Rasuul.

 

“Wa mwanzo walioyazua Mawlid huko Cairo ni watawala wa Kifaatwimiyyah (Mashia) katika karne ya nne. Walizua Mawlid aina sita: Mawlid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mawlid ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Mawlid ya Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anha), Mawlid ya Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Mawlid ya Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na Mawlid ya Khalifa aliyekuwepo.” [‘Ali Mahfuudh katika kitabu chake al-Ibda‘ Fii Madh-har al-Ibtidaa‘, uk. 251].

 

Je, Wanachuoni wamesema nini kuhusu hii Dola ya Faatwimiyyuun ‘Ubaydiyyah ambayo imeanzisha jambo hili (Mawlid ya Nabiy)? Amesema Imaam Shaamah, mwana-historia na Muhaddith (aliyeboboea katika mas-alah ya Hadithi za Nabiy [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam]), mwandishi wa kitabu ar-Rawdhatayn Fiy Akhbaar Dawlatayn, uk. 200 – 202 kuhusu Faatwimiyyuun ‘Ubaydiyyah: “Wao walijidhihirisha kwa watu kuwa wao ni masharifu (watukufu) kutoka kwa Faatwimah hivyo wakamiliki na kutawala ardhi na kuwatendesha nguvu waja. Na wametaja kipote cha Wanachuoni wakubwa kuwa wao hawakustahiki hilo na nasaba yao si sahihi bali walikuwa wanajulikana zaidi kwa banu ‘Ubayd. Na baba wa ‘Ubayd alikuwa ni katika kizazi cha wakanaji Allaah na Mmajusi na inasemekana kuwa babake alikuwa Myahudi mfua vyuma kutoka Shaam. Jina la huyu ‘Ubayd lilikuwa ni Sa‘iyd, lakini alipofika Morocco alijiita ‘Ubaydullah na akajidai kuwa yeye ni katika ukoo wa ‘Alawi Faatwimiy na madai yake ya nasaba hiyo siyo sahihi. Yeye hakutajwa na yeyote miongoni mwa wajuzi wa nasaba za ‘Alawi, kipote kikubwa cha Wanachuoni wametaja kinyume cha hayo. Alijinasibisha na Bani Mahdiyyah wa Morocco, naye alikuwa Zindiyq muovu, adui wa Uislamu na alijidhihirisha Ushia wake. Alikuwa na hima ya kuiondoa mila ya Kiislamu pamoja na kuwaua mafaqihi wengi pamoja na Wanachuoni wa Hadiyth. Kusudio lake kubwa lilikuwa kuwaondosha kabisa ili dunia ibaki na wanyama pekee na hivyo kumakinika katika kuleta uharibifu katika itikadi zao na kuwapoteza lakini Allaah Anaitimiza nuru Yake japokuwa watachukia makafiri.” 

 

Kizazi chake kiliinukia katika hilo huku wakijitokeza wakati kukiwa na fursa na isipokuwa hivyo walikuwa wakijificha na kufanya vituko vyao kwa siri. Walinganizi wake walitumwa katika nchi yote huku wakiwapoteza wale wanaoweza miongoni mwa waja. Balaa hii ilibakia kwa Uislamu kuanzia mwanzo wa Dola yao mpaka mwisho wake yaani Dhul-Hijjah 299 hadi 567 Hijri.

 

Katika siku zao za utawala hawa Rawaafidh (Mashia) waliongezeka sana na hivyo wakawa wanahukumu watu kwa kuwawekea vikwazo na wakaweza kuharibu itikadi za mapote ya watu waliokuwa wakiishi katika majabali na mapango ya Shaam kama Nusayriyyah, Druze na Hashashiyyun (Assassins), wote wakiwa aina moja na wao wenyewe. Waliweza kuwatumia kwa sababu ya udhaifu wa akili zao na ujinga wao, hivyo kuwapatia fursa Wazungu (Crusaders – watu wa msalaba) kuziteka ardhi za Shaam na Bara Arabu mpaka Allaah Alipowapatia Waislamu ushindi chini ya uongozi wa Swalaah ud Diyn Hasan al-Ayyubi ambaye aliweza kuzirudisha nchi hizo kwa Waislamu.

 

Makhalifa 14 walipita, ambao walikuwa wanajiita masharifu na nasaba yao ni kutokana na Majusi au Mayahudi mpaka likawa maarufu baina ya watu wa kawaida hivyo kuiita dola hiyo, Dola ya Faatwimah na Dola ya ‘Alawi na ilihali uhakika ni Dola ya Kimajusi au ya Kiyahudi wakanaji Allaah.

 

Na miongoni mwa uovu wao ni kuwa walikuwa wakiwaamrisha makhatibu kwa hilo (yaani wao ni Alawiyyah Faatwimiyyuun) na hayo yalikuwa yakisemwa juu ya minbar na wakiandika katika kuta za Misikiti na sehemu nyinginezo. Na alihutubu yeye mwenyewe mtumishi wao kwa jina Jawhar, aliyeteka nchi ya Misri na kujenga mji wa Cairo. Alisema ndani yake: “Ee Rabb mswalie mja wako na rafiki yako tunda la Unabii na dhuria wako mwenye kuongoza muongofu anayepelekesha mambo. Naye ni Abi Tamiym Imam Mu‘iz-ud-Diinil Llah, Amiri wa Waumini kama ulivyowaswalia baba zake walio tohara na waliomtangulia kwa kuchaguliwa, maimamu waongofu.” Amesema uongo adui wa Allaah, hakuna khayr kwake wala kwa watangu wake wote wala kwa dhuria wake waliobakia na kizazi cha Unabii tohara miongoni mwao.

 

Na yule mwenye lakabu ya Mahdi, laana ya Allaah iwe juu yake aliwachukuwa wajinga na kuwasalitisha kwao wale wenye fadhila. Alikuwa akiwatuma kwenda kuwachinja mafakihi na Wanachuoni katika firasha zao. Na akawasaliti Waislamu kwa Warumi na alikuwa na ujeuri mwingi na kuchezea mali na kuwaua watu. Alikuwa na kipote cha walinganizi (ma-Du‘aat) wake waliokuwa wakifanya kazi ya kuwapoteza watu kwa uwezo wao wote. Wao walikuwa wakiwaambia baadhi ya watu: “Huyo ni Mahdi mtoto wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na dalili (huja) ya Allaah kwa viumbe vyake.” Na kwa wengine: “Huyu ni Rasuli wa Allaah na dalili ya Allaah.” Na kwa wengine: “Yeye ni Allaah, Muumbaji, Mwenye kuruzuku.” Hapana Rabb muabudiwa wa haki ila Allaah tu, Naye Hana mshirika, Ametukuka na Hana upungufu wala kasoro aina yoyote kwa yale wanayoyasema madhalimu kwa kiburi kikuu. Alipoangamia alichukua hatamu za uongozi mtoto wake anayeitwa, Qaaim, naye alizidisha shari yake juu ya uovu wa babake maradufu. Akatoka na kuwatusi Rusuli na alikuwa akinadi masokoni na sehemu nyenginezo: “Mlaanini ‘Aishah na mumewe. Mlaanini pango na vinavyounganishwa.”

 

Ee Allaah! Mswalie Nabiy Wako na Swahaba zake na wakeze walio twahara na uwalaani hawa makafiri walioasi na kuvuka mipaka katika ukanaji wa Allaah na Uwarehemu waliopambana nao na ikawa ndio sababu ya kuing’oa mizizi na utawala wao. Waislamu katika zama za utawala wao walipata dhiki na shida kubwa kwa ukatili, kiburi na ujeuri wao uliochupa mipaka.

 

Na juu ya Mawlid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyoona asli yake na mwanzilishi wake ni kutokamana na Baatwiniyyuun (Faatwimiyyuun) waliokuwa na asli ya Kimajusi Kiyahudi waliohuisha mwito wa watu wa msalaba. Na hapa tunawaambia ya kwamba: Je, inajuzu na kusihi kuifanya chimbuko letu katika 'Ibaadah ni kutoka kwa watu hawa? Nasi tunarudia mara nyingine tena kuwa zile karne zilizo bora na kufadhilishwa ambazo waliishi watangu wetu wema hakukuwa na athari wala kufanywa mfano wa hizi 'Ibaadah. Hawakufanya wao wala wale waliokuwa na uadui nao na hata wale wajinga katika watu wa zama hizo na watu wa kawaida. Basi nasi hatujishughulishi katika yale waliyoyafanya na kujishughulisha nayo wao.

 

Katika kuelezea yalivyoanza Mawlid, 'Abdulla Saleh Farsy anasema:

 

"Walioanza Mawlid ni watu wenye Madhehebu za Kishia, hawa Shia Ismailiya walizitawala nchi za Kisuni tangu mwaka 297 H (909) mpaka 567 H (1171) (muda wa miaka 270).

 

Walipotoka katika nchi hizo waliacha hiyo ada yao ya kumsomea Mawlid Nabiy na Imamu zao. Basi Suni wakaendeleza Mawlid ya Nabiy, wakayawacha yote mengine.

 

Mawlid ya Mwanzo Rasmi Kusomwa na Suni:

 

Mawlid ya mwanzo Rasmi yalisomwa na Suni ni Mawlid aliyokuwa akiyasoma Mfalme Mudhaffar Din- Mfalme wa kaskazi ya Iraq ambaye alikuwa shemeji wa mfalme mkubwa wa Kiislamu, Mfalme Salahud Din (Saladin - maarufu). Mawlid makubwa kabisa hayo. Yalikuwa yanahudhuriwa na watu wa pande zote zilizokuwa karibu na hapo, kwa shangwe kubwa kabisa lisilokuwa na mfano.

 

Mfalme huyo alizaliwa mwaka 549 H (1154 wa kizungu); na akatawala hapo mwaka 586 H (1190) na akafa 630 H (1233) - miaka mia saba na khamsini na sita (756) kwa tarikhi ya kiislamu, na miaka mia saba na thalathini na tatu kwa tarikhi ya Kizungu. Basi ada ya kusoma Mawlid haikuanza miaka mingi sana. (Tafsiri ya Mawlid Barzanji - Kadhi Sheikh Abdulla Saleh Farsy, Zanzibar, Uk.(iv) )

 

 

3.0 Mazazi Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) 

 

Ni maarufu kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa baada ya kuaga dunia babake. Lakini wana-taariykh wametofautiana kuhusu mwaka na mwezi aliozaliwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Safi-ur-Rahmaan Mubarakpuri, mwanachuoni aliyepata zawadi ya kwanza katika mashindano ya kuandika historia ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameandika yafuatayo katika kitabu chake: “Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bwana wa Rusuli, alizaliwa katika mtaa wa Bani Haashim katika mji wa Makkah, Jumatatu, tarehe 9 Rabi’ul Awwal, mwaka ule ule wa ndovu na miaka arobaini baada ya utawala wa Kisra (Khsru Nushirwan) yaani tarehe 20 au 22 Aprili 571 BI (Baada ya kuzaliwa ‘Iysaa), kulingana na alivyohakikisha mwanachuoni mkubwa Muhammad Sulayman al-Mansourpuri...” [Ar-Rahiyqul Makhtuum, uk. 62].

 

Sirajur Rahmaan katika kitabu chake amesema:

 

“Tukio hili la ndovu lilitokea mwezi wa Al-Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa siku hamsini na tano, kama wanavyothibitisha Wanachuoni wengi. Nayo inawafiki mwisho wa mwezi wa Februari au mwanzo wa Machi mwaka 571 M.” [Al-Mustafa, nakala ya AMYO, 1993, uk. 11].

 

Kutokana na mapokezi hayo mawili tunaweza kuiweka tarehe ya kuzaliwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baina ya tarehe 25 Swafar na tarehe 25 Rabiy’ul Awwal na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anajua zaidi.

 

‘Afiyf ‘Abdul-Fattaah at-Twabbarah na Abul Hasan ‘Ali wamesema katika vitabu vyao kuwa:

“Aminah alizaa alfajiri siku ya Jumatatu tarehe 9 au 12 ya Rabiul Awwal, mwaka wa ndovu. Mahmuud Pasha, maarufu kutoka Misri, amefanya hesabu ya tarehe ya kuzaliwa na kupata kuwa ni Jumatatu tarehe 20 Aprili mwaka 571 BI, inayokwenda sambamba na tarehe 9 Rabiul Awwal.” [Ma‘al Ambiyaa Fil Qur-aanil Kariym, uk. 338 na Muhammad RasulluLLaah, uk. 91].

 

Inaonekana kuwa Wanachuoni na wanahistoria wa wakati huu wamechukua tarehe 9 ya Rabi’ul Awwal kuwa ndiyo aliyozaliwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Siyratun Nabiy na The Life of the Prophet].

 

Hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kuificha siku hiyo ya kuzaliwa kwake Anaijua Yeye mwenyewe. Hivi sasa watu wamevuka mipaka katika kuisherehekea siku na mwezi huo na bado kuna tofauti kwa siku ya kuzaliwa kwake.

 

Jambo ambalo linajulikana kwa uhakika bila ya utata wowote ni siku aliyozaliwa, kwani haya aliyasema kwa kauli ambayo haina maana mbili.

 

Imepokewa kwa Abu Qataadah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa juu ya kufunga (Swawm) ya Jumatatu. Akasema: “Hiyo ilikuwa ni siku niliyozaliwa na ndio siku niliyopatiwa Utume au niliyoteremshiwa Wahyi.” [Muslim].

 

Na ili tuwe tumemfuata vilivyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Sunnah zake inatakiwa tuwe tunafunga siku ya Jumatatu kila wiki na jambo hilo litakuwa linatukaribisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

 

4.0 Kubainisha Hukumu Ya Mawlid

 

Jueni, Allaah Aturehemu sote ya kwamba Mawlid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayapo katika shariy'ah na hakuna dalili katika Kitabu wala Sunnah wala Ijma’a wala Qiyaas inayoonyesha usahihi wa jambo hilo. Na hakuna pia hata dalili ya kiakili wala kimaumbile, na jambo lolote linalokuja kwa njia hii basi huwa ni uzushi muovu usiotakiwa katika Dini.

 

Amesema al-Haafidhw Ibn Rajab“Na asili ya Bid‘ah ni ile inayozuliwa na isiyokuwa na asili katika shariy'ah inayokuwa ni dalili kwayo.” [Jaami‘ul-‘Uluum wal Hikam, Mj. 2, uk. 127].

 

Na amesema tena: “Na chochote kinachozuliwa na yeyote na kisha kikinasibishwa na Dini na kikawa hakina asli (misingi) katika Dini atarudishiwa mwenyewe. Huo utakuwa ni upotevu na Dini ipo mbali na kitu hicho. Ni sawa ikiwa hilo limefungana na mambo ya ki-itikadi au amali (matendo) au kauli zilizo wazi na zilizofichika.” [Jaami‘ul-‘Uluum wal Hikam, Mj. 2, uk. 128].

 

Bid‘ah katika lugha ni “Kila lenye kuzuka (uzushi)” na katika shariy'ah ya Kiislamu ni “kuzuka kitu katika Dini baada ya kukamilika” (yaani baada ya mafunzo ya Nabiy [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam]) [Said Musa, Majadiliano Juu ya Mawlid, Chapa ya Kwanza, 1985, Dar es Salaam, uk. 1}.

 

Ufisadi na uharibifu wa kuruhusu jambo hili upo wazi kabisa, na hapa tunanukuuu baadhi ya nukta katika mas-ala hayo. Nayo ni kama yafuatayo:

 

Ya Kwanza: Jambo hili halikufanywa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala hakuamrisha lifanywe wala hawakufanya Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wala hata mmoja miongoni mwa Tabi‘iyna wala waliowafuata wala hawakufanya Waislamu katika zama zilizokuwa bora za mwanzo. Na hizi zilikuwa ni zile karne tatu za mwanzo kuanzia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka mwaka 300 Hijri. Jambo hili lilianzishwa na watu kama tulivyotangulia kueleza waliokuwa karibu na ukafiri kuliko Imani nao ni Baatwiniyyuun na baada ya karne hizi tatu bora.

 

Jambo hili likifanywa kwa kukaririwa ni kwamba yule mwenye kufanya anaingia katika adhabu kali aliyoahidi Allaah Aliyetukuka kwa mwenye kufanya. Allaah Anasema:

 

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿١١٥﴾

Na atakayempinga Rasuli baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini; Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Jahannam. Na uovu ulioje mahali pa kuishia.  [An-Nisaa: 115].

 

Hivyo, yule anayefanya Mawlid bila shaka hafuati njia ya Waumini miongoni mwa Swahaba, Tabi‘iyna na wanaowafuatia.

 

Ya Pili: Mwenye kufanya amali hii anaingia katika yale aliyoyatahadharisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema:

 

“Na tahadharini na mambo ya kuzuliwa kwani kila uzushi ni upotofu” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ahmad, Ibn Maajah na ad-Darimi kutoka kwa Abi Najiih al-‘Irbaadh bin Saariyah [Radhwiya Allaahu 'anhu]. At-Tirmidhiy amesema hii ni Hadiyth Hasan Sahiyh. Isnadi yake ni Sahihi na imesahihishwa na Ibn Hibbaan). Na katika riwaya nyingine: “Na kila upotevu ni wa motoni.”

 

Na kauli yake: “Kila uzushi ni upotofu” ni sentensi ya kijumla na inaingia kila jambo lililozuliwa ambalo halina asili na msingi katika Dini ya Allaah. Na Wanachuoni wameafikiana kwa hilo, hivyo ni uzushi mpotofu unaompeleka mwenye kufanya kuingia Motoni, Allaah Atuepushe sote na adhabu hiyo ya moto.

 

Ya Tatu: Yeyote mwenye kufanya bid‘ah hii hatapata ujira kwa kitendo hicho bali atarudishiwa mwenyewe kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Mwenye kufanya amali isiyokuwa na hukumu yetu, itakataliwa” (Muslim kutoka kwa ‘Aaishah [Radhwiya Allaahu 'anha]). Na katika jambo hilo haitoshi kuwa mtu ana niya nzuri bali hapana budi kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ya Nne: Allaah Aliyetukuka Anasema: 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3].

 

Na yule anayesema kuwa Mawlid ni 'Ibaadah nasi tunamuabudu Allaah kwayo anaikadhibisha aayah hii, na kufanya hivyo ni kumkufuru Allaah Aliyetukuka. Na akiwa anaiswadiki aayah hiyo atalazimika kusema kuwa Mawlid si 'Ibaadah.

 

Kukubali kuwa ni 'Ibaadah ni kama unampatiliza Allaah na Rasuli Wake kwamba hawakutuonyesha 'Ibaadah hii tukufu ambayo tunajileta kwayo karibu na Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na akisema kuwa mimi sisemi kuwa jambo hilo ni 'Ibaadah wala kuwapatiliza Allaah na Rasuli Wake, naye anaamini aayah hii, atalazimika kurudi katika kauli ya haki ya kwamba jambo hili ni uzushi ulioingizwa katika Dini. Tunamuomba Allaah Atuongoze na Waislamu wate kwa Analolipenda na la Kumridhisha.

 

Ya Tano: Kufanya na kujihimiza katika uzushi huu wa Mawlid ni kama mtu anamtuhumu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alifanya hiyana na hakuwa ni mwenye kutimiza amana, tunajilinda kwa Allaah kwa hilo. Hii ina maana ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alificha kwa Ummah huu na hakuwaonyesha 'Ibaadah hii tukufu ambayo inamkaribisha mwenye kuifanya na Allaah.

 

Amesema Imaam Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Yeyote mwenye kuzua katika Uislamu Bid‘ah ambayo anaiona ni njema, bila shaka amedai ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya hiyana katika kufikisha ujumbe (aliopatiwa na Allaah), kwani Allaah Anasema: 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3].

 

Hivyo jambo ambalo halikuwa Dini siku hiyo halitakuwa leo ni katika Dini.” [Al-I‘tiswaam ya ash-Shaatibiy, Mj. 1, uk. 49].

 

Ya Sita: Yeyote mwenye kufanya amali hii anakwenda kinyume na shariy'ah na kujitia katika mashaka kwani shariy'ah ishaweka yale yanayotakiwa kufanywa na mja kwa njia na namna maalumu. Na viumbe wamefupishiwa juu yao kwa kuwekewa amri na makatazo na ikatujulisha kuwa yaliyo khayr yapo ndani yake na shari ni kuyaepuka, kwani Allaah Anajua yaliyo na maslahi kwa waja. Na Allaah Hakutuma Mitume na wala Hakuteremsha Vitabu isipokuwa aabudiwe Yeye kwa yale Anayotaka Yeye. Hivyo, yule mwenye kuzua Bid‘ah hii (yaani ya Mawlid) ameyatupilia mbali haya yote akidai kuwa ipo njia nyingine ya kufanya 'Ibaadah na kwamba yale mambo yaliyoletwa na shariy'ah si lazima. Hivi ni kama kusema kwa ulimi wa hali hii yake kuwa mtungaji shariy'ah anaelewa na yeye pia anajua. Na huenda ikawa kuwa yeye anafahamu jambo ambalo mtungaji shariy'ah halijui. Ametakasika Allaah, huu ni uongo mkubwa wa wazi kabisa na uhalifu wa hatari na dhambi ya wazi na upotevu mkubwa.

 

Ya Saba: Hakika katika kusimamisha bid‘ah hii ni kupotosha msingi miongoni mwa misingi ya shariy'ah, nako ni kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumfuata kwa kila jambo, kwa wazi na siri. Inabidi pia tujiondoshe na ule ufahamu finyu wa kuwa kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kucheza na kupiga ngoma wakati na siku maalumu katika mwaka. Na wale wanaotekeleza jambo hilo wanasema ya kwamba hiyo ndio dalili ya wazi kuwa wao wanampenda Nabiy (tujiondoshe na ule ufahamu finyu wa kuwa kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yeyote asiyefanya hayo basi anamchukiza na hivyo kuchukiwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na jambo hili bila shaka ni kuipindua ile maana ya mapenzi kwa Allaah na Rasuli Wake, kwani mapenzi kwa Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lazima yawe ni katika kufuata Sunnah zake zote. Kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kufuata zaidi sunnah zake kuliko kumsifu sana kama Anavyosema Allaah: 

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-'Imraan: 31].

 

Kumpenda si kumkumbuka kwa kumsifu mara moja kwa mwaka tena kwa njia isio sawa bali kila siku na kumsifu bila kufuata Sunnah zake hakuna faida wala thawabu.  

 

Kumpenda iwe zaidi kuliko hata nafsi zetu kama walivyompenda Swahaba  - 'Umar ilipoteremka aayah:

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ

Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. [Al-Ahzaab: 6]. 

 

Alisema “Ee Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakika wewe ni kipenzi kwangu kuliko chochote isipokuwa nafsi yangu” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Bado ee ‘Umar! Mpaka niwe ni mwenye kupendwa zaidi kwako kuliko nafsi yako.” 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah sasa wewe ni kipenzi kwangu kuliko chochote hata kuliko nafsi yangu.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Sasa ee ‘Umar.” Maana yake ni kuwa sasa umefikia ile daraja ya kunipenda. Kuhusu aayah hii Al-Bukhaariy amehadithia kuwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kasema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Hakuna Muumini yeyote isipokuwa mimi ni wa kupatiwa kipa umbele kwa watu duniani na Aakhirah. Someni mkitaka: 

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ

Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. [Al-Ahzaab: 6]. 

 

Sisi hatuwezi kufikia kiasi cha mapenzi ya Swahaba waliokuwa nayo na kujitolea mhanga kwa roho zao, watu wao, mali zao, n.k. Visa vingi vipo vya kusisimua mwili vinavyothibitisha mapenzi yao kwake mfano kisa cha Khabbaab bin al-Aratt, Khubayb, Ummu ‘Ammaarah Nusaybah bint Ka‘ab, Zayd, Bilaal bin Rabaah, Zunayrah, Sumayyah, Ammaar, na wengineo.

 

Yule mwenye kufanya mahaba kwa Mtume ni kufanya haya Mawlid anabadilisha shariy'ah ya Allaah ambayo inasema kuwa mapenzi sahihi inakuwa ni katika kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Bali hii ndio ile hakika ya mapenzi ambayo yamleta mtu karibu na Allaah na kumjaalia yeye atoke katika zile ada za kufananisha na yale wafanyao Wakristo katika sikukuu zao. Na kwa hili tunaelewa ya kwamba: “Haihuishwi (haifanywi) Bid‘ah isipokuwa huondoka Sunnah miongoni mwa Sunnah madhubuti.”

 

Ya Nane: Haya Mawlid yanafanana kwa uwazi kabisa na Dini ya Ukristo, ambayo wafuasi wake wanasherehekea mazazi ya Masihi ('Iysaa). Na hakika ni kuwa sisi tumekatazwa kushabihiana na wao kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Na yeyote mwenye kushabihiana na watu yu pamoja nao.” [Iqtidhwaa’ as-Swiratwil Mustaqiym ya Ibn Taymiyyah, Mj. 2, uk. 581].

 

Ya Tisa: Ni maalumu na yenye kueleweka kwa kila mmoja ya kwamba Swahaba ndio waliokuwa wakimpenda zaidi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko wana Aadam wengine kwa ujumla na Waislamu wengine hasa katika wale waliokuja baada yao. Lakini watu ambao wanafanya bid‘ah hii ya Mawlid wanasema kinyume ya hayo kwamba wale wasiosoma na kushirikiana nao huwa hawampendi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni tuhma kubwa kwa watu ambao walijitolea mhanga katika kumhami Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kutekeleza Sunnah zake na kujitolea mhanga kwa mali yao, familia zao na hata nafsi zao. Allaah Awaridhie kwa yale waliyokadimisha ili kuundeleza Uislamu. ni jambo ambalo lajulikana kuwa Allaah Amewaridhia na Kuwataja katika aayah kadhaa za Qur-aan na pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewaridhia kwa waliyotanguliza. Na yeyote mwenye kuwatuhumu basi yeye mwenyewe ima atakuwa ni kafiri wa dhahiri au mnafiki. Allaah Anasema:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا﴿١٨﴾

Kwa yakini Allaah Amewawia radhi Waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chini ya mti, (Allaah) Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao; basi Akawateremshia utulivu, na Akawalipa ushindi wa karibu. [Al-Fat-h: 18].

 

Na Amesema tena Aliyetukuka:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah: 100].

 

Imepokewa kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dalili ya Imani ni kuwapenda Answaar na dalili ya unafiki ni kuwachukia Answaar.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Imepokewa kwa al-Baraa’ bin ‘Aazib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hawapendi Answari isipokuwa Muumini na hawachukii Answari isipokuwa Mnafiki. Kwa hiyo Allaah Atampenda anayewapenda na Kuwachukia anayewachukia.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Hawa Swahaba wa ki-Answaar hawangependwa na Allaah isipokuwa wao walikuwa msitari wa mbele katika kumpenda na kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani Allaah Amesema hilo na unaweza kuirudia aya ya 31 ya Suwraah Aal-‘Imraan tuliyotangulia kuitaja. Twaba'an Swahaba wa ki-Muhajirina pia wapo katika aayah tulizozitaja pamoja na Hadiyth nyingi ambazo hatukuzinukuu hapa.

 

Ya Kumi: Hakika mwenye kufanya haya Mawlid ameingia katika yale aliyoyakataza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa uwazi kabisa. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Msinitukuze kama Manaswara walivyomtukuza 'Iysaa mwana wa Maryam. Kwa hakika mimi ni mja, hivyo semeni: Mja wa Allaah na Rasuli Wake.” [Al-Bukhaariy].

 

Hakika amekataza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumtukuza na kumsifu kupita kiasi sifa ambazo zinapindukia kwani hilo ndilo lililowafanya Manaswara kupotea katika njia ya haki.

 

Na katika hayo ni kukataa kuitwa hata “Khayrul Bariyyah (Mbora wa viumbe).” Na inatosha kumuita Rasullullah (Rasuli wa Allaah) kama alivyoitwa na mwenyewe Allaah au walivyokuwa wakimuita Maswahaba zake.

 

Inatutosha Hadiyth hii tukufu: Imepokewa kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu), amesema: Alikuja mtu kwa Mtukufu wa Daraja (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akasema: “Yaa Khayral Bariyyah (Ee mbora wa viumbe).” Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Huyo ni Ibraahim ('Alayhi salaam).” [Muslim]. Allaah Anasema:  

وَاتَّخَذَ اللَّـهُ إِبْرَاهِيمَ خَلِيلًا ﴿١٢٥﴾

Na Allaah Amemchukua Ibraahiym kuwa ni kipenzi. [An-Nisaa: 125]

 

Haya yanafanywa leo katika Mawlid, ambamo kunatumiwa mali mengi na kuimbwa ndani yake nyimbo zinazomtukuza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aina kubwa na kuvuka mipaka katika hilo. Na katika beti nyengine ni kumpatia hasa sifa za ubwana ambazo Anastahiki Allaah peke Yake.

 

Ya Kumi na Moja: Bid‘ah ya Mawlid ni kuwa tumevuka mipaka yanayokubaliwa na shariy'ah na tumevuka mipaka katika tuliyoamriwa katika kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na tumevuka mipaka katika kusimamisha siku kuu za Kiislamu. Hakika ni kuwa hakuna katika shariy'ah yetu isipokuwa 'Iyd mbili na atakayezua ya tatu basi atakua amevuka mipaka ya kishariy'ah.  

 

Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anaeleza ya kwamba alipohama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah walikuwa na siku mbili walizokuwa wakicheza ndani yake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika Allaah Aliyetukuka Amewabadilishia siku zilizo bora kuliko hizo – Siku ya Fitr ('Iydul Fitwr baada ya kufunga mwezi wa Ramadhwaan) na Siku ya Adh-haa ('Iyd kubwa ya baada ya Hijjah).” [An-Nassaaiy, nayo ni Sahihi].

 

Ya Kumi na Mbili: Kufanya Mawlid ni Ghuluw (kuvuka mipaka) iliyokatazwa kwa haiba ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ni jambo linampeleka mtu katika shirki kubwa iliyopigwa vita na Uislamu na huo ni ukafiri unaomtoa mtu katika Uislamu. Hakika ni kuwa ghuluw kwa watu wema ndiyo iliyokuwa sababu ya kaumu zilizopita kuingia katika shirki na kuabudu asiyekuwa Allaah. shariy'ah imekuja kuziba mapengo na kukataza kitu chochote ambacho kinaweza kumepeleka mtu katika shirki.

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutahadharisa sana na ghuluw pale aliposema: “Tahadharini na ghuluw kwani waliangamia waliokuwa kabla yenu kwa sababu ya ghuluw” (Ahmad, nayo ni sahihi). Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wameangamia wenye kuvuka mipaka.” Aliyarudia haya mara tatu (Muslim kutoka kwa Ibn Mas‘uud [Radhwiya Allaahu 'anhu]). Na hii imejumlisha ghuluw aina zote katika Itikadi na amali za 'Ibaadah.

 

Na inajulikana kabisa kuwa sababu ya shirki ambayo imepatikana kwa wana Aadam ni kuvuka mipaka ya shariy'ah katika kuwatukuza watu wema. Imepokewa na [Al-Bukhaariy] kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: Allaah Aliyetukuka amesema: 

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا﴿٢٣﴾

Wakasema: Msiwaache waabudiwa wenu; na wala msimwache Waddaa, na wala Su’waa’a, na wala Yaghuwtha, na Ya’uwqa, na Nasraa. [Nuwh: 23]

 

“Akasema haya yalikuwa majina ya watu wema katika kaumu ya Nuwh. Watu hawa walipoaga dunia, shetani alikuja kwa kaumu yao na kuwashawishi wajenge jengo la ukumbusho katika sehemu walizokuwa wakikaa na waweke ndani yake sanamu na waziite kwa majina yao. Walifanya hivyo, nao hawakuabudiwa mpaka walipoaga dunia na elimu ikasahauliwa.”

 

Na fananisha yale yaliyotokea kwa kaumu ya Nuwh ('Alayhis -salaam) mbali na kuwa hawakuwa ni wenye kuabudu chochote hapo mwanzo lakini baadae wakaingia katika shirki. Na sababu ya haya, nayo ni njia moja ya ghuluw na utazame yanayotokea katika Mawlid kwa kupatikana shirki kwa kumuomba asiyekuwa Allaah na kumpatia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa za uungu kama kupelekesha kwake mambo katika huu ulimwengu na kujua kwake elimu ya ghaibu.

 

Na Mawlid hayawezi kufana bila beti za burdai, Allaah Atuongoze na Atusaidie. Na lau kama hakungekuwa na uharibifu mwengine isipokuwa huu basi ingetosha kuharamisha na kutoa onyo kali kuhusu jambo hilo.

 

Ya Kumi na Tatu: Kufurahi siku hii na kulisha watu na kutoa sadaka ndani yake na kudhihirisha bashasha kwa yale mapenzi kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na wameafikiana wanachuoni wote kuwa siku hii ya tarehe 12 Rabi‘ul Awwal ni siku aliyefariki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Vipi sasa watu watakuwa wanafurahi kwa siku kama hiyo? Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anatuhadithia kuwa hakuna siku ambao watu wa Madiynah walikuwa na furaha ya hali ya juu kama siku aliyohamia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mji huo. Na hakuna siku ya huzuni kabisa kwa watu wa Madiynah kama siku aliyoaga dunia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inaonekana kama sisi tunakwenda kinyume na maadili ya wale watu bora waliokuwa wakimpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kuliko nafsi zao wenyewe.

 

Ama siku aliyozaliwa Wanachuoni wametofautiana sana kama tulivyotangulia kueleza hapo awali. Hivi itakuwaje 'Ibaadah kubwa yenye kumleta karibu mja na Allaah iwe katika siku ambayo watu wametofautiana. Ibn Hajar amesema katika kuisherehesha Hadiyth Na. 3641 kwamba wametofautiana Wanachuoni katika mwaka hasa aliozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ama wakati aliofariki hauna tatizo kabisa (Fat-hul Baariy).

 

Na Ibn al-Haaj amesema: “Kisha ajabu iliyo kubwa ni vipi watafanya watu Mawlid kwa kuimba na kuwa na furaha kwa ajili ya mazazi yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama yaliotangulia katika mwezi huu mtukufu nao ndio mwezi alioaga dunia na kuelekea kwa Mola wake Mlezi. Huu ni wakati ambao Ummah ulikutwa na kupatikana na msiba mkubwa ambao hauwezi kufanana na msiba mwengine wowote milele. Hivyo, watu wanatakiwa wawe na huzuni pamoja na kulia na kila mtu kujitenga kwa nafsi yake kwa yale yaliyomkuta…” [al-Madkhal, Mj. 2, uk. 15].

 

Ya Kumi na Nne: Sherehe hizi zinajumlisha mambo mengi ya madhambi makubwa na mazito ambayo yanawapendeza watu wenye kufuata matamanio yao. Na ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatueleza kwamba: 

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ

Je, umemuona yule aliyejichukulia hawaa zake kuwa ndio mwabudiwa wake... [Al-Jaathiyah: 23].

 

Katika vikao hivyo huwa na taarabu, nyimbo na kuchanganyika baina ya wanaume na wanawake na katika baadhi ya nchi hali hufika mpaka watu kunywa pombe. Tunaona kama katika nchi ya Tanzania na Kenya katika miaka ya sabiini na themanini wasichana ambao kawaida hawapewi ruhusa kutoka majumbani mwao au kusafiri, huwa wanapewa ruhusa kwenda katika sherehe hii kwani wazazi walikuwa wanaona kuwa wanajikurubisha kwa Allaah. Lakini ni maarufu kuwa hawa wasichana ndio walikuwa wanapata fursa ya kukutana na wapenzi wao.

 

Wengi wetu tumeyashuhudia hayo katika miaka ya sitini na kabla ya hapo na baada ya hapo mpaka katika miaka ya sabiini waalimu waliokuwa wakitoka Lamu kwenda kusoma Mawlid katika visiwa na vitongoji vyengine. Mambo ambayo yalikuwa yakitendwa na kutendeka ni kinyume kabisa na Uislamu na madhambi makubwa zaidi yakifanywa na Wanachuoni. Kwa sababu ya ujinga katika Dini hawa mabwana walikuwa wanazini na mabibi wa watu na kupatiwa kama tunu wasichana mabikra wawe ni wenye kulala nao kwa hoja kuwa kitovu cha mwalimu kikigusana na kitovu cha msichana au mwanamke basi msichana au mwanamke yule hataingia Motoni. Allaah Atuepushie na Atuongoze katika yaliyo ya sawa.

 

Itakuwaje matendo mabaya yote haya yawe ni katika kujikurubisha na Allaah Aliyetukuka. Upotofu ulioje katika mambo haya yanayofanywa kwa kisingizio cha Dini.

 

Ya Kumi na Tano: Kufanywa na kujumlisha mambo ya kufuja na kupoteza mali kwa watu wasiostahiki kabisa. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametukataza kufuja mali wala kuwa mabakhili kwani hizo si sifa za Waumini. Anasema:

وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًا ﴿٦٧﴾

“Na wale ambao wanapotoa huwa hawafanyi israfu na wala hawafanyi uchoyo na wanakuwa wastani baina ya hayo..” [Al-Furqaan: 67].

 

Kuna vitu ambavyo vinatakiwa vishughulikiwe sana na Waislamu leo kama kulipa mshahara walimu wa Madrasah ambao wanaishi katika hali iliyo duni kabisa. Kulipa mishahara ya Maimamu ambao nao wamekuwa omba omba na wengine kufanya uganga wa ujanja ujanja ili kujipatia rizki zao, pamoja na kutoa mali za kutunza Misikiti na kusaidia Waislamu watoto mayatima, wajane na mengineo ambayo ni ya msingi na yenye kumpatia mwenye kufanya thawabu nyingi, lakini lil-asaf yote haya hatuyafanyi.

 

Hivi karibuni (yaani mwaka huu wa 1426 H) katika mji wa Nairobi, baadhi ya Mashekhe waligoma kufanya zafah (zefe) za kila mwaka kwa sababu hela wanayopatiwa ni kidogo. Walikuwa wanaomba nyongeza hata kwa wanafunzi ambao wanawachukua kwa shughuli hiyo. Maslahi ya kibinafsi zaidi kuliko mapenzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)!

 

Na miaka ya nyuma na hadi sasa kuna baadhi ya sehemu panapokaribia mwezi wa Rabiy'ul Awwal, baadhi ya Mashekhe na Maustaadh wa Mawlid hupita kila duka na sehemu za biashara kukusanya mchango wa Mawlid na huku wakiwadanganya wafanyibiashara kuwa wanachotoa kwa ajili ya kusherehekea mazazi ya Nabiy (Mawlid) watapata ujira mfano wa Jabal Uhud, Uongo na ulaghai wa aina gani huu!! Tuzindukeni ndugu Waislam kabla hatujaswaliwa.

 

Ya Kumi na Sita: Hakika katika hizi Mawlid ambazo zimeongezeka maradufu na kuenea katika kila sehemu na katika baadhi ya miezi watu husherehekea Mawlid kwa takriban mara 28. Hakika katika hili kuna kutumia nguvu nyingi na juhudi tele na fedha na wakati, hivyo kuwageuza watu kwa yale ambayo wanapangiwa na maadui zao. Hivyo, kila siku ni kucheza rumba, muziki na Mawlid. Ni wakati gani tutajishughulisha kujifunza dini yetu na kujua mikakati inayoandaliwa dhidi yetu na maadui?

 

Walipokuja wakoloni katika nchi za Kiislamu walijaribu kumaliza kila ishara za Kiislamu na kuwatoa watu na dini yao na walijaribu kueneza uchafu baina yao. Na lolote ambalo litawageuza Waislamu waliwahimiza na kuwabarikia, mfano ni sehemu za starehe na upuuzi na mfano wake. Na mfano wa hayo ni uzushi unaowatoa watu katika maadili ya Kiislamu ya kihakika, miongoni mwayo ikiwa ni uzushi wa Mawlid na mengineyo. Bali uzushi huu ni katika sababu kwa Waislamu kubaki nyuma na kutoendelea mbele ya watu wengine.

 

Amesema mwenye al-Manaar (Mj. 2, uk. 74–76): “Mawlid ni kama masoko ya ufasiki, kwani ndani yake yamo mahema ya uchafu na sehemu za pombe na wachezaji dansi ambamo wanajumuika wanaume ili kuangalia wachezaji hao wa kike ambao wanakaa bila stara na sehemu nyengine za uasherati wa maneno na vitendo vikikusudiwa kuchekesha watu. Watazame wenye macho pale walipowasili Waislamu kwa baraka ya Taswawwuf (kumfikia Mwabudiwa kwa tafkira na kujitenga na watu) na Itikadi za wafuasi wake pasi na ufahamu wala kuchunga shariy'ah. Wamewachukua mashekhe kuwa miungu na wakawa wanakusudia kuzuru makaburi ili wapate kutekelezewa haja zao na kuponywa wagonjwa wao na kuongezeka riziki baada ya kuwa awali ilikuwa kwa ajili ya mazingatio na ukumbusho wa vielelezo. Ikiwa mara nyingi wanasimulia visa vilivyobuniwa, hivyo kufuta yale mambo yote mema kama ya kuamrisha mema, kukataza mabaya na kushirikiana katika khayr.

 

Na natija ya hayo yote ni kuwa Waislamu waliacha yale maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuyaendea yale yanayomridhisha Asiyekuwa Yeye, hivyo kuwachukua wengine kuwa miungu na kuwa kama mkware anayefanya analotaka mara nyingi. Hapana ajabu kwa kuwa ujahili unapozagaa na Imani kudhoofika na kuharamishiwa yale Waumini waliyoahidiwa na Allaah ya kupata ushindi kwani wao wamepotoka katika kikundi kilichopatiwa sifa ya Imani.

 

Hakukuwa na matendo yoyote katika haya katika karne ya kwanza wala ya pili na hapana dalili yoyote ya haya katika Qur-aan wala Sunnah. Hakika haya yalikuja kwa sababu ya kufuata ada au adui kutoka katika jamii nyingine. Wanapoona kaumu yetu mfano wa hizi sherehe wanadhania kuwa wanapofanya mfano wa amali hizo basi wanakuwa na utukufu na huhisi jambo katika nafsi zao wale watu wengine. Aina hii ni kama ile ya kuchukua miungu na hii ni sababu kubwa kuchelewa Waislamu katika maendeleo na kuanguka kwao.”

 

Na sikiliza anavyotuambia mwanahistoria al-Jabritiy katika kitabu chake ‘Ajaa’ibul Aathaar (Mj. 2, uk. 201 na 249): “Wakoloni wa Kifaransa pindi alipoitawala Misri chini ya uongozi wa Napoleon Bonaparte, Masufi na watu wa Mawlid walikuwa wameshindwa kuyafanya Mawlid. Hivyo, Napoleon aliamuru kuyahuisha na kutoa fedha kwa ajili yake.” Na amesema katika Madhhwarut Taqdiys Bizawaal Dawlatil Fransiys, uk. 47: “Na ndani yake (yaani katika mwaka wa 1213 Hijri katika mwezi wa Rabiy’ul-Awwal), aliuliza mkuu wa askari kuhusu Mawlid ya Nabiy na kwa nini  hawafanyi kama desturi yao? Alitoa udhuru Shaykh al-Bakriy kwa kuwa hali haikuwa mzuri na mambo kurudi nyuma na ukosefu wa fedha. Askari hakukubali sababu hizo na akasema: ‘Hapana budi tufanye’. Hivyo, alimpatia Shaykh al-Bakriy Riyaal mia nane (800) za Kifaransa ili zimsaidie. Wakatundika kamba na taa za kandili na wakajumuika Wafaransa siku ya Mawlid, wakacheza na kupiga matwari na ngoma zao na kuwasha moto na mabomu ambao yalikuwa yakipaa kwenye hewa.”

 

Na kama ulivyosema msemo wa Kiingereza: “History repeats itself (Historia inajirudia yenyewe).” Jambo hili linaonekana katika maisha leo na hasa katika kisiwa cha Lamu ambapo Mawlid yalianzishwa mara ya kwanza takriban miaka 120 iliyopita hivi. Na watu wengi wa Mawlid wakawa hata wanasema ya kwamba mji huo mdogo ni Makkah ndogo, hivyo mwenye kuzuru wakati huo wa Mawlid huwa ana thawabu nyingi ya kama kwenda Makkah. Ni mizani gani iliyotumiwa kufikia hilo, hili halipo katika Qur-aan wala Sunnah wala Ijmaa wala haliingii katika Qiyaas. Leo katika kisiwa hicho japokuwa sherehe hizo zilikuwa zimerudi nyuma na kuanguka lakini Balozi ya Marekani Kenya inasaidia katika Mawlid hayo ya Lamu kwa takriban miaka mitatu sasa.

 

Tunaweza kujiuliza, je lengo lao ni nini katika kuhimiza na kuyafadhili Mawlid na Bid‘ah nyengine? Tunajua wazi kuwa Ufaransa ilipotawala nchi za Waislamu ilikuwa inawanyanyasa na kuwaadhibu, sasa vipi wataweza kufadhili sherehe za kidini? Na ni jambo ambalo si siri kwa hata mtoto mdogo kuwa Marekani leo ni adui mkubwa wa Waislamu na Uislamu kwa kumsaidia Israili, kuwaua Waislamu Palestina, Iraq, Afghanistan na pia misimamo yao dhidi ya Uislamu. Vipi wataendelea kuwaua Waislamu katika sehemu tofauti duniani kisha waje wafadhili shughuli ambazo zinasemekana kuwa ni za kidini na kuwapatia mishahara waalimu wenye misimamo fulani. Tuzingatie sana jambo hili Waislam, je, mambo haya mawili yanaweza kujumuika pamoja?

 

Na hali kama hiyo vilevile tunaiona Tanzania na katika miji ambayo Mashia wamo, utakuta Mashia wanatoa fungu kila mwaka za kusimamishwa shughuli za Mawlid kuanzia matorobali, chakula, taa za kutundikwa kwa mapambo, vipaaza sauti n.k., na hata katika siku za karibuni waliweka mitambo midogo ya satellite ili wenye matelevisheni majumbani mwao waweze kuyaona Mawlid hayo hai (live). Na kwanini Mashia wasihakikishe wanayasimamia na kuyapigania yasife na hali wao ndio waanzilishi?

 

 

5.0 Ubaya Wake

 

Shirk Katika Mawlid

 

1. Maneno yanayomsifu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanavuka mpaka hadi humpandisha cheo cha kuwa kama Allaah wakati yeye mwenyewe alituonya sana tusimfanye kama ‘Iysaa (‘Alayhis salaam) alivyofanyiwa na wafuasi wake.

 

2. Kumsimamia wakati wanapotaja kuzaliwa kwake ni kuamini kuwa roho yake inarudi pale.  Jambo hili ni la kumchukiza mwenyewe alipokuwa hai, vipi walifanye kama kweli wanampenda?

 

(Hakuna aliyekuwa mwenye kupendwa zaidi mbele ya Swahaba kuliko Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini hawakuwa ni wenye kumuinukia walipokuwa wakimuona kwa sababu alisema kufanya hivyo ni Makruhu). [Tafsiyr Ibn Kathiyr].

Pili kuamini hivyo ni itikadi isiyo na asili ya shariy'ah.

 

3. Tunajishabihisha kama Manaswara wanaosherehekea Krismasi, wakati Allaah Ameshatuonya: 

وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ۗ قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّـهِ هُوَ الْهُدَىٰ ۗ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُم بَعْدَ الَّذِي جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ ۙ مَا لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿١٢٠﴾

Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao. Sema: “Hakika mwongozo wa Allaah ndio mwongozo (pekee).” Na ukifuata hawaa zao baada ya yale ambayo yaliyokujia katika elimu, basi hutopata kutoka kwa Allaah mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru.” [Al-Baqarah: 120].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katuonya kuwa tukijishabihisha nao basi na sisi ni kama wao:

“Yeyote atakayeshabihiana na watu basi ni katika wao (mfano wao).”

 

Maneno yanayomsifu yanavuka mpaka hadi humpandisha cheo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kama Allaah wakati yeye alituonya sana tusimfanye kama ‘Iysaa (‘Alayhis-salaam):

“Msinitukuze kama walivyomtukuza Manaswara ‘Iysaaa mwana wa Maryam. Kwa hakika mimi ni mja, hivyo semeni: Mja wa Allaah na Rasuli Wake.” [Al-Bukhaariy]. 

 

Mkishakuwa mnawaiga wasiokuwa Waislamu watakutieni katika mambo ya haramu na muyafanye bila kuzingatia wala kutafakari. Na kuna faida gani kufuata mambo ya dini zilizofutwa na dini yetu – Uislamu? Wao wenyewe Manaswara na Mayahudi wameiga kutoka kwa mushirikina; haikubaliki kuabudu kama walivyokuwa wakiabudu waabuduo masanamu. Sio halali kufanya hivyo.

 

4. Na tujue pia kuna makosa mazito katika kitabu cha Barzanjiy na kama utapenda kusoma na kupata sifa za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi ni bora kwako kuzisoma sifa hizo na maisha yake kutoka kwenye vitabu vilivyo sahihi na ambavyo ni vingi, badala ya kujiingiza katika kitanzi.

 

5. Ubaya ambao ni mkubwa zaidi ni kuwa kule kuzua jambo ambalo halipo katika Dini ni kusema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikhini ujumbe na hakuufikisha kama ilivyopaswa. Imaam Maalik alikaririwa akisema: “Mwenye kuzua Bid‘ah katika Uislamu anayoiona kuwa ni nzuri, basi huyo amedai kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliukhini ujumbe.” Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]. 

 

Hivyo, jambo lolote ambalo halikuwa Dini wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haliwezi kuwa Dini sasa. Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya: “Lau mngaliacha Sunnah za Mtume wenu mngalikufuru.” [Muslim].

 

6. Wenye kuzua huwa wamefanya kinyume na wamekhalifu amri ya Rabb wao Mlezi na Nabiy wao, na kujitia kuwa wao wanajua dini zaidi kumshinda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli wake, ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا ۚ قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا ۚ فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

Msifanye wito wa Rasuli baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Kwa yakini Allaah Anawajua miongoni mwenu wale wanaoondoka kwa kunyemelea. Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr: 63].

 

7. Ubaya mwengine ni kuwa hayo Mawlid hayakupendelewa na watangu wema (Swahaba, watu wema wa karne tatu bora za mwanzo ambazo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezitaja kwa wema) na wala hawakufanya wala hawakuyajua. Na tufahamu sherehe katika Uislamu zimewekwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nazo ni ‘Iyd mbili na hakuna sherehe nyengine ya tatu.

 

8.     Ile fikra ya kwamba Mawlid ndiyo si katika Dini lakini itakuwaje tuwaambie watu ambao tayari wamezoea? Kusimama na kusema hivyo itaonekana ni kama hatuna msimamo na hivyo kuogopa watu. Huu ni ubaya mkubwa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

 إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧٥﴾

Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki wake wandani. Basi msiwakhofu, na nikhofuni Mimi mkiwa ni Waumini.” [Al-'Imraan: 175].

 

 

6.0 Kauli Za Wanachuoni

 

Wametoa fatwa wanachuoni wa Kiislamu wa kilimwengu mbali na khitilafu zao za sehemu na zama na Madhehebu zao za Kifikihi kuwa haifai Mawlid na kuwa hiyo ni Bid‘ah iliyozuliwa ambayo haina chanzo wala asili katika Uislamu. Na baadhi yao ni:

 

1- Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyah, ambaye ni miongoni mwa wanachuoni wa Shaam amesema: “Baadhi ya watu, kwa kuwaiga Manasara wanafanya kwa kudai mazazi ya ‘Iysaaa (‘Alayhis Salaam), au kwa sababu ya mapenzi yao kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au kupenda kwao kumtukuza, wanasherehekea mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni japokuwa kuna utata mkubwa baina ya wanachuoni kuhusu tarehe hasa aliyozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Waislamu wa mwanzo hawakufanya hilo, japokuwa kulikuwa na sababu nzuri kumheshimu na kuyaonyesha mapenzi yao kwake na hakukuwa na kikwazo chochote katika kufanya hilo. Hivyo, lau kusherehekea mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yalikuwa ni jambo la thawabu na zuri wangekuwa na haki zaidi ya kututangulia katika hilo, kwani yale mapenzi yao na heshima yao kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yalikuwa ni makubwa kuliko yetu. Na pia walikuwa na hamu zaidi ya kutekeleza matendo mema kiujumla kuliko sisi.” [Iqtidhwaa’ asw-Swiraatwil Mustaqiym Mukhaalafatu Aswhaabil Jahiym, Mj. 2, uk. 619 na Majmuu‘ al-Fataawaa, Mj. 1, uk. 312].

  

2- Shaykh Taajud Diyn ‘Umar ibn ‘Aliy al-Iskandariy ana kijitabu kwa jina al-Mawrid Fiy al-Kalaam ‘Alaa ‘Amalil Mawlid, ambaye ni mwanachuoni wa Maalikiy aliyefariki Alexandria Misri mwaka wa 734 Hijri amesema kuwa Mawlid hayafai.

  

3- Abuu ‘Abdillaah Muhammad al-Hufaar ana fatwa kuhusu kupinga mas-ala haya, naye ni mwanachuoni kutoka Morocco.

  

4- Mwanachuoni Ibn al-Haaj Abu ‘Abdullah Muhammad bin Muhammad al-‘Abdariy, alikuwa akifuata Madh-hab ya Maalikiy aliyefariki Misri mwaka 732 Hijri ana maneno mazuri na matamu kuhusu uzushi wa Mawlid.

  

5- Shaykh ‘Allaamah Muhammad Bukhayt al-Mutwii‘iy al-Hanafiy, Mufti wa zamani wa Misri naye alipinga jambo hilo.

 

 

6- Shaykh ‘Aliy Mahfuudh katika kitabu chake al-Ibdaa‘ Fii Madhwaar al-Ibtidaa‘.

  

7- Imaam Ash-Shaatwibiy ana fatwa kwa jina Fataawaa al-Imaam ash-Shaatwibiy kuhusu mas-ala haya, naye ni mwanachuoni wa Maalikiy wa Hispania (Andalus).

  

8- Shaykh Abu Atw-Twayb Muhammad Shamsul Haqq al-‘Adhiym Aabaadiy, naye ni miongoni mwa wanachuoni wa Bara Hindi (India). Kuhusu hili tazama kitabu cha Shaykh At-Tuwayjiriy, uk. 235.

  

9- Shaykh Bashiyr ud Diyn al-Qanuujiy, katika wanachuoni wa India ambaye alikuwa ni mwalimu wa Abu Atw-Twayb (Tazama kitabu cha at-Tuwayjiriy).

  

11- Shaykh Muhammad bin ‘Abdis-Salaam Khadhwar Ash-Shuqayriy katika kitabu chake as-Sunan wal Mubtadi‘aat.

  

12- Shaykh al-Islaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.

  

13- Shaykh ‘Abdur-Rahmaan bin Hasan Aaal Shaykh kama alivyoeleza katika ad-Durar as-Sunniyah.

  

14- Shaykh Muhammad bin Ibraahiym ana kijitabu ambacho ndani yake amepinga Mawlid na pia tazama fatawa zake (Mj. 3, uk. 48 – 95).

  

15- Shaykh ‘Abdullaah ibn Muhammad bin Humayd katika kitabu chake Hidaayah an-Naasik ilaa Aham al-Manaasik.

 

16- Imaam ‘Abdul-‘Aziz ibn ‘Abdillaah bin Baaz katika kijitabu chake Hukmul Ihtifaal Bilmawlid an-Nabawiy ambapo amesema: “Haijuzu mikusanyiko ya Mawlid ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala mengine, kwani hayo ni katika mambo ya bid‘ah yaliyozuliwa katika dini, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuyafanya wala Makhalifa wake waongofu, wala wengine miongoni mwa Swahaba wala Matabiina walio katika karne zilizo bora; nao ni wajuzi zaidi wa Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko watu wengine. Nao pia ni wakamilifu wa mapenzi zaidi kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wenye kufuata Sharia Yake kuliko waliokuja baada yao.”

 

17- Shaykh Humuud bin ‘Abdillaah at-Tuwayjiriy katika kitabu chake Ar-Rad al-Qawiy ‘alaa ar-Rifaa‘iy wal Majhuul wa Ibn ‘Alawiy wa Bayaan Akhtwa’uhum Fiy al-Mawlid an-Nabawiy.

  

18- Imaam Muhammad Swaalih al-‘Uthaymiyn kama tulivyonukuu maneno yake hapo juu.

  

19- Shaykh Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan ambaye amepinga kufanywa kwa Mawlid katika kitabu chake Kitaabut Tawhiyd, uk. 115 - 117.

 

Hawa wote ni Mashaykh kutoka katika maeneo ya Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Bara Hindi, lakini wapo pia wanachuoni wengi katika Afrika Mashariki ambao wamepinga shughuli hii ya kusomwa Mawlid. Inatosha hapa kutaja baadhi yao, nao ni:

 

i.         

Shaykh Fayswal al-Laamiy, ambaye alikuwa ni Shaykh mkubwa Lamu, naye alikuwa msitari wa mbele katika kupinga na watu walipokosa kumsikiliza alihama kutoka kijiji cha Lamu na kukaa katika kijiji cha jirani cha Shella. Alisomesha na kuacha misingi barabara ya Sunnah na hiki ni kijiji ambacho watu wake wachache ambao wamebakia na misingi ya kusoma hubidi kwenda Lamu ili kufanya shughuli yao hiyo. Alikufa mwanzo wa karne ya ishirini.

 

ii.         

 Shaykh Al-Amin Mazrui.

 

iii.         

Shaykh Muhammad Qaasim Mazrui.

 

iv.         

Shaykh 'Abdullah Swaalih Farsy ambaye amesema: “Mawlid ni uzushi uliozuka baada ya kupita hao watu bora aliowasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hata mjukuu wa huyu aliyetunga Mawlid ya Barzanjy akaifanyia ufafanuzi kitabu hicho akaiita Alkawkabul Anwaar aliandika katika sahifa ya 4 maneno haya‘Jua kuwa kusoma Mawlid ni bid’ah (uzushi) kwani halijapokelewa jambo hilo kwa hao ulamaa waliokuwa karne tatu tukufu za mbele huko zilizosifiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)’. Basi inatosha shahada hii ya huyu mjukuu wa huyu Barzanjy. Imekuwa ‘Washahida Shaahidun min ahlih’ yaani akashuhudia shahidi wao wenyewe” (Bid-a, uk. 31).

 

v.         

Wanachuoni wengi katika mlango wa al-Ma‘aawiy waliokuwa Lamu walipinga jambo hilo isipokuwa Shaykh Muhammad ibn ‘Aliy, ambaye kwa leo anatukuzwa na hata kufanyiwa ziara siku maalum na masharifu kwa sababu ya kuunga msimamo wao. Ni kwa ajili ya msimamo huu wa wanachuoni wa mlango huo ndio ukapata mpaka leo unapokwenda katika Msikiti ambao unashughulikiwa na wao kuwa Mawlid hayasomwi, hata kitabu cha Barzanjiy hakipatikani huko.

 

Kwa hizi kauli za Wanachuoni na walinganiaji hawa wachache tunatumai kuwa kila Muislamu ataijua haki na kuifuata bila ya matamanio na hawaa za nafsi yake.

 

 

7.0 Hitimisho

 

Sisi kama ndugu moja katika Imani ni wajibu wetu kufikisha ujumbe na nasaha kwa kila Muislamu, na uongofu unatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Siku ya Kiyama ndio patakuwa na kivumbi (adhabu kali) waliofuata watajitetea na waliofuata pia watajitetea, lakini haileti. Hebu tuzisome na tuzizingatie aya mbili zifuatao: 

إِذْ تَبَرَّأَ الَّذِينَ اتُّبِعُوا مِنَ الَّذِينَ اتَّبَعُوا وَرَأَوُا الْعَذَابَ وَتَقَطَّعَتْ بِهِمُ الْأَسْبَابُ﴿١٦٦﴾وَقَالَ الَّذِينَ اتَّبَعُوا لَوْ أَنَّ لَنَا كَرَّةً فَنَتَبَرَّأَ مِنْهُمْ كَمَا تَبَرَّءُوا مِنَّا ۗ كَذَٰلِكَ يُرِيهِمُ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ حَسَرَاتٍ عَلَيْهِمْ ۖ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنَ النَّارِ ﴿١٦٧﴾

Wale waliofuatwa watakapowakana wale waliowafuata wakiwa wameshaiona adhabu; na yatawakatikia mafungamano yao. Na watasema wale waliofuata: “Lau tungelipata fursa ya kurudi (duniani) tungewakana kama walivyotukana.” Hivyo ndivyo Allaah Atakavyowaonyesha ‘amali zao kuwa ni majuto juu yao. Na wala hawatokuwa wenye kutoka motoni.” [Al-Baqarah: 166-167].

 

Tufahamu kuwa katika mambo ya dini alishasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na yametosha, wala hakuna tena kuwa Shaykh fulani naye kasema. La Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) linachukuliwa na la Shaykh linawekwa kando. Safari moja mtu mmoja alimuuliza Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mas-ala fulani, naye akayajibu mas-ala hayo kwa Hadiyth sahihi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Yule mtu akasema: “Lakini amesema Abu Bakr na ‘Umar.” Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia: “Inahofiwa kukuteremkieni mawe ya maangamizo kutoka mbinguni. Mimi ninasema, ‘Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), nawe unasema Abu Bakr na ‘Umar wamesema.”

 

Ingawa inavyoonekana kuwa wasomaji Mawlid hasa na watu wa Bid‘ah kwa ujumla ni wengi katika baadhi ya sehemu, watu wa haki na ukweli wanatakiwa wafuate haki japokuwa ni wachache. Inatakiwa kila Muislamu akumbuke aayah ifuatayo: 

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah. Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo.” [Al-An'aam: 116].

 

Na kama Waislamu hatufai wala hatutakiwi kufa moyo kwa kuona watu hawatusikilizi bali tunatakiwa tuendelee na ulinganiaji. Na tuelewe kuwa jazaa ya amali yetu hiyo iko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema: 

إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾

“...hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri. [Yuwsuf: 87].

 

Jukumu letu ni kufikisha kwa hekima na njia iliyo nzuri, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿٥٦﴾

Hakika wewe huwezi kumhidi umpendaye; lakini Allaah Humhidi Amtakaye, Naye Anawajua zaidi wenye kuongoka.” [Al-Qaswasw: 56].

 

Hata hivyo ni jambo la kumshukuru sana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuona kila mwaka unavyosogea na Mawlid nayo yanakosa nguvu na wenye kuyasherehekea wanayaacha. Hayo ni matunda ya elimu, pamoja na mafunzo ya Mashaykh wanaoshikamana na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pia na vijana wengi waliokwenda nje kupata elimu ya juu na sahihi na kurudi kuwafunza wenzao.

 

Ile tabia na mila ya kusubiri ‘shekhe aseme nasi tufuate’, imeanza kupungua kwa sababu wengi hivi sasa wanasoma na hata wakisikiliza, basi husikiliza na kufuata yale yaliyo na dalili na kuyaacha yale maneno matupu.

 

Tumeona jinsi Mawlid yalivyokuwa yakisomwa ndani ya misikiti na kupigwa madufu humo ndani na kuchezwa, kisha polepole baada ya kukemewa tabia hizo na wasomi, madufu yakahamishwa nje ya msikiti, kisha ule mchanganyiko uliokuwepo katika zafah (zefe) baina ya wanaume na wanawake na kucheza, kushikana, kudhkiri, na kuimba pamoja, wote umepungua ama kuachwa kwa hivi sasa baada ya kusemwa sana na kukemewa na watetezi wa Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata ule mkusanyiko wa pamoja kwenye viwanja vya msikiti baina ya wanaume na wanawake, hivi sasa umekuwa hauonekani sehemu nyingi AlhamduliLLaah.

  

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuonyeshe njia ya haki kama ni haki na Atupatie hima ya kuweza kuifuata kama inavyotakiwa, na batili kama batili na Atupatie moyo wa kuweza kuiepuka. Tunamuomba Atupatie hatima njema na mwisho wetu uwe ni mwema na mzuri.

 

Share