Mume Anaweza Kumlipia Mke Kufanya Hijjah. Kuna Sharti Zozote Zinazopaswa Kutimizwa?

SWALI:

AAWW!

Nauliza:

Mume kumtolea nauli ya matumizi mke kwenda HIJJA inasihi? Kama jibu ni ndiyo, kuna pre-requisites e.g. Jee kama yeye mwenyewe an uwezo? Si Hijja inamjuzu mwenye uwezo tu.


JIBU

:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunapenda kukumbusha ndugu muulizaji kuacha kufupisha salaam unapoandika, unapoteza fadhila na ujira kwa kufanya hivyo.

Kama tunavyoelewa kuwa Hijjah ni nguzo ya tano kwa Waislamu nayo ni Faradhi kwa waume na wake. Hiyo ni kuwa taklifu zote za amali katika Uislamu ni faradhi kwa wote. Allaah Anasema:

Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, Tutamhuisha maisha mema; na Tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda(16: 97).

Na Hijjah imefaradhishwa kwa wote pindi yanapopatikana masharti Fulani. Allaah Anasema:

Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah  imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Allaah  si mhitaji kwa walimwengu (3: 97).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “…Na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo” [Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy kutoka kwa ‘Umar bin al-Khatwaab  (Radhiya-Allaahu ‘anhu)].

Ibara hii ya Aayah na Hadiyth ina maana ya kuwa kila Muislamu ni lazima ahiji mara moja katika maisha yake akiweza kufanya hivyo. Uwezo una tafswili nyingi na yaliyo muhimu ni: -

  1. Awe na afya nzuri ya kuweza kustahamili mazito ya safari.

 

  1. Kuwe na usalama njiani – kwenda na kurudi

 

  1. Awe na uwezo wa kutoa gharama za safari na kuacha masurufu yote ya wale wanaomtegemea. 

Ikiwa sharti moja katika hayo limekosekana basi Hijjah haijamlazimu mtu huyo. 

Hivyo,  jibu ni kwamba inafaa kwa mume kumpeleka mkewe Hijjah ikiwa atakuwa ana uwezo huo. Na inapendeza zaidi ikiwa watakwenda pamoja kwani hilo litaongeza mahaba baina yao. Na kwa ajili hiyo alipokuja mtu kwa Mtume (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).) akamwambia kuwa mkewe anakwenda Hijjah naye amejiandikisha kwenda katika Jihadi, Mtume (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aende na mkewe kuhiji.

 

Na ni msingi wa Uislamu kuwa ((Yeyote mwenye kumuelekeza mtu mwengine katika kheri atapata thawabu sawa na mwenye kufanya hiyo amali)) [Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kutoka kwa Ibn Mas‘uud na Abu Hurayrah (Radhiya-Allaahu ‘anhumaa)]

Na hivyo hivyo ikiwa mke ni muweza kuliko mumewe anaweza kumsaidia mumewe kumpeleka Hijjah na pia atapata ujira mkubwa. Ikiwa mke ana uwezo anaweza kujipeleka mwenyewe baada ya kupata mahri wa kusafiri naye. Na wakati huo inakuwa ni lazima kwake kwa sababu masharti yote yametimia. Ikiwa hana uwezo haiwi ni lazima kwake lakini ikiwa atasaidiwa kutekeleza Faradhi hiyo basi hakuna tatizo lolote. Na hii ni ‘Ibadah ambayo ni tofauti na ‘Ibadah nyingine ambazo mtu hata akiwa mgonjwa anatakiwa afanye mwenyewe kama Swalah, lakini Hijjah ikiwa  mgonjwa huwezi kwenda mwenyewe unaweza kumpatia mtu hela zinazohitajika akaenda kukuhijia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

  

Share