Kisa Cha Aswhaabul-Kahf (Watu Wa Pangoni) - 4

 

Kisa Cha Asw-haabul Kahf (Watu wa Pangoni) – 4

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Baada ya kumalizika kisa cha Asw-haabul-Kahf, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaendelea kutupa mwanga na mfunzo kuhusu sababu ya kuteremshwa kisa hicho, pamoja na funzo muhimu kwa Muislamu kuhusu kusema In Shaa Allaah pale anapotaka kutenda jambo la mustaqbal.

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)

 

وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَىٰ أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَـٰذَا رَشَدًا ﴿٢٤﴾وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا ﴿٢٥﴾قُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا ۖ لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ ۚ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

23. Na wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile:  Nitalifanya hilo Kesho. 24. Isipokuwa (useme): In Shaa Allaah. Na mdhukuru Rabb wako unaposahau.  Na sema: Asaa Rabb wangu Akaniongoa njia iliyo karibu zaidi ya uongofu kuliko hii.  25. Na walikaa pangoni mwao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.  26. Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Yake Pekee ghayb za mbingu na ardhi. Kuona kulioje Kwake na kusikia! Hawana pasi Naye mlinzi yeyote na wala Hamshirikishi katika hukumu Zake yeyote. [Al-Kahf: 23-29].

 

 

Umuhimu Wa Kusema In Shaa Allaah:

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ ﴿٢٤﴾

23. Na wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile:  24. Isipokuwa (useme): In Shaa Allaah.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamfundisha Rasul wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba anapoazimia kufanya kitendo, lazima asema 'In Shaa Allaah' (Allaah Akipenda) kwani Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ndiye Mwenye Qudra (uwezo) wa kila kitu, Ndiye Mwenye Kudabiri mambo yote, na Ndiye Mjuzi wa mambo ya 'ghayb' (yasiyoonekana). Hakuna jambo linalowezea kutendeka ila kwa matakwa Yake.

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) amesema:

 

قَالَ سُلَيْمَان بْن دَاوُد لَأَطُوفَنَّ اللَّيْلَة عَلَى سَبْعِينَ اِمْرَأَة وَفِي رِوَايَة تِسْعِينَ اِمْرَأَة وَفِي رِوَايَة مِائَة اِمْرَأَة.  تَلِد كُلّ اِمْرَأَة مِنْهُنَّ غُلَامًا يُقَاتِل فِي سَبِيل اللَّه فَقِيلَ لَهُ  وَفِي رِوَايَة قَالَ لَهُ الْمَلَك.  قُلْ إِنْ شَاءَ اللَّه. فَلَمْ يَقُلْ فَطَافَ بِهِنَّ فَلَمْ يَلِد مِنْهُنَّ إِلَّا اِمْرَأَة وَاحِدَة نِصْف إِنْسَان فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ قَالَ إِنْ شَاءَ اللَّه لَمْ يَحْنَث وَكَانَ دَرَكًا لِحَاجَتِهِ وَفِي رِوَايَة وَلَقَاتَلُوا فِي سَبِيل اللَّه فُرْسَانًا أَجْمَعِينَ"

“Nabiy Sulaymaan bin Daawuwd (‘Alayhimus salaam) alisema: "Usiku wa leo nitawatembelea nitafanya kitendo cha ndoa kwa wanawake sabini. Katika riwaayah nyingine: wake tisini. Katika riwaayah nyingine wake mia. Kila mmoja wao azae mtoto wa kiume ambao watapigana  katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akaaambiwa. Katika riwaayah nyingine:  Malaaika akamwambia: sema In Shaa Allaah, lakini hakusema. Akawatembelea wanawake hao lakini hakuna aliyezaa isipokuwa mmoja tu ambaye alizaa mtoto aliyeumbika nusu tu, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:”Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, angelisema In Shaa Allaah, asingeliharibu kiapo chake na hivyo ingelimsaidia kupata alichotaka Katika riwaayah nyingine: Wangelipigana kama wapanda faraskwa ajili ya Allaah” [Fat-h Al-Baariy 6: 41, Muslim 3: 1275].

 

 

 

Sababu Ya Kuteremka Aayah Hizo:

 

 

Ibn 'Abbaas amesema: “Quraysh (Makafiri wa Makkah) walimtuma An-Nadr bin Al-Haarith na 'Uqbah bin Abi Mu'iytw kwa mapadri Wayahudi walioko Madiynah na wakawaambia "Nendeni na waulizeni kuhusu Muhammad na wasimulieni kuhusu yeye Muhammad anayoyasema, kwani wao ni watu wa kwanza wa kupewa vitabu na wanayo elimu ya Manabii kuliko sisi".

 

 

Wakaenda Maquraysh hao wawili na walipofika Madiynah waliwauliza mapadri ya Kiyahudi kuhusu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wakawaelezea Mayahudi sifa zote za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha wakasema: "Nyinyi ni watu wa Tawraat na sisi tumekuja kwenu ili mtujulishe kuhusu sahibu yetu".

 

 

 

Marabai wa kiyahudi wakawaambia, "Muulizeni mas-alah matatu tutakayokupeni mkamuulize. Pindi akijibu haya mas-ala matatu, basi yeye ni Nabiy aliyetumwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Lakini akishindwa kujibu basi atakuwa anajisemea mambo yasiyokuwa ya kweli, na hapo mfanye mnavyotaka.

 

 

Muulizeni:

 

  1. Kuhusu vijana wa wakati wa kale ni kisa chao. Kwani kisa chao ni cha kustaajabisha. (Asw-haabul-Kahf – vijana Wa pangoni)

 

  1. Nini kisa cha mtu aliyesafiri sana hadi akafika Mashariki na Magharibi ya dunia, yaani Dhul-Qarnayn.

 

  1. Muulizeni kuhusu roho (nafsi) ni kitu gani hicho?

 

 

An-Nadr na 'Uqbah wakarudi Makkah kwa Maquraysh na kuwaambia, "Enyi Quraysh! Sisi tumekuja na uamuzi wa suluhisho ambalo litatatua na kumaliza mashaakil baina yetu na Muhammad. Mapadri Wayahudi wametuambia tumuulize Muhammad mas-ala matatu". Wakawaelezea mas-ala yenyewe, kisha wakamuendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) umuuliza hayo mas-ala.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

أُخْبِرُكُم غَدَا عَمَّ سَأَلْتُم عَنْهُ

Nitakujulisheni kesho mambo mliyoyauliza

 

 

Lakini hakusema In Shaa Allaah. Wakaondoka zao kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakaa siku kumi na tano bila ya Jibriyl (‘Alayhis-salaam) kumjia kama ilivyo kawaida yake kumpa Wahyi (ufunuzi) kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Watu wa Makkah wakaanza kumtilia shaka na kupita kusema, "Muhammad katuahidi kutujibu mas-ala tuliyomuuliza siku ya pili na hadi leo siku ya kumi na tano zimepita hakutujibu lolote katika hayo".

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafikwa na huzuni sana kwa kuchelewa kupata Wahyi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Akasikitika kuhusu maneno ya watu wa Makkah waliyokuwa wakisema. Kisha Jibriyl (‘Alayhis-salaam) akaja kumteremshia Suwrah ya 'Al-Kahf' ambayo ilimliwaza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kuwa na huzuni kutokana na maneno ya watu wa Makkah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akanza kumfunulia Wahyi kwa kumwambia: 

 

 

فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا ﴿٦﴾

6. Basi huenda ukaiangamiza nafsi yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili yao kusikitika kutokuamini kwao usimulizi huu (Qur-aan). [Al-Kahf: 6].

 

 

Maana: “Usijiangamize nafsi yako kwa majuto". Qataadah kasema, "Kujiua kwa hasira na huzuni kwa ajili yao" [Atw-Twabariy 17:597-598].

 

Mujaahid kasema, "kwa hamu." [Atw-Twabariy 17:598].

 

 

Pia ina maana kwamba: "Usisikitike nao, wewe fikisha kwao ujumbe tu na yeyote atakayekwenda njia ya haki basi ni kwa ajili ya manufaa yake, na atakayekwenda njia ya upotofu basi ni khasara yake mwenyewe, kwa hiyo wewe usijiangamize nafsi yako kwa huzuni juu yao."

 

Aayah zinaendelea:  

 

 

  إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ﴿٧﴾ وَإِنَّا لَجَاعِلُونَ مَا عَلَيْهَا صَعِيدًا جُرُزًا ﴿٨﴾

7. Hakika Sisi Tumefanya vilivyoko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili Tuwajaribu nani miongoni mwao mwenye ‘amali nzuri zaidi. 8. Na hakika Sisi bila shaka Tutafanya vilivyo juu yake kuwa udongo wenye ukame. [Al-Kahf: 7-8].

 

 

Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaaAkampa fundisho Rasuli wa Allaah Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kusema In Shaa Allaah anapokusudia jambo lolote: 

 

 

 وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَىٰ أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَـٰذَا رَشَدًا ﴿٢٤﴾

23. Na wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile:  Nitalifanya hilo kesho. Isipokuwa (useme): In Shaa Allaah. Na mdhukuru Rabb wako unaposahau.  Na sema: Asaa Rabb wangu Akaniongoa njia iliyo karibu zaidi ya uongofu kuliko hii.

 

 

 وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ...

Na mdhukuru Rabb wako unaposahau. 

 

 

Maana: Ukisahau kusema In Shaa Allaah basi sema pale unapokumbuka. Hii ni rai ya Abu 'Aaliyah na Al-Hasan Al-Baswriy [Atw-Twabariy 17:645.

 

 

Ibn 'Abbaas aliifasiri Aayah hii kuwa mtu anaweza kusema In Shaa Allaah hata baada ya mwaka ikiwa amesahau kusema baada ya kuweka kiapo au kusema atafanya jambo fulani. Hivi atakuwa amefanya Sunnah ya kusema In Shaa Allaah hata kama baada ya kuvunja kiapo. Hii vile vile ni rai ya Ibn Jariyr [At-Twabariy 17:646].

 

Lakini kasema hii haina maana kwamba inafidia kuvunja kiapo cha mtu, bali mtu anapovunja kiapo lazima afanye kafara yake (malipo ya kiapo). Na Allaah Anajua zaidi.

 

وَقُلْ عَسَىٰ أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَـٰذَا رَشَدًا ﴿٢٤﴾

24. Na sema: Asaa Rabb wangu Akaniongoa njia iliyo karibu zaidi ya uongofu kuliko hii. 

 

 

Maana: “Ee  Nabiy: Ikiwa umeulizwa jambo lolote ambalo hulijui, basi muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kurudi Kwake ili Akuongoze kujibu lililo haki". Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo Kuhusu Kusema In Shaa Allaah

 

 

Inampasa kila Muislamu anapokusudia jambo au anapotoa ahadi fulani aseme

In Shaa Allaah, kwani uwezekano wa kutendeka jambo au kutokutendeka kunategema na kupenda Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hii ni kwa sababu hatuna ujuzi wa mambo ya ghaibu. Mfano wanapoagana watu kukutana siku au mahali au saa kadhaa huenda isiwezekani kwa sababu:

 

 

  1. Huenda mmoja wao akaaga dunia kabla ya siku hiyo ya kukutana.

 

  1. Sehemu walioagana inaweza kuwa imefikwa na maafa ikawa haiko tena.

 

  1. Inawezekana kutokea dharura ikashindikana kukutana wakati uliopangwa.    

 

 

Kwa hiyo ni muhimu sana kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwezeshe jambo kutendeka kwa uwezo na matakwa Yake.

 

 

Maswali Matatu Aliyoulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Na Makafiri wa Makkah:

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametaja kuhusu maswali matatu aliyoulizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maquraysh wa Makkah katika Aayah zifuatazo: 

 

 

1- Kuhusu Aswhaabul-Kahf:     

 أَمْ حَسِبْتَ أَنَّ أَصْحَابَ الْكَهْفِ وَالرَّقِيمِ كَانُوا مِنْ آيَاتِنَا عَجَبًا ﴿٩﴾

9. Je, unadhani kwamba watu wa pangoni na maandiko walikuwa ni ajabu miongoni mwa Aayaat (miujiza, ishara) Zetu? [Al-Kahf: 9]

Zikaendelea Aayah kutaja kuhusu vijana hao wa pangoni kama ilivyoelezwa katika kisa chao.

 

 

2-Kuhusu Dhul-Qarnayn:

 

 وَيَسْأَلُونَكَ عَن ذِي الْقَرْنَيْنِ ۖ قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُم مِّنْهُ ذِكْرًا ﴿٨٣﴾

83. Na wanakuuliza kuhusu Dhul-Qarnayn. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nitakusomeeni kuhusu baadhi ya khabari zake. [Al-Kahf: 83].

 

 

3-Kuhusu Roho:

 

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾

85. Na wanakuuliza kuhusu roho. Sema: Roho ni katika amri ya Rabb wangu. Na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu. [Al-israa: 85].

 

 

 

Muda Walioishi Aswhaabul-Kahf Pangoni:

 

 

Kisa chao kimemalizikia katika Qur-aan kwa kutajwa muda walioishi vijana hao pangoni:

 

 وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا ﴿٢٥﴾ قُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا ۖ لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ ۚ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

25. Na walikaa pangoni mwao miaka mia tatu na wakazidisha tisa. 26. Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Yake Pekee ghayb za mbingu na ardhi. Kuona kulioje Kwake na kusikia! Hawana pasi Naye mlinzi yeyote na wala Hamshirikishi katika hukumu Zake yeyote.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamtajia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) muda waliokaa pangoni nao ni kuanzia wakati Alipowapa usingizi wa kufa hadi wakati Alipowafufua, kisha walipojulikana na watu wakati ule. Muda wenyewe ulikuwa ni miaka mia tatu na tisa kwa hesabu ya mwandamo wa mwezi. Tofauti ya miaka mia ya mwandamo na mia ya Sola (Solar) ni miaka mitatu. Ndio maana baada ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutaja miaka mia tatu Ameongeza miaka tisa. Yaani miaka 3 x 3 = 9.

 

قُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا ۖ

26. Sema: Allaah Anajua Zaidi muda waliokaa.

 

 

Maana: “Utakapoulizwa kuhusu muda waliokaa na wewe huna ujuzi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi usijibu kitu ila:

 

 اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ 

Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Yake Pekee ghayb za mbingu na ardhi.

 

 

Maana: Hakuna yeyote anayejua jambo hilo isipokuwa Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pamoja na viumbe Aliowachagua  kuwajulisha. (Hii ni rai ya ‘Ulamaa zaidi ya mmoja kama Mujaahid na wengineo waliokuja katika kizazi cha mbele).

 

 وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا ﴿٢٥﴾   

25. Na walikaa pangoni mwao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.

 

 

Qataadah amesema: “Hii ni rai ya Ahlul-Kitaab (Watu Waliopewa kitabu) lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameikanusha kwa Kusema:

 

  قُلِ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا

26. Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa.

 

 

Maana: Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anajua zaidi kuliko wanayosema watu [Atw-Twabariy 17: 647]. Hii pia ilikuwa ni rai ya Mutwarraf bin 'Abdillaah [Atw-Twabariy 17:648]. Lakini rai hii iko wazi kujadiliwa kwa sababu Ahlul-Kitaab walivyosema wameishi katika pango kwa muda wa miaka mia tatu bila ya kutaja miaka tisa, walikuwa wakikusudia miaka ya sola (Solar) na si miaka ya mwandamo wa mwezi (kama ambavyo Waislamu tunavyotumia kwa kalenda zetu) na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  Amesimulia yale waliyotaja kwani Asingelisema:

 وَازْدَادُوا تِسْعًا

Na wakazidisha tisa

 

 

Maana iliyo dhahiri ya Aayah ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) kutaja uhakika wenyewe na Hakusimulia yale waliyosema Ahlul-Kitaab. Hii ni rai ya Ibn Jariyr (Rahimahu Allaah). Na Allaah Anajua zaidi.

 أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ

Kuona kulioje Kwake na kusikia!

 

Maana: Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawaona na Kuwasikia. Ibn Jariyr amesema: "Lugha imetumika hapa ya ufasaha kudhihirisha Himdi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)" [Atw-Twabariy 17:650].

 

 

Kifungu cha maneno haya kinaweza kufahamika kwa kumaanisha jinsi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alivyokuwa na uwezo wa Kuona kila kilichokuweko na jinsi gani Alivyokuwa na uwezo wa Kusikia kila kinachosikilizwa kwani hakuna kinachofichika Kwake.

 

Inasemekana kuwa Qataadah amesimulia kuhusu kauli hii: 

 أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ

 

Kuona kulioje Kwake na kusikia!

 

"Hakuna anayesikia au kuona zaidi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)" [Atw-Twabariy 17: 650]

 

 

Maana: Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ndiye Mwenye uwezo wa Kuumba na Kuamrisha. Hakuna wa kupindua Ufalme Wake. Hana mshauri, msaidizi wala mshirika, Ametakasika na Ametukuka. 

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

  1. Mja kumfanyia Adabu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kutokusema 'nitafanya jambo fulani' ila baada ya kusema In Shaa Allaah.

 

  1. Adabu ya mja anaposahau kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) amtaje japokuwa anapokumbuka baada ya muda kupita. Na akiapa basi hakimfai kiapo mpaka amtukuze isipokuwa ikiwa imeambatana na maneno yake pale pale.

 

  1. Utajo sahihi wa muda waliokaa vijana katika pango kwa muda wa miaka mia tatu na tisa kwa hesabu ya miaka mwandamo wa mwezi.  

 

 

 

Mwisho

 

 

Marejeo:

Tafsiyr Ibn Kathiyr

 

 

 

Share