Yupi Yatima Zaidi? Aliyefiwa Na Mama Au Baba?

 

Yupi Yatima Zaidi? Aliyefiwa Na Mama Au Baba?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Ndugu zangu waislam, Nina maswali mawili ambayo ningewashkuru sana nikijuwa majawabu yake, jee yatima, ni alofiwa na mamake, au baba au wazazi wote wawili? Yupi wafaa kumtizama zaidi?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika ni kuwa binaadamu yatima ni yule aliyefiliwa na baba kabla ya yeye kubaleghe. Kijana au msichana akisha baleghe huwa haitwi tena yatima.

 

 

Yatima wote wanaofiwa na wazazi wake wawili au baba au mama wote ni yatima na wanahitaji kuangaliwa ipasavyo ili kupata fadhila zake ambazo fadhila hizo ni sawa tu mbele ya Allaah(Subhaanahu wa Ta'aalaa), ikiwa ni kumlea aliyefiwa na wazazi wawili au mmoja.

 

 

Hata hivyo kutokana na Swali lako, bila shaka yule ambaye amekosa baba na mama anakuwa ni yatima kamili na anahitaji kuangaliwa na kwa huruma zaidi kwa ajili ya kukosa wazazi wote na pia atakuwa zaidi ni mwenye kuhitaji kuangaliwa kwa matumizi ya malezi yake.    

 

 

Kisha anafuatia yule aliyefiwa na baba kwani baba kawaida ndiye mwenye kuleta masarufu nyumbani. Kwa hiyo uangalizi wa kumhudumia kwa ajili ya kulelewa kwake unahitajika zaidi kuliko yule anayefiwa na mama.

 

 

Lakini tunarudia kumalizia tena kuwa wote hayo ni Yatima na kuwalea na kuwahurumia ni wajib wetu na fadhila zake ni kubwa mno kama tulivyopata mafunzo katika Qur-aan na Sunnah:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatuelezea kuhusu kuwatazama mayatima kwa pale Aliposema:

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka. [Al-Insaan: 8].

 

Kutomtazama yatima ni jambo ambalo si zuri katika Uislamu kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

فَذَٰلِكَ الَّذِي يَدُعُّ الْيَتِيمَ ﴿٢﴾

Basi huyo ndiye anayemsukuma yatima. [Al-Maa'uwn: 2].

 

 

Na zipo fadhila kubwa zilizowekwa na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wenye kuwatazama mayatima. Anasimulia Sahl bin Sa‘d (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, "Mimi na amtazamaye yatima tutakuwa hivi Peponi”, akaonyesha kidole chake cha kati na cha shahada na kuvipambanua [al-Bukhaariy].

 

 

Amesema Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Yeyote anayemtazama yatima akiwa ni jamaa yake au si jamaa yake, mimi na yeye tutakuwa pamoja Peponi kama hivi, na Maalik (akaelezea) kwa kuashiria kwa kidole chake cha shahada na cha kati zikiwa karibu [Muslim].

 

 

Ulaji wa mali ya mayatima ni miongoni mwa madhambi makubwa ambayo mtu anatakiwa ajiepushe kabisa.

 

Amesema Allah Aliyetukuka:

إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖ وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا ﴿١٠﴾

Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma hapana shaka kwamba wanakula katika matumbo yao moto, na watauingia moto uliowashwa vikali mno. [An-Nisaa: 10].

 

Na Amesema Aliyetukuka:

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ 

Na wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia ya ihsaan .. [Al-An'aam: 152].

 

Na Amesema Aliyetukuka:  

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَىٰ ۖ قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ ۖ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ ۚ

Na wanakuuliza kuhusu mayatima. Sema: Kuwatengeneza ni khayr.  Na Allaah Anamjua fisadi na mtengenezaji. [Al-Baqarah: 220].

 

 

Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Jiepusheni na madhambi saba yanayoangamiza". Watu wakauliza: "Ee Rasuli wa Allah ni yapo hayo?" Akasema: "Kumshirikisha Allaah, na uchawi, na kuua nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia siku ya vita na kuwatuhumu kwa zinaa wanawake waliohifadhiwa na Allaah, Waumini wasiyo na habari ya zinaa". [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Hivyo ni vyema kuwatazama mayatima kwa kadiri ya uwezo wako na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Atakubariki hapa duniani na Kesho Akhera kukuweka mahali pema.

 

 

Ingia katika kiungo kifuatacho pia upate pia maelezo zaidi kuhusu kulea yatima:

 

Jukumu La Kulea Yatima

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share