Bid’ah Inayopambana Na Sunnah (Je, Kuna Bid'ah Nzuri Katika Dini?)

 

Bid’ah Inayopambana Na Sunnah (Je, Kuna Bid'ah Nzuri Katika Dini?)

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Yaliyomo

 

Wenye Kupinga Bid’ah

 

Kauli Za Baadhi Ya 'Ulamaa

 

Bid’ah Njema Na Bid’ah Ovu

 

Basi Na Hii Bid’ah Pia

 

"Ni’imat Al-Bid’ah Haadhihi"

 

 

Shukrani zote ni Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), tunamshukuru, tunategemea kwake msaada, na tunajikinga kwake kutokana na shari za nafsi zetu na ‘amali zetu ovu. Yule ambaye Allaah Atamuongoza basi hapana wa kumpoteza, na yule Atakayemhukumu kumpotosha (kwa kukataa kwake uongofu), basi hapana wa kumuongoza.

 

Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah, Pekee Asiye mshirika, na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mtume wake na mjumbe wake na kipenzi chake na mbora wa viumbe vyake.

 

Amma baad,

 

Hakika ya maneno ya kweli kupita yote ni kitabu cha Allaah, na muongozo ulio bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na shari ya mambo ni kuzuwa mepya katika dini, na kila uzushi ni Bid’ah na kila Bid’ah ni upotovu na kila upotovu mahali pake ni Motoni.

 

Wenye Kupinga Bid’ah

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mwanzo wa hutuba zake akitamka maneno haya:

 

"Na shari ya mambo ni kuzuwa mepya (katika dini), na kila uzushi ni Bid’ah na kila Bid’ah ni upotovu na kila upotovu mahali pake ni Motoni."

 

Na hii ni dalili ya hadhari aliyokuwa akiichukuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuwakataza umati wake kuzuwa mambo mepya katika dini.

 

Waislamu wote wanakubaliana kuwa tumekatazwa kufanya kitendo cha Bida'h, nayo ni kuzuwa mambo katika dini ambayo Allaah hajayatolea amri Yake. Hitilafu iliyokuwepo ni kuwa wengine wanasema ipo Bida'h njema na Bida'h potovu, wakati wengine wanasema kuwa Bida'h zote ni potovu kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kila uzushi ni Bid’ah."

 

Kutoka kwa Al-‘Irbaadh bin Saariyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutolea mawaidha yaliyotutoa machozi na kuzilainisha nyoyo. Tukamuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah, haya ni (mfano wa) mawaidha ya kutuaga, kwa hivyo nini unatuusia?" Akasema: "Nimekuacheni juu ya weupe, (juu ya kitu kisafi) usiku wake sawa na mchana wake, hapotoki akatoka humo isipokuwa mwenye kuangamia. Na atakayeishi miongoni mwenu ataona khitilafu nyingi, basi fuateni mliyokwishayajuwa katika Sunnah yangu (mafundisho yangu), na mafundisho ya Makhalifa wema waongofu watakaokuja baada yangu. Yakamateni kwa magego." [At-Tirmidhiy, Abu Daawuud, Imam Ahmad na wengine.]

 

Na akasema:

 

"Atakayezusha katika amri yetu hii (dini yetu) lisilokuwemo anarudishiwa. (halikubaliwi).

[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wenye kupendelea kufanya sherehe za Maulidi wanatafsiri kitendo cha wenzao wenye kuyapinga kwa kukataa kuisherehekea siku hii kuwa ni watu wasiompenda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Bila shaka kadhia hii si nyepesi kama inavyodhaniwa, na pia kukifasiri kitendo cha kukataa kuisherehekea Maulidi kuwa ni kutompenda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika mambo ya ghushi na kuufumbia macho ukweli.

 

Ukweli ni kuwa mwenye kukataa kuisherehekea siku hii anakataa kwa ajili ya kuogopa kufanya kitendo cha uzushi ambacho yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajapata kukifanya.

 

Ni kitendo kinacholeta khitilafu nyingi baina ya Waislamu, na si katika Sunnah yake (mafundisho yake) kama alivyotamka Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam, na hakijawahi kutendwa na yeyote kati ya Makhalifa wema waongofu waliokuja baada yake.

 

Mwenye kuacha kufanya kitendo kilichozushwa kwa sababu ya kuhofia kuingia makosani, bila shaka huyo hawezi kutuhumiwa wala kulaumiwa, bali kinyume chake ni kuwa mtu huyo yupo katika usalama kuliko mwenye kufanya kitendo ambacho asili yake hata kama atakiacha hatopata dhambi, kwa sababu hapana amri yoyote katika dini juu kitendo hicho.

 

Katika Hadiyth niliyotangulia kuitaja, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Nimekuacheni juu ya weupe, (juu ya amri kisafi) usiku wake sawa na mchana wake, hapotoki akatoka humo isipokuwa mwenye kuangamia."

 

Kwa hivyo mwenye kuiacha sherehe hiyo au kitendo chochote kingine kilichozushwa katika dini kwa ajili ya kuogopa asije akaingia katika Bid’ah, huyo anajiepusha na "khitilafu nyingi" alizozitaja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na anasalimika, kwa sababu anajiweka juu ya weupe aliotuwachia juu yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kauli Za Baadhi Ya 'Ulamaa

 

Allaah Anasema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْأِسْلامَ دِيناً

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]

 

'Ulamaa wanasema:

 

"Kile ambacho siku ile ilipoteremshwa aya hii hakikuwemo katika dini, basi leo hakiwezi kuwemo pia. Allaah keshaikamilisha dini yake na hakiwezi kukubalika tena kipya isipokuwa kile tu aliochotuletea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)."

 

Amesema Imaam Ash-Shawkaaniy:

 

"Ikiwa Allaah Keshaikamilisha dini Yake kabla hajaichukuwa roho ya Nabiy Wake, sasa ni kipi tena hiki wanachokizuwa baada ya kukamilika kwake? Na ikiwa wanaamini kuwa ni katika dini, basi huko ni kutuhumu kuwa dini haijakamilika. Na ikiwa wanaamini kuwa si katika dini, basi pana faida gani kujishughulisha na (kuliendeleza) jambo lisilokuwemo katika dini?" (Qawl al Mufiyd uk. 38)

 

Bid’ah Njema Na Bid’ah Ovu

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kila uzushi ni Bid’ah na kila Bid’ah ni upotovu."

 

Na akasema:

"Atakayeanzisha mwenenedo mwema " سُنَّةً حَسَنَةً katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenendo mbaya سُنَّةً سَيِّئَةً atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika madhambi yao ". [Muslim na At-Tirmidhy na An-Nasaiy na wengine]

 

Wengine wakaifahamu vibaya Hadiyth hii, wakadhani kuwa; kwa vile pana kitu kinachoitwa: " سُنَّةً حَسَنَةً Sunnatun Hasanah (Sunnah njema), kwa hivyo bila shaka mkabala wake ipo pia حَسَنَة بدعة   Bid’atun Hasanah' (Bid’ah njema), wakati ukweli ni kuwa hapana kitu kama hicho katika dini. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  "Kila uzushi ni Bid’ah."  Kisha akarudia tena, akasema:

 

"Na kila Bid’ah ni upotovu."

 

Amelitamka neno 'KILA' mara mbili katika sentensi moja, kwa ajili ya kusisitiza juu ya umuhimu wake, kwani angeliweza kusema: 'Kila Bid’ah ni uzushi na upotovu.' Bila ya kulirudia neno 'KILA' mara ya pili.

 

Inaeleweka wazi kuwa katika Hadiyth hii Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anazungumza juu ya Sunnah njema na siyo Bid’ah njema, kwa hivyo hapana haja ya kuiunganisha Hadiyth hii na mambo mawili haya yenye kutofautiana.

 

Huenda ikawa wanajaribu kuiunganisha Hadiyth hii na ile kauli ya ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliposema: نعمت البدعة هذه "Ni’imat al Bid’ah haadhihi", (kauli ambayo tutaisherehesha kila tukiendelea mbele InshaAllaah).

 

Baadhi ya 'Ulamaa wakasema:

 

"Mtu atakayeisimulia Hadiyth hii ya "Atakayeanzisha mwenendo mwema ...سُنَّةً حَسَنَةً kwa nia ya kuipitisha Bid’ah yake, kisha asikielezee kisa kilichomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ayatamke maneno haya, basi huyo anakuwa sawa na mtu aliyeisoma kauli ya Allaah: 

َفوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ

...Basi ole wao wanaoswali

:Kisha akanyamaza, asiikamilishe kauli hiyo kwa kusoma

 الَّذِينَ هُمْ عَن صَلاتِهِمْ سَاهُونَ

Ambao wanapuuza Swalaah zao

 

Ili kuifahamu vizuri Hadiyth hii lazima tukisimulie kisa kilichomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atamke maneno yale.

 

Kutoka kwa Jurayr bin AbdiLlaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Lilikuja kundi la watu wa kabila la kibedui (kabila la Madhr) wakiwa wamevaa nguo zilizoraruka, hawana viatu, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaiona hali yao kuwa walikuwa na shida. Akamuamirsha Bilaal aadhini, kisha ikaqimiwa Swalah, na baada ya kuswali Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawahutubia watu na kuwahimiza kuwapa sadaka watu hao. Watu wakakawia kufanya hivyo mpaka ilionekana (huzuni) katika uso wake. Kisha mtu mmoja katika watu wa Madiynah akatoa sadaka Dinari zake na wengine wakaanza kutowa Dirham na wengine nguo zao na wengine pishi za ngano na wengine tende, kisha mwengine akaleta bahasha aliloshindwa kulibeba kisha watu wakafuatiliana mmoja baada ya mwingine mpaka yakaonekana marundu mawili ya nguo na chakula mpaka nikauona uso wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uking’ara kwa furaha ndipo aliposema:

 

"Atakayeanzisha mwenendo mwema " سُنَّةً حَسَنَةً katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenenedo mbaya سُنَّةً سَيِّئَةً atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo mpaka siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika madhambi yao ". [Muslim na At-Tirmidhy na An-Nasaaiy na wengine]

 

Anasema Imam Ash-Shaatwibiy:

 

"Katika Hadiyth hii, neno kuanzisha hakujakusudiwa kwa maana ya kuvumbuwa au kuzusha, bali kumekusudiwa kuhuisha matendo yaliyothibiti kuwa yamewahi kutendwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na dalili ni kuwa kilichomfurahisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kitendo cha kutoa sadaka kwa wingi, na la pili ni aina ya sadaka; marundu ya nguo na marundu ya vyakula. Kwa hivyo sadaka haiwezi kuwa katika uzushi (Bid’ah), kwa sababu uzushi ni katika matendo yasiyokubaliana na sheria, kinyume na sadaka." [Imam Ash-Shaatwibiy – Al-I’tiswaam juz. 1, uk. 233]

 

Basi Na Hii Bid’ah Pia

 

Haiwezekani pasemwe kuwa pana Bid’ah njema katika dini, kwa sababu vitu hivi viwili haviwezi kwenda sambamba hata siku moja – haviwezi kukubaliana, hasa kwa vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) keshatamka kuwa:

 

"Kila uzushi ni Bid’ah na kila Bid’ah ni upotovu."

 

Kauli hiyo imetamkwa na kiumbe mwenye ulimi fasaha kupita ndimi zote zilizoumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na ni kiumbe mwenye kuelewa vizuri kile anachokitamka. Kwa hivyo haikubaliki tena aje mtu atuambie kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajakusudia kuwa Kila uzushi ni Bid’ah, bali ipo Bid’ah njema na nyengine potovu.

 

Huenda mtu akaliona jambo lake kuwa ni zuri akadhania kuwa ni Bid’ah na lisiwe Bid’ah, au huenda akaipenda Bid’ah yake akiona kuwa ni njema lakini haiwezi kuwa njema. Lakini mtu anapokiri kuwa kitendo fulani ni Bid’ah, kisha aseme kuwa ni Njema, hilo ni jambo lisilowezekana.

 

Mwengine atasema:

 

"Kujenga shule pia ni Bid’ah hasanah, kwa sababu wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapakuwa na shule." Tunamuambia kuwa kweli hilo ni jambo jema, lakini hicho sicho alichokusudia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali alichokusudia ni Bid’ah katika mambo ya dini aliposema: "Atakayezusha katika amri yetu hii (na maana yake ni amri ya dini yetu)."

 

Kujenga shule ni katika wasila, ni njia ya kuifikisha elimu na siyo elimu yenyewe ambayo ni ibada, kama vile microphone 'kipaza sauti' ni wasila, njia ya kuifikisha sauti ya Qur-aan na hotuba kwa watu, na Qur-aan na hotuba ndiyo ibada, na watu wanapopanda gari kwenda Makkah, hilo gari ni wasila, njia ya kuwafikisha watu, lakini siyo ibada, ibada ni kule kuhiji na kufanya ‘Umrah.

 

Kwa hivyo mtu anapojenga shule hakusudii kuwa lile jengo ni ibada, bali jengo ni njia ya kuifikisha elimu kwa wanafunzi, na anapoingiza vipaza sauti Msikitini hakusudii kuwa chombo kile ni ibada bali ni njia tu ya kuwafikishia watu sauti, kama vile mtu anapopanda gari kwenda kuhiji, anajua kuwa gari lile si ibada bali ni njia ya kumfikisha kwenye ibada anayoitaka. Na hii ndiyo njia wanayotumia Maulamaa katika kutoa hukmu.

 

Wakati mwenye kuleta Bid’ah yake, huyo anakusudia kuwa ni ibada, kwa kuiwekea njia yake ya kufanya na makatazo yake na kuvumbua ndani yake mambo mengi yasiyoteremshiwa amri ya Allaah juu yake.

 

"Ni’imat Al-Bid’ah Haadhihi"

 

Kutokana na ile kauli ya ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliposema: "Ni’imat al-Bid’ah haadhihi" Mtu anaweza kusema kuwa ipo Bid’ah njema.

 

Ukweli ni kuwa ‘Umar hapa alilikusudia neno Bid’ah kwa maana ya kilugha na si kwa maana ya Fiq'hi. Inajulikana kuwa katika kamusi ya Fiq'hi, neno Bid’ah lina maana nyingine tofauti na maana ya neno hilo katika kamusi ya lugha.

 

Neno 'Bid’ah' katika lugha ni neno zuri sana, kwani maana yake ni uvumbuzi wa mambo, kama vile madawa na mambo ya idara na ziraa nk. Lakini neno hilo hilo 'Bid’ah' katika dini maana yake ni mbaya, lakini katika mambo ya kidunia, Bid’ah ni kitu kizuri. Ndiyo maana mtu katika dini akiambiwa kitendo ulichofanya ni Bid’ah hukasirika, lakini anapoanzisha kitu kipya katika mambo ya kidunia akaambiwa "Ni Bid’ah nzuri sana hiyo," hufurahi sana.

 

Inajulikana pia kuwa katika lugha ya Kiarabu neno moja linaweza kubeba maana moja katika kamusi ya lugha, na neno hilo hilo likabeba maana nyingine katika kamusi ya Fiqhi ya dini, kwa mfano:

 

Neno Swalah, katika lugha ya Kiarabu maana yake ni du’aa, na neno hilo hilo katika kamusi ya Fiqhi maana yake ni; ibada inayoanza kwa takbira na ina maneno na vitendo maalum ndani yake na inamalizika kwa kutoa salaam.

 

Neno Zakaah, katika kamusi ya lugha ya Kiarabu maana yake ni kujitakasa, na neno hilo hilo katika kamusi ya Fiqhi ni ile; mali anayopewa masikini baada ya kukamilisha muda maalum.  Katika maudhui haya, sisi tunazungumza juu ya Bid’ah katika kamusi ya dini.

 

Zipo sababu mbali mbali zinayoifanya ile kauli ya ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa aliikusudia kilugha, na siyo kidini:

 

Sababu ya kwanza ni kuwa kitendo cha ‘Umar kuirudisha tena Swalah ya Taraawiyh katika mwezi wa Ramadhwaan si kitendo cha Bid’ah kisheria kwa sababu kitendo hicho kilifanywa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaswalisha Swahaba muda wa siku tatu, kisha akaacha kwa sababu alihofia isije ikafaridhishwa na kuwa nzito kwao. Baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki dunia, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akairudisha tena Swalah ile kwa sababu hapakuwepo tena na ile hofu ya kufaridhishiwa, ndipo ‘Umar alipofurahi alipowaona watu wote wamesimama nyuma ya Ubay bin Ka’ab wakiswali jama’ah, akasema: "Ni’imat al-Bid’ah haadhihi." Hii haikuwa Bid’ah kisheria, bali ilikuwa ni kuihuisha Sunnah iliyoanzishwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyewahi kuwaswalisha mara tatu kisha akaacha kwa sababu iliyotoweka baada ya kufariki kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na yeye ‘Umar akaweza kuirudisha tena.

 

Na sababu ya pili ni kuwa kitendo cha ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakiwezi kuwa cha Bid’ah hata kama kitendo hicho atakianzisha yeye, na hii inatokana na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia kutajwa aliposema:

 

"Fuateni mliyokwishayajuwa katika Sunnah yangu (mafundisho yangu), na mafundisho ya Makhalifa wema waongofu watakaokuja baada yangu. Yakamateni kwa magego."

 

‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni katika Makhalifa wema waliokuja baada yake, kwa hivyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameturuhusu kufuata mafundisho yao.

 

Tunamaliza kwa kusema kuwa Bid’ah ya kisheria, Bid’ah katika dini, kwa maana ya kuzusha jambo jipya ambalo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kulitenda haiwezi kuwa njema hata siku moja.

 

Anasema Mwanachuoni Faqiyh, Muhammad bin Swaalih bin ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu):

 

"Mtu aingie msikitini kwa mfano, awakute watu wanaswali Sunnah zao kila mmoja peke yake kama kawaida wakimsubiri Imam awaswalishe jama’ah, kisha mtu huyo awaambie watu: 'Jamani mnaonaje tukaswali Sunnah jama’ah kwa pamoja badala ya kila mtu peke yake."

 

Watu bila shaka watamuambia: "Unataka kutuletea uzushi gani tena?" Yule mtu atawaambia: "Hapana, si uzushi kwani tunamswalia nani? Si tunamswalia Allaah? Isitoshe, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) keshawahi kuswali Swalah za Sunnah jama’ah, kama vile Swalah za Tahajjud na aliwahi pia kuswali Taraawiyh na akaswali Swalah za kupatwa kwa jua na pia mwezi na aliswali Swalah za ‘Iyd jama’ah, na zote hizo ni Sunnah."

Watu bila shaka watamjibu: "Lakini jambo hili unalotuita ndani yake halijawahi kufanywa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)."

 

Na hapa ndipo penye hekima yote," anaendelea kusema Mwnachuoni huyo Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu), "nayo ni kuwa kitendo chochote katika dini asichowahi kukifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au kutuamrisha kukifanya basi hiyo ni baatwil, hata kama ni Swalah ya kumswalia Allaah!

 

 

 

Share