Mama Hataki Kunyonyesha - Nini Hukmu Yake?

 

SWALI:

 RAMADHAN KARIM WA SAUMUL MAKBUL NDUGU ZANGU NYOTE WA ALHIDAAYA. SWALI LANGU NI KUHUSU KUNYONYESHA. KAMA MTU AMEZAA NA AKAAMUA ASIMNYONYESHE MTOTO, KWA SABABU KWANZA MAZIWA HUWA YANAMJAA SANA NA ULE UZITO UNAMLETEA TAKLIF SANA, PILI HUWA HANA RAHA HATA KUWA NA MUMEWE, ANAJIONA ANAONGEZA MWILI SANA. ALINYONYESHA WA KWANZA LAKINI AKAONA NI TAKLIF KWAKE. SASA SWALI NI MBELE YA ALLAAH [SW] ANA DHAMBI? KWA SABABU SI TAKLIF NI HARAM? INSHAALLAH MUTATUELEZA. SHUKRANI SANA

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali. Hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ameweka mambo kwa maslahi ya mwanaadamu kwa ujumla. Hata hivyo kwa kujua maumbile ya mwanadamu kwa baadhi yao wenye kupata taklifu Akawaachia uamuzi wenyewe wachague lile ambalo halitawapatia taklifu au uzito. Allaah Aliyetukuka Anatueleza:

Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyostahiki jihadi yake. Yeye Amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini” (22: 78).

Qur-aan inatufahamisha kuhusu jukumu la mama la kumnyonyesha mtoto wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuambia:

Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili” (31: 14).

Hili la kunyonyeshwa mtoto Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amempatia mama lakini hakulilazimisha. Ndio Akasema Aliyetukuka:

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada” (2: 233).

Kwa hiyo, mama anaweza kumuachisha kumnyonyesha mtoto lakini baada ya kuridhiana na baba wa mtoto (mumewe). Haifai mama kuchukua uamuzi wake peke yake katika mas-ala nyeti kama hiyo.

Mbali na kuwa inakubaliwa Kiislamu kumuachisha mtoto kunyonya lakini maslahi ya mtoto ni lazima yatizamwe na asiwe ni mwenye kudhulumiwa. Ni kuwakumbusha dada na mama zetu ambao wana nia ya kumuachisha mtoto kunyonya kwa sababu moja au nyingine kama alivyouliza muulizaji wafanye baada ya kunyonyesha kwa uchache mwezi mmoja. Maziwa ya mwanzoni ya mama (tamari) yana kinga kubwa sana kwa mtoto na hivyo anainukia akiwa na siha nzuri.

Tafadhali ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi kuhusu faida za kumnyonyesha motto:

Je Kuna Malipo Kama Hukumnyonyesha Mtoto?

Tufahamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Haikalifishi nafsi ila kwa iwezalo nafsi. Hivyo tunamuambia dada yetu akiwa anaona taklifu awe ni mwenye kushauriana na mumewe kwa maslahi ya mama na mtoto lakini asiwache kumnyonyesha mtoto mwezi ule wa mwanzo.

Tunamuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amuondolee taklifu dada yetu aliyeuliza swali na wengine mfano wake.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share