Aliy (رضي الله عنه) Alimpa Bay'ah (Ahadi Ya Makubaliano) Abu Bakr (رضي الله عنه)?

 

SWALI:

Mwanzo ningependa kumshukuru Allah(subhanahu wataala)kwa kuwezab kutujumuisha na kutunufaisha kwa website hii aliyoipa nguvu na kuendeleza kwa kheri na ninawashkuru sana ndugu zangu kwa kumtumikia Allah (subhanahu wataala), Allah (subhanahu wataala awajaaliye kila la kheri inshaallah. ndugu yangu nina suala ambalo linanitatiza mno na suala lenyewe ni hivi, Je sayyidna Ali na nana Fatma (radhiyallahu anhum) walimbai Abubakar Assidiq (radhiyallahu anh)? na waliridhika ukhalifa wake.naomba munifafanulie tafadhalini,Jazakumullah

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 Shukurani kwa swali lako. Na ili  kukusaidia kukuondosha kwenye huu utata unaoletwa na Marafidhah (Mashia) ashughulisha Waislamu kwa kuwaingizia watu utata na mashaka kwenye Dini yao.

 Hakika inavyojulikana na ilivyo kwenye vitabu vya Kihistoria ni kuwa 'Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) alimpa bay'ah Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) mara mbili. Mara ya kwanza ni baada ya siku mbili na mara ya pili inasemekana ni baada ya miezi sita, alifanya hivyo kuijadidi bay'ah yake ili kufuta yale yaliyojiri kuhusiana na tukio la ardhi ya Fadak ambalo unaweza kulisoma hapa:

 Kisa Cha Ardhi Ya Fadak - Baina Ya Abu Bakr Asw-Swiddiyq Na Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘Anhuma)

Na hata vitabu vya Marafidhah wenyewe vinasema hayo, soma nukuu hizi zifuatazo:

Atw-Twabrasiy amesimulia kutoka kwa Imaam Muhammad Baaqir kwamba Usaamah alipokwenda kwenye Jihaad, Mtume wa Allaah akafariki, habari zilimfikia Usaamah, akarejea na jeshi lake Madiynah. Akaona kundi kubwa limemzunguka Abu Bakr; alipoona hilo, akaenda kumuuliza 'Aliy bin Abi Twaalib na akamuuliza: "Nini hiki?" 'Aliy bin Abi Twaalib akamjibu: "Ni kama hivyo unavyoona!" Usaamah akamuuliza: " Je, wewe vilevile ulimpa bay'ah yako yeye (Abu Bakr)?" 'Aliy bin Abi Twaalib akamjibu: "Ndio."

[Al-Ihtijaaj, uk.50, Iliyochapishwa Mashad, Iraq]

 Na vilevile kitabu kingine cha Mashia kinaeleza:

'Ali bin Abi Twaalib alimwambia Az-Zubayr: "(Japokuwa) tulipatwa na hasira wakati wa mashauriano (ya Saqiyfah), tunaona kuwa Abu Bakr ni mwenye kustahiki zaidi kuwa Khaliyfah; alikuwa ni Swahaba wa mjumbe wa Allaah katika pango. Tunajua kuhusu maisha yake na tunajua kuwa Mjumbe wa Allaah alimuamrisha kuswalisha (kuwa Imaam wa Swalah) wakati wa uhai wake (Mtume)." Kisha ('Aliy) akampa bay'ah (Abu Bakr). [Sharh Nahjil Balaaghah, Ibn Abil Hadiyd; Mjalada 1, uk.132]. Nahjul Balaaghah ni kitabu maarufu cha Kishia.

Kwa hiyo ukweli wa habari hizo uko kwenye vitabu vya Ahlus Sunnah na hata kwenye vitabu vya hao Mashia ingawa wenyewe ima wanapotosha makusudi au hawajui yaliyomo ndani ya vitabu vyao, na wakiyaona hayo huja kuyakataa au kuyasema kama ada yao siku zote wanapokamatwa kwa hoja, hudai kuwa hakuna kitabu sahihi isipokuwa Qur-aan!! Lakini wanapopata hoja ya kuwaunga wao mkono kwa madai yao, basi kitabu hicho walichopatia hoja yao, kinakuwa sahihi japo si Qur-aan!!!

 

Hiyo ndio hali ya Mashia malaghai wababaishaji wapotoshaji.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share