Ni Nani Wana Wa Israaiyl Na Ipi Nchi Yao?

SWALI

A/Alaykum: Ndugu zangu naomba kuuliza habari   Kuhusu  Wana-israil. Swali langu ni Kua hii Israil ni ya watu gani. Na kama sio hao waisrail: Je? Wanastahiki kuwepo sehemu gani walioahidiwa ikiwa ni kama nchi yao kihali.Maana tunafahu ya kwamba. Nabii Issa (A.S) alikuja kwa ajili ya Kondoo Waliopotea au Wanaisrail.Kama sijakosea hapo. Na Huyu Nabii Issa (a.s) alipokuja kwa ajili ya wanaisrail Ilikua ni nchi ipi. Na Wanaisrail wakati hou si walikua na nchi,.Kiufupi nilikua nataka kujua tu hawa waisrail nchi yao ni ipi.au wanatakiwa wachaganyike na wapelestina ikiwa ni kama nchi moja. Mungu Awabarik kwa kazi yenu ya kujitolea.kwa kuwafahamisha Ndugu zetu wa kiislamu na waliokua si waislamu. 

Waasalam Alaykum   Warahmatul llway wabarakat.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani sana ndugu yetu kwa swali lako hilo ambalo ni zuri na muhimu sana kwa Waislamu kuweza kulifahamu. Waislamu wengi suala hili tumekuwa hatulielewi kabisa au tunalielewa wanavyotaka walowezi wa Kizeyuni na washirika wao wa karibu walio Marekani katika madhehebu ya kimisheni ya kisasa.

Mwanzo tungependa kutoa taarifa fupi kuhusiana na ibara tatu: Wana wa Israili, Mayahudi na Wazeyuni.

Wana wa Israili ni kabila la jamii iliyozalikana na Nabii Ya‘quub (‘Alayhis Salaam) ambaye jina lake jengine lilikuwa ni Israil. Hivyo, kizazi cha watoto wake kumi na wawili kikawa kinaitwa Bani Israili (Wana wa Israili). Miongoni mwao wapo Waislamu kuanzia enzi hizo za awali na wengine ni makafiri.

Mayahudi ni makafiri kati ya Wana wa Israili. Katika hili Anatuelezea Allaah Aliyetukuka: “Walialaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa Wana wa Isarili kwa ulimi wa Daawuud na ‘Iysa bin Maryam. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakapindukia mipaka” (5: 78).

Pia, “Tukambarikia yeye (Ibraahiym) na Is-haaq. Na katika kizazi chao walitokea watendao wema na wanaodhulumu nafsi zao waziwazi” (37: 113).

Ama Uzeyuni ni chama cha kisiasa kilichoanzishwa na Dkt. Theodore Herzl mwaka wa 1895 chenye uana memba wa Mayahudi pekee. Malengo yao yako wazi kabisa na lengo la msingi ni kuiteka na kuitawala Palestina milele. Nchi ambayo wanataka kuifanya ni ya Mayahudi pekee kusiwe na watu aina nyengine yoyote.

Jambo ambalo tunatakiwa tulifahamu ni kuwa wengi miongoni mwa wanaojiita Mayahudi au Wana wa Israili sasa si Waisraili kidamu. Hawa wengi wao ni wale walioingia katika Uyahudi takriban karne kumi na moja iliyopita, lakini kwa maslahi yao wenyewe wakawa wanajiita kuwa wao pia ni Mayahudi. Jambo hili limeyakinishwa na watafiti hata wasiokuwa Waislamu. Tukiangaza katika ulimwengu sasa huenda tukajiuliza, je, wazawa halisi wa Nabii Ibrahim ni wapi? Hebu tutizame nukuu zifuatazo:

“Huwezi kufanya mapatano baina ya pande mbili ukiwa wewe ndiye mwenye matatizo. Amerika haiwezi kutatua tatizo kwa sababu ilisaidia kuanzisha kwa hila iliyo wazi na lengo ambalo litaendelea kuihudumikia vyema. Hii ilitokana na mfoko wa wasiwasi wa karne ya 19 kwa Wazeyuni wa Kizungu – mapambano ya Mayahudi wa Kaukazi (Caucasian) [1] kuanzisha ‘Nyumba ya Mayahudi’ nje ya mabara ya Amerika na Ulaya.

Kweli, kafara ya Hitler ilikuwa ya siku za usoni. Lakini ilicheza dauru muhimu na kuu kwa mataifa ya Kikristo kugeuza ghafula muelekeo wao kwa Mayahudi. Japo kuwa uzio kwa Mayahudi ulibaki mkali, hisia za hatia zilianza kupenya katika dhamiri za Wazungu.  Kwa nini tusiutumie Uzeyuni na tuue ndege wawili kwa jiwe moja? Wasaidie Mayahudi kupata nchi mbali na Bara Ulaya mahabubu, na kwa hivyo punguza hatia na ondoa uzio. Wazeyuni walijitoa kutumiwa na wanyanyasaji wao wa awali na kuwa ala ya kuwaibia na kuwatesa watu wengine kabisa – Waarabu. Kwa muda mrefu tumemeza madai ya ulaghai na udanganyifu wa Uzeyuni kuwa Mayahudi wa Ulaya ni Wasemiti – dhuria wa Judah (Yudah).

Matendo ya Israili yanathibitisha hayo. Mayahudi wote ambao si Wazungu (wale wanaohamia Israili kutoka mataifa ya Kiarabu na Afrika kuanzia 1948, kama Wafalasha kutoka Habeshi) ni raia wa daraja la pili. Ni kwa nini Israili inacheza michuano ya kimataifa ya kandanda katika Bara Ulaya na wala sio Bara la Asia? Ahadi za Amerika hazivunjwi bali zinatekelezwa vilivyo. Usaidizi wake kwa Israili ni mwingi zaidi kuliko nchi zote zilizobaki zikichanganywa pamoja. Mbali na fedha taslimu, [2] kuna elimu nyeti ya kisayansi, teknolojia na ya kivita ambayo Amerika haithubutu wala kubahatisha kuipatia taifa lolote” (Why American Arbitration is Fraudulent (Kwa Nini Usuluhishi wa Amerika ni wa Udanganyifu, Sunday Nation, Nairobi, April 21, 2002, uk. 9).

Uhusiano wa Mayahudi kiutendaji ulikatika kabisa Palestina kwa takribani miaka 1,800 (yaani kuanzia 135 BI mpaka karne ya ishirini). Katika kipindi hiki, hawakuwa na nguvu wala uwezo wa kisiasa au kitamaduni au wa uongozi, bali walikatazwa kabisa na mafundisho ya dini yao kurudi huko. Na zaidi ya 80% ya Mayahudi wa wakati huu, kulingana na utafiti wa Mayahudi wenyewe, mfano wa mwandishi mashuhuri Arthur Koestler, hawana uhusiano wowote wa kihistoria na Palestina. Hivyo hivyo, hawana uhusiano wowote wa kinasaba na Banu Israili. Mayahudi wengi leo wanatokana na kizazi chenye asili ya Khazari (Ashkenazi), ambao ni katika kabila la Tatari-Waturuki wa kale waliokuwa wakiishi kaskazini mwa Kaukazi walioingia Uyahudini katika karne ya nane Miladi (M). Ikiwa kamwe Mayahudi wana haki ya kurudi basi sio Palestina bali ni kusini mwa Urusi.

Kuongezea ni kwamba dai lao la mafungamano na uhusiano na Palestina haliwezi kusimama mbele ya hakika kuwa Banu Israili wengi walikataa kumuunga Nabii Musa (‘Alayhis Salaam) katika safari ya kwenda ardhi tukufu. Hivyo hivyo, wengi wao walikataa kurudi Palestina kutoka Babeli baada ya Mfalme Cyrus alipojitolea na kuahidi kuwalinda. Na katika historia yao yote mpaka leo, idadi ya Mayahudi wanaokaa Palestina hawazidi 40% ya Mayahudi duniani hata katika kipindi chao kizuri na bora zaidi.

Sasa tukija katika sehemu waliyoahidiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) walipokuwa wako Misri utumwani wakati wa Nabii Musa (‘Alayhis Salaam) ni Palestina wala Israili kwani wakati huo kulikuwa hakuna nchi hiyo katika ulimwengu. Hasa katika miaka hiyo eneo hilo lilikuwa likiitwa ardhi ya Wakanaani. Ahadi waliyopatiwa wao ni kama ifuatayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema kupitia kwa ulimi wa Nabii Musa (‘Alayhis Salaam): “Enyi watu wangu! Ingieni katika hiyo ardhi iliyotakaswa ambayo Allaah Amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika” (5: 21).

Amesema al-Kalby: Ardhi tukufu ni Damascus, Palestina na baadhi ya sehemu za Jordan. Amesema Qatadah: Hiyo ni Shaam yote (Dkt. Muhsin Muhammad Swaalih, At-Tareeq ilal Quds, Filistinul Muslimah, Chapa ya kwanza, uk. 56). Ama mufasirina wengine wanasema kuwa hiyo ni ardhi ya Palestina.

Je, hii aya imewapatia Mayahudi wirathi wa moja kwa moja katika ardhi ya Palestina? Je, huu ni wirathi wa majukumu au wa damu? Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kuhusu Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) amesema: “Na pindi Mola wako alimpomfanyia Nabii Ibraahiym mtihani kwa Amri nyingi, naye akatimiza. Akamwambia: ‘Hakika Mimi nitakufanya kiongozi wa watu’. Ibraahiym akasema: ‘Je, na katika kizazi changu pia?’ Akasema: ‘Ndio lakini ahadi Yangu haitawafikia madhalimu wa nafsi zao” (2: 124).

Kwa hivyo ahadi ya Allaah haiwachanganyi madhalimu. Ni udhalimu gani ulio mkubwa kuliko kukufuru na kueneza uharibifu katika ardhi ambao unashinda ule wa Bani Israili uliofanywa na unaofanywa. Kuna dhulma gani kuliko ya Maisraili kuwafanyia ndugu zetu wa Palestina. Lakini ni Sunnah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kuwapatia nguvu madhalimu ili wawatie adabu Waumini ili waweze kurudi katika njia sahihi ya Uislamu. hili ni fundisho kwetu na kurudi kwetu katika utukufu na nguvu ni kushikamana kwetu na Qur-aan na Sunnah.

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza kuhusu kuhama kwa Nabii Ibraahiym na Luut (‘Alayhimas Salaam):

Na tulimuokoa yeye (Nabii Ibraahiym) na Luut tukampeleka kwenye ardhi tuliyoibariki kwa ajili ya ulimwengu wote” (21: 71).

Katika msafara wao huu kutoka Ur, Iraq walipitia kusini mwa Uturuki, kaskazini mwa Syria na baadae Nablus kisha Ramallaah baadae al-Quds, kisha Bi-ir Sab-a na kumalizika kwa safari yao huko Misri. Wakati wa kurudi kutoka Misri walipitia Gaza kisha wakachukua njia baina ya Bi-ir Sab-a na Khaliyl (Hebron) na baadae kufanya makazi yake katika mji wa Khaliyl. Wale wana wa Israili wa asili ikiwa wana haki ya kurudi basi warudi Ur na wale ambao hawana damu ya Israili warudi Urusi.

Ni kweli kabisa kuwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) alizaliwa, kuishi na kufanya Da‘wah yake katika nchi ya Palestina. Na yeye alitumwa kuwaongoza Wana wa Israili pamoja na kuwaita katika Uislamu ama ibara ya kondoo waliopotea ni ya Biblia na wala sio katika machimbuko ya sharia yetu. Lakini inatakiwa ifahamike kuwa kuwepo kwake katika nchi hiyo haimaanishi kuwa ni ya kwao, Wana wa Israili. Leo wapo watu wengi kutoka Afrika Mashariki waliohamia nchi za ng’ambo (Marekani na Bara Ulaya) kwa sababu moja au nyengine mpaka wakapata uraia wa nchi hizo. Je, watu hawa hudai kuwa nchi hizo ni za kwao? Jambo hili haliingii katika mizani ya mantiki. Tunafahamu kuwa alipozaliwa Nabii ‘Isa (‘Alayhis Salaam) nchi hiyo ya Kanaani ilikuwa inatawaliwa na Kaesari (Dola ya Kirumi) na wana wa Israili hawakuwa ni wenye kuwa na mamlaka aina yoyote. Tufahamu kuwa wakati huo kulikuwa katika nchi hiyo makabila kadhaa yasiyokuwa ya Kiisraili. Sasa ni hoja gani ambayo tutaweza kutoa kuonyesha kuwa ardhi hiyo ilikuwa yao.

Sasa sisi Waislamu tuko chini ya mashambulizi ya vyombo vya habari ambazo zinapotosha uhakika wa mambo. Ni hakika ya kihistoria kuwa Waisraili walitawala kwa kipindi kifupi sana katika nchi ya Palestina. Hakika ni kuwa Waislamu wameamriwa wawafanyie wema watu wa Kitabu, na bila shaka yoyote waliwatendea wema wa hali ya juu ambao haukuonekana katika historia ya mwanadamu. ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliposafiri kutoka Madiynah kuelekea al-Quds ili kukabidhiwa funguo za mji wa al-Quds kutoka kwa kasisi wa Kirumi, Sophronius mwaka 15 H (636 M) walitia saini mkataba ambao ulijulikana kwa jina “Mkataba wa ‘Umar”. Wakristo wakati ule kuona njama na ukaidi wa Waisraili walimwambia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) asiwaruhusu kabisa Waisraili kuishi katika mji wa al-Quds kwani wataleta zogo kubwa. Usamehevu wa Waislamu pamoja na huruma yao kwa walimwengu iliwafanya kuwaruhusu na kuweka makazi yao katika nchi hiyo.

Mayahudi waliuliwa kwa kiasi kikubwa pindi Waislamu walipofukuzwa Andalusia (Spain) mwaka 1492 M. Walipata ulinzi kwa kuhamia katika nchi za Kiislamu kama Morocco, Misri, Palestina, Iraaq, Uturuki, Yemen na nchi nyenginezo. Walipata haki zao pamoja na usaidizi ambao hawajawahi kupatiwa na dola yoyote nyengine. Hivyo, Waisraili wakikubali utawala wa Kiislamu wataendelea kuishi katika nchi hizo kama dhimmi (raia wasiokuwa Waislamu wanaopatiwa hifadhi katika Dola ya Kiislamu). Kwa hiyo, wakikubali hilo wataendelea kuishi katika nchi hizo na kupatiwa haki zao.

Ifahamike kuwa dola ya kwanza ya Waisraili katika ardhi ya Kanaani ni ile iliyoanzishwa wakati wa Nabii Yusha bin Nuun (‘Alayhis Salaam) takriban mwaka wa 1210 KI (Kabla ya kuzaliwa Nabii ‘Isa), nayo haikubali kwa muda mrefu kwani alipofariki Waisraili walizozana sana. Utawala wao pia haukuenea Palestina yote kwa mipaka yake ya sasa. Baada ya mzozano wa muda mrefu Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Alimchagua Twaaluut awe mfalme wao ili arudishe tena nguvu na utukufu wao. Waisraili waliokuwa Waislamu chini ya uongozi wa Twaaluut waliweza kuwashinda Wapalestina waliokuwa mapagani na kushika baadhi ya ardhi zao mwaka 1025 KI. Kwa maelezo ya ziada kuhusu mapambano hayo tazama Qur-aan 2: 246 – 251.

Katika mwaka wa 1004 KI, Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) alifanywa mfalme wa dola hiyo changa iliyoanzishwa na mfalme Twaaluut. Katika miaka yote hiyo Waisraili hawakuweza kuiteka na kuutawala mji wa al-Quds. Mji huo uliingia katika dola hiyo katika uhai wa Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) mwaka wa 995 KI. Utawala wake na mtoto wake Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) katika thuluthi mbili (2/3) ya ardhi ya Palestina sasa kama nchi moja uliendelea mpaka mwaka wa 922 KI mwaka alioaga dunia Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam).

Baada ya hapo dola hiyo ya Kiislamu iligawanyika na kuwa dola mbili. Utawala wao ulimalizika kabisa katika ardhi hiyo mpaka mwaka 15 Mei 1948 walipotunukiwa nchi hiyo na Muingereza kinyume na mikataba ya kimataifa na haki za wanati (raia) wake.

Jibu hili ni kwa mujibu wa swali lililoulizwa na ndugu yetu. Ikiwa ndugu atataka ziada kuhusu hata Biblia inasema nini kuhusu ardhi hiyo tutaweza kuchambua hilo. Wao wanasema kuwa ardhi hiyo ni ya ahadi lakini mistari ya Biblia inakanusha hilo.

Na tawfiki yote inatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala).

Na Allaah Anajua zaidi



 

 
 



 

[1]   Jamii/asili ya KihindiKizungu. Tazama TUKI Kamusi ya Kiingereza – Kiswahili  110.

[2]   Kwa sasa Amerika inaisaidia Israeli kwa dola bilioni tano za Kimarekani kila mwaka.

 

Share