Uzazi: Swawm Kwa Mwenye Mimba Na Mwenye Kunyonyesha

SWALI:

Assalam aleikum W.W.
Nashukuru kwanza kuwa nachombo kama hichi cha kutufunza dini yetu yaki slam.]
kwanza nduguzangu wa islam mimi niko naswali limenishinda kujua lakufanya. mimi ni mama na mtoto wa mmyezi sita sasa ,nimesha olewa ni na mme .nayishi hapa ulaya inakuwa vigumu kujuwa mambo mengi yakuhusu dini yetu yakislam.

SWALI ,langu nihili ,mimi mwaka jana sikujaliwa kufunga mwezi mtukufu wa ramadhani ,kwa sababu nilikuwa na mimba kubwa sana ikawa vigumu mimi kuweza kuvunga huwo mwezi mtukufu.

baada ya  kujifunguwa nikaaanza kukunyonyesha mpaka leo nanyonyesha ,sasa sijaweza kulipa ramadhani inayo kwisha ,hivi nawona kufunga ina nipa shida kwa sabu mtoto ana nyonyosana alafu hapa ulaya hivi ni simer time ,mchana  hua mrefu sana ,mfano magharibi inayingiya  saane usiku ,unawona al fadjri ina anza kumi namoja   asubuhi .mimi kwa sabu nina mtoto mdogo nawona inaweza kuwa vigumu kwa sababu na nyonyesha. nilikuwa nawuliza vile nitaka vyo fanya ,niweze kulipa ramadhani yenye sija funga ,nawona na ramadhani nyingine inayingiya ,nawuliza ?naweza kufunga ramadhani hiyi inayo kuja,alafu niyifunge baada.?????
nazidi kuwatakiya amani  ya ALLAH iwejuu yenu .
kilalakheri

 


 

JIBU:

Bismillahi Waswalaatu Wassalaam 'Alaa RasuliLlaah  صلى الله عليه وسلم

Suala hili lina rai mbili; wapo Wanachuoni wanaoonelea mwanamke mwenye deni la funga na aliacha kwa kujikhofia mimba yake au kiumbe aliyekuwa tumboni mwake, basi alipe na atoe kafara. Na wengine wanaonelea kwamba mwanamke mwenye mimba au mwenye kunyonyesha anahesabika katika fungu la wagonjwa, ikiwa kama anajikhofia mwenyewe au anakhofia mtoto kwa hiyo anaruhusiwa kutokufunga Ramadhaan, ila alipe tu siku alizoacha kufunga.

وَمَنْ كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

{{Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine}} Al-Baqarah: 185

 

Hadiyth ifuatayo inaonyesha ruhusa hii ya kutokufunga mwenye mimba au mwenye kunyonyesha:

 قال النبي صلى الله عليه وسلم : "(( إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى وَضَعَ عَنْ الْمُسَافِرِ الصَّوْمَ وَشَطْرَ الصَّلاةِ ، وَعَنْ الْحَامِلِ والْمُرْضِعِ الصَّوْم))َ رواه الترمذي  وصححه الألباني في صحيح الترمذي  

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema; ((Allaah سبحانه وتعالى Ameondosha shuruti ya kufunga kwa msafiri, na nusu ya Swalah, na mwanamke mwenye mimba na mwenye kunyonyesha)) [At-Tirmidhiy na ni Swahiyh kutoka kwa Shaykh Al-Abaaniy].

 

Lakini kama hana khofu kuwa yeye au mtoto wake wataathirika na Swawm basi inambidi afunge kutokana na amri ya Allaah سبحانه وتعالى Asemaye:

فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمْ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

{{Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge}} Al-Baqarah: 185

 

Ama kuhusu kulipa deni la Ramadhaan, kuna ikhtilaaf ya rai za 'Ulamaa, lakini rai iliyokubalika na wengi ni kuwa alipe siku nyingine kwani yeye hukumu yake itakuwa ni kama ilivyo katika Aayah hii: mtu aliye mgonjwa:

فَمَنْ كَانَ مِنْكُمْ مَرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

{{Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine}} Al-Baqarah: 184  

 

Kulipa deni la Ramadhaan linatakiwa lilipwe kabla ya Ramadhaan nyingine na anaweza mtu kuchelewesha hadi mwezi wa Sha'abaan. Lakini kama ikiwa hakulipa hadi imeingia Ramadhaan nyingine bila ya sababu yoyote basi itakuwa ni dhambi na itabidi alipe baada ya Ramadhaan na afanye 'Kafara', nayo ni amlishe maskini mmoja kila siku alizokuwa hakufunga. Lakini kama alikuwa na sababu ya kuchelewesha kulipa kama mwenye kuumwa au mwenye mimba au mwenye kunyonyesha basi anatakiwa alipe tu deni bila ya kufanya 'Kafara' ambayo ni kulisha maskini kwani yeye atakuwa miongoni mwa Aayah:

فَمَنْ كَانَ مِنْكُمْ مَرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

{{Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine}} Al-Baqarah: 184

 

Na kulipa kwake ni kwamba si lazima afunge siku zote mfululizo bali anaweza kufunga na kupumzika hadi amalize kufunga.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share