Kizazi Cha Nuuh Ndicho Kilichoanza Kizazi Upya Cha Binaadamu?

SWALI:

Swali langu linahusu wakati wa nabii Nu-h a.s.w.

Maswali yangu ni mawili ambayo naomba unifafanulie.

1. Je kaumu yake iliyogharikishwa ndiyo ilikuwa ulimwengu wote wa wakati huo? Na kwamba baada ya gharka ulimwengu ulianza upya?

2. Na twafahamu kwamba alibeba kila kiumbe jozi ya kike na kiume. Je kwa wanaadamu alikuwa na watu wangapi ambao walianzisha ulimwengu mwingine?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo linalohusu wakati wa Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam). Tunapashwa habari ya Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) katika Qur-aan pale ilipotueleza:

 

 

Na hakika Tulimtuma Nuuh kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhalimu. Nasi Tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na Tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote” (29: 14 – 15).

 

Kuhusu Nuuh (‘Alayhis Salaam), watu wote kabla yake walizamishwa katika mafuriko hakubaki kiumbe chochote duniani ila wale tu aliowapakia katika jahazi kama Alivyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).  Idadi ya watu waliokuwepo wakati wa Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) ilikuwa ni kidogo na Ummah ulikuwa sehemu moja. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Alipoleta gharka ilikuwa ni kwa ulimwengu wote. Bila shaka, baada ya msukosuko huo na gharka hiyo ulimwengu ulianza tena upya kama ulivyoanza wakati wa Nabii Adam (‘Alayhis Salaam).

 

Kuhusu wanadamu waliokuwa ndani ya safina walikuwa kidogo na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hakutupatia idadi yao hasa bali maelezo ni kama Aayah zifuatazo kuhusu kubeba viumbe viwiliwili na kugharika wengineo:

 

((وَأُوحِيَ إِلَى نُوحٍ أَنَّهُ لَن يُؤْمِنَ مِن قَوْمِكَ إِلاَّ مَن قَدْ آمَنَ فَلاَ تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُواْ يَفْعَلُونَ)) ((وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا وَلاَ تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُواْ إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ))  ((وَيَصْنَعُ الْفُلْكَ وَكُلَّمَا مَرَّ عَلَيْهِ مَلأٌ مِّن قَوْمِهِ سَخِرُواْ مِنْهُ قَالَ إِن تَسْخَرُواْ مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنكُمْ كَمَا تَسْخَرُونَ)) ((فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُّقِيمٌ ))  ((حَتَّى إِذَا جَاء أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ قُلْنَا احْمِلْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلاَّ مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ وَمَنْ آمَنَ وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلاَّ قَلِيلٌ))   ((وَقَالَ ارْكَبُواْ فِيهَا بِسْمِ اللّهِ مَجْرَاهَا وَمُرْسَاهَا إِنَّ رَبِّي لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ))   ((وَهِيَ تَجْرِي بِهِمْ فِي مَوْجٍ كَالْجِبَالِ وَنَادَى نُوحٌ ابْنَهُ وَكَانَ فِي مَعْزِلٍ يَا بُنَيَّ ارْكَب مَّعَنَا وَلاَ تَكُن مَّعَ الْكَافِرِينَ))(( قَالَ سَآوِي إِلَى جَبَلٍ يَعْصِمُنِي مِنَ الْمَاء قَالَ لاَ عَاصِمَ الْيَوْمَ مِنْ أَمْرِ اللّهِ إِلاَّ مَن رَّحِمَ وَحَالَ بَيْنَهُمَا الْمَوْجُ فَكَانَ مِنَ الْمُغْرَقِينَ)) ((وَقِيلَ يَا أَرْضُ ابْلَعِي مَاءكِ وَيَا سَمَاء أَقْلِعِي وَغِيضَ الْمَاء وَقُضِيَ الأَمْرُ وَاسْتَوَتْ عَلَى الْجُودِيِّ وَقِيلَ بُعْداً لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ))

 

((Na akafunuliwa Nuuh akaambiwa: Hataamini yeyote katika watu wako ila wale waliokwisha amini. Basi usisikitike kwa waliyokuwa wakiyatenda))  

 

((Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa))

 

((Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli))

 

((Nanyi mtakuja jua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu)). 

 

((Hata ilipo kuja amri Yetu, na tanuri ikafoka maji, Tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali zako, isipokuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu; na watu walioamini. Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu)) 

(( Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Allaah kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) 

 

((Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuuh akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri))

 

((Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuuh) akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Allaah ila Aliyemrehemu Mwenyewe. Na wimbi likawatenganisha, akawa katika waliozama))  

 

((Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu waliodhulumu!))

 

[Huud: 36-40]

 

 

Ibara aliyoitumia Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ni kuwa wale waliobebwa katika safina ambao walikuwa Waumini ni wachache. Maana hasa ya wachache anaijua Yeye Mwenyewe Aliyetukuka. Hata hivyo, Wanachuoni wamefanya Ijtihaad yao kuhusu hilo na wapo Mufassiriyn waliosema kuwa walikuwa watu 80, miongoni mwao walikuwa watoto wake 3 nao ni Saam, Haam na Yaafith na wake zao. Wengine wanasema walikuwa watu 72 na wengine kumi. Hawa ndio walioeneza tena kizazi za wana Aadam mpaka tukapatikana sisi. Hiki ni kizazi alichosema Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):

 

Enyi kizazi tuliyowachukua pamoja na Nuuh! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani” (17: 3).

 

Na pia:

 

 أُوْلَئِكَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ مِن ذُرِّيَّةِ آدَمَ وَمِمَّنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ وَمِن ذُرِّيَّةِ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْرَائِيلَ وَمِمَّنْ هَدَيْنَا وَاجْتَبَيْنَا

((Hao ndio Aliowaneemesha Allaah miongoni mwa Manabii katika uzao wa Aadam, na katika uzao wa wale tuliowapandisha pamoja na Nuuh na katika uzao wa Ibraahiym na Israaiyl, na katika wale Tuliowaongoa na Tukawateua)) [Maryam: 58

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share