Taraawiyh: Kuswali Rakaa Nne Nne Taraawiyh Badala Ya Mbili Mbili Inafaa?

  SWALI:

 

A'Kumww maulamaa hukunilipo mambo ni tofauti nalivyokuwa east africa yani tarawee tunaswali lakaa nne nne badala ya mbili mbili inakuwaje

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Swalah ya taraawiyh huswaliwa raka'ah mbili mbili, kila baada ya raka'ah mbili unatoa salaam.Hii ni kutokana na dalili:

 

((صلاة الليل مثنى مثنى فإذا خشيت الصبح أوتر بواحدة))" أخرجه البخاري 

((Swalah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na   ukiogopa  kukukuta asubuhi  basi Swali Witr  [Raka'ah] moja))  [Al-Bukhaariy]

 

Hata huko Tanzania na Afrika Mashariki ndivyo inavyoswaliwa hivyo. Na kawaida kila baada ya raka'h nne ndio kunakuwa na mapumziko marefu kidogo na ndio maana ikaitwa taraawiyh kwa sababu Maswahaba walikuwa wakipumzika kila baada ya raka'ah nne.

 

 

Na ilivyo hata sehemu nyingine utakuta watu wanachukua mapumziko makubwa baada ya raka'ah nne na hata kufanya mawaidha kidogo au wengine kupumzika na kunywa maji kisha wakaendelea tena kuswali nne zilizobaki ambazo kila baada ya raka'ah mbili kunatolewa salaam.

 

Ilivyo Sunnah, Swalah ya Tarawiyh ni raka'ah nane jumla na witr tatu na hivyo zote kuwa 11. Hii imethibiti kwenye Hadiyth ifuatayo:

 

عن عائشة رضي الله عنها قالت:  " ما كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يزيد في رمضان  ولا في غيره على إحدى عشرة  ركعة ...    متفق عليه

 

Kutoka kwa 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anha) ambaye amesema: "Hajapata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzidisha katika Ramadhaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Ama utakuta baadhi ya misikiti huswali raka'ah 20, nayo pia ingawa haijathibiti katika Sunnah, lakini kutokana na Hadiyth nyingine isemayo kuwa ((Swalah ya usiku ni raka'ah mbili mbili....)) ndio pia imekuwa tunaweza kuswali hivyo ikiwa msikiti tunaoswali wanafanya hivyo. Ila ni bora zaidi kuswaliwa raka'ah 8 na tatu za witr ambazo jumla ni 11 kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni kwa sababu kuswali rakaa chache hizo zinaweza kuswaliwa kwa vizuri kabisa, zikapatikana unyenyekevu, kisomo kizuri cha Qur-aan sio cha kuharakiza kama zinaposwaliwa rakaa ishirini. Mapendekezo haya ni kutokana na jinsi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiswali rakaa chache lakini akiziswali kwa vizuri kabisa kama alivyosimulia Mama wa Waumini 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anha):

 

 

عن عائشة رضي الله عنها قالت:  " ما كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يزيد في رمضان  ولا في غيره على إحدى عشرة  ركعة يصلي أربعا فلا تسال عن  حسنهن وطولهن ثم يصلي أربعا فلا تسأل عن حسنهن وطولهن ثم  يصلي  ثلاث"  متفق عليه

 

Kutoka kwa 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anha) ambaye amesema: "Hajapata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzidisha katika Ramadhaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja  akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali  tatu" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa hiyo endelea kuswali na hao ndugu zako, na Swalah yako sahihi kabisa inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 
Share