'Aqiyqah Anayofanyiwa Mtoto Mchanga Katika Sunnah

'Aqiyqah Anayofanyiwa Mtoto Mchanga

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

 

Assalam alyekum

Mimi naomba kuelimishwa kuhusu suala zima la hakiki kwa mtoto. je ni utaratibu upi ambao inatubidi kuufuata ili kufikia mafundisho kama alivyotufundisha bwana Mtume (s.a.w.)

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza tunakunasihi kutokufupisha maamkizi ya Kiislaam na Thanaa au kuwatakia Radhi Swahaba na mengineyo ambayo watu wanakosea kama hivyo. Jambo hilo limekemewa  na ‘Ulamaa wetu. Bonyea viungo vifuatavyo upate faida:

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

Ama kuhusu suala la kumfanyia mtoto 'Aqiyqah, kwanza tufahamu maana ya 'Aqyqah.

 

‘Aqiyqah maana yake ni kukata. Na katika sharia ni mbuzi anayechinjwa kwa ajili ya mtoto aliyezaliwa anapofika siku ya saba tokea kuzaliwa kwake.

 

‘Aqiyqah ni Sunnah iliyotiliwa mkazo kwa mwenye uwezo nayo.

 

 

Na hili ni jukumu la wazazi kumfanyia mtoto wao kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 “Kila mtoto amefungika na ‘Aqiyqah yake, itachinjwa kwa ajili yake siku ya saba na atapewa jina, na atanyolewa kichwa chake” (Ahmad na An-Nasaaiy).

 

 

Kwa ajili ya shughuli hiyo ni lazima achinjwe mnyama anayefaa kuchinjwa kwa ajili ya Udh-hiyah kwa kuzingatia kusalimika kwake na kasoro yoyote kama kuwa kilema au kukosa jicho na umri wake uwe zaidi ya mwaka.

 

 

Baada ya kuchinjwa mnyama huyo akiwa ni mbuzi au kondoo ni Sunnah kumgawa kama inavyogaiwa nyama ya Udh-hiyah. Baadhi ya nyama watakula watu wa nyumbani, na nyingine utatoa sadaka.

 

 

Ni vyema na ndio sahihi zaidi kuchinja siku ya 7 ama riwaya za siku ya 14 au 21 au 28 hazina uhakika sana. Kwa hiyo mtu ajihimu sana kuchinja siku hiyo ya saba. Ikiwa hakuweza kwa sababu fulani fulani, basi Maulamaa wanasema kuwa anaweza kufanya wakati wowote katika uhai wake.

 

 

‘Aqiyqah ya mtoto wa kiume ni mbuzi wawili na wa kike ni mbuzi mmoja kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja mbuzi wawili alipozaliwa Hasan” (At-Tirmidhiy).

 

 

Japokuwa zipo riwaya nyingine ambazo zinaonyesha kuwa mtoto wa kiume na wa kike wanachinjiwa mbuzi mmoja mmoja.

 

 

Wanachuoni wamekanusha  riwaya hizi kwa kusema ni vyema kwa mvulana kuchinjiwa mbuzi wawili lakini ikiwa mzazi hana uwezo basi atachinja mmoja.

 

 

Ikiwa mtoto atakufa kabla ya siku ya saba basi hatochinjiwa.

 

 

Pia ni Sunnah siku ya saba hiyo unayofanya 'Aqiyqah, kumpa mtoto jina, na jina liwe zuri na haswa bora kama alivyofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama majina ya uja wa Allaah kama, 'Abdur-Rahmaan, 'Abdullaah n.k. au majina ya Mitume, Maswahaba na wema waliotangulia.

 

 

Na si vizuri kuwaita watoto majina mabaya au yasiyo na maana kama; Vita, Pondamali, Chausiku, Kufakulala n.k.

 

 

Na pia amfanyie tahniyk, tahniyk ni kumlambisha mtoto tende alizozitafuna au asali au kitamu chochote atakachokipata.

 

 

Kuna baadhi ya 'Ulamaa wamependekeza kumuadhinia mtoto anapozaliwa kwenye sikio lake la kuume ili liwe jambo la kwanza analosikia mtoto ni neno la Tawhiyd, lakini maelezo au Hadiyth zilizosimuliwa kuhusu kumuadhinia mtoto sikio la kulia na kumkimia sikio la kushoto, hakuna iliyo sahihi kwa mujibu wa Wanachuoni wabobezi wa elimu ya Hadiyth.

 

 

Hayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kwa wazazi wanaporuzukiwa watoto.

 

 

Tunatumai ya kuwa tutakuwa tumejibu swali lako na kwa manufaa zaidi bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Kufanya 'Aqiyqah Ni Lazima Au Sunnah?

http://alhidaaya.com/sw/node/813 

 

‘Aqiyqah –Inafaa Kuwafanyia Watoto Wanapokuwa Wakubwa – Tofauti ‘Aqiyqah Ya Mtoto Wa Kiume Na Wa Kike

http://alhidaaya.com/sw/node/2518

 

Anaweza Kujifanyia Mwenyewe 'Aqiyqah Ukubwani Ikiwa Hakufanyiwa Na Wazazi Wake?

http://alhidaaya.com/sw/node/3957

 

Nani Mwenye Jukumu la Aqiyqah?

http://alhidaaya.com/sw/node/3004

 

‘Aqiyqah; Je, Ni Lazima Wapatikane Mbuzi Weupe Tu?

http://alhidaaya.com/sw/node/5224

 

Afanye ‘Aqiyqah Nchi Za Njei Anakoishi Ambako Hakuna Jirani Waislamu Au Afanye Nyumbani Walioko Masikini?

http://alhidaaya.com/sw/node/4827

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

www.alhidaaya.com

 

 

Share