Malipo Baina Ya Waja Huwa Duniani Na Akhera Kwenda Hesabu? Vipi Wanalipizana?

 

Malipo Baina Ya Waja Huwa Duniani Na Aakhirah

Kwenda Hesabu? Vipi Wanalipizana? 

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalamu alaykum warahmatulah wabarakatu.

Napenda kutoa pongezi kwa uongozi mzima wa al-hidaya kwa kazi nzuri wanayoifanya. 

Ningependa kujua ukweli na uthibiti katika quran kama malipo hapa hapa duniani na akhera huenda hisabu. Na kama kweli je mpaka hizi zama zetu watu hulipwa hapa hapa duniani? Na malipo hayo huwa vipi? Naomba nifafanuliwe... Natanguliza shukrani zangu za dhati kwa ushirikiano wenu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Ibara hiyo si ukweli mtupu wala uongo mtupu, hivyo imekaa baina ya ukweli na uongo. Mwanzo tufahamu kuwa ibara au msemo huo ni wa Kiswahili ambao hauwezi kukubalika moja kwa moja kama zilivyo semi nyingine nyingi za Kiswahili zilizo maarufu.

 

Huenda wakati mwengine mtu akalipiwa hapa hapa kwa sababu alidhulimiwa na hivyo akanyanyua mikono yake ili kumuomba Allaah Aliyetukuka. Hata hivyo, Aakhirah ndio hesabu na malipo kulingana na Hadiyth nyingi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kwa hayawani sio tu wanaadamu. Hebu tutazame Hadiyth mbili zifuatazo:

 

1.     Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mtaendelea kurudisha haki za watu Siku ya Qiyaamah mpaka kondoo asiye na pembe (atawekewa pembe) ili alipize kwa aliyekuwa na pembe (duniani)” [Muslim].

2.     Amepokea Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Je, mwamjua aliyefilisika?” Wakasema: “Aliyefilisika miongoni mwetu ni yule asiyekuwa na pesa taslimu wala vyombo”. Akasema: “Hakika aliyefilisika katika ummah wangu, ni wale watakaokuja Siku ya Qiyaamah na Swalah, Swawm na Zakaah. Hata hivyo, amemtusi huyu, na kumsingizia huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu. Thawabu zake huchukuliwa akapatiwa huyu, na huyu mwengine kwa thawabu zake. Zinapomalizika thawabu zake na kabla ya hukumu kumalizika, huchukuliwa madhambi yao akapatiwa yeye, kisha akaingizwa Motoni” [Muslim].

 

Kwa hiyo, malipo makubwa zaidi na yenye vishindo ni ya Siku ya Qiyaamah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share