Kuvaa Fulana Inayoonyesha Mabega

 

Kuvaa Fulana Inayoonyesha Mabega

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Swali langu ni, je nivibaya kuva flana ambayo yaonyesha mabega nyumbani mbele ya ndugu zako ama Haifai? Kama haifai je kwa nini watu wakienda umra wavaa kitambara yenya kuacha baadhi ya mwili wazi.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ama kuhusu suala lako ni kuwa Uislamu umeweka kanuni njema za mavazi kwa wanaume na wanawake. Muislamu mwanaume anatakiwa awe ni mwenye kuvaa vazi lenye muruwa na lenye kwenda sambamba na unavyotaka Uislamu. Mwanaume anapokuwa nyumbani akiwa na ndugu zake wa kiume peke yao hakuna vibaya kwani uchi wa mwanaume akiwa na wanaume wenziwe ni baina ya kitovu na magoti. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

 

"Baina ya kitovu na magoti ni uchi" [Abu Daawuud, na al-Albaaniy amesema ni Hasan].

 

 

Kwa hiyo, hakutakuwa na ubaya wowote wa kufanya hivyo. Ikiwa kwa neno ‘ndugu’ unamaanisha nduguze wanaume na wanawake basi haitakuwa ni heshima kukaa mbele ya ndugu wa kike katika hali hiyo.

 

 

Ama kuhusu mas-ala ya Umrah hilo ni suala jingine lenye kanuni zake. Pengine pia huenda mtu akauliza kwa nini katika Umrah na Hajj wanaume na wanawake wanachanganyikana mbali na kwamba Uislamu umekataza hilo. Sasa ‘Ibaadah hizi zina kanuni tofauti na ‘Ibaadah nyingine nazo tumeilimishwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kuhusu hilo tunalipata katika kauli ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliweka nia ya kutekeleza ‘Umrah kutoka al-Jiranah kwa kuvaa Ihraam kwa kuacha mabega yao wazi, wakaileta Ihraam kutoka chini ya makwapa yao ya kulia ilhali wakifunika mabega yao ya mkono wa kushoto [Ahmad na Abu Daawuud].

 

 

Wanazuoni wengi wana muono kama huo na wanadai kuwa kwa kufanya hivyo kunasaidia katika ramal (kukimbia kidogo kidogo) wanapofanya Twawaaf.

 

 

Ama katika Swalah mwanaume hafai kuacha mabega yake. Hii ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kuswali na nguo moja huku mabega yake yakiwa wazi [al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah Radhwiya Allaahu ‘anhu].

 

 

Hata hivyo, inajuzu kwa mwanaume kutoyafunika mabega yake nje ya Swalah [Abu Maalik, Swahiyh Fiqhus Sunnah, Mj. 1].

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Ikiwa nguo ni pana anafaa mtu ajitatie nayo, na ikiwa ni dhiki (ndogo) aweza kuifanya kuwa izari (nguo ya chini/ kikoi)” [al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Jaabir [Radhwiya Allaahu ‘anhu]).

 

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kuswali kwa suruali bila ya nguo ya juu [Abu Daawuud, na al-Albaaniy amesema ni Hasan].

 

 

Hivyo, mabega yanatakiwa yafunikwe katika Swaalah lakini ikiwa mtu hana nguo za kujifunikia sehemu yake ya juu pamoja na mabega ndipo anaruhusiwa kujifunika baina ya kitovu na magoti. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share