Wasifu Wa Luqmaan Mwenye Hikmah

Wasifu Wa Luqmaan Mwenye Hikmah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Luqmaan alizaliwa katika Bara la Afrika. Jina lakeni Luqmaan bin 'Anqa' bin Sa’duwn. Ama Ibn Jariyr atw-Twabariy, yeye anasema jina lake lilikuwa Luqmaan bin Tharan kutoka watu wa Aylah (Quds).

 

 

Alikuwa ni mtu mwema aliyefanya juhudi katika ‘ibaadah na kutunukiwa busara. 

 

 

Alikulia katika msitu na kutembea bila viatu. Kule kukutana kwake na wanyama kulifanya awe mwenye nguvu, ujasiri, madhubuti na kutoogopa chochote. Alikuwa na ada ya kutafakari sana kuhusu uumbaji na viumbe vilivyomzunguka.   Huko kulimfanya awe ni mwenye kujifunza vitu vizuri vizuri kila uchao.

 

 

Luqmaan alishikwa na wafanya biashara wa utumwa waliovamia Afrika na kuuzwa kama mtumwa. Alijikuta amevuliwa uhuru wake, hivyo kumfanya asiweze kutembea wala kuzungumza anavyotaka. Huu ulikuwa ni mtihani wa kwanza aliolazimika kuuvumilia. Aliumia katika utumwa lakini alivumilia kwa kusubiri huku akiwa na matumaini kuwa Allaah (‘Azza wa Jalla)    Atamtoa katika janga hilo.

 

 

Aliyemnunua alikuwa ni mtu mzuri, mwema na mwenye busara. Hivyo, alimtendea wema Luqmaan. Aliweza kutambua kuwa Luqmaan alikuwa si mtu wa kawaida kwa werevu aliokuwa nao. Mtu huyu mwenye huruma aliacha wasiya kuwa anapoaga dunia tu Luqmaan aachwe huru. Na alipokufa, ombi hilo lilitekelezwa na hivyo kumfanya Luqmaan kwa mara nyingine tena kuwa huru.

 

 

Luqmaan alisafiri kwa muda na kuweka makazi yake pamoja na wana wa Israili. Alichaguliwa kwa hakimu katika utawala wa Nabiy Daawuwd ('Alayhis-salaam), naye aliheshimiwa na watu wote kwa busara yake na hukumu zake za uadilifu. Alioa na kulea familia.

 

Amesema Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa): “Luqmaan alikuwa mtumwa wa kutoka Ethiopia akifanya kazi ya useremala.”

 

 

'Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema, nilimuuliza Jaabir bin 'Abdillaah kuhusu Luqmaan. Akasema: “Alikuwa mfupi na pua mseto na alikuwa Mnubi.”

 

 

Imesimuliwa na Yahya bin Sa'iyd al-Answaariy kutoka kwa Sa'iyd bin al-Musayyib akisema: “Luqmaan ni mtu mweusi kutoka Misri.”

 

 

Al-Awza'iy amesema: “Niliambiwa na 'Abdur-Rahman bin Harmalah kuwa mtu mmoja mweusi alikuja kwa Sa'iyd bin AI-­Musayyib akimuomba sadaka.  Sa'iyd alimwambia: Usihuzunike kwa sababu ya rangi yako nyeusi kwani kulikuwa miongoni mwa walio bora kati ya watu ni watu weusi watatu: Bilaal bin Rabaah, Mahja (mwachwa huru 'Umar bin Al-Khatwaab) na Luqmaan, mtu mweusi mwenye busara, kutoka Nubia, ambaye midomo yake ilikuwa mipana.”

 

 

Imepokewa kwa Ibn Wahb: “Mtu mmoja alikuja kwa Luqmaan, mwenye hekima na kumuuliza: Je, wewe ni Luqmaan? Je, wewe ni mtumwa wa fulani?” Akajibu: “Naam.” Yule mtu akasema: “Wewe ndiye yule mchungaji mweusi?” Luqmaan akasema: “Ama kuhusu rangi yangu nyeusi, inaonekana dhahiri, kwani ni lipi linalokustaajabisha?” Akasema yule mtu: “Umekuwa ukizuriwa na watu kila mara ambao wanakubali hukumu yako.” Luqmaan akasema:  “Ee ndugu yangu! Ukifanya ninayokuambia utakuwa kama hivi.” Yule mtu akasema: “Ni nini hayo?” Luqmaan akasema: “Inamisha macho yako, chunga ulimi wako, kula kilicho halaal, kuwa mtwaharifu, timiza ahadi, kuwa mkarimu kwa wageni, waheshimu majirani, acha lisilokuhusu. Zote hizi zilinifanya mimi nikawa hivi.”

 

 

Hata hivyo, wanazuoni wengi wana rai na muono kuwa Luqmaan alikuwa si Nabiy bali mtu mwenye busara. Zaidi ya hayo, ametajwa katika Qur-aan na amesifiwa na Allaah (‘Azza wa Jalla)  Ambaye Ametusimulia wasiya wake kwa mwanawe pale aliposema:

 

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan (31:13)]

 

Kwa hiyo, alimuonya mwanawe na kumkataza kuingia katika shirki.

 

Na kuhusu dhulma kumaanisha shirki ni Hadiyth:

 

حَدَّثَنَا أَبُو الْوَلِيدِ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنِ الأَعْمَشِ، عَنْ إِبْرَاهِيمَ، عَنْ عَلْقَمَةَ، عَنْ عَبْدِ اللَّهِ، قَالَ لَمَّا نَزَلَتِ: ((‏الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ‏))‏ قَالَ أَصْحَابُ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم أَيُّنَا لَمْ يَلْبِسْ إِيمَانَهُ بِظُلْمٍ فَنَزَلَتْ: ((‏لاَ تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ‏))

Ametuhadithia Abul Waliyd amesema, ametuhadithia Shu‘bah amesema, na amenihadithia Bishr amesema, ametuhadithia Muhammad toka kwa Shu’bah toka kwa Sulaymaan toka kwa Ibraahiym toka kwa ‘Al-Qamah toka kwa ‘Abdullaah amesema: Ilipoteremka:

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

Wale walioamini na hawakuchanganya iymaan zao na dhulma; hao ndio watakaopata amani nao ndio waliohidika. [Al-An‘Aam (6:82)]..

 

Swahaba wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) walimuuliza: Nani kati yetu ambaye hakuidhulumu nafsi yake? Hapo Allaah (‘Azza wa Jalla) Akateremsha:

 

  لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan (31:13)]

 

[Al-Bukhaariy]

 

 

Nasaha nyenginezo ambazo Luqmaah alimnasihi mwanawe ni kuwatendea wema wazazi, kutokua na kibri, kusimamisha Swalaah, kuamrisha mema na kukataza maovu, kusubiri, kutonyanyua sauti, kutokuwa na kiburi na  kadhalika kama Alivyotupa maelezo hayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

 يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿١٦﴾ يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾ وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ ۚ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ ﴿١٩﴾

 

Ee mwanangu! Hakika likiweko (zuri au ovu) lolote lenye uzito wa punje ya hardali, likawa katika jabali au mbinguni au ardhini, Allaah Atalileta tu. Hakika Allaah ni Mwenye kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.  Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.  Na wala usiwageuzie watu uso wako kwa kiburi, na wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah Hampendi kila mwenye kujivuna mwenye kujifakharisha. Na kuwa wastani katika mwendo wako, na teremsha sauti yako, hakika sauti inayokirihisha zaidi bila shaka ni sauti ya punda. [Luqmaan: 16 – 19]

 

 

Ibn Abi Haatim amesema:  Niliambiwa na babangu kutoka kwa Qataadah aliyesema: Allaah (‘Azza wa Jalla)  Alimpatia fursa Luqmaan kuchagua baina ya Unabii na kuwa na hikmah, naye akachagua hikmah. Baadaye, Jibriyl (‘Alayhis-salaam) alikuja kwake akiwa amelala na kummiminia hikmah. Luqmaan alianza kuitamka siku ya pili yake.

 

 

Inasemekana kuwa Luqmaan aliulizwa kwa nini alichagua hekima juu ya Unabii. Alisema: “Lau kama Allaah Alinipatia Unabii ningeukubali na ningejaribu sana kupata radhi Yake, lakini Alinichaguza. Niliogopa kuwa dhaifu sana kwa Unabii hivyo nikachagua busara.”

 

 

Masimulizi haya si sahihi kwani mpokeaji mmoja Sa'iyd bin Bashiyr, si mwaminifu. Hata hivyo, Salaf wengi wa mwanzo na wanazuoni, kama Mujaahid, Sa'iyd bin Al-Musayyib and Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhum) walikuwa na muono kuwa ile kauli ya Allaah inayosema:

 

 وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ أَنِ اشْكُرْ لِلَّـهِ ۚ وَمَن يَشْكُرْ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿١٢﴾

  Kwa yakini Tulimpa Luqmaan hikmah kwamba: Mshukuru Allaah. Na anayeshukuru, basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na anayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote. [Luqmaan: 12]

 

 

Hii ina maana uchambuzi na ufahamu wa kidini. Kwa hiyo, hakuwa Nabii na hakuna chochote kilichoteremshwa kuonyesha kuwa aliteremshiwa Wahyi.

 

 

Hikmah Na Nasaha Nyenginezo Za Luqmaan:   

 

 

Kutoka kwa Damurah As-Saariy Ibn Yahia:

 

 

“Nimeambiwa na baba yangu kutoka kwa 'Abdah Ibn Sulaymaan kutoka kwa Ibn Mubaraak kutoka kwa 'Abdur-Rahmaan al Mas'uwd  kutoka kwa 'Awn Ibn 'Abdillaah akisema:  Luqmaan alimwambia mwanawe: Ee mwanangu ukikutana na watu anza kwa salaam (Assalaamu 'alaykum). Kisha kaa upande na usiseme kitu hadi waseme wao. Ukiwaona wanamdhukuru Allaah, waunge, lakini wakishughulika na mengine, geuka uondoke mbali nao na tafuta wengineo (wanaomdhukuru Allaah).

 

 

Nimeambiwa na baba yangu kutoka kwa 'Amr Ibn 'Uthmaan kutoka kwa Damura Ibn Hafsw Ibn 'Umar akisema: Luqmaan aliweka gunia la chembe za haradali karibu yake na akaanza kumpa nasaha mwanae, kwa kumpa kila nasaha moja chembe moja ya hardali hadi zikaisha zote. Akasema: “Ee mwanangu nimekupa nasaha ambazo zingepewa mlima ungelipasuka.”

 

 

'Abdur-Razaaq amesema: Niliambiwa na Hasan kutoka kwa Al-Junayd kutoka kwa Sufyaan akisema: Luqmaan alimwambia mwanae: “Ee mwanangu! Sijapata kujuta kwa sababu ya kukaa kimya. Ikiwa maneno ni fedha basi kukaa kimya ni dhahabu.”  

 

Ibn Jariyr amenukuu kwamba Khaalid ar-Rabaai alisema: Luqmaan alikuwa mtumwa wa ki-Ethiopia aliyekuwa na ujuzi wa useremala. Bwana (Tajiri) wake alimwambia: “Tuchinjie kondoo huyu.” Akamchinja, kisha akamwambia: “Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni bora kabisa.” Akampelekea ulimi na moyo. Baada ya siku kupita, alimtaka tena amchinjie kondoo, akachinja kisha Bwana wake akamwambia tena: “Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni viovu kabisa.”  Akamletea vile vile ulimi na moyo. Bwana wake akamuuliza: “Nilipokutaka uniletee viungo bora kabisa umeniletea ulimi na moyo; na nilipokutaka uniletee viungo viovu kabisa umeniletea hivyo hivyo, kwanini?” Luqmaan akamwambia: “Hakuna vilivyo bora kuliko hivi vinapokuwa vizuri, na hakuna vilivyo viovu kabisa kuliko hivi vinapokuwa vibaya.” [At-Twabariy: 20:135]

 

 

Basi tujifunze na tuzingatie mafunzo mengi tunayopata kwenye kisa hiki na nasiha za mja mwema huyu Luqmaan aliyejaaliwa na Allaah (‘Azza wa Jalla) hikmah na tutekeleze na kufundisha watu.

 

 

 

Share