Daku: Ufafanuzi Wa Wakati Wa Mwisho Wa Kula Daku

 

SWALI:

Kuhusu kula daku, hapo naomba ufafanuzi hasa maana huku sisi hatuswali Alfajir twaswali Assubhi, sasa tukiwaruhusu watu kula mpaka wakati wa adhana ya mwisho mi nahisi tutakuwa tushawalisha watu mchana. Wajua hawa watu wanaoandaa nyakat za swala wao wenyewe wanasema tufanye makadirio ya nyakati swala. Naomba unifafanue pia hapo.

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako la nne. Kuhusu ufafanuzi wa swali  la:

Wakati Wa Mwisho Wa Kula Daku

 

Ndugu kwa wakati huu wetu wa sasa tunafaa tusiwe na utata wowote kwani waliotutangulia wlifanya bidii kwa kufanya utafiti hadi wakatuwekea jedwali ya machomozo ya jua na machweo yake.

Ni vizuri kuwa na jedwali ya mwaka mzima na kutazama wakati wa kuingia Alfajiri ya kweli ambao ndio wakati wa uhakika wa adhana ya pili. Katika kipindi cha hasa Ramadhaan maratibu wa Msikiti wenu mzungumze na kamati au Imaam aelezwe mwadhini wakati wenyewe na hapo hakutakuwa na utata wowote. Labda tukitoa mfano itaeleweka zaidi nayo tukichukua wakati wa adhana ya pili na machweo kwa mji wa Mombasa ambao nyakati zake zitakaribiana na Dar es Salaam. Kwa tarehe 10 Oktoba 2007 adhana ya pili ilikuwa saa kumi na dakika 49 ilhali machweo ni kumi na mbili (12) na dakika 13. Hatudhani kuwa jedwali kama hizo hazipo Dar na hata kama hazipo kwa uzoefu wa Waislamu nyakati za kula na kusitisha kula hazitakuwa ni zenye kuwashinda wao au kutojua.

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema kuhusu nyakati hizo:

Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku” (2: 187)

 

Huu ni muongozo tosha kwetu sisi na kukosea kwa baadhi ya watu katika kufuata hayo haifai kutufanya sisi kutoweza kutotekeleza ‘Ibaadah zetu. Hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametupatia nyakati za kuweza kufunga na mwenye kuelewa huwa hana tatizo. Mwisho wa kula ni kubainika kwa weupe wa Alfajiri, na huo ni weupe wa pili ambapo wakati wa Swalah hiyo huwa umeingia. Unapopatikana weupe huo basi inafaa usitishe kula lakini ikiwa unakula ukiwa na hakika kuwa bado Alfajiri kuingia kisha ukashtuka kuwa umekosea hilo halitaathiri Swawm yako ya siku hiyo. Mwisho wa kufunga ni kuingia usiku kwa kuchwa kwa jua na haifai kuongeza dakika 5 au 10 kwa kisingizio cha kuhakikisha kuwa kweli jua limekuchwa. Jua likizama tu mfungaji anafaa afungue.

Lakini kama tulivyosema hapo juu ni kuwa tatizo hili linafaa lisiwepo kwa ajili ya juhudi zilizofanywa kuhusu suala hilo kwa miaka mingi.

Na Allaah Anajua zaidi

Share