Taraawiyh: Idadi Ya Rakaa Za Taraawiyh, Mwisho Wake, Jinsi Ya Kuziswali Rakaa Tatu Za Witr

 

 

Idadi Ya Rakaa Za Taraawiyh, Mwisho Wake, Na Jinsi Ya Kuziswali Rakaa Tatu Za Witr

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalaam aleykum wa rahmatullah waabarakaatuh,

 

nina swali lingine mwenzangu anauliza yeye ni mvivu wa kuswali taraawiyh kwa muda wake maana akishashiba anakua amechoka sasa huwa anaswali usiku akiamka kama saa 8 au 9 sasa je taraweh mwisho wake ni hadi karibu na alfajiri au? mimi nikidhsani mwisho ni saa 6 tu.

Pia sasa hivi ktk kusoma soma alhidaaya nimeona kwamba MTUME swalalahu aleyhiwasalam alikua hazidishi rakaa 11 ktk swala za usiku khasa ktk mwezi wa ramadhan sasa hiyo idadi ni pamoja na witri 3 jumla ndio ziwe 11 au?na kama nikizidisha 11 ni vibaya au?

pia wamesema witri usiswali 3 pamoja yaani uswali 2 kisha 1 isaliwe pekeyake hapo imenichanganya kwani mimi siku zote huwa naswali 3 kwa pamoja.

Jazaakallahu kheir

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Kuhusu mwisho wa kuswali Taraawiyh, ni kabla ya Alfajr ukimalizia na Witr.

Swalaah ya Taraawiyh ndio hiyo hiyo Qiyaamul-Layl na kwa mwezi huu wa Ramadhwaan inaitwa Qiyaamur Ramadhwaan au Taraawiyh. Mazoea yaliyojengeka ni kuiswali baada ya 'Ishaa, lakini wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiswali 'Ishaa kwa kuichelewesha kabla kidogo ya katikati ya usiku na baada ya hapo wakiendelea na Qiyaam (Taraawiyh). Ilijulikana kwa jina la Taraawiyh kwa sababu Maswahaba walikuwa wakiswali na hupumzika kila baada ya Rakaa nne au mbili, na kipumziko hicho kikaitwa Taraawiyh na ndio hiyo Swalaah ikachukua mkondo wa jina hilo wakati wa Maswahaba.

Ama kuhusu Rakaa alizoswali Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ushahidi wa Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) iliyopokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim ni kuwa alikuwa hazidishi Rakaa 11 wakati wa Ramadhwaan na usio wa Ramadhwaan katika Swalaah zake za usiku. Na hizo ni 8 Taraawiyh (Qiyaamul-Layl) na 3 Witr hivyo jumla ni 11.

 
Ama kuzidisha zaidi ya hizo hakuna ubaya kwani inasemekana kuwa wakati wa Maswahaba walipokuwa Waislam wanaongezeka na kuwa na mchanganyiko wa wazee na watoto, walikuwa wakiswali 20 hadi 36 wakizifanya Rakaa fupi fupi lakini nyingi kwa sababu ya watu kuchoka na kisimamo kirefu.

 

Kuna Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo anasema: "Swalaah ya usiku ni Rakaa mbili mbili, na ukikhofu kuingiwa na Alfajr basi malizia kwa Witr japo moja" [Al-Bukhaariy]

Hadiyth hiyo inaonyesha kuwa mtu anaweza kuswali Rakaa nyingi azitakazo lakini mwisho amalizie kwa Swalaah ya Witr ambayo ndio Swalaah ya mwisho wa usiku.

 

Lakini mtu kubakia katika yale yaliyothibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndio bora zaidi na salama.

Hivyo kushikamana na Rakaa 11 ni vizuri zaidi japo Sunnah hiyo imekuwa haitekelezwi na wengi na hata huko katika miji miwili mitakatifu tunaona kila mwaka katika Ramadhwaan Sunnah hiyo imeachwa.

 

Na kuhusiana na swali lako la namna ya kuswali hiyo Swalaah ya Witr, ni hivi:

 

Kuswali Rakaa mbili kwanza kisha utoe salaam. Kisha unamalizia na Rakaa moja na kutoa salaam.

Au kuswali Rakaa zote tatu kwa tashahhud (kikao) moja ya mwisho tu na kutoa salaam.

 

Haifai kuswali Rakaa tatu zote pamoja kwa kuleta Tashahhud mbili kama vile Swalaah ya Magharibi, bali ni kuitofautisha na Swalaah ya Magharibi kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((… ولا تشبهوا بصلاة المغرب))

 ((… wala msiifananishe (hiyo Witr) na Swalaah ya Magharibi)) [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy, Ibn Hibbaan, Ad-Daraaqutniy]  

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo kwa faida ziyada:

 

Swalah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Niyyah?

051 - Qunuut Katika Swalah Ya Witr

027 - Kisomo Chake (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Swalah Ya Witr - Sifa Ya Swalah Ya Mtume

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share