SWALI:
According to the Sunnah (I am not exactly certain which hadith) it is stated that whoever says Shahada on the death bed or while dying is going to Jannah! What is exactly means by this? Does it mean anybody who says Shahada during the last seconds of his life will go to
Shukran.
* A Swahili answer is ok too - samahani kuandika kiengereza
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tunashukuru kwa swali lako hili ambalo umeliuliza kwa lugha ya kiingereza na sisi tunalijibu kwa lugha ya Kiswahili
Kwa uwezo wa Allaah Aliyetukuka tutajaribu kukufahamisha
Ama kuhusu kalimah ya mwisho ikiwa ni kauli ya Laa ilaaha illa Allaah mwenye kuisema ataingia Peponi basi ipo Hadiyth iliyo sahihi. Imepokewa kwa Mu‘aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote ambaye maneno yake ya mwisho yatakuwa ni Laa ilaaha illa Allaah ataingia Peponi” (Ahmad, Abu Daawuud na al-Haakim, na akasema Isnadi yake ni sahihi, na imesahihishwa na al-Albaaniy na Shu‘ayb al-Arna’uutw amesema ni Hasan).
Ndio Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuusia sana tuwe ni wenye kumlakinia kwa kumkumbusha pole pole awe ni mwenye kutamka kalimah hiyo kama alivyopokea Abu Sa‘iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Walakinieni maiti zenu kwa Laa ilaaha illa Allaah” (Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy). Kuwalikinia maiti zenu ina maana ya wanapokuwa katika kutokwa roho siyo baada ya kuaga dunia.
Uhakika wa Hadiyth hiyo ni kuwa yeyote anayetamka shahada kabla ya kuaga dunia basi huyo ataingia Peponi
Hivyo tusighurike kwa kuwa wakati huu twaweza kuisema kalimah hiyo bila matatizo yoyote wakati huo mambo yatakuwa tofauti kabisa. Ikiwa tunataka tusipate shida wakati huo inafaa tuwe ni Waislamu wa kweli wenye kufuata maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tukifanya hivyo tutakuwa na maisha ya sahali hapa duniani na wala hatutakuwa na maisha ya dhiki Kesho Akhera.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atujaalie ni wenye kufuata mema na mazuri na kuwa na hima katika kuyaacha yaliyo mabaya na Aturehemu pamoja na kutujaalia kuweza kutamka shahada wakati wa kufa kwetu, Aamiyn.
Na Allaah Anajua zaidi