Kumsilimisha Kafiri Na Hukmu Ya Kuoana

 

SWALI:

 S/A....asanteni sana kwa kuchukuwa time yenu na kulishughulikia swala langu. NATAKA NIJUE HUKMU YA KUSILIMISHA MTU ALAFU AKAKUOWA AU KUMUOWA especially like white people and e.t.c.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola   wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunashukuru kwa swali lako kuhusu mas-ala ya kusilimisha na ikafungamana na ndoa. Tunakukumbusha pia wewe na ndugu zetu wengine wawe ni wenye kuandika Salaam kwa ukamilifu kama tulivyofundishwa na Mtume wetu kipenzi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatujulisha thawabu zake. Hivyo kufupisha namna hiyo “S/A” au “A.A.W.W” ni mambo ambayo hatujafundishwa na pia yanatukosesha thawabu zilizotajwa.

 

Tukirudi kwenye swali, hakuna jambo zuri kama Muislamu kufanya Da‘wah (ulinganiaji) kwa wasiokuwa Waislamu si kwa watu weupe bali kwa binaadamu wote kwa njia moja au nyingine. Jambo hilo lina thawabu kubwa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Akakuongoza Allaah kwa (kuwa sababu ya kuongoka) mtu mmoja kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu” (al-Bukhaariy).

 

Ifahamike kuwa isiwe lengo la kufanya hivyo ni kuoa unayemsilimisha au kuolewa naye. Lengo kubwa ni kufikisha ujumbe na kutaka radhi za Allaah Aliyetukuka.

 

Hata hivyo ni ubinaadamu kwa mtu kumpenda mwanamme au mwanamke kwa sababu moja au nyingine. Sasa ikiwa umempenda mwenza uliyemsilimisha haifai kucheza naye kwa njia yoyote ile bali inafaa umuoe kisheria ili muweze kuishi kama mume na mke. Hakuna makosa yoyote kisheria kwa kumsilimisha na baadaye wawili hao kuoana lakini kwa uzoefu ulivyo kuna matatizo mengi kwa sababu moja au nyengine. Sababu kuu inayojitokeza ni kuwa mtu husilimu kwa sababu ya kuoa au kuolewa hivyo baada ya kupata matakwa yake hutoka kidogo kidogo katika Dini mpya aliyoingia.

Nadhani katika hili hapana budi ila ni kuwapatia nasaha dada na kaka zetu katika Imani kuhusu mas-ala hayo. Tufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana tuwe ni wenye kuoa au kuolewa na mwenye Dini na maadili mema. Mtu ambaye amesilimu sasa Dini na maadili yake bado hayajulikani. Kwa hiyo, ni vyema kabla ya kuoana aliyesilimu apelekwe sehemu kwa muda fulani ili apate kufundishwa Dini mpaka imkolee. Katika kipindi hicho inaweza kujulikana ule umadhubuti wake katika Dini. Ikiwa itashindikana basi ni afadhali utafute yule ambaye ni Muislamu tayari.

 

Kipo kisa kilichotokea Mombasa wakati wa u-Qaadhi wa aliyefariki Shaykh Muhammad Qaasim Mazrui, baada ya Mzungu mmoja kusilimu na kutaka kuoa msichana wa Kiislamu. Wazazi wa msichana wakaenda kwa Shaykh ili kupata ushauri naye akawaambia wamletee huyo mwanamme aliyesilimu. Alipofika ofisini kwake Shaykh alimjaribu kwa kumwambia kuwa msichana hataki tena kuolewa kwa hivyo yeye aweza kuendelea na Uislamu wake. Papo hapo Mzungu huyo alimaka kwa kusema: “Ikiwa msichana amekataa basi mimi sina haja na Uislamu”.

 

Hivyo, tusiingie katika mtego kama huo kwa kupoteza wasichana wetu au watoto watakaozaliwa katika ndoa hiyo. Tuweni na tahadhari.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share