Mahdi Atakayekuja Kutuongoza Ni Nani?

SWALI:

 

Swali langu huyu Mahdi ni nani katika Uislamu mwenzanu anasema ni kiongozi atakaye kuja kutuongoza kabla ya nabi issa je ni kweli?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu Mahdi anayetarajiwa nasi Waislamu. Zipo Hadiyth nyingi za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinazotufahamisha kumhusu.

 

Kwa muhtasari ni kuwa Mahdi ni mtu ambaye atakuja mwisho wa wakati kabla Qiyaamah. Ujio wake ni miongoni mwa alama kubwa za Qiyaamah. Jina lake litakuwa kama la kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yaani ataitwa Muhammad bin ‘Abdillaah. Atakuwa katika ukoo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Atakapokuwepo yeye hapa ulimwenguni ndio Allaah Aliyetukuka Atamtuma Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam). Atakapoteremka Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) huko Damascus itakuwa ni wakati wa Swalah ya Alfajiri na Imaam atakuwa ndio anajitayarisha kuswalishwa. Imaam atakapomuona Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) atataka kumwachia aswalishe lakini Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) atakataa na kumuacha Imaam ndiye awe ni mwenye kuswalisha. Mahdi atakuwa ndiye mwenye kurudisha amani na usalama katika ulimwengu na kuutawala Kiislamu.

 

Hadiyth kumhusu Mahdi ni hizi zifuatazo:

"Hakutakosekana kuwa na kikundi katika Ummah wangu, wakipigana juu ya haki wakiwa washindi haki Siku ya Qiyaamah… kisha 'Iysaa bin Maryam atashuka, na Amiri wao (Waislamu) atasema: 'Njoo utuswalishe katika Swalah!' Atasema: 'Hapana, nyinyi ndio ma-Amiri juu ya kila mmoja kama heshima kutoka kwa Allaah kwa Ummah huu'" (Muslim).

 

Hadiyth hiyo iko katika Swahiyh Muslim na imepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma). Hadiyth hiyo ni sahihi kabisa na haina tashwishi yoyote ile.

 

Na makusudio hapo juu kwenye Hadiyth kwa neno' "Amiri wao (Waislamu) atasema: "Njoo utaswalishe katika Swalah", makusudio hapo 'Amiri' ni Mahdi. Kutokana na mapokezi yaliyosimuliwa na Abu Na'iym na Al-Haarith bin Usaamah, yanasema hivi: "Amiri au Kiongozi wao Mahdi atasema..." Ibnul-Qayyim anasema, "Isnaad yake ni Nzuri."

Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Lau siku moja tu itabakia kwa huu ulimwengu, Allaah Atairefusha siku hiyo, mpaka Amlete mtu aliyetokamana nami au familia yangu ambaye jina la babake litakuwa sawa na babangu. Naye mtu huyo atajaza usawa na uadilifu kama ilivyokuwa imejaa unyanyasaji na dhuluma." [Abuu Daawuwd]. Hapa kunatajwa kuja kwa Mahdi.

 

Katika Hadiyth nyingine, Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anha) amehadithia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mahdi atakuwa katika familia yangu, katika kizazi cha Faatwimah." [Abu Daawuud na Ibn Maajah].

 

Muhimu ifahamike kuwa huyo Mahdi aliyetajwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), si Mahdi anayetajwa na Mashia, kwani wa Mashia wao ni wa kutungwa na wanadai kuwa yupo kajificha pangoni kwa miaka 1200 sasa na hawajui atatoka lini!!

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share