Mama Amecha Watoto Wa Kike Wawili Wanaume Watatu Aliachika Kwa Mumewe Kabla Kufariki

 

Mama Amecha Watoto Wa Kike Wawili Wanaume Watatu

Aliachika Kwa Mumewe Kabla Kufariki

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Namshuru Allah, mwingi wa rehema na mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na ndogo ndogo na natakia reheme Nabii wetu mtukufu, Muhamaad Salla Allahu alayhi wa sallaam. Baada ya haya, swali langu ni je, Kama mama amefariki na ameacha watoto watano, wakike wawili (mmoja ana mme mmoja hana) na wakiume watatu, je mali aliyoiacha inatakiwa kugawiwaje? Wakati anapatwa na mauti alikuwa ametengana na mumewe kwa talaka ila mumewe bado yu hai. Je mirathi inatakiwa iweje?

Allah awabariki. Ameen

 

 

 

JIBU:

 

Kwanza tunakunasihi kutokufupisha maamkizi ya Kiislaam na Thanaa au kuwatakia Radhi Swahaba na mengineyo ambayo watu wanakosea kama hivyo. Jambo hilo limekemewa  na ‘Ulamaa wetu. Bonyea viungo vifuatavyo upate faida:

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Awape subira wafiwa na wawe ni wema kwa mama yao hata baada ya kufa kwa kumuombea du‘aa asamehewe na Allaah na Awekwe mahali pema pamoja na wema.

 

Hakika ni kuwa tutachukua dhahiri ya swali lenyewe kuwa mama huyo hakuwa na wazazi. Mwanzo ni kuwa mtalaka wake hatakuwa na wirathi kwani aliyekufa hakuwa mkewe wakati huo. Hivyo, watakaorithi ni watoto wake tu – mtoto wa kiume atapata sehemu mbili ya mtoto wa kike. Mafungu yanakuwa sawa kwa watoto wakiwa wameoa, wameolewa, hawajaoa au kuolewa.

 

Kwa hiyo, kila mtoto wa kiume atapata robo (¼) ya mali yalioachwa na aliyefariki ilhali kila msichana atapata thumuni (1/8). Huo ndio mgao wa warithi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share