Kwa Nini Watoto Wa Nabii Ibrahiym Tofauti Kwa Ukabila?

 

SWALI:

assalamu  alaykum ningependa kujua  kwamba  kwanini watoto wa nabii ibrahim ni tofauti mmoja ni baba wa waarabu na mwengine  ni baba wa majushi  sasa ningependa munifahamishe kwanini iwe hivyo assalamu alykum


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwako ewe ndugu yetu kwa swali lako zuri. Bila shaka inaeleweka kuwa sote (wanaadamu) tu ndugu katika ubinadamu kwani baba yetu ni mmoja. Kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akatujaalia kuongozeka kwa kiasi kikubwa sana. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Enyi watu! Mcheni Mola wenu Ambaye Amekuumbeni katika nafsi moja. Na Akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na Akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni Allaah ambaye kwaye mnaombana” (4: 1).

Kwa uwezo Wake pia Akatufanya kutoka na mwanamme mmoja na mwanamke mmoja kuwa mataifa na makabila tofauti ili tupate kujuana wala sio kukejeliana (49: 13). Tunaweza kujiuliza vipi sote tumetokana na Nabii Aadam (‘Alayhis Salaam) na mkewe Hawwaa na sasa tumekuwa watu wa makabila na lugha tofauti? Kwa nini tusiwe wa kabila moja? Jawabu la hii ni ile kauli ya Allaah Aliyetukuka: “Na katika Ishara Zake (za kuonyesha uweza Wake) ni kuumba mbingu na ardhi, na kuhitilafiana ligha na rangi zenu. Kwa yakini katika haya zimo Ishara kwa wenye ujuzi” (30: 22).

Na kutuonyesha uwezo Wake (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Lau Angependa Mola Wako  Angewajaalia watu wote kuwa Ummah mmoja lakini wanaendelea kutofautiana” (11: 118).

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Alimpatia mwanaadamu ufahamu na elimu ya vitu vyote kwa kuweza kuvipatia majina ili kwayo aweze kufundisha wengine na kutoa majina kwa vinavyokuja baadaye. Kwa njia hii wanaadamu wakaweza kwa kila kizazi kilipokuwa kinazaana kujipatia jina la familia hiyo.

Tukija kwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) inaeleweka kuwa alikuwa na wake wawili ambao kwao alipata watoto wawili waliopata umaarufu na kuchaguliwa kuwa ni Manabii – Ismaa‘iyl na Is-haaq (‘Alayhimas Salaam). Kwa vile aliye mkubwa alipelekwa na kukulia katika wangwa wa Makkah ulio Saudi Arabia sasa, naye (Nabii Isma‘iyl) na huko akaoa mke wa Kiarabu, alipachikwa Uarabu na hilo ndilo lililoenea. Ndio kwake alizaliwa katika kizazi cha baadaye aliyekuwa maarufu kwa jina Quraysh mpaka watu hao wa Makkah wakawa wanaitwa ma-Quraysh. Huyu Quraysh naye katika vizazi vyake vya baadaye alikuwa na waliopata umaaraufu mkubwa katika historia yao mpaka kila aliyepata umaarufu familia na ukoo wake ukatangaa kwa jina lake lililokuwa ndilo jina la ukoo kwa waliokuja baadaye kama Bani (ukoo au wana) Haashim, Bani Umayyah, Bani al-Muttwalib, Bani Zuhrah, Bani Taym, Bani ‘Adiyy, Bani ‘Abdil-Manaaf, Bani ‘Abdid-Daar na kadhalika.

Tukichukua mtoto wa Nabii Ibraahiym, yaani Is-haaq (‘Alayhis Salaam) jina lake halikutangaa sana hivyo halikuweza kufanya kabila au ukoo. Lakini mtoto wake kwa jina Ya‘quub (‘Alayhis Salaam) aliyejulikana kwa jina lake maarufu la Israaiyl ndiye aliyekuwa chanzo cha kizazi cha watoto 12. Baba na watoto wake walitangaa na kuwa maarufu. Kwa kuwa Manabii wengi waliokuja baada ya Ya‘quub (‘Alayhis Salaam) walikuwa ma-Nabii isipokuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa ajili hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akawa Anawaita kwa jina la Bani Israaiyl (Wana wa Israili). Hakika ni kuwa mtoto wake hakuwa ni baba wa Majusi au kama ulivyoandika kimakosa Majushi kwani hao walikuwa ni waabudu moto waliokuwa wakiishi zaidi katika nchi ya Iran. Bani Israaiyl walikuwa ni mchanganyiko wa kizazi cha Nabii Ya‘quub (‘Alayhis Salaam), miongoni mwao wapo Waumini na wengine walio wengi makafiri. Waliokufuru miongoni mwao wanaitwa Mayahudi.

Kwa ufupi hapana tatizo katika hilo kwani ni elimu moja aliyopatiwa mwanaadamu na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Hiyo pia ni kuonyesha dalili za kuwepo Yeye Aliyetukuka, miujiza Yake na uwezo Wake ulio mkubwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share