Kutoa Aibu Ya Mwenzio Ni Ghiybah (Kusengenya)

 

Kutoa Aibu Ya Mwenzio Ni Ghiybah (Kusengenya)

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Allaah akulipeni kila ya kheri kwa kuanzisha nafasi hii yakuweza kuuliza masuali yetu.

nilikuwa nauliza hili:-

 

Ukiwa watu tumekaa pamoja na mwezetu miongoni mwa sisi  akatoa aibu ya mtu mwengine bila ya kumtaja jina sasa je hii hukumu yake nini? yaani itakuwa ndo tayari ushasengenya au vipi?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Bila shaka kutoa aibu ya mtu mwingine itakuwa ni kujichumia dhambi na vile vile itaanguka katika hukmu ya ghiyba (kusengenya) ambayo mtu huadhibiwa na vile vile ni kupoteza mema yako unayofanya kuwa anapewa huyo unayemsengenya. Mwenye kuzidi kusengenya huendelea kupoteza thawabu zake hadi anapokuwa hana kilichobakia katika mema yake, hapo tena hujazwa madhambi ya wale aliowasengenya.

 

Tumeonywa sana uovu huu katika Qur-aan na Sunnah.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَيْلٌ لِّكُلِّ هُمَزَةٍ لُّمَزَةٍ ﴿١﴾

Ole kwa kila mwenye kukebehi na kukashifu watu kwa ishara na vitendo na kwa kila mwenye kufedhehesha kwa ulimi. [Al-Humazah: 1]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allahu 'anhu amesema: "Humazah ina maana yule anayetukana na kufedhehesha wenzao" [At-Twabariy 24:596] 

 

Waislamu tunatakiwa tuheshimiane na kusitiriana aibu zetu. Kwani Rasuli  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

عن ابن عمر رضي اللَّه عنهما أَنَّ رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : (( المُسْلِمُ أَخُو المُسْلِمِ ، لا يظْلِمُه ، ولا يُسْلِمهُ ، منْ كَانَ فِي حَاجَةِ أَخِيهِ كَانَ اللَّهُ فِي حاجتِهِ ، ومَنْ فَرَّج عنْ مُسْلِمٍ كُرْبةً فَرَّجَ اللَّهُ عنْهُ بِهَا كُرْبَةً مِنْ كُرَبِ يوْمَ الْقِيامَةِ ، ومَنْ ستر مُسْلِماً سَتَرهُ اللَّهُ يَوْم الْقِيَامَةِ)) متفقٌ عليه

Kutoka kwa ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) kwamba Rasuli(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu ni ndugu wa Muislamu, haimpasi kumdhulumu wala kumsalimisha kwa adui, atakayemsaidia haja ndugu yake Allaah Atamkidhia naye haja yake, atakayemuondoshea dhiki Muislamu mwenzake, Allaah Atamuondoshea dhiki katika dhiki za Qiyaamah, atakayemsitiri Muislamu (duniani), Allaah Atamsitiri siku ya Qiyaamah)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

عن أَبي هريرة رضي اللَّه عنه قال : قال رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : ((المُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِم لا يخُونُه ولا يكْذِبُهُ ولا يخْذُلُهُ ، كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حرامٌ عِرْضُهُ ومالُه ودمُهُ التَّقْوَى هَاهُنا ، بِحسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أَنْ يَحْقِرَ أَخاهُ المسلم)) رواه الترمذيُّ وقال : حديث حسن

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiwya Allahu 'anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu ni ndugu wa Muislamu, hamkhini wala hamuongopei, wala hamuudhi. Muislamu kwa Muislamu mwenzake ni haramu (kuvunja) heshima yake, (kula) mali yake, (kumwaga) damu yake. Taqwa iko hapa. Kila mtu inampasa atahadhari na haya kwani inatosheleza pekee kumdhararu nduguye Muislamu kuwa ni kutenda ovu)) [At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan]

 

Bonyeza hapa upate maelezo zaidi yanayohusu uovu wa ghiybah;

 

Kusengenya (Ghiybah) Japo Anayesengenywa Anayo Sifa Yenyewe Ni Dhambi 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share