Kisa Cha Aswhaabul-Kahf (Watu Wa Pangoni) - 3

 

Kisa Cha Asw-haabul Kahf (Watu Wa Pangoni) – 3

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Aayah zinaendelea kuhusu Asw-haabul Kahf:

 

وَكَذَٰلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ ۖ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا ۖ رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ ۚ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ ۖ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ ۚ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ ۗ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاءً ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا ﴿٢٢﴾

21. Na hivyo ndivyo Tulivyowatambulisha kwa watu ili wajue kwamba ahadi ya Allaah ni haki. Na kwamba Saa haina shaka yoyote humo. Pale walipozozana baina yao kuhusu jambo lao. Wakasema: Jengeni jengo juu yao; Rabb wao Anawajua vyema. Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Bila shaka tutajenga Msikiti juu yao.  22. Watasema: Watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na (wengine) wanasema: Watano na wa sita wao ni mbwa wao -   kwa kuvurumisha bila ya kujua. Na (wengine) wanasema: Saba na wa nane wao ni mbwa wao. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Rabb wangu Anajua zaidi idadi yao. Hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu. Basi usibishane nao isipokuwa mabishano dhahiri (Tuliyokufunulia Wahy), na wala usimuulize yeyote kuhusu khabari zao. [Al-Kahf: 21:22].

  

Watu wa mji waliyokuja kuwatambua na wakajenga jengo katika pango lao:

 

وَكَذَٰلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ ۖ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا ۖ رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ ۚ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾ 

21. Na hivyo ndivyo Tulivyowatambulisha kwa watu ili wajue kwamba ahadi ya Allaah ni haki. Na kwamba Saa haina shaka yoyote humo. Pale walipozozana baina yao kuhusu jambo lao. Wakasema: Jengeni jengo juu yao; Rabb wao Anawajua vyema. Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Bila shaka tutajenga Msikiti juu yao. [Al-Kahf: 21].

 

 

Wanavyuoni miongoni mwa Salaf wamesema kwamba wakati huo watu walikuwa wana shaka kuhusu kufufuliwa kwao. 

 

 

Ikrimah kasema: “Kulikuwa na kundi lililosema kuwa roho zao ndio zilizofufuliwa na si miili yao, kwa hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kawafufua watu wa pango wakaenda sokoni wakajulikana na watu ili iwe uthibitisho wa kufufuliwa kwao kikamilifu; yaani kiroho na kimwili. [Taariykh Atw-Twabariy 2: 9].

 

 

Wametaja kuwa walipomtuma mmoja wao kwenda mjini kununua chakula, alijibadilisha shakili yake na akatumia njia nyingine kabisa mpaka akafika mji wa Daqsus. Akafikiri kuwa si muda mrefu tokea walipoondoka, na hali kumbe ni karne baada ya karne, kizazi baada ya kizazi, ummah baada ya ummah zimepita na nchi pamoja na watu wake wamebadilika wote. Hakuona alama zozote za mji alizozitambua na wala hakumtambua hata mtu mmoja.

 

 

Akaanza kuzungukwa na akili na kusema peke yake.  "Labda nina wazimu au nimehadaika?  Au ninaota?" Kisha akasema: "Wa-Allaahi mimi si lolote katika hayo (yaani kuwa na wazimu au kuota), niliyoyaona usiku wa jana (hapo mwanzoni walipokuwa kabla ya kulala katika pango miaka yote hiyo) ni tofauti kabisa na haya ninayoyaona sasa".  Kisha akasema: "Bora nitoke nikimbie". Akatoka kwenda kwa muuzaji mmoja aliyekuwa anauza chakula, akampa zile pesa alizokuwa nazo, na kumtaka amuuzie chakula.  Yule mtu alipoziona zile pesa hakuzitambua kwa hiyo akampa jirani yake (muuzaji mwenziwe) naye pia hakuzitambua. Zikawa zinazunguka kwa wenye maduka kila mmoja hazitambui. Mmoja wao akasema "labda huyu mtu kapata hazina". Wakaanza kumuuliza kutaka kujua nani yeye na wapi kazipata zile pesa.  Je, kapata bahati ya kupata hazina?   Wakamuuliza nani wewe?  Akasema: "mimi ni mtu wa mji huu huu, nimeishi hapa jana na Decianus ndio alikuwa mfalme". Wakamhukumu kuwa ni mwendazimu na wakamchukuwa kumpelekea kwa mkuu wa serikali (gavana) ambaye alimuuliza maswali mbali mbali kuhusu hali yake kutaka kujua vizuri vipi anazo pesa za karne na vipi anasema kuwa jana tu aliishi na mfalme Decianus?

 

 

Mkuu wa serikali alishangazwa na akachanganyikiwa na akili. Kijana wa Asw-haabul-Kahf alipotaja kuhusu wenzake walio pangoni, mfalme wa nchi ile na baadhi ya watu wakaenda katika lile pango. 

 

 

Kijana wa Aswhaabul-Kahf akamwambia: "Acha nianze kuingia mimi kwanza ili niwajulishe wenzangu (Aswhaabul-Kahf waliobakia)." Wakaingia katika pango na mfalme akawasalimia na kuwakumbatia vijana. Kumbe yeye hakuwa mshirikina bali alikuwa   Muislamu (aliamini Tawhiyd ya Allaah) na jina lake aliitwa Tedosis.  Asw-haabul-Kahf wakafurahi kuonana naye. Wakaketi kuzungumza na mfalme kisha wakaagana. Mfalme na watu wake walipoondoka, vijana wakarudi zao kulala na hapa tena Allaah akawafisha. [Taariykh At-Twabariy 2:9].

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Maana ya:

 وَكَذَلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ

21. Na hivyo ndivyo Tulivyowatambulisha kwa watu.

 Kama vile Tulivyowafanya walale na kuamka na kiwiliwili chao kizima, Tumekifanya kisa chao kijulikane kwa watu waliokuwapo wakati ule. 

 

 لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ

Ili wajue kwamba ahadi ya Allaah ni haki. Na kwamba Saa haina shaka yoyote humo. Pale walipozozana baina yao kuhusu jambo lao. 

 

 

Kuhusu kufufuliwa kwao: Wengine waliamini kisa chao, na wengine walikikanusha, kwa hiyo Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Aliwafanya watu wa pango watambulike kama ni uthibitisho, aidha kwa mapendeleo yao au dhidi yao. 

 

 

Watu hapo wakasema:

   ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ ۚ 

 

Jengeni jengo juu yao; Rabb wao Anawajua vyema.

 

Yaani, zibeni mlango wa pango wabakie humo tuwaache kama walivyo.

 

 

 قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَى أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾  

Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Bila shaka tutajenga Msikiti juu yao.

 

 

Hawa waliosema hivi ni wale watu waliokuwa na ukubwa, nguvu na vyeo fulani. Lakini walikuwa watu wema au wabaya? Kuna majadiliano kuhusu jambo hili kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

 

 لَعَنَ اللَّهُ الْيَهُودَ وَالنَّصاَرَى اتَّخَذُوا قُبُورَ أَنْبِيَائِهِمْ وَصَالِحِهِمْ مَسَاجِدَ

 “Allaah Kawalaani Mayahudi na Manaswaara, wamefanya makaburi ya Manabii wao kuwa ni misikiti” [Fat-h- Al-Baariy 1: 634].

 

 

Ni onyo kutoka kwa Allaah kwamba walivyofanya hivyo kujenga msikiti kwenye makaburi ni shirk kubwa.  

 

 

Idadi ya watu wa pangoni:

 

 

  سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاء ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا ﴿٢٢﴾

22. Watasema: Watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na (wengine) wanasema: Watano na wa sita wao ni mbwa wao -   kwa kuvurumisha bila ya kujua. Na (wengine) wanasema: Saba na wa nane wao ni mbwa wao. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Rabb wangu Anajua zaidi idadi yao. Hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu. Basi usibishane nao isipokuwa mabishano dhahiri (Tuliyokufunulia Wahy), na wala usimuulize yeyote kuhusu khabari zao. [Al-Kahf: 22].

 

 

  سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ…..﴿٢٢﴾

22.  Watasema: Watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na (wengine) wanasema: Watano na wa sita wao ni mbwa wao -   kwa kuvurumisha bila ya kujua… 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuelezea kuwa kulikuweko na mgogoro kuhusu idadi ya vijana hao waliokuwako pangoni.  Aayah inatuonyesha rai tatu na hakuna ya nne.  Na Allaah Anatuonyesha kuwa rai mbili za mwanzo si za kweli kwani kasema,

 

 رَجْمًا بِالْغَيْبِ

kwa kuvurumisha bila ya kujua.

 

 

Maana; wanasema bila kuwa na elimu yoyote, kama vile mtu anayerusha mshale bila ya kuwa na shabaha fulani, huwa hawezi kufikia (kudunga) panapostahiki kufikiwa, na akifikia basi itakua ni bahati tu sio kusudio. 

 

 

Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anataja rai ya tatu na wala Hakutaja kuwa ni kweli au sio kweli.

 

وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ

Na (wengine) wanasema: Saba na wa nane wao ni mbwa wao.

 

 

Ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee Mwenye ujuzi wa idadi yao:

قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم 

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Rabb wangu Anajua zaidi idadi yao.

 

Kwa maana: Ni bora zaidi pale kunapokuwa na shaka ya jambo kama hili, kulirudisha katika ujuzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Si sawa kutaka kuingilia mambo bila ya kuwa na elimu. Tukipewa elimu kuhusu jambo tulieleze, ikiwa haikutufikia elimu basi tuepuke kueleza jambo tusilolijua. 

 

 

Kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيل

Hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu..

 

Qataadah kasema kwamba: “Ibn 'Abbaas kasema: Mimi ni mmoja wa wachache waliotajwa katika Aayah hii. Idadi yao walikuwa ni watu saba." [Atw-Twabariy 17: 642].

  

 

 فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاء ظَاهِرًا

Basi usibishane nao isipokuwa mabishano dhahiri (Tuliyokufunulia Wahy),

 

 

Maana ya ‘mabishano ya juu juu’: kwa upole, kwani  sio jambo kubwa na la muhimu kulijua. 

 

 

وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا ﴿٢٢﴾

na wala usimuulize yeyote kuhusu khabari zao.

 

Maana: Hawana ujuzi kuhusu jambo hilo isipokuwa wanabahatisha tu kwa yale yasiyoonekana. Hawana ushahidi kutoka kwenye chanzo cha uhakika.  Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amekuleta wewe ee Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ukweli (haki) ambao hauna shaka au kubabaisha. Ukweli ambao unatakiwa uwekwe mbele ya vitabu vyote vya nyuma.  

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

  1. Kuthibitisha kufufuliwa na malipo ambayo wameyakanusha watu Wa Makkah.

 

  1. Kusadikisha kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Allaah Kawalaani Mayahudi na Manaswaara, wamefanya makaburi ya Manabiy wao kuwa ni misikiti” na  kauli yake “Hakika anapokuweko mtu mwema na anapokufa, hao humjengea katika kaburi lake msikiti na wakaweka picha yake (sanamu lake), hao ni viumbe wa shari (wabaya kabisa) siku ya Qiyaamah" [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

  1. Kusadikisha kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mtafuata nyendo za watu wa kabla yenu shibiri baada ya shibiri, dhira'a baada ya dhira'a”. Na hii imethibitika kutokana na Waislamu waliowajengea Awliyaa wao (Wapenzi wao) na waja wema misikiti karibu na makaburi yao.

 

  1. Kudhihirisha ikhtilaaf ya Ahlul-Kitaab na kutokuwa na uhakika wao kwa matukio ya historia.

 

  1. Kudhihirisha idadi ya vijana wa pangoni kwamba ni saba na wanane wao ni mbwa wao.

 

.../4

 

Share