Avunje Ndoa kwa sababu Walizini Kabla ya Ndoa?

 

SWALI:

 

Sheikh suala hili linanitatisha sana na kunikosesha raha katika maisha yangu, naomba jawabu kutoka kwenu. jee inafaa kuomba talaka kama unahisi ndoa yako inahitilafu na unawasiwasi, ndoa yenyewe imefungwa baada ya mwanamke na mwanamme kzini kabla ya kuowana, lakini mwanamke alikuwa hana mimba. kwani IBADHI wanasema ndoa haisihi na SUNNI wanasema ndoa inasihi, jee UISLAM unasemaje iko ndoa au hakuna? na inafaa kuomba talaka kama ndoa ipo ilikujitoa wasiwasi?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa muulizaji swali hili. Na inaonyesha kuwa mas-ala haya ya uasherati au mafungamano ya kimwili baina ya mume na mke yamekithiri. Inatakiwa tuwe ni wenye kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) popote tulipo na kila wakati. Na kama wanaadamu huwa tunakosea, hivyo tunapokosea au kufanya dhambi basi hapo hapo turudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kumuomba msamaha na kutubia toba ya kweli kweli. Na pia tufanye mambo mema ili yafute hayo mabaya na ya madhambi.

 

Mwanzo inatakiwa tufahamu kuwa zinaa ni kitendo kibaya sana kilichokatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na yeyote mwenye kufanya amali hiyo basi angefaa apatiwe adhabu ya kisheria hapa duniani. Kwa kuwa hakuna dola ya Kiislamu kwa wakati huu na nchi nyingi tunazoishi si za Kiislamu wala Waislamu wengi, anatakiwa mkosa afanye toba ya sawasawa pamoja na kufanya mema mengi kadri ya uwezo wake.

Ni wazi kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Husamehe madhambi yote ikiwemo dhambi la uzinzi kama Alivyosema:

Sema: Enyi waja Wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Allaah; bila shaka Allaah Husamehe dhambi zote; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu” (39: 53).

Na hasa kuhusu kusamehewa dhambi la zinaa, anasema Aliyetukuka:

Na wale wasiomwomba mungu mwengine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara. Atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaama, na atadumu humo kwa kufedheheka. Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Allaah Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allaah” (25: 68 – 71). Tafadhali tazama sehemu zilizopigwa msitari kwa kuweza kuelewa zaidi Aayah zilizo juu.

Kisha ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi katika mas-ala kama yako:

Ndoa Ya Wazinifu

Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa

Wazinifu Waliotubu Wanaweza Kufunga Ndoa Na Waliotakasika

Ndoa Ya Waliofanya Zinaa

Na kuhusu mas-ala ya kusamehewa kwa dhambi hilo, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:

Mche Allaah popote ulipo. Na ufuatilize jambo baya kwa jema, litalifuta (hilo baya)” (at-Tirmidhiy, ambaye amesema ni Hadiyth Hasan, na katika baadhi ya nuskha ni Hasan Swahiyh, pia na Ahmad, ad-Daarimiy, nayo ni Hadith Swahiyh).

 

Kuhusu mas-ala haya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Mwanamume mzinifu hatamwoa ila mwanamke mzinifu au mwanamke mushrik, na hamna atakayemwoa mwanamke mzinifu isipokuwa mwanamume mzinifu au mushrik; na ndoa kama hizo zimeharamishwa kwa Waumini wa kweli. …Isipokuwa wale wenye kutubu baada ya hayo na kujirekebisha; bila shaka Allaah ni Msamehevu na Mrehemevu” (24: 3, 5).

    

Ikiwa watu hao wawili wamefanya zinaa wanaweza kuoana kisheria baada ya kutenganishwa kwa muda. Muda huu ni wa kuhakikisha kuwa yule mwanamke hana mimba yoyote na kwa sababu binti hakuwa na mimba basi hakuna tatizo la wao kuoana. Muda unaweza kuanzia miezi mitatu au kutegemea uamuzi wa Qaadhi ikiwa katika sehemu hiyo yupo mmoja.

 

Kuhusu Aayah hizi anasema Ibn Kathiyr: “Amesema Imaam Ahmad kuwa haifai ndoa baina ya wazinifu mpaka watubu, akitubu inasihi Nikaah. Na hivyo ndivyo alivyosema Imaam Abu Muhammad bin Abi Haatim ambaye amemnukuu Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa alikuja mtu ambaye amezini akamuuliza kama anaweza kumuoa yule mwanamke baada ya kuwa ametubia, lakini watu wamemwambia haifai kwa kumsomea Aayah ya 3 (hapo juu). Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alimwambia hiyo si mahali pake unaweza kumuoa. Na wanazuoni wengine wanasema kuwa Aayah hii imetenguliwa hukumu yake na ile Aayah, ‘Na waozeni wajane miongoni mwenu’ (24: 32), yaani Waislamu” (Tafsiyrul Qur-aanil ‘Adhiym, Mj. 3, uk. 270 – 272).

 

Hakika ni kuwa wametofautiana wanazuoni wa zamani katika jambo hili katika makundi mawili:

 

a)    Kuharamishwa ndoa, nayo ni rai ya ‘Aliy, al-Baraa’, ‘Aaishah na Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhum).

b)    Kujuzu ndoa na aliyezini, nayo ni rai ya Abu Bakr, ‘Umar, Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhum) na ni madhehebu ya Jamhuur na huo ndio msimamo wa Mafakihi wanne na Maimamu waliojitahidi.

 

Dalili za Rai ya Kwanza

 

Wametoa dalili wanaoharamisha kwa dhahiri ya ayah nayo ni kauli ya Aliyetukuka:

Mwanamume mzinifu hatamwoa ila mwanamke mzinifu au mwanamke mushrik” (24: 3).

Wakasema: Dhahiri ya Aayah hii ni habari na uhakika wake ni kukataza na kuharamisha kwa dalili nyengine katika Aayah hiyo:

Na ndoa kama hizo zimeharamishwa kwa Waumini wa kweli”.

Na amesema ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu): Anapozini mtu yeyote anatenganishwa baina yake na mkewe, na hivyo hivyo akizini mke.

 

Na wametoa dalili kwa yaliyotokea kwa Marthad bin Abi Marthad (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa Swahaba, naye alizini na ‘Inaaq, mwanamke malaya Makkah wakati wa ujahiliya. Alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kumuomba ruhusa amuoe. Alimuomba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) mara mbili bila kujibiwa. Alipomuomba mara ya tatu, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alimsomea Aayah hii na akamwambia asimuoe (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

Na zipo Hadiyth nyengine kutoka kwa Ibn ‘Umar na ‘Ammaar (Radhiya Allaahu ‘anhum) zinazoelezea jambo hilo.

 

Dalili za Rai ya Pili (Rai ya Jamhuur)

 

Wametoa dalili zao kwa kuruhusiwa ndoa kama ifuatavyo:

 

(i)      Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu aliyezini na mwanamke na akataka kumuoa, akasema: “Mwanzo ni uchafu na mwisho ndoa, na haramu haifanyi halali kuwa haramu” (atw-Twabaraaniy na ad-Daaraqutwniy).

 

(ii)      Iliyopokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa: “Alipokuwa Abu Bakr yuko Msikitini mara akaja mtu ambaye alikuwa anataka kumwambia kitu lakini hakuweza kueleza kwa ufasaha. Abu Bakr alimwomba ‘Umar amchukue yule mtu kando ili amdadisi kuwa anataka kusema nini. Alipomwuliza, alimwambia kuwa kuna mgeni aliyemtembea naye amezini na binti yake. Hapo ‘Umar alimpiga kwenye kifua chake na kumwambia: ‘Ole wako, kwa nini usingesitiri aibu ya binti yako?’ Abu Bakr aliamuru wote wawili wapatiwe adhabu, kisha akawaoza na kuhamishwa mbali na mji kwa mwaka mmoja” (Qaadhi Abu Bakr Ibn al-‘Arabiy, Ahkaamul Qur-aan, Mj. 3, uk. 1319).

 

(iii)     Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliulizwa kuhusu mas-ala hayo, akasema: “Mwanzo ni uchafu, na mwisho ni ndoa. Mfano wa hilo ni kama mfano wa mtu aliyeiba tunda katika bustani, baada ya hapo alikuja kwa mwenye bustani na kununua kutoka kwake matunda yake. Aliyoiba ni haramu, na aliyonunua ni halali” (Tafsiyrul Qurtwubiy, Mj. 12, uk. 170).

 

iv)      Wameawili Aayah hii tukufu: “Mwanamume mzinifu hatamwoa ila mwanamke mzinifu au mwanamke mushrik” (24: 3). Hii imechukuliwa kwa ujumla na wingi wake, na maana yake ni kuwa fasiki (asi) mwovu ambaye ni mzinifu hatamani kuoa Muumini mwanamke mwema, hakika ni kuwa yeye ana hamu ya kuoa aliye asi mwovu mfano wake au mshirikina. Na mwanamke asi mbaya hana hamu ya kuolewa na Muumini mwema miongoni mwa wanaume, kwani hakika yake ni kuwa yeye ataka jinsi ya mfano wake wa asi na mushirikina.

 

(v)     Na wamesema baadhi ye wengine: Aayah hii hukumu yake imetenguliwa na Aayah nyengine ya Suratun Nuur: 32 (Tafsiyr Aayaatul Ahkaam minal Qur-aan, Mj. 2, uk. 36 – 37).

 

Na Dkt. ‘Aliy ‘Abdul-Haliym Mahmuud katika kitabu chake at-Tarbiyyatul Islaamiyyah Fiy Suuratin Nuur, uk. 36 – 41 amesema yafuatayo: “Muislamu hafai kuoa au kuolewa na mzinifu ambaye bado yupo katika kazi hiyo na wala hajatubia. Wanazuoni wengine wanaona kuwa makusudio ya Aayah hii tukufu ina maana ya jimai kwa neno Yankihu… Katazo hapa ni ikiwa wazinifu wamepatiwa adhabu haitofaa kuolewa au kuoa mwengine na hiyo ni kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam):

Haoi mzinifu aliyepigwa mijeledi isipokuwa mfano wake’ (Abu Daawuud). Na wanazuoni wengine wanasema Aayah hii ilikuwa ni hasa kwa Marthad (Radhiya Allaahu ‘anhuma) na kahaba aliyeitwa ‘Inaaq. Na wengine wanasema yeyote mwenye kuzini na mwanamke anafaa amuoe na asiolewe na mwengine yeyote, nayo ni kauli ya Ibn ‘Umar, Saalim, Jaabir ibn Zayd, ‘Atwaa’, Twaawuus, Maalik ibn Anas na Abu Hanifah”.

 

Kwa muhtasari ni kuwa wazinifu wakitubia na kujirekebisha basi wanaweza kuoana. Ondoa wasiwasi wako kuhusu ndoa yako kwani wasiwasi unaletwa na shetani naye kwetu ni adui wa wazi kabisa isipokuwa uwe unataka kumuacha kwa nafsi yako mwenyewe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share