Mauaji Ya Palestina


SWALI:

 

Salam alaikum,

Mimi ninaumwa sana na dhuluma na mauaji yanayofanywa na Israel kwa Palestine.  Swali langu ni hili wale waliouawa wana ujira gani kwa ALLAH?  Je, wataweza kusameheka madhambi yao yaliyopita kwasababu wamedhulumiwa nafsi zao?

Napenda kujua pia hawa Waisrael wana hukmu gani kwa Allah kwa mauaji haya?

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Shukrani kwa swali lako hilo kuhusu Mashariki ya Kati hasa nchi za Palestina na Lebanon ambamo kwa sasa mauaji ya kinyama yanaendelea bila ya kusita. Hii ni dhulma ya wazi na hata wasiokuwa Waislamu wenye utu wamekerwa sana na hilo na kutaka wanaadamu wote wasusie bidhaa za Israel na Marekani kwa ujumla ambao ndio wanaosaidia sana mauaji hayo. Wasioona udhalimu huu wa dhahiri ni wanyama wasiokuwa na ustaarabu wa aina yoyote.

Ni sikitiko kuona kuwa nchi za Waislamu mbali ya kuwa wana mali nyingi na silaha za kutosha hawajaweza hata kupeleka usaidizi wa kijeshi na misaada mingine muhimu. Hata kukata uhusiano wa kibalozi wameshindwa. Mbali na hivyo wamezidi kuimarisha mipaka yao na Israel ili hata misaada isiingie kutoka nchi zao kwenda kusaidia Palestina.

Kuja katika swali lako ni kuwa wale waliouliwa na udhalimu wa kibepari wakitetea haki zao na huku wakiwa ni Waislamu Waumini basi jazaa yao ni kubwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Hii ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema:

Hakika Mimi sitapoteza juhudi (amali) ya mfanya juhudi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke” (3: 195).

Na Amesema tena kwa uwazi zaidi,

Wafanyaji wema, wanaume na wanawake, hali ya kuwa ni Waumini, Tutawahuisha maisha mema, na Tutawapa ujira wao Akhera mkubwa kabisa kwa sababu ya yale mema waliyokuwa wakiyatenda” (16: 97).

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea kuhusu mashuhadaa wa Ummah wake katika Hadiyth tofauti, miongoni mwayo ni:

Imepokewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu tauni? Akasema: “Ilikuwa adhabu ya Allaah ikiwashukia waliokuwa kabla yenu, Allaah Akaijaalia kuwa ni rehema kwa Waumini. Hakuna mja atakayekuwa ndani ya mji wenye (tauni), akakaa humo ndani bila ya kutoka, huku akiwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Anafahamu kuwa hakuna chenye kumsibu isipokuwa aliyomuandikia Allaah ila anakuwa na ujira kama wa shahidi (anayeuliwa katika Jihaad)” (Al-Bukhaariy).

Na amesema Sa‘iyd bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu), nimemsikia Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Mwenye kuuliwa kwa ajili ya (kutetea) mali yake ni shahidi, mwenye kuuliwa kwa ajili ya damu yake ni shahidi, na mwenye kuuliwa kwa ajili ya dini yake ni shahidi, na mwenye kuuliwa kwa ajili ya familia yake pia ni shahidi” (Abu Daawuud, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Amesema Suwayd ibn Muqarrin (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuuliwa kwa kudhulumiwa ni shahidi” (An-Nasaaiy).

Hivyo, tunaona jinsi gani wale Waislamu wenye kuishi nchi za dhulma nao wakasubiri katika hilo pamoja na kufuata maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuacha makatazo yao watakavyopata ujira mkubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka.

 

 

Kwetu sisi tusiwasahau ndugu zetu kwa du'aa pamoja ma kuwasadia kwa njia mbalimbali na kususia bidhaa za maadui.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share