Kuzuia Kukata Nywele Na Kukata Kucha Ni Kwa Familia Nzima Au Kwa Mtu Mmoja Anayechinja Au Kugharamia Uchinjaji?

 

Kuzuia Kukata Nywele Na Kukata Kucha Ni Kwa Familia Nzima

Au Kwa Mtu Mmoja Anayechinja Au Kugharamia Uchinjaji?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Maelezo mliyotoa kuwa mwenye kutia nia ya kuchinja azuwiye kukata nywele na makucha. Swali langu, je ni watu wote katika nyumba wajizuie au ni mtu anayelipia tu kuchinja? Mfano baba ndiye mwenye kulipa, je mkewe naye azuie kukata nywele na makucha na watoto pia? Nitashukuru kupata jibu haraka hali tumeshaingia katika siku kumi na hatuna hakika nalo jambo hili.
 
Wa Billah tawfik.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwenye kupasa kuzuia kukata nywele na kucha ni mtu mmoja katika nyumba, aghlabu ni baba mwenye kulipia kuchinja, yaani mwenye kumiliki uchinjaji. Hii ni kutokana na kauli ya Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((إذا رأيتم هلال ذي الحجة وأراد أحدكـم أن يضحّي فليمسك عــن شعره وأظفاره) وفي راوية: ((فلا يأخذ من شعره ولا من أظفـاره حتى يضحّي)) مسلم

Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mkiuona (Utakapoandama) mwezi wa Dhul-Hijjah na ikiwa yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake)

Na katika riwaya nyingine ((Asikate nywele wala kucha mpaka akimaliza kuchinja)) [Muslim na wengineo] 

 

Amri hiyo inampasa kutekeleza mwenye kuchinja ikiwa atachinja mwenyewe au hata kama anawakilisha mtu kumchinjia. Ama wale ambao kwa ajili yao wanachinjiwa yaani watu aliowajibika nao kuwachinjia, wao haiwahusu amri hiyo kwani kauli imetaja  ((ikiwa yuko anayetaka kuchinja)), hivyo haikutajwa kwa ujumla na kama ingeliwajibika watu wote katika nyumba basi kungebainishwa.

 

Vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichinja kwa ajili ya familia yake na hakuna mapokezi yoyote yanayoonyesha kuwa aliwaamrisha ahli yake wazuie kukata nywele na kucha.

 

Kadhaalika, kuna maswali mengi yanaulizwa kuhusiana na kucha kukatika yenyewe au kucha kutokezea kumuumiza, anaweza kuiondosha kwani hiyo ni dharura na ni kuondosha dhara. Wanachuoni wanaona hakuna ubaya katika hilo, na hata zile nywele zenye kutoka wakati wa kuzichana au ndevu zinapochanwa zikatoka moja moja; yote hayo hakuna ubaya, isipokuwa mtu anatakiwa ajitahidi asitumie nguvu na alainishe nywele zake kwa maji au mafuta ili zisiwe ngumu wakati wa kuzichana, kuepusha kukatika.

 

Na Allaah Anajua zaidi  

 

Share