Nani Ahlul-Kitaab Na Wanawake Gani Tumeruhusiwa Kuwaoa?

SWALI:

asalaam alaykum,naitwa abdalah said heka ndugu zangu ktk uislamu mimi binafsi kabla ya swali langu nawashukuru kwa ujumbe wenu kwetu sisi waislamu kwani nimefaidika sana na mawaidha kupitia ALHIDAAYA ALLAH awafanyie wepesi ktk kuuwendeleza uislamu.  shekhe swali langu la kwanza nataka kujua hawa ahlilkitab ni akina nani?na ivi sasa bado tunao.swali la 2 ni wanawake gani tulioruhusiwa kuwaoa sisi waislamu bila ya wao kusilimu? Asane

 


JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

 

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa Du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia AL HIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atutakabalie hizo Du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

 

 

Nani Ahlul-Kitaab Na Wanawake Gani Muislamu Ameruhusiwa Kuoa?

 

Ahlul-Kitaab (Waliopewa vitabu, ni Manaswara (Wakristo) na Mayahudi).  

Ibn Qudaamah رحمه الله  alisema katika [Al-Mughniy 7/99]: 

"Hakuna tofauti ya rai za maulamaa kuhusu kuruhusiwa kuwaoa wanawake wa Kitabu. Na miongoni mwa walio na rai  hii ambayo ilisimuliwa kutoka  kwao ni 'Umar, 'Uthmaan, Talhah, Hudhayfah, Salmaan, Jaabir na wengineo". 

Ibn Al-Mundhir kasema:  

"Hakuna usimulizi ulio sahihi kutoka kizazi cha mwanzo kusema kwamba hivyo ni haraam. Al-Khallaal amesimulia katika Isnaad yake kwamba Hudhayfah, Talhah, Al-Jaaruud ibn Al-Mu'alla na Udhaynah Al-'Abdi wote walioa wanawake wa Ahlul-Kitaab. Hii pia ilikuwa ni rai ya Maulamaa wengine wote".

 

Ushahidi mkuu kuhusu masuala haya ni Aayah ambayo Allaah سبحانه وتعالى  Anasema (Na imefasiriwa kuwa na maana):

 ((الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلُّ لَّهُمْ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلاَ مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ وَمَن يَكْفُرْ بِالإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ))

((Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. (vitu vyote vilivyo halaal, katika chakula Allaah Alichokifanya halaal kama nyama iliyochinjwa, maziwa, mafuta, mboga, matunda) Na chakula (Wanyama waliochinjwa na wengine wanolika) cha waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manaswara) ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manaswara) kabla yenu, mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uasherati wala kuwaweka kinyumba. Na anayekataa kuamini (Tawhiyd ya Allaah na nguzo zote za Imani yaani kuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, Siku ya kufufuliwa, na Qadhaa na Qadar) bila shaka amali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara)) [Al-Maaidah: 5]

 

 

Masharti ya kuwaoa Ahlul-Kitaab

 

Sharti La Kwanza:

 

Lakini kuna sharti ya kuwaoa hao kama ilivyo katika Aayah kuwa: (wanawake wema miongoni mwa waliopewa Kitabu)

 

Abu Ja'afar Muhammad ibn Jariyr At-Twabariy ametoa maana ya 'muhswana' (mwema) katika Jaami' Al-Bayaan Ta-wiyl Aayatil-Qur-aan 8/165. "Muhswana ina maana kwamba ni mwanamke ambaye mwema aliyesitirika na msafi (kutokana na machafu ya zinaa) ambaye anajihifadhi sehemu zake za siri kutokana na kitendo cha Zinaa kama Aayah inavyosema:

((وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا))

(Na Maryam binti wa 'Imraan, aliyelinda ubikira wake)) [At-Tahriym: 12]

Kwa maana kwamba amejilinda na kila kitendo chenye shaka na amejihifadhi na mwenendo wa uasherati. 

 

Vile vile maana ya Muhswanaat (wanawake wema) ni wale ambao walio huru na walio katika stara. (Yaani katika heshima na aliye bikra, asiye mhuni) Ibn Kathiyr (Allaah Amrehemu) amesema katika Tafsiyr yake:

"Hii ni rai ya Maulamaa wengi wao na hii ndivyo inavyoelekea kuwa hali yenyewe.  Asije kuwa dhimiyah (mwanamke asiye Muislam aliye katika hifadhi ya Kiislam) lakini pia asiyekuwa katika stara (heshima, bikra). Ikiwa atakuwa katika hali hii atakuwa amepotoka na mwenye ufisadi, na mumewe atamalizikia kuwa kama inavyoeleza katika methali: "Amenunua tende mbaya na amekhiniwa katika uzito na mizani pia".

 

Maana iliyo dhahiri katika aayah ni vile ilivyomaanisha "al-Muhswanah" (mwanamke mwenye stara, (aliyekuwa bikra, asiyekuwa mhuni) naye ni mwanamke aliyejiepusha na zinaa kama Allaah سبحانه وتعالى Anavyosema katika Aayah nyingine:

((مُحْصَنَاتٍ غَيْرَ مُسَافِحَاتٍ وَلاَ مُتَّخِذَاتِ أَخْدَانٍ))

((….wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara)) [An-Nisaa: 4:21]

 

Lakini tunasisitiza kuwa ni mwanamume pekee anayeweza kufunga ndoa na Ahlul-Kitaab, ama mwanamke wa Kiislamu haruhusiwi kuolewa na mwanamume wa Ahlul-Kitaab

 

Sharti Ya Pili:

 

Ni kwamba mwanamume awe ndiye mwenye mas-uliyah na nyumba na watoto, kwani kwa Hikma ya Allaah سبحانه وتعالى  Amemfanya   mume awe kiongozi wa nyumba kwa sababu itakuwa ni wepesi kwake kumuongoza mkewe. Na inabidi Muislamu anapooa Ahlul-Kitaab ajitahidi awezavyo kumuongoza katika dini ya Uislamu.

 

Sharti Ya Tatu:

 

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amependekeza Muislamu aoe wanawake Waislamu walioshika dini. Kwa hiyo kwanza ni kufanya jitihada ya kuwaoa wanawake Waislamu walioshika dini kisha tena kama haikuwezekana ndio aelekee kwa Ahlul-Kitaab.      

Na ifahamike kuwa ni bora na usalama kabisa kutokuoa wanawake wa Kitabu khaswa kwa siku hizi ila ikiwa atakubali kusilimu kisha atazamwe tabia yake na kama ataendeleza dini yake sawa sawa. 

 

Ibn Qudaamah (Allaah Amerehemu) alisema:  Kwa vile hali ni hii, ni bora kutokuoa mwanamke wa Kitabu kwa sababu 'Umar aliwaambia wale waliowaoa wanawake wa Kitabu "Waacheni (Wapeni talaka)" kwa hiyo wakawapa talaka isipokuwa Hudhayfah. 'Umar akamuambia: "Mpe talaka".  (Hudhayfah) akasema:  "Je, Unashuhudia kuwa yeye ni haraam?"  Akasema:  "Yeye ni mkaa wa moto wenye kuwaka, mpe talaka".  Akasema:  "Je, Unashuhudia kuwa yeye ni haraam?"  Akasema:  "Yeye ni mkaa wa moto wenye kuwaka". Akasema: "Najua kuwa yeye ni mkaa wa moto wenye kuwaka lakini yeye ni halali kwangu". Baada ya muda akampa talaka na akaulizwa "Kwa nini hukumpa talaka alipokuamrisha 'Umar?" Akasema:  "Sikutaka watu wafikiri kuwa nimefanya kosa (kwa kumuoa)". 

Labda alikuwa akimpenda au labda kwa sababu walipata mtoto pamoja kwa hiyo alimpenda". [Al-Mughniy 7/99]

 

Vile vile Hadiyth hii ifuatayo Sahiyh inasema:

((Ibn 'Umar alipokuwa akiulizwa kuhusu kumuoa mwanamke Mkiristo au Myahudi, alikuwa akisema: "Allaah Ameifanya kuwa ni Haraam kwa Muumini kuoa wanawake wanaomshirikisha Allaah katika ibada, na sijui lililo kubwa zaidi kuliko kumshirikisha Allaah katika ibada na kadhalika kama mwanamke kusema 'Iysaa ni Mungu ingawa yeye ni mja tu wa Allaah"))  [Al-Bukhaariy]

 

Shaykh Ibn Baaz (Allaah Amrehemu) alisema:  "Ikiwa mwanamke wa Kitabu anajulikana kuwa ni mwenye stara (sio muhuni) na kujiepusha na njia ambazo zinampeleka mtu katika uasherati, inaruhusiwa kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Ameruhusu hivyo na Ameturuhusu kuwaoa wanawake wao na kula nyama zao.

 

Lakini siku hizi kuna khofu kwamba wale wanaooa huenda wakakutana na uovu zaidi. Wanaweza kuwaita katika dini yao na wanaweza kuwalea watoto wao katika Ukristo.  Kwa hiyo hatari ipo hakika na ni kubwa. Ili kuwa katika amani, Muumini ni bora asiwaoe. Na katika hali nyingi hakuna uhakika kama mwanamke hatofanya vitendo vya uasherati au hatowaleta watoto waliotoka katika uhusiano wa mwanzo. Lakini mwanamume akitaka kufanya hivyo basi hana dhambi kwake ili ajiweke katika stara na ainamishe macho yake kwa kumuoa. Ajitahidi kumuita katika Uislamu na awe na hadhari na uovu wake na hadhari ya kumruhusu asimvute yeye au watoto wake katika ukafiri". [Fataawa Islaamiyyah, 3/172]

 

 

Hivi Sasa Je, Tunao Ahlul-Kitaab?

 

Hivi sasa tunao Ahlul-Kitaab nao ni Wakristo na Mayahudi. Lakini wao wamekufuru na kumshirikisha Allah. Kwa hiyo ni makafiri na washirikina, kutokana na Qur-aan.

 

((اتَّخَذُواْ أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُواْ إِلاَّ لِيَعْبُدُواْ إِلَهًا وَاحِدًا لاَّ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ))

((Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Allaah, na pia Masiyh bin Maryam. Na wala hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayomshirikisha nayo)) [At-Tawbah: 9:31] 

 

Lakini wametolewa katika kuharamishwa kuolewa wanawake wao kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Anasema katika aayah yenye maana:

((وَلاَ تَنكِحُواْ الْمُشْرِكَاتِ حَتَّى يُؤْمِنَّ وَلأَمَةٌ مُّؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ وَلاَ تُنكِحُواْ الْمُشِرِكِينَ حَتَّى يُؤْمِنُواْ وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ أُوْلَئِكَ يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ وَاللّهُ يَدْعُوَ إِلَى الْجَنَّةِ وَالْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِ وَيُبَيِّنُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ))

((Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanawaitia kwenye Moto, na Allaah Anawaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini Yake. Naye Huzibainisha Aayah zake kwa watu ili wapate kukumbuka)) [Al-Baqarah: 2:221]

 

Washirikina waliotajwa katika Aayah hii ni wale walio nje ya Ahlul-Kitaab mfano Baniani, Majusi, Mabudha na kadhalika.    

 

Kwa hiyo 'Watu wa Vitabu' ni makafiri na washirikina, lakini Allaah سبحانه وتعالى Ameturuhusu kula nyama zao na kuwaoa wanawake wao ikiwa watakuwa wenye stara (wenye heshima sio wahuni). Hii imeruhusiwa kutokana na maana ya Aayah iliyo katika Suratul-Baqarah 2:221 (tulioitaja hapo juu).

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

 

 

Share