Malaika Wanaoandika Mema Na Maovu Ya Mja Wanajua Siri Za Allaah?

 

Malaika Wanaoandika Mema Na Maovu Ya Mja Wanajua Siri Za Allaah? 

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asasalm alykum.

Naomba tusaidiane juu ya suala hili.

Tunaamini kua Allah subhanahu wa taala, yeye ndie anaejua mazuri yetu na mabaya yetu, sasa ni hivi, hawa malaika wanaoandika mema na mabaya yetu huwa wao wanajuaje na hii siri ni ya allah subhanahu wa taala peke yake, kwa sababu Mashekh wanatufundisha kua chochote ufanyacho Allah subhanahu wa taala yeye ndie anaejua. Je na hawa malaika wawili na wao huwa wanajua kuhusu jambo hili la thawabu na dhambi juu yetu sisi wanaadam na majini. Naomba Radhi Kama Nitakua Sijafahamika Vizuri. Naomba Jibu In Shaa Allaah

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Malaika wanaoandika mema na maovu.

Malaika ni viumbe kama viumbe vingine ambao wameumbwa na Allaah Aliyetukuka. Ghaibu inajulikana na Allaah Aliyetukuka peke Yake. Hata hivyo, tufahamu kuwa Malaika umbile lao ni tofauti nao wameumbwa kutekeleza maagizo ya Allaah Aliyetukuka peke Yake. Allaah Aliyetukuka Anasema yafuatayo kuhusu sifa za Malaika:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6].

 

Kwa kuwa Malaika wote wana zile sifa za kutomuasi Allaah Aliyetukuka na wanatenda wanayoamrishwa, basi yao wanayoyafanya yanakwenda sambamba na Anayotaka Allaah, Muumba wa kila kitu. Tukifahamu hilo basi hakutakuwa na utata kwa yale wanayoandika Malaika hao wawili ambao Allaah Aliyetukuka Amewataja:

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf: 18].

 

Kwa hiyo, Malaika hawa wanarekodi maneno hata minong’ono na matendo ya mja. Na wao wanaweza kufanya hayo kwa kuwa hiyo ni kazi waliopatiwa na Allaah Aliyetukuka, hivyo, wamepatiwa uwezo wa kuweza kutekeleza hilo bila tatizo lolote.

 

Na kwa kuwa Malaika waliopatiwa kazi hii tayari wamepatiwa maelekezo ya jambo ambalo ni thawabu au dhambi kunakuwa hakuna shida. Na kwa hiyo Malaika wanatekeleza kazi zao bila ya shida wala utata wowote.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share