Mpangaji Shekhe Hataki Kulipa Kodi Hataki Kufanya Kazi

 

Mpangaji Shekhe Hataki Kulipa Kodi Hataki Kufanya Kazi

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Mama yangu ananyumba yake kubwa self container ambayo tunaishi famile nzima Ambapo uislam wetu uko wa kawaida wa kuswali, kutenda mema, kufanya kazi n.k ila uani kunaa vyumba viwili ambavyo ilipofika 1999 alipampangisha sheikh mmoja na mke wake na watoto wawili ambao   wote amewazalia kipindi yupo hapa. Kubwa huyu sheikh hana kazi na kufanya kazi hataki kwa madai yeye anafanya kazi ya Allaah (SWT) Vvilevile hapa mtaani pana msikiti ambae pia yeye ni Imam mkuu, na yuko kwenye mabaraza mbalimbali ya kiislam kama vile baraza kuu la Taifa Tanzania. ambavyo haimuungizii kipato chochote kwa madai yake, Sasa basi ulipaji wake wa pango ni kwa tabu sana akawa mke wake anandugu zake nchi za nje  wakimletea pesa kwa ajili ya matumizzi anachukua kiasi analipa pango, Mke wake huyu akawa anamshinikiza mume wake akafanye kazi ili waipukane na kuomba lakini bila mafanikio, yule mwanamke kuona maisha magumu naye ana elimu yake ya form six, akaomba kazi  ya utawala katika serikali ya mkoa  mmojawapo akaenda zake  huko  kwa ajili ya kazi na vilevile hukohuko ndio nyumbani kwa wazazi wake, Kipindi anaondoka akatuaga kwamba kwa sasa yule mume atajitegemea kwa kila kitu hata pango atalipa mwenyewe yeye anaondoka na watoto wake inawezekana asirudi tena hapa. ana muacha mume wake sababu hataki kufanya kazi hata akimchukua huko atakuwa ni mzigo tu.

 

Yule mume wakagombana sana kuhusu  hilo lakini ikawa habna budi akasema yeye atabaki palepale.

 

Sasa imefika mwaka sasa tangu yule mwana mke aondoke na huyu sheikh

 

Hajalipa Pango La Nyumba Wala Maelezo Yoyote Kwa Mwenye Nyumba.

 

 

Kutokana Na Hali Hiyo Mwenye Nyumba  Ameamua Kutaka Kumpa Notisi Ya Kuhama Na Kumsamehe Kodi Ya Awali, Kwa Huruma  Twamuonea Lakini Atakaa Vile Mpaka Lini Naye Ni Mwanamume Wa Miaka 45 Sasa. Hataki Hata Kujifunza Chochote Wala Udereva, Uselemala Au Kazi Yoyote Ambayo Inafaa.

 

Kwa Kuwa Alllah Amewaruzuku Upeo Na Ufahamu Mkubwa Zaidi Yetu Basi Twaomba Mtusaidie Tumfanyeje Mtu Huyu.

Wasalaam

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika maelezo hayo yanashangaza sana kuhusu huyo mpangaji unayemuita Shekhe. Tuna wasiwasi mkubwa sana na cheo hicho mnachompa.

 
 

Mara nyingi huu ndio mtindo unaotumiwa na wale wanaojiita mashekhe kuwakandamiza wengine kwa njia moja au nyengine. Je, yeye ni bora kuliko Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Manabii (‘Alayhimus-salaam)wengine. Manabii (‘Alayhimus-salaam) wote walikuwa wanakula chakula cha jasho lao kwa kufanya kazi.

 

 

Kutofanya kazi si uchaji wa Allaah kwani kazi ni Ibadah. Kwa ajili hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا ﴿١٠﴾وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾

Na Tukafanya usiku kuwa kama libasi la kufunika.Na Tukafanya mchana kuwa ni wa kutafutia maisha. [An-Nabaa: 10 – 11].

 

 

Hii ayah inaonyesha umuhimu wa kufanya kazi. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) pia Anatueleza kuwa tunapomaliza Swalah ya Ijumaa tutawanyike katika ardhi ili tutafute fadhila za Allaah (62: 10).

 

 

Fadhila Zake zinapatikana katika kufanya kazi. Ikiwa hata siku kuu ya wiki ambayo ni Ijumaa tunaamriwa tufanye kazi kwa nini huyo shekhe (mwanamme) anabweteka tu kwa kumtegemea mkewe ambaye anafaa awe ni mwenye kuhudumikiwa. Hakika ni kuwa kufanya kwake hivyo inaonyesha picha mbaya sana juu ya Uislamu. Huko ni kudhalilisha Dini ya Kiislam na kuipaka matope kwani yeye anaonekana ni mwakilishi wa Dini katika jamii.

 

 

Hakika mtakuwa mmefanya hisani kubwa kwa kumsamehe ijara (kodi) ya mwaka mzima na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Atawabariki kwa hilo. Lakini kumuacha akae hapo hivi hivi ndio mnazidi kumfanya aoze na kuvunda. Ushauri wetu ni kuwa mumpe notisi kama ya mwezi mmoja huenda akapata fahamu na kujirekebisha. Ikibidi kama hajajirekebisha, mchukulieni hatua za kisheria ima kwa kumshitaki kwa wakubwa zake waliomuajiri kwani anawaibisha nao vilevile ikiwa wao ni chombo cha kusimamia Uislam na hali yeye anakiwakilisha hicho chombo kudhulumu Waislam badala ya kusaidia Waislam.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Amzindue, afahamu wajibu wake na hivyo kufanya kazi kama wanaume wengine.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi
Share